Monday, November 26, 2007

Watu weusi tuna akili ndogo?


**********************

na Padri Privatus Karugendo.

JAMES Watson, mwanasayansi maarufu sana duniani na mshindi wa nishani ya Nobel katika tiba mwaka 1962, ameleta mjadala mkubwa baada ya kudai kwamba mtu mweusi ana akili ndogo kuliko mtu mweupe. Kauli yake hiyo imeshikiwa bango na wapinzani wa ubaguzi wa rangi kwa kuwa inamdhalilisha mtu mweusi.

Huyu si mtu wa kwanza kusema hivyo, tofauti ni kwamba yeye ameisemea kisayansi zaidi. Siku za nyuma waziri mkuu mmoja wa Japan alipata kusema maneno kama hayo kwamba anatilia shaka uwezo wa mtu mweusi. Waziri mwingine wa Japan na yeye alishanukuliwa kusema hivyo hivyo. Wote baadaye waliomba radhi lakini ujumbe ulifika.

Chika Onyeani katika kitabu chake cha Capitalist Nigger naye anashangaa ni kwa nini Mwafrika atukanwe namna hiyo na mawaziri wa Japan lakini bado waendelee kununua bidhaa toka Japan. Anaelezea pia kwamba jamii yote ya watu weusi inafanana kwa kiasi kikubwa.

Kwa mfano ukikutana na Mmarekani mweusi aliyezaliwa na kukulia Marekani au Carribean au Afrika kwenyewe, bado wana tabia zile zile ambazo zinatia shaka kama kweli akili za Waafrika si ndogo kwa kiasi fulani.

Ukianza kuangalia matokeo mbalimbali yanayotokea Afrika, kuanzia enzi za miaka ya nyuma, unaanza kuwa na wasiwasi kuhusu hali na uelewa wa mtu mweusi. Historia inatuambia kwamba, hadi karne ya 16 kiwango cha maendeleo kati ya Ulaya na Afrika kilikuwa sawa.

Tunaambiwa pia kwamba miaka ya 1960 baadhi ya nchi za Kiafrika zilikuwa mbele kimaendeleo au katika usawa mmoja na nchi za Asia ambazo leo ziko mbali kimaendeleo. Bado unajiuliza ni wapi kwenye matatizo? Kwa nini Waafrika waachwe nyuma kila leo?

Inavyoelekea ni kwamba bara la Afrika linakuwa kama kigezo kizuri cha kupima maendeleo na mabara mengine. Ripoti za umasikini duniani zinaonyesha kwamba umasikini duniani umepungua kwa kiasi kikubwa lakini kwa Afrika unaonyesha kuongezeka. Mbaya zaidi hakuna ishara ya watu hao kutoka katika utando huo wa umasikini walikonasa kabisa.

Idadi ya watu waliopungua umasikini kidunia unatokana na kukua kwa uchumi wa China na India, nchi zenye idadi kubwa zaidi ya watu duniani. Kwa hivyo, uwezo wao wa kupunguzia watu wao umasikini unachangia takwimu za kidunia zionekane nzuri lakini kwa Afrika hakuna mabadiliko mazuri.

Ukipima baadhi ya kauli za hawa tunaowaita wabaguzi utagundua kuna ujumbe wanawasilisha. Kama tukichukulia Tanzania kama mwakilishi wa Waafrika, tunaweza tukajadili baadhi ya hoja na kujipima ni kweli tuna akili ndogo kijenetiki au mazingira yetu yanatufanya tuwe na uwezo mdogo wa kutumia akili zetu au tujiulize ni wapi tumeteleza?

Tanzania hii ina rasilimali nyingi sana lakini bado hatujaweza kufika popote pa maana. Tunasaini mikataba ya hovyo kabisa ambayo inampa mgeni mamlaka ya kuchukua rasilimali jinsi anavyotaka huku wenyeji tukibaki hoi kabisa. Tuna mapori ya kutosha na mito na maziwa ya kutosha lakini bado tunaagiza chakula nje ya nchi.

Tuna watu wanajilundikia mabilioni ya fedha benki huku watu wa kijijini kwake hawana maji ya kunywa. Kuna watu wananunua samani za mabilioni ya Shilingi kwenye nyumba walizojengewa na Serikali wakati ambapo Shule ya Sekondari ya Azania, iliyopo katikati ya jiji kuu la nchi, ina wastani wa tundu moja la choo kwa wanafunzi 300!

Shule karibu zote mpya zilizojengwa, kuanzia za msingi hadi za sekondari, zina uhaba mkubwa wa vyoo. Hivi ni vitu vya msingi kabisa lakini bado hatujaweza kuvitatua.

Bado tunazipa likizo ya kodi kampuni kubwa huku tukifuatilia vikodi vidogo vidogo vya wafanyabiashara wadogo au hata wachuuzi. Kampuni kubwa zinaruhusiwa kubeba hasara na kuipeleka kwenye mahesabu ya mwaka ujao kwa miaka kadhaa lakini hiyo hiyo kampuni inayopata hasara inaendelea kufanya biashara!

Sasa hivi tunasifiwa kwa kuweza kufuatilia kodi kwenye biashara ndogo ndogo huku tukiwa hatujafanya lolote la maana kwenye kodi za makampuni makubwa. Uwezo wa Serikali wa ukusanyaji hupimwa na kuongezeka kwa kodi za makampuni makubwa (Corporate Tax) na si kuongezeka kwa kodi za mapato zinazotokana na kuajiri watu wachache.

Ni lazima tukae chini tujiulize: Kunani katika akili zetu? Tunavuna madini ya Tanzanite lakini hatuwezi kuyauza. Tunasema tuna mafuta lakini tukitaka kuyachimba tunamwita Mzungu, japokuwa tumekuwa tukizalisha wahandisi na wanajiolojia kila mwaka. Lazima tujiulize kama elimu yetu ina mushkeli au la!

Sasa hivi tunajigamba kuwa na vyuo vikuu karibia 30 lakini bado tunaagiza vijiti vya kuchokonolea meno kutoka Malaysia. Ni lazima tujiulize tulipoteleza. Ni lazima wakati mwingine tujiulize kama kweli hatuna mushkeli kwenye akili zetu.

Maamuzi yenye maslahi ya taifa yanachukua muda mrefu kuchukuliwa. Wananchi wamekuwa wakipigia kelele suala la Richmond lakini imechukua miezi kadhaa kuchukua uamuzi wa kulichunguza. Kampuni iliyoshindwa kazi.

Katika hali ya kawaida, ilibidi maamuzi ya haraka yachukuliwe na taarifa ipatikane ili wananchi waondoe hisia mbovu. Wapi? Imechukua miezi ndio maamuzi yanatoka. Ni dhahiri mazingira haya yataifanya hata taarifa yake itiliwe shaka.

Maamuzi yenye maslahi ya taifa yanatakiwa yachukuliwe mapema ili kusafisha hisia mbovu. Wenzetu wanaosemwa kuwa na akili kuzidi sisi leo wameweza kushughulikia mambo yenye maslahi ya taifa na kuondoa umimi kwanza. Ni lazima tujitathimini na kujiuliza kama kweli tuko sawa na wengine.

Kwenye makala yangu ya juma lililopita, nilitoa hoja kwamba tunajipima kwa viongozi wetu.Katika hali ya kawaida kiongozi wa watu maskini ni lazima aishi maisha yanayofanana na watu wake; maisha ya kimaskini. Lakini kama kiongozi wa watu maskini anaishi kwenye utajiri unaopindukia, ni lazima kuna kasoro.

Magari zaidi ya 30 yenye thamani ya Shilingi milioni 60 kila mmoja, kupita katika vijiji vya watu maskini kwa kisingizio cha kukagua maendeleo, ni jambo la kuleta mashaka kama kweli hatujateleza mahali au kuzua wasiwasi juu ya ubora wa akili zetu.

Viongozi wetu wanapokwenda kuomba pesa kule nchi za nje, wanafikia na kuishi kwenye mahoteli ya kitalii. Kwa nini akili zetu zisitiliwe shaka? Kiongozi wa watu maskini, anayekwenda kuomba misaada ya watu maskini, anafikia hoteli ya kitalii!

Yamekuwepo malalamiko ya chini chini ambayo kwa namna fulani ni matusi, kwamba wale wanaotoa pesa wakija kuzifuatilia, wanasafiri kwa usafiri wa kawaida. Kama ni ndege wanapanda daraja la tatu, lakini viongozi wetu wanasafiri daraja la kwanza!

Ipo mifano mingi inayoonyesha dalili nyingi za kuwafanya wenzetu wawe na mashaka juu ya ubora wa akili zetu. Mheshimiwa Ndesamburo, juzi, bungeni, alitoa ushuhuda kwamba asilimia 98 ya watu walio na simu za viganjani wanazitumia kutongoza wanawake, kuzungumza umbea, kutuma ujumbe wa mapenzi na kupanga mipango ya ujambazi. Labda asilimia mbili ndio wanatumia simu kwa mipango ya biashara na maendeleo.

Hili ni jambo la kushangaza kwani Tanzania ni kati ya nchi zinazosifika Afrika kwa kuingiza kwa wingi simu za viganjani na makampuni ya simu hizi yanapata faida kupindukia.

Siku za karibuni Benki ya Dunia ilitoa taarifa ya mamilioni ya dola zilizotolewa barani Afrika kwa ajili ya kukuza kilimo lakini wanashangaa na kujiuliza; mbona mapinduzi ya kilimo kwa bara la Afrika hayajafanikiwa kama ilivyotokea Asia?

Najua vyombo hivi navyo vina unafiki wa kutosha kwa sababu wanatumia nchi masikini kujineemesha pia. Lakini cha kujiuliza mbona fedha za namna hiyo zimefanya mapinduzi sehemu nyingine? Kwa nini zisifanye mapinduzi Afrika? Kwa nini tukubali kutumiwa kama nguruwe wa majaribio na sisi tusifaidi kama nchi nyingine?

Tunapaswa kujitathmini hapa. Mara nyingi sana wanaharakati wanaopingana na misaada ya nje huwalaumu watoaji kwamba wanakuja na misaada yao kuja kuitumia huku kwetu wakijineemesha wenyewe. Mimi huwa nauliza kama umeona msaada hautafaidisha taifa kwa nini uukubali?

Kwa hivyo tunawalaumu pia wanaopokea misaada isiyo na tija. Lakini wanaopokea wanaangalia maslahi yao binafsi kwamba watafaidi wao na si taifa. Wenzetu wa Asia wanawarudishia wataalamu wa Benki ya Dunia na IMF fedha zao kama wakigundua hazitakuwa na manufaa, na ndio maana kuna ushahidi wa kitaaluma kwamba mikopo na misaada mingine imeweza kusaidia sana kuleta mapinduzi Asia. Sisi bado tunalia. Tujiulize tatizo lilipo.

Tutalaani wabaguzi hawa, tutashika mabango na kuandamana lakini kabla ya kwenda tujiulize sababu ya kukwama kwetu. Tusikimbilie kulaumu Wazungu kama chanzo cha matatizo yetu.

Kuna wale rafiki zangu wanaolaani ukoloni na ukoloni mamboleo. Malaysia na Ghana zilikuwa zote koloni la Uingereza na zilipata Uhuru mwaka mmoja (1957). Wamalaysia walikuwa wanakwenda Ghana kujifunza kilimo cha mawese. Leo hii Ghana inajifunza kila kitu toka Malaysia kikiwemo kilimo cha mawese!

Tanzania ni mika 46 ya Uhuru sasa. Tuache kuendelea kulia na kulalamikia ukoloni. Sisemi haukuleta madhara lakini tutalia mpaka lini? Tunachukua hatua gani za kuondoa hayo makovu? Au hatua zenyewe ni hizo za kuwaita tena wakoloni waje kuwekeza kwa kuwasamehe kodi?

Hawakatai kuja. Watakuja watatula halafu watatutukana. Hawasemi hadharani lakini wanasemea chinichini kwamba hawa Waafrika ni wajinga.

Wazungu wengi wanaobishana na kauli ya Watson si kwamba wanasikitika sana. Wanaonyesha usoni kwamba wamechukia lakini moyoni wanasema ni kweli hawa wana ujinga wao mkubwa. Wanatutetea ili waendelee kutuvuna. Hawataki tukae chini na kujitathmini tulipoenda mrama.

Nachukia sana kuitwa kiumbe dhaifu hasa kiakili. Nachukia kwa sababu naupenda Uafrika na weusi wangu. Nawapenda Waafrika wenzangu. Nachukia sana wanapoambiwa kwamba wana ubongo dhaifu. Lakini nahisi kuna mahali kama watu weusi tumeteleza.

Kuna ushaidi unaoonyesha kwamba tumefanya mambo ambayo akili zetu zinatakiwa zihojiwe. Kama mtu anaiba mabilioni ya fedha za umma kwenye nchi masikini na kuyaweka Ulaya au kuwekeza mahali popote, huku kukiwa na wananchi wanaokufa kwa kukosa dawa ya Malaria, basi, tuna ulazima wa kujiuliza tuliko na kasoro.

Kama viongozi wanawaibia wanachi wao waliowachagua kuwawakilisha bila aibu yoyote inabidi tuhoji akili zetu. Kama wananchi nao wanaridhika na hila za viongozi wao bila kuchukua hatua madhubuti, basi tuhoji akili zetu.

Kama kijenetiki tuna akili ndogo, basi, hatuna cha kufanya labda ufanyike utaratibu wa kutuunganisha kijenetiki na hao wenye akili zaidi. Kama akili ndogo zinatokana na kukataa kutumia uwezo tuliopewa basi tunaweza kujirekebisha.

Hata kama Watson ataomba radhi kama wale mawaziri wa Japan walivyofanya, atakuwa ameshapeleka ujumbe mzito wa watu weusi kujichunguza! Ujumbe huu ni mzito kwa taifa letu la Tanzania.

Kutoka gazeti la Raia Mwema.

Mjukuu wa Shaaban Robert Aendeleza Kiswahili London…

Wiki hii inayoanza leo Jumatatu 26.11.2007, hapa London, Dada Amina ataanza masomo rasmi kufundisha Kiswahili. Madarasa hayo yatakayokuwa ya bure halafu baadaye yaanze kuwa ya malipo kwa wananchi wa hapa Uingereza.

Amina Waziri.

Hadi juzi Jumamosi tunaelezwa wanafunzi ishirini tayari walishajisajili kwa uchu na mate. Madarasa haya yatafundishwa kila siku katika Kituo cha Waafrika kilichopo New Cross, kusini ya London. Mtanzania Amina Waziri ni mtu wa kujituma sana…

Toka utotoni maisha yake yamekuwa yakusafiri safiri, kuhama hama, kutembelea sehemu kadhaa nchini Tanzania na dunia. Ukizungumza naye ni mtu anayejieleza vizuri, anayejua anasema nini, mwanamawasiliano. Hii ni kwanza kutokana na kazi ya baba yake mzazi, Mzee Waziri Juma aliyekuwa Waziri na Balozi wetu nchi mbalimbali. Mama yake Amina alikuwa binti yake mwandishi maarufu wa Kiswahili, Shaaban Robert. Kwa hiyo da Amina ana damu ya mwanafasihi na mmoja wa viongozi wetu mahsusi.Alizaliwa Tanga, tarehe 14 Februari, 1960 na kuanza shule ya vidudu Mbeya, darasa la kwanza Kaloleni Arusha. Toka hapo ikaanza sasa safari ya kusoma shule kadhaa (Tanga, Tabora, Dar es Salaam) akiongozana na wazazi waliokuwa katika wadhifa wa kiserikali. Akasoma China, Sudan hadi alipoingia kidato cha kwanza Shule ya Kisutu, Dar es Salaam, mwaka 1973. Baada ya kusoma shule kadhaa za sekondari (Korogwe, Sudan Sisters mjini Kahrtoum) alimalizia kidato cha nne shule ya Ifakara mwaka 1978. Miaka kumi na tatu iliyofuata alifanya kazi ya mhudumu wa ndege (air hostess) shirika la Air Tanzania na kusafiri kila mahali Bongo na Afrika Mashariki. Aliishi pia Bujumbura, Burundi. Toka mwaka 1991 anaishi London, mzazi wa watoto tisa (walio hai watano) na wajukuu wawili. Keshafanya kazi za mhudumu wa mahoteli, dereva wa teksi, mwangalizi wa wazee na watoto na kufuzu diploma ya Theolojia na Nasaha (counselling) na kuchapa kitabu chake cha kwanza mwaka jana kiitwacho : “Oneness.” Kitabu hicho chenye picha ya marehemu binti yake Comfort (aliyefariki mwaka 2002) kinaelezea harakati za mwanamke wa Kiafrika kupambana na maisha na kuyamudu.Nilimhoji Amina karibuni baada ya moja ya safari zake nyingi kwenda nyumbani. Haya hapa mazungumzo yetu.

FM : Ulikuwa nyumbani karibuni. Je, ulikwenda kufanya nini?

Amina: Hususan na lengo la safari yangu ya nyumbani hivi karibuni ni mshawasha na mwamko wa kufanya kazi za Mungu, na pia kwenda kufanya utafiti nitaweza kufanya nini ili nitoe mchango wangu katika kuwasaidia wapendwa wananchi, na vile vile kwenda kuwaona ndugu wazazi na marafiki .

FM: Mwaka jana ulikwenda nyumbani pia. Tueleze tofauti ya uliyoyaona mwaka jana na mwaka huu.

Amina: Naam, mwaka jana mwezi wa Agosti nilienda kwa mara ya kwanza baada ya miaka 16 tangu nilipoondoka tarehe 13 Machi 1991, tofauti niliiyoiona hapo na safari hii ,ni kubwa. (kicheko) Mwaka huu nimeona kuna mwamko mpya wa kimawazo, nadharia, na pia kimaendeleo, labda pengine ni kwasababu wakati huu nilikuwa katikati ya mji, ambako niliweza kuonana na watu wa tabaka mbalimbali, wengi walikuwa na ari ya kimapinduzi, ya kimaendeleo, na wala hawakuwa na mcheche wa kutaka kutika nchini, zaidi walisisitiza ushirikiana kati ya waliopo nje ya nchi na wao ili kuleta sura mpya ya maendeleo.

FM: Kuna ugumu gani wa maisha kwa Wabongo kwa jumla?

Amina: Watanzania , kama , watu katika nchi yeyote changa bado wapo kwenye hali ya kuvuta hatamu, hali hii ni ngumu na ya utata, hasa wakijilinganisha na mataifa makubwa, hivyo bado sana , katika sera nyingi bado watu wana sita sita, hii ni hali ya kawaida kabisa katika hatua za maendeleo, bado watu wanashindwa kutoa mawazo yao bila woga, hii inasababisha masahihisho kushindwa kufanyika, na maendeleo kuzorota, laiti , wananchi wengepewa mwanya wa kidemokrasia , kutoa mawazo yao , bila kuvunja sheria wala heshima, nina hakika tungekuwa mbali. Kiuchumi, kiafya, kisiasa,kinadharia, kimawazo nk.

FM: Kuna urahisi gani wa maisha kwa jumla kwa Wabongo?

Amina: Watanzania , ni miongoni mwa mataifa machache ulimwenguni yenye sifa ya uadilifu na utulivu, sifa ambazo ni ngumu kuzikuta kwingi duniani. Kuna amani ya pekee, muda wote nilipokuwa nyimbani, sikusikia lugha chafu, sikusika mikimiki ya mwizi kukimbizwa, hata kwenye sehemu ya kuuza pombe sikuona maajabu yeyote, ya kushangaza, nidhamu ya vijana na watoto, ndio usiseme, ukweli ni kwamba Tanzania tunastahili hongera. Pia watu ni wakarimu na waaminifu na vyakula ni vingi na bei zake ni safi kabisa, nilishangazwa na ubora wa mbao na ujuzi wa maseremala , hasa magereza, na ujenzi wa nyumba bora na nzuri.

FM: Nini mustakbala wa maisha? Je, kuna matumaini gani?

Amina: Watanzania wakipewa sauti ya kusema wanataka nini wafanyiwe, kama nyumba bora, maji safi, umeme bila mikato, kazi za kudumu, mashule mengi ya fani mbalimbali, mahospitali na zahanati, barabara nzuri, sehemu za bustani wazi, maduka yenye bidhaa zetu wenyewe za ubora na bei nafuu, teknolojia mbalimbali,Tanzania itashinda na itakuwa taifa la mfano bora kama mengi duniani sababu tunao watu wenye sifa za kiutu na uaminifu na bidii ya kazi.

FM: Wewe unataka kufanya nini kusaidia nchi yetu na watu wetu?

Amina: Freddy, nataka kufanya kila kitu kuisaidia nchi yangu, na watu wangu, nipo katika harakati za kukusanya nguvu hapa na pale, nataraji kuanzisha vituo vya mafunzo hasa kwa wale ambao wamekumbwa na maafa ya maisha , kama, wajane, wafungwa, wazee, vilema, tayari nimeona kuna mashule mengi ya watu binafsi, lakini akina kabwela hawana namna ya kuzigusa, na wafungwa ndio wannanisumbua sana roho yangu, maana wengi wakitoka jela ndio hivyo tena, hawana chao; washaathirika, kila wanapokwenda hawana msaada wowote,majina yao tayari yameshaingia dosari, na wajane pia, wana tabu kubwa, hivyo nataka kufanya kitu kwa wasiojiweza..

FM: Suala la wanawake. Unaonaje maendeleo yao ukilinganisha enzi zile ulipokuwa ukiishi Bongo na sasa?

Amina: Kina mama Bongo wanastahili sifa na hongera, kote vijijini na mijini, wao ndio wameshika hatamu, wengine wachuuzi, wengine wafanya kazi, na hata wale kina mama wanaopiga uasharati ,ili wapate riziki, pia wanaangalia familia zao vizuri sana, naomba usinielewe vibaya, si kama naunga mkono zoezi hilo, la hasha, lakini, kama ukiwakuta makwao , kamwe huwezi kujua kama wana tabia hii, maana wana beba majukumu ya familia yote. Enzi zetu bongo, wanawake walikuwa na woga na waliachia waume wawafanyie mambo mengi. Lakini sasa hata kina mama vijijini wanataka kwenda shule kupata ujuzi.

FM: Umeanza kufundisha Kiswahili hapa London. Nani wanafunzi wako na unaionaje kazi hiyo?

Amina: Wanafunzi wangu wengi ni kutoka visiwa vya Karibi: Jamaika, Trinadad- Tobago, St Lucia, St Vincent, Guyana, Kyuba, Grenada, St Kitts, na hata Waingereza ambao wanataka kuja kufanya kazi Tanzania. Pia baadhi ya Waafrika ambao wanapenda kujua lugha yetu.Naipenda sana kazi hii maana inanipa amani na kuona kwamba ninaweza kutoa mchango wangu kwa wengi , hasa , Wakaribi ambao wana kiu cha kutaka kujua lugha ya asili ya mtu Mweusi. Suala la utumwa limewatia pengo, wanaona wameibiwa silaha ya lugha, kwani lugha ni amana kubwa.

FM:Je, Kiswahili kinapendwa na watu wa aina gani ughaibuni, hususan Uingereza?

Amina: Cha kufurahisha sana ni jinsi ambavyo lugha yetu inapendwa sana, hasa na Waingereza, labda kwa vile hawa ni watu ambao kwao kitu chochote kina thamani kubwa, na kama nilivyosema awali wenzetu Wakaribi, wako radhi kulipa chochote wajue Kiswahili, na hasa jamii hii ya watoto waliozaliwa huku, ambao hawajui lugha nyingine zaidi ya Kiingereza, wanapenda sana nao wajidai eti tu waaongee Kiswahili , mradi tu wawakoge wenzao.

FM:Je, unaonaje maendeleo ya lugha ya Kiswahili hii leo nyumbani?

Amina: Nilichogundua , ni kwamba lugha yetu imechuja, imejaa maneno duni, wala siyo katika msamiati wa fasihi, hata kule kwetu Tanga , nilishangaa kuwaona watu wamekitia Kiswahili maji, sio tena kile Kiswahili cha awali, enzi za mababu na mabibi zetu.

FM: Vijana kwa wazee wengi wanaanza kutumia lugha ya mseto “usio na mguu wala kichwa.” Kuna desturi hii leo ya kuchanganya sana Kiswahili na Kiingereza. Lugha haileweki kama ni Kiswahili au Kiingereza. Vijana hawajui Kiingereza wala Kiingereza. Je, nini maoni yako?

Amina:Twaweza kupiga msasa, lakini tuzingatie kuwa ligha za miji mkikubwa huwa ni za barabarani, hata Kiingereza, Kiarabu, Kihindi nk, lakini, ile lugha ya mashuleni, vyuoni, serekalini, isitiwe dosari, huo ni urithi wetu, lazima tuuhifadhi kwa udi na uvumba.

FM:Unatukuza sana dini ya Kikristo. Nini nafasi yake kwa watu wetu duniani?

Amina: Kweli namtukuza sana Yesu Kristo, na kweli nampenda mno maana, aliuacha mbiguni ufalme wake uliotukuka , akaja duniani kudhalilika kwa kila mtu, ili afungue lango kuu la pepo, alicholeta Yesu. Hakuna mwingine yeyote awezaye kuleta ni kusameheana au msahamaha. Hakuna, katu katu, binadamu awezaye kusamehe, ila yeye tu, wote tuna magutu, japo tunadai tumesamehe na tumesahau, lakini ukiguswa tu yote yanarudi kama wimbi, na kisasi juu, ndio maana namfuata Yesu, ili nami niweze kusamehe, nimwangalie yeye tu, maana yeye ndie njia, ukweli na maisha ya milele.

FM:Kumekuwa na kukosoa Waafrika kuwa tumeacha dini zetu na kuiga dini za kigeni (Uislamu na Ukristo). Wasanii kama Fela Kuti wa Naijeria, walidai Waafrika tunajidunisha kwa kuabudu dini zilizoletwa na watu wa tamaduni nyingine. Tunajidunisha na kukopi nje. Nini maoni yako.

Amina: Kumkana Yesu ni kujikana wenyewe, nani aliezaliwa bila najisi isipokuwa Yesu? Na nani aliekufa akafufuka ila Yesu? Tena kabla ya kufufuka aliekwenda jehanamu kuhubiri Injili, ili kutoa nafasi nyingine, daima!

Kutoka: Freddy Macha´s Kitoto wordpress dot com
Binti wa Karume sasa auanika mtandao wa rushwa Kisutu.

*Adai haki inauzwa, wanyonge wanaonewa
*Akiri anajua ni msalaba mzito, lakini ataubeba
*Asema hana tatizo na Mahakimu, bali rushwa
*Asema mteja wake alitishiwa kwa kesi ya Babu Seya

Na Hassan Abbas

SIKU chache baada ya kutokea hali ya sintofahamu kati yake na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu, Bibi Addy Lyamuya, Wakili wa Kujitegemea ambaye pia ni binti wa Rais Amani Karume wa Zanzibar jana amefanya mahojiano maalum na gazeti hili na kusisitiza kuwa hana ugomvi na hakimu yeyote bali anapigania haki za wanyonge, wanaolazimika kununua haki kwenye mahakama hiyo.
Fatuma Karume.

Fatuma katika mahojiano hayo, amewabainishia Watanzania kuwa yeye kama wakili aliyefundishwa vyema maadili ya kazi yake na pia anayeenzi wosia wa babu yake, hayati Mzee Abeid Amani Karume, siku zote amefundishwa kupigania haki inapotaka kuchafuliwa na ubatili.

"Nilipoanza kulishughulikia suala hili, nilijua utakuwa msalaba mkubwa kwangu, lakini kama babu yangu alivyokuwa jasiri kiasi cha kuwaongoza Wazanzibar kupata haki zao, nami nimejifunza kutonyamazia uovu," alisema wakili huyo ambaye jana aliuweka hadharani mtandao wa rushwa ulioenea katika mfumo wa mahakama hasa kwa baadhi ya Mahakimu wa Mahakama ya Kisutu, Dar es Salaam na kuitaka jamii ilijadili tatizo hilo.

Chanzo cha yote

Anasema yeye kimsingi anaifanya kazi ya uwakili ikiwa ni sehemu ya wito wake binafsi aliokua nao tangu mdogo wa kutotaka kuona wanyonmge wanaonewa.

"Nilipoanza kazi hii nilikuwa natetea sana wanyonge hasa katika hizi kesi za madai na mambo ya ndoa, lakini nikaziacha na kujihusisha zaidi na masuala mengine," alianza kusema.

Akaongeza kuwa hata hivyo kutokana na kuwa na moyo wa huruma akajikuta akishindwa kukwepa kuwatetea wanyonge hao kila walipomfuata awasaidie.

"Hata hii kesi ilipokuja, kimsingi mteja wantu ni mtu wa kawaida, lakini nikajitoa kama sehemu ya wito wangu nimsaidie apate haki yake ya kuonana na mtoto wake mpendwa," aliongeza.

Wakili Fatuma akieleza msingi wa kesi hiyo, aliliambia gazeti hili kuwa inahusu baba na mama waliotengana ambapo mume ambaye ndiye mteja wake, aliiomba mahakama awe na fursa ya walau kuonana na mwanae kwa siku chache katika wiki.

"Nilimtetea katika kesi hiyo na Agosti 2, mwaka huu tukashinda. Hukumu ilimpa haki mteja wangu ya kuwa na mwanawe kuanzia kila Ijumaa kisha Jumapili awe anamrudisha kwa mama yake," alifafanua.

'Kansa' yaanza

Wakili Fatuma akiwa anaonekana mwenye huzuni, alisema wakati mteja wake akifuatilia hukumu hiyo ndipo alipoanza kuombwa rushwa ili hati ya hukumu yake isainiwe na akalazimika kutoa.

Anasema katika tukio la pili, baada ya kupewa hukumu yeye akiwa wakili alibaini kuwa mteja wake hakuwa amepewa hati ya amri ya mahakama na akamshauri aende tena Mahakama ya Kisutu kuiomba ili aweze sasa kuanza kupata haki yake ya kuwa na mwanawe.

"Alipofika kwa Hakimu akaambiwa alichotoa siku ya kwanza kilikuwa hakitoshi. Akajipapasa na kutoa alichokuwa nacho lakini bado akaambiwa hakitoshi.

"Hii ni aibu kwa taifa hili kwa msimamizi wa haki kufikia hatua anauza haki namna hii," alisema wakili Fatuma na kuongeza: "Yule mteja wangu akawa ameishiowa hela hivyo akamwomba rafiki yake aliyekuwa akisubiri nje ya mahakama amsaidie."

Akaongeza kuwa jamaa huyo alilazimika kwenda benki ya Barclays na kutoa dola 100 ambazo walimkabidhi Hakimu huyo.

"Huyu jamaa aliyekwenda kutoa fedha zake benki ili amsaidie mteja wangu, yupo na yuko tayari kutoa ushahidi," alisema.

Wakili Karume akieleza jinsi Mahakamu walivyofikia hatua ya kuwa na mtandao wa aina yake wa kudai rushwa na ambao unawakera wananchi wengi, anasema baadaye kesi hiyo ilichukua taswira nyingine tena kufuatia mawakili wa upande wa mke kuwasilisha maombi ya kutaka kesi hiyo ifanyiwe marejeo kwa kuangaliwa upya.

Anasema Hakimu huyo (jina tunalo), alimpigia tena simu mteja wake na kumtaka waonane kwenye hoteli ya Sea Cliff.

"Mteja wangu alisita kwenda kwa sababu alikuwa akijua huko angeendelea kuombwa hela zaidi. Hakimu yule akatuma hata sms (ujumbe mfupi wa maandishi) ambao tunao kama ushahidi akimsisitiza mteja wangu waonane," aliongeza.

Sea Cliff-Agosti 26, 2007

Wakili Fatuma anasema kuwa kabla ya kwenda kuonana na Hakimu huyo kwenye Hoteli ya Sea Cliff iliyoko pembezoni mwa Bahari ya Hindi jijini Dar es Salaam, mteja wake alimpigia simu na kueleza nia ya kutaka kumrekodi Hakimu huyo.

"Aliponieleza nia yake nikamwambia sawa, fanya hivyo kwa sababu hali ile iliendelea kumchosha mteja wangu," alisema wakili Fatuma.

Kitisho cha Babu Seya

Anasema wakiwa hotelini hapo bila Hakimu huyo kufahamu kuwa alikuwa akirekodiwa, alianza kwa kumrubuni mteja wa wakili Fatuma kwa kumshangaa anavyowalipa hela kwa watu wengine (mawakili) ambao alidai hawezi kumsaidia.

Katika kanda hiyo yenye urefu wa takribani dakika 12, Hakimu huyo pia katika mazingira mengine yenye utata, alisikika akimshawishi jamaa huyo aachane na suala la kutaka akae na mtoto wake kwani kuna athari siku atakazokuwa akikaa naye, anaweza kusingiziwa mambo kama yaliyomkuta Babu Seya.

"Hakimu yule anasikika mbali ya kudai hela akimtishia pia mteja wangu kuwa yanaweza kumkuta ya Babu Seya kama ataendelea kung'ang'ania kukaa na yule mtoto," alisema kwa uchungu wakili Fatma.

Hoi kwa wiki moja

Akizungumzia jinsi alivyostushwa na yaliyokuwa yakiendelea mara baada ya kupelekewa rekodi ile, wakili Fatuma ameliambia gazeti hili kuwa alipatwa na mshituko mkubwa.

" Nilipata 'broken heart' (jakamoyo), sijui unaweza kueleza vipi katika Kiswahili, lakini niliumwa sana na niliumia kiasi cha kushindwa hata kwenda ofisini kwa muda wa wiki moja.

"Nikajiuliza nafasi yangu ni ipi katika kusaidia suala hili?Nilijua pia kuwa hilo linaweza kunigharimu na ni msalaba mkubwa kwangu?Nikafikiria niliache,lakini nikajiuliza ni wanyonge wangapi wanalazimika kuinunua haki na nani ataibadili hali hii?

"Mimi nimefundishwa vyema sheria kule Uingereza, nayajua maadili yangu kama mwanasheria, nina moyo wa uchungu kama mwanajamii mwingine na pia hii kazi siifanyi kwa shida, ningeweza kukaa nyumbani, mume wangu akanilisha, lakini naifanya kazi hii kwa wito.

"Nilipoisikiliza ile sauti ya yule Hakimu anavyoomba rushwa kwa kujiamini, nilijua pia moyoni mwangu kuwa huu ni mtihani katika maisha yangu na haya yaliyotokea niliyawaza kabla," alisema.

Anasema rafiki yake mmoja ambaye kwa sasa ni wakili nchini Uingereza aliyekuwa hapa nchini ndiye aliyempa moyo kulisimamia kidete suala hilo na kutolinyamazia.

Kazi yaanza

Wakili Fatuma anasema baada ya kuamua kulisimamua suala hilo, alimpigia simu Hakimu husika na kumuuliza ni kwa nini alikuwa anachukua rushwa kwa mteja wake.

"Nilipoongea naye kwa simu awali tuliongea vizuri lakini nilipomgusia suala la kwa nini anachukua rushwa kutoka kwa mteja wangu na kumueleza ushahidi nilionao, alijifanya yeye si Hakimu wa Kisutu na akakata simu.

"Mteja wangu aliwasilisha malalamiko yake TAKUKURU. Nami sikukata tamaa nililifikisha suala lile tena kwa kumwekea rekodi ile aisikilize Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Kisutu, Bw. Sivangilwa Mwangesi lakini nikashangaa Hakimu yule aliendelea kusikiliza kesi yangu na nyingine za wananchi wakati uadilifu wake ulishakuwa shakani.

"Mimi tulipokutana naye Hakimu huyo (anayetuhumiwa) mahakamani nikamwomba ajitoe katika kesi yangu kwa sababu tayari uadilifu wake ulikuwa shakani na kimaadili hakupaswa kuendelea kusikiliza kesi za wananchi. Alisita lakini nikasimamia hoja yangu na hatimaye akajitoa," alisema.

Mtandao wa njama

Wakili Karume anawahakikishia watanzania kuwa hakuwa na ugomvi na Hakimu Addy Lyamuya wala Hakimu mwingine wa mahakama hiyo, lakini anasema tangu kesi hiyo ilipohamishwa kutoka Hakimu mmoja hadi mwingine alikuwa akihisi maofisa hao wa mahakama kama vile wamechukizwa na vitendo vyake vya kufuatilia mambo kwa kina.

"Sijui nini kilitokea. Sikuwahi kugombana na Mahakimu awali kwa sababu uwakili sijaanza mwaka huu wala mwaka jana. Nahisi baada ya kuona ninasimamia haki ipasavyo, walikuwa na hali fulani tofauti dhidi ya kesi yangu," alisema.

'Tume' ya Kisutu
Akizungumzia ripoti iliyotolewa juzi na Mahakama ya Kisutu kuhusu sintofahamu iliyotokea, wakili Fatuma anashangaa kuona jinsi misingi ya asili ya haki yake ya kusikilizwa ilivyokiukwa.

"Sikuitwa kujieleza na hili linashangaza, kwani hata maelezo yangu ya maandishi niliyawasilisha jana (juzi) mchana wakati ambapo kumbe tayari Hakimu Mwangesi alikuwa akiongea na waandishi akitoa ripoti ya uchunguzi wake,sidhani hata kama alisoma maelezo yangu wala kuwaita mashahidi wangu.

Juzi Hakimu Mwangesi alisema hajapokea tuhuma za rushwa dhidi ya mmoja wa mahakimu wake na jana alipoulizwa kwa njia ya simu kuhusu suala la kutomsikilia wakili Fatuma Karume katika uchunguzi wake, alikiri kutofanya hivyo lakini akasema alitumia maelezo ya awali ya malalamiko ya wakili huyo.

Akizungumzia hilo Fatuma ansema: "Misingi ya haki za asili inaeleza bayana kuwa lazima uitwe na kujitetea dhidi ya tuhuma zako. Hili halikufanyika lakini pia nashangaa kwa nini hata nilipotoa tuhuma za rushwa, haukufanyika uchunguzi na wala sikuitwa kutoa ushahidi zaidi."

Anasema kwa uzoefu wake akiwa wakili, sehemu kubwa ya haki za wananchi inauzwa na kuitaka jamii isimame kidete kuibua maovu zaidi yaliyoko katika idara ya mahakama kwa sababu kama haki itauzwa hakuna thamani tena ya maisha ya mwanadamu.

"Wazee wetu, Mwalimu Nyerere na babu yangu, Mzee Abeid Karume walituasa sana kuhusu rushwa. Ni heri mtu ale rushwa sehemu nyingine lakini si katika sehemu ya utoaji wa haki kama mahakamani.

"Rushwa ikishamiri katika mahakama kuna haja gani ya watu kusomea taaluma kama sheria, Ni bora kesi zikasikilizwe Jangwani ambako watu watakuwa wakiweka dau kwa kutumia fedha ili wenye nazo washinde.

"Lakini kama kuna taaluma na misingi ya sheria inayopaswa kufuatwa, basi wananchi na vyombo husika viamke. Kuna mtandao mbaya sana wa rushwa katika mahakama hasa kwa baadhi ya Mahakimu wa Kisutu," alisisitiza.

Tuhuma za wakili Fatuma Karume kuhusu rushwa katika mahakama, zimekuja wakati pia ikiwa ni miaka takribani 11 sasa tangu ripoti mashuhuri ya Jaji Warioba, ilipobainisha kuwepo kwa vitendo viongi vya rushwa katika sehemu mbalimbali ikiwemo Idara ya Mahakama.

Wananchi mbalimbali pia wamekuwa wakilalamikia vitendo vya kukithiri kwa rushwa katika mahakama mbalimbali hapa nchini.

Katika mahojiano yake na gazeti hili hivi karibuni, Jaji Warioba alionesha kutilia shaka kama muongo mmoja sasa, ripoti yake imefanyiwa kazi katika kuwabana wala rushwa.

Sunday, November 25, 2007


The British Prime Minister`s wife, Sarah Brown (1st Left), and First Lady Salma Kikwete tour the Muhimbili National Hospital in Dar es Salaam. They were taken around by the Director General of the country`s main referral hospital, Prof Leonard Lema (R).

Kutoka: http://haki-hakingowi.blogspot.com/


Wakongo nao je?

NIMON TIKA LALA - "Pardon Cheri"Burudani ya Jumapili - Mziki wa Mapouka

Mziki huu wa Mapouka asili yake ni kutoka Ivory Coast. Uchezaji wake ni kama ngoma nyingi za kiasili za Kiafrika. Tukifuatilia mada ya jana Jumamosi 24.11.2007 yenye kichwa cha habari "Kufuru tupu" angalieni wenyewe miziki na ngoma zetu za asili jinsi zilivyo na zinavyochanganya watu tuliosahau kuwa kucheza kinamna namna ni asili ya Waafrika. Zaidi kuhusu Mapouka toka wikipedia.
WASIFU WA JUMAPILI

MAJUKUMU MA-3 MUHIMU ULIYONAYO KWA MPENZI WAKO!

Tunakutana tena mpenzi msomaji wangu kupitia safu hii nikiamini kwamba umzima kabisa na unaendelea vyema na majukumu yako ya kila siku. Mimi namshukuru Mungu kwani afya yangu ni bomba, kama kawaida naendelea kukuletea 'majamboz' yanayogusa maisha yetu ya kimapenzi.

Swali ambalo nalazimika kulifafanua zaidi ni lile la wale wenye hisia kwamba, wapenzi wao wanawasiliti.....


Hakika walio wengi kila wanapokuwa mbali na wapenzi wao hujihisi kusalitiwa, lakini sasa unachotakiwa kujiuliza ni kwamba, unaweza kumchunga mpenzi wako asiwe na uhusiano usiofaa na mtu mwingine zaidi yako kama akiamua? Hakika ni kitu kisichowezekana! Nasema haiwezekani kwa sababu kama mpenzi wako hajatulia, hajatulia tu na anaweza kila mara akawa anakueleza kwamba hawezi kukuumiza lakini huyo huyo siku moja akaja kukufanyia mambo ya ajabu.

Sasa ufanyeje basi ili uweze kuishi maisha ya amani? Kinachotakiwa kwa sisi tulio katika mapenzi ni kuwaamini wapenzi wetu kwa asilimia zote wala tusiwe na shaka pale wanapokuwa mbali na sisi.

Tuamini yale wanayotuambia na tusipende kuwafuatilia sana wapenzi wetu katika maisha yao labda itokee umepata tetesi kuwa laazizi wako anakuzunguka, hapo sasa fanya uchunguzi na muwekee mitego ili kumnasa.

Baada ya kugusia kidogo mada hiyo ya wiki iliyopita sasa nirudi katika mada yangu ya wiki hii. Nazungumzia kitu ambacho nimegundua watu wengi walio katika mapenzi hawakitambui.

Hiki si kingine bali ni majukumu uliyo nayo wewe ambaye umeamua kuingia katika uhusiano wa kimapenzi na mtu uliyempenda kwa dhati kabisa. Ukishindwa kuyatimiza majukumu hayo hesabu tu kwamba huwezi kudumu katika uhusiano kwani ni lazima mpenzi wako atakutosa.

Tufahamu tu kwamba, majukumu katika uhusiano wa kimapenzi yapo mengi lakini leo nitazungumzia matatu makubwa ambayo kila aliye katika mapenzi anatakiwa kuyatekeleza ipasavyo.

Kumridhisha kimapenzi:
Lengo la kila mtu kuanzisha uhusiano wa kimapenzi na mtu fulani ni kupata mapenzi ya kweli na mapenzi ya kweli hayo hayawezi kupatikana kama hutamridhisha mpenzi wako ipasavyo.

Ninaposema hivyo baadhi yenu hukimbilia moja kwa moja kwenye mambo ya sita kwa sita. Sawa hapo ndipo kwenye mzizi wa kipengele hiki. Kimsingi utakuwa ukijiweka katika mazingira magumu kama utashindwa kumpatiliza mpenzi wako katika mambo flani.

Unachotakiwa kufanya ni kuwa mtundu na mbinifu wa vitu ambavyo ukimuonjesha mpenzio hatafikiria kukuacha. Tatizo walio nalo wengi ni kutokuwa tayari kubadilika kwa kujifunza. Nimekuwa nikiandika mara kwa mara mambo ambayo unaweza kufanya ya kamdatisha mpenzi wako, lakini wengine bado wanakubali kuuacha uhusiano wao unadorora bila kuchukua hatua zozote.

Kumhudumia kwa hali na mali:
Kwa wapenzi walioshibana kisawasawa kusaidiana katika mambo flani flani ni jambo la kawaida. Tukisema huduma tunajumuisha vitu vingi na si kwa pande moja tu kama ilivyozoeleka kwamba mwanaume ndiye mwenye jukumu la kumhudumia mpenzi wake. Wanaofahamu hivyo watakuwa wanakosea kwani huduma hutolewa pande zote mbili japo zinakuwa katika viwango tofauti.

Niwakumbushe kuwa, tunaposema kumhudumia mpenzi wako kwa hali na mali ni kuhakikisha unamfanyia kila jambo ambalo ni muhimu katika maisha yake. Mfano hakikisha anakula vuzuri, anavaa smati, kumpeleka hospitali pale anapokuwa anaumwa, akiwa na shida msaidie. Kwa kufanya jambo hili hakika wapenzi mtakuwa mmehudumiana na mwisho wa siku kuliweka penzi lenu katika hali nzuri.

Usiishie hapo akiwa na shida ya pesa na akaomba msaidie, fanya kila uwezalo kuhakikisha unampatia. Kwa kufanya hivyo itadhihirisha kwamba unamdhamini na kumjali na hayo ndio mapenzi sasa.

Kumliwaza asipokuwa na raha:
Tulio wengi wapenzi wetu wanafanya kazi na wakati mwingine unaweza kumuona mpenzi wako amerudi kutoka kazini akiwa hana raha, hakika ni jukumu lako kuhakikisha unamfurahisha na kumuuliza ni kitu gani kilichomuweka katika hali ile.

Kama mpenzi wako ana upendo na wewe atakueleza sababu ya yeye kuwa katika hali hiyo na wewe kujua jinsi gani unaweza kumrudisha katika hali yake ya kawaida.

Lakini ikumbuke kwamba, hawezi kukwambia iwapo wewe utachukulia poa pale atakaporudi akiwa katika hali tofauti na siku zote. Mwanamke au mwanaume anayeweza kumpa raha mwenzake ni yule aliyechangamka na mcheshi hasa anapomuona mpenzi wake akiwa hayupo katika 'mudi'.

Sasa basi nawashauri wapendanao kuona umuhimu wa kuliwazana. Mnapokuwa katika wakati mgumu kimaisha mpe maneno ya faraja kama vile "pole na kazi mpenzi wangu mbona huna raha? Muulize ni nani kamkosea, wakati huo si kwa kumkaripia, tumia lugha laini ili hata kama alitaka kukuficha kilichomkasirisha akwambie.

Ni hayo tu kwa leo, tuonane tena wiki ijayo kwa makala nyingine ila kama una ushauri, maoni kuhusiana na jambo lolote la maisha ya kimapenzi.

Wasiliana nami kupitia namba 0784-600047 au
barua pepe: zekaima@yahoo com

Kutoka GlobalPublishers TZ


Tovuti ya JWTZ Yazinduliwa...

Kwa mara ya kwanza, jeshi la wananchi la Tanzania(JWTZ) limezindua tovuti yake yenye lengo la kuongeza Ushirikiano kati yao na wananchi. Tovuti hiyo ni www.tpdf.go.tz iliyoznduliwa rasmi jana jijini Dar es Salaam na Mnadhimu mkuu wa jeshi hilo,Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo pichani, kwenye bwalo la maofisa wa jeshi hilo Upanga, Dar es salaam.

Luteni Jenerali Abdulrahaman Shimbo alisema lengo la tovuti hiyo ni ukuaji wa sayansi na teknolojia hali inayofanya dunia kuwa kijiji kutokana na ukweli kwamba sekta ya mawasilianano kupanuka, '' JWTZ lliona si vyema kuendelea kufunga funga mambo yetu na kuwa wapweke na tunaamini tovuti yetu ni endelevu, tunawaomba wananchi kutembelea tovuti hii na kutoa maoni yao kuhusu utendaji wetu na kutushauri. tupo tyari kuyapokea na kuyafanyia kazi yote mtajayotushauri kwa lengo la kuboresha jeshi jeshi,'' alisema Luteni Jenerali Shimbo.

Unaweza kupata habari nyingi juu ya jeshi letu la JWTZ kwa kutembelea WWW.TPDF.GO.TZ

Kutoka: http://haki-hakingowi.blogspot.com


Kamati ya Madini yaanza kumeguka


*Mjumbe ajiondoa ni iliyoundwa na Kikwete
*Aitupia lawama CHADEMA kwa maneno maneno

Na Mwandishi Wetu

MMOJA wa wajumbe 12 wa Kamati ya Kupitia Upya Mikataba ya Madini ametangaza kujitoa.

Akizungumza na gazeti hili Dar es Salaam jana, mjumbe huyo Bw. Peter Machunde, kutoka Soko la Hisa la Dar es Salaam (DSE), alisema tayari amewasilisha barua yake kwa Rais.

Bw. Machunde alisema alifikia uamuzi huo kwa masikitiko makubwa na moyo mzito na kuomba ridhaa ya Rais amkubalie ingawa alimteua kwa heshima kubwa kuwa mmoja wa wajumbe.

Alisema uamuzi wake huo umetokana na kusikia maoni na wasiwasi wa baadhi ya watu, ambao alisema walionesha shaka na au kutoridhishwa na uteuzi wake na hivyo kumfanya atafakari kwa kina, kama kuwapo kwake katika Kamati kusingeipunguzia uwezo na uhalali wake miongoni mwa wanajamii.

Bw. Machunde alisema kilichomsikitisha sana ni maoni na wasiwasi wa baadhi ya watu wakishabikiwa na CHADEMA, waliopinga ushiriki wake kwenye Kamati.

"Binafsi nisingependa kuona kuwapo kwangu ndani ya Kamati kunawapa watu hao na chama chao kisingizio cha kumzuia mwanachama mwenzao ashiriki," alisema akimaanisha Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Bw. Zitto Kabwe.

Alisema hata hivyo kimsingi, Kamati ya Rais ilipokewa vizuri na Watanzania walio wengi kwa kuwa kuundwa kwake kulizingatia maslahi ya Taifa na ni Kamati iliyojumuisha watu wenye uwezo mkubwa na wanaotoa uwakilishi mpana wa jamii.


"Ni kwa sababu hii nimesikitishwa sana na ninashindwa kuelewa, pale baadhi ya viongozi wa CHADEMA wanapoingiza ajenda za kisiasa na kuhusisha chama chao katika suala zito na muhimu kwa maslahi ya nchi yetu.

"Huu ni upungufu kwa chama ambacho kimetumnia suala hilo kwa muda sasa hapa nchini, kuelezea upungufu wa sera na sheria na iweje sasa Rais anapounda Tume kwa maslahi ya Taifa, wao tena ndio wawe kipingamizi cha suala hilo," alisema.

Akizungumza kwa masikitiko, Bw. Machunde alielezea kusikitishwa kwake na mwelekeo wa mtizamo wa baadhi ya Watanzania kushutumiana na kutoaminiana na kujenga mazingira ya wao kujionesha kwenye jamii kwamba wana uchungu na nchi hii, ikiwa ni pamoja na raslimali zake, kuliko wengine.

"Ni imani yangu, kwamba wote tunaipenda nchi yetu kwa kiwango kinacholingana...nimeumizwa na kufadhaishwa sana na dhana inayojengwa na kuenezwa na viongozi wa CHADEMA, kwamba katika ushiriki wangu kama mjumbe wa Kamati hii, nisingeweka maslahi ya nchi yetu mbele.

"Hakuna tusi kubwa kama kudhaniwa kwamba unaweza kuisaliti nchi yako na kuitambua heshima na imani uliyopewa na Rais," alisema na kuwafananisha CHADEMA na genge la wababaishaji.

Alieleza kusikitishwa kwake na kuwapo hila za makusudi za kutaka kuidhoofisha Kamati hiyo kimamlaka, kwa kutumia mbinu chafu za kutumia majina ya watu kukidhi matakwa yao kisiasa.

Alisema huko ni kutojiamini na kutoamini mtu mwingine, licha ya kuwa wana mwakilishi wao Katika Kamati na tena ni kiongozi wa ngazi za juu kabisa.

Bw. Machunde ni mtaalamu wa masuala ya fedha, uwekezaji miradi na masoko ya mitaji mwenye Shahada ya Juu ya Uhasibu (CPA) na ambaye amekuwa mjumbe wa Bodi ya Taifa ya Uhasibu (NBAA) kwa miaka sita mfululizo.

Alimalizia akisema yeye si mwanasiasa na wala hana jukwaa la kisiasa, la kuelezea na kutetea rekodi yake ya mapenzi, uzalendo na utumishi kwa nchi yake.

"Rais aliponiteua kuingia Kamati hii, niliamini kwamba Kamati ina jukumu kubwa na muhimu kuliko sifa na heshima ya mtu mmoja au chama chochote cha siasa na bado nitaendelea kuamini hivyo, hata nikiwa nje ya Kamati," alisema.

Wajumbe waliosalia kwenye Kamati hiyo ni Mwenyekiti wake, Mwanasheria Mkuu wa Serikali mstaafu, Jaji Mark Bomani, Bw. Zitto, Mbunge wa Bariadi Mashariki, Bw. John Cheyo na Mbunge wa Kyela, Dkt. Harrison Mwakyembe.

Wengine ni Mbunge wa Msalala, Bw. Ezekiel Maige, Bw. David Tarimo wa Kampuni ya PriceWater Coopers na Bibi Maria Kejo ambaye ni Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa katika Wizara ya Katiba na Sheria.

Wajumbe wengine ni Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Bibi Salome Makange, Kamishina wa Sera wa Wizara ya Fedha, Bw. Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi katika Wizara ya Ardhi, Bw. Edward Kihundwa na Mbunge wa zamani wa Ilala, Bw. Iddi Simba.

Saturday, November 24, 2007

Kwenye habari za hapo chini "Utamaduni wetu" hapo chini tunaoneshwa utamaduni wa Watanzania kwenye mavazi. Wenzetu Wanaijeria, wanathamini sana sehemu hiyo ya utamaduni wao ya mavazi. Ukienda kwenye hafla, na tafrija zao, mavazi hayo ni mtindo mmoja!!!

Inapohusu utamaduni wa kucheza ngoma na dansi:

Ngoma nyingi za baadhi ya makabila ya Tanzania, zina miondoko ya kinamna hiyo. Ngoma za makabila mengi ya kusini na ya pwani, miondoko kama inavyoonyesha hapo chini ni ya kawaida. Ngoma kama Sindimba, Sikinde, Msondo na kadhalika. Jinsi gani miondoko hii inavyochukuliwa na tamaduni za kizazi kipya ndio suala kubwa hapa. Kufuru inayozungumziwa hapa ni jinsi gani inavyochezwa na wapi inaonyeshwa kwenye hiki kizazi kipya! Habari hizo hapo chini kutoka: Global Publishers Tanzania.


Na Richard Bukos
Shabiki mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, katikati ya wiki iliyopita alifanya kufuru tupu katika ukumbi wa DDC Kariakoo, jijini Dar es Salaam baada ya kunengua kwa staili za ajabu na kuwaacha hoi watu waliomshuhudia....

Tukio hilo ambalo lilishuhudiwa na mwandishi wetu, lilitokea usiku wa Jumanne iliyopita wakati kundi la Jahazi Modern Taarabu lilipokuwa likitumbuiza.

Ilikuwa kama mchezo wa kuigiza kwani baada ya muziki kukolea, dada huyo aliyekuwa 'ameunasa' mtungi vilivyo alinyanyuka alipokuwa amekaa na kupanda jukwaani kwa kasi, kisha kuanza kukata mauno kwa ustadi mkubwa na kuwafanya wapenzi wa kundi hilo kuduwaa.

"Huyu dada ni kiboko, anafaa kuwa mnenguaji wa bendi kubwa hapa nchini," alisema shabiki mmoja wa kikundi hicho aliyeonekana kunogewa na viuno vya dada huyo.

Hata hivyo, baada ya kumaliza kufanya mambo yake jukwaani dada huyo alijikuta akijuta, baada vijana wa kihuni kumvamia na kumtaka kuondoka naye kusikojulikana.

Kama si juhudi za mabaunsa wa kundi hilo, wakishirikiana na wale wa ukumbi huo, dada huyo angechukuliwa na vijana hao na kufanyiwa kitu mbaya.


Baadhi ya wanamitindo wa kibongo wakionesha mitindo ya mavazi mbalimbali inayowafaa wana wa kiafrika. Lakini kikubwa kinachonishangaza wabunifu wa mavazi wanajitahidi sana kubuni mavazi mbalimbali ambayo mtu yeyote yanamfaa, lakini sioni mavazi hayo yakivaliwa kwa wingi kama haya mavazi yaliyomo ndani ya maduka ya butiki. Wenzetu (wazungu) wakija ndio mavazi yanayowavutia na huyanunua kwa wingi na kurudi nayo makwao, huku sisi wenyewee aaah kama vile hayatuhusu, why wabongo kwaniniiiii jamaniiiii tuna niniiiii tusiotaka kuthamini vya kwetu.

Kutoka kwa Michuzi Junior blogspot dot com

Bi. Fatma Karume.


TAARIFA KWA UMMA

Sisi Chama cha wanasheria Tanzania Bara tumepokea kwa masikitiko nakala ya barua kutoka kwa Hakimu mkazi wa Mahakama ya Kisutu Mh. Addy Lyamuya kwenda kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Kisutu kuhusu malalamiko dhidi ya Wakili Msomi wa kujitegemea Fatma Karume kwenye shauri la ndoa kati ya Bwana Sadiq Ahmed Walji (Petitioner) na Bibi Saeeda Hassan (Respondent) leo tarehe 22/11/2007.

Barua hii ilieleza malalamiko dhidi ya Wakili Msomi Fatma Karume ambaye ni mwanachama wa chama cha Wanasheria Tanzania Bara ambaye anatuhumiwa kusumbua mahakama na kuchelewesha kesi kwa vurugu ambazo hazikuwa za lazima tarehe 21/11/2007 katika mahakama ya Kisutu wakati shughuli za mahakama zinaendelea.

Tumeijibu barua ya Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Kisutu na kumhimiza Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama wa Kisutu, Mheshimiwa Mwangesi, ayasikilize malalamiko haya ili kuthibitisha ukweli wa tukio hilo kwa haraka. Sisi kama Chama wa Wanasheria tuna wajibu wa kutetea wanachama wetu pale wanapoonewa na pia tuna wajibu wa kuwachukulia hatua kuendana na sheria na kanuni zetu pale inapothibitika kwamba mwenendo wao umekiuka maadili ya taaluma yetu.

Tuko tayari kushirikiana na Mahakama kufikia maamuzi ya kweli na haki. Endapo itathibitika kwamba Wakili Msomi Fatma Karume aliyafanya hayo yanayodaiwa itakuwa ni kitendo ambacho kitastahili kukemewa/kukaripiwa na kutolewa adhabu kwa mujibu wa kanuni za sheria kwa sababu ni kinyume na maadili ya Mawakili ambao wana majukumu kama maafisa wa Mahakama kulinda uhuru, kuiheshimu na kuisaidia Mahakama kufikia maamuzi huru na haki.


Joaquine De-Mello
Rais,
Tanganyika Law Society
22 Novemba 2007

Kutoka kwa Maggid Mjengwa.
BINTI WA KARUME ARUSHA KOMBORA.


*Adai Mahakama Kisutu inanuka rushwa
*Asema amewasilisha ushahidi Takukuru
*Asisitiza yu tayari kukabiliana na lolote


BINTI wa Rais, Amani Abeid Karume, ambaye ni wakili wa kujitegemea, Fatma Karume, anayedaiwa kufanya fujo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Dar es Salaam juzi, ameibuka na kueleza kusikitishwa kwake na madai hayo huku yeye mwenyewe akitoa tuhuma nzito za rushwa dhidi ya mahakimu wa mahakama hiyo.
Fatma alitoa tuhuma hizo wakati alipofanya mahojiano ya ana kwa ana na Tanzania Daima jana jioni wakati alipotakiwa kueleza kile kilichotokea katika mahakama hiyo juzi na uamuzi wake, baada ya Chama cha Wanasheria Tanzania (TLS) kutoa tamko la kusikitishwa na tukio hilo na kutaka uchunguzi ufanyike.

Wakili huyo, alisema baadhi ya mahakimu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu wanajihusisha na vitendo vya rushwa, jambo aliloeleza kuwa alikuwa tayari ameshalitolea malalamiko yake rasmi katika Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (Takukuru).

Akizungumzia matokeo ya mzozo wake huo wa juzi, Fatma alisema alikuwa tayari kukabiliana na hatua zozote zitakazochukuliwa dhidi yake kwa sababu tu ya kupigania haki anayoamini alidhulumiwa katika misingi isiyofaa.

“Niko tayari hata kufutwa uwakili. Natetea haki yangu ambayo naamini nilinyang’anywa, nimeingia kufanya kazi hii kwa sababu ya kutetea wananchi, hivyo siwezi kuona nikidhulumiwa nikanyamaza kimya. Enzi za utumwa zilishapitwa na wakati, ni bora nikalime nazi kuliko kupoteza haki yangu,” alisema Fatma kwa kujiamini.

Alisema hata kama yeye ni mtoto wa rais, bado anayo haki ya kudai kile anachodhani anadhulumiwa, kwani naye ni mtu kama walivyo watu wengine, na kimsingi akakataa suala lake kuhusishwa na urais wa baba yake.

Kuhusu kuwapo kwa rushwa, binti huyo wa Rais wa Zanzibar alisema anao ushahidi wa kutosha unaomuonyesha mmoja wa mahakimu waandamizi wa mahakama hiyo akiomba rushwa kutoka kwa mteja wake, Sadiq Walji.

“Ninao ushahidi wa uhakika hakimu (alimtaja jina), aliomba rushwa (akataja kiasi cha fedha zilizoombwa na hakimu huyo)…tena alimfuata mteja wangu katika Hoteli ya Sea Cliff Agosti 26 mwaka huu, na alimpatia fedha na akamrekodi bila ya yeye kujua ‘tape recorder’ (kinasa sauti). Hili ushahidi wa sauti yake tulishauwasilisha Takukuru na wamelifanyia uchunguzi kwa muda mrefu.

“Nasema hivi, Mahakama ya Kisutu inanuka rushwa. Inahusisha mahakimu na waendesha mashitaka. Rushwa imetawala pale, tena huyo hakimu kesho (leo) anapelekewa barua yake…mimi siyo mwehu hata kidogo, nasema hili kwa uhakika na serikali na watu wote wajue kuwa Mahakama ya Kisutu pana rushwa kila mahali,” alisisitiza wakili huyo wa kujitegemea.

Akizungumzia madai ya kufanya fujo ndani ya mahakama wakati kesi inaendelea, wakili Karume aliyefika kwa ajili ya kumuwakilisha Walji, kwenye kesi namba 60/2006 ya madai ya mtoto wa miaka miwili iliyokuwa ikisikilizwa mbele ya Hakimu Mwandamizi, Addy Lyamuya, alisema hakimu huyo alimkosea, hali iliyosababisha malumbano.

Alisema, Hakimu Lyamuya alitaka kuipanga kesi hiyo tarehe za mbali bila sababu za msingi, jambo ambalo wakili Karume alipingana nalo kwa kuwa Hakimu Adolf Mahay, alikwishatoa uamuzi Agosti mwaka huu kuwa mtoto huyo wa mteja wake anayeishi kwa Saeeda Hassam , awe akiruhusiwa kila Ijumaa kwenda kwa baba yake na kurudishwa kwa mama yake Jumapili.

Fatma alisema licha ya uamuzi huo, mama wa mtoto huyo alikuwa akikaidi amri hiyo, hali ambayo ilimfanya yeye awasilishe ombi la kutaka mwanamke huyo achukuliwe hatua za kisheria kwa kosa la kuidharau amri halali ya mahakama hiyo.

“Licha ya kumuomba hakimu aipange leo, alikataa na kunijibu kwa ukali na akanionyeshea kwa ishara kwamba mimi ni mwendawazimu….nikamuuliza, madaraka hayo nani kampa ya kunionyeshea kwa ishara mimi ni mwendawazimu? Akaanza kuniambia nisimpangie kazi…nikashikwa na hasira na kutoka mahala nilipokuwa nimesimama na kumwambia zama za utumwa zilishapita katika nchi yetu, hivyo siwezi kukubali kuona navunjiwa heshima nikanyamaza kimya na nikamweleza kabisa nakwenda kumshitaki kwa wakubwa wake wa kazi.

Alisema baada ya kumweleza maneno hayo, hakimu alikwenda kumshitaki kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi na pia alikwenda kumshitaki kwa Jaji Kiongozi Amir Manento lakini hata hivyo alisema malalamiko yake hakuwa ameyapeleka kwa viongozi hao kwa maandishi.

“Licha ya kumweleza yote haya, hakimu hakutaka kunisikiliza na badala yake akanionyeshea kwa ishara kwamba, mimi ni mwendawazimu….ndipo nilipomweleza kwamba hawezi kazi na kwamba naenda kumshitaki kwa wakubwa wake wa kazi,” alisema Karume.

Fatma alisema pia kuwa, juzi asubuhi alikwenda kumshitaki Lyamuya kwa Hakimu Mkuu Mfawidhi wa mahakama hiyo, Sivangilwa Mwangesi, pia alikwenda kumshitaki kwa Jaji Kiongozi, Amir Manento, lakini hata hivyo alisema malalamiko yake hakuwa ameyapeleka kwa viongozi hao kwa maandishi.

“Habari zilizoandikwa jana kwakweli zimeniumiza sana…kwani Lyamuya aliniita mimi mwendawazimu na mbaya zaidi, Mahayi anasema kwamba alijitoa kwenye kesi ninayoitetea kwa sababu nilimfokea. Haya mambo si ya kweli,” alisema Fatma katika mahojiano jana.

Katika tukio la juzi, Fatma alikuwa akituhumiwa kutoa maneno makali dhidi ya Hakimu Lyamuya, hali iliyodaiwa kusababisha hakimu huyo ajitoe kuendelea kusikiliza kesi inayomhusu mwanasheria huyo.

Tukio hilo la aina yake lilitokea katika chumba cha mahakama, wakati hakimu huyo alipotaka kuanza kusikiliza kesi ya madai namba 60/2006 ambayo ilianza kujadiliwa na hakimu huyo juzi hiyo kwa mara ya kwanza, tangu apewe jalada hilo.

Katika kesi hiyo, Fatma anamwakilisha Sadiq Walji, ambaye ni mdaiwa katika kesi hiyo ya madai ya mtoto. Mdai katika kesi hiyo namba 60/2006 ni Saeeda Hassam.

Kabla Hakimu Lyamuya kuanza kusikiliza kesi hiyo, Wakili Fatma, aliiomba mahakama kuahirisha kesi hiyo hadi kesho, kwa ajili ya kuanza kusikilizwa kwa shauri hilo.

Kutokana na hali hiyo, hakimu alimtaka karani wake kuangalia kwenye kitabu cha kumbukumbu (diary) kama siku hiyo itafaa kusikilizwa kwa shauri hilo. Hata hivyo, karani alimweleza hakimu kuwa siku hiyo zimepangwa kesi nyingi za kusikilizwa, labda waipange Januari 13, mwakani.

Kwa mujibu wa taarifa za juzi, Hakimu Lyamuya alikubaliana na maelezo ya karani wake na kumweleza wakili huyo kwamba kesi hiyo itasikilizwa tarehe hiyo.

Baada ya hakimu kupanga tarehe hiyo, Wakili Fatma anadaiwa kuwa alianza kufoka kwa sauti ya juu akitaka mahakama isikilize kesi hiyo jana jambo ambalo Hakimu Lyamuya alilikataa kwa kueleza kuwa hakuwa na nafasi.

Wakili huyo aliendelea kuomba mahakama kupanga kesi hiyo Januari 2 mwakani, ombi ambalo hakimu huyo alilikataa na kumweleza tarehe hiyo mahakimu watakuwa mapumziko, ndipo wakili huyo alipoanza kutoa kauli kali dhidi ya hakimu huyo.

“Kwanza wewe hujui kazi na ni mara yako ya kwanza kuniona mimi… hunijui ni nani, sasa nitakuonyesha… nitaandika barua kwa wakubwa wako wa kazi na kuwaeleza kwamba hujui kazi,” alidaiwa kusema Fatma hiyo juzi.

Kutokana na tafrani hiyo, mahakama ilishindwa kuendelea kusikiliza shauri hilo wala kulipangia tarehe na badala yake jalada la kesi lilirudishwa kwa uongozi wa mahakama hiyo, ili limpangie hakimu mwingine kusikiliza kesi hiyo.

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya tafrani hiyo juzi, Hakimu Lyamuya, alisema ameshangazwa na vitendo vya utovu wa maadili vilivyoonyeshwa na wakili huyo na kueleza hajafikiria kuchukua uamuzi wa kumfungulia kesi.

Chanzo: Gazeti la Tanzania Daima la Ijumaa, Novemba 23, 2007

‘Asilimia 40 ya vifaa vya umeme vya nje ni bandia’

Nashon Kennedy, Mwanza
HabariLeo; Saturday,November 24, 2007 @00:03

ASILIMIA 40 ya vifaa vyote vya umeme vinavyoingizwa nchini ni bandia na hutumiwa na watumiaji bila ya wao kuzitambua bidhaa hizo.

Hayo yalielezwa jana na Mkuu wa Idara ya Kudhibiti Bidhaa Bandia kutoka Tume ya Ushindani nchini, John Mponela, alipowasilisha mada juu ya utaratibu wa kisheria wa mapambano dhidi ya bidhaa bandia zinazoingizwa nchini katika semina ya siku moja iliyowashirikisha washiriki kutoka mashirika yasiyo ya kiserikali, watu binafsi na wadau mbalimbali.

Mponela alisema bidhaa hizo bandia zimeshamiri zaidi kwenye vifaa vya ujenzi, umeme, vifaa vya elektroniki, dawa, viberiti, dawa za viatu na zile za meno.

Alisema sababu kubwa ya uingizaji wa bidhaa hizo ni pamoja na ulegezaji wa masharti ya biashara ulioanza miaka ya 1980 na kuwapo kwa suala zima la utandawazi.

Utafiti uliofanywa na Kampuni ya Kimataifa ya Marekani (ICR) unakisia kuwa kwa Tanzania pekee, Kampuni ya Sigara (TCC) inapoteza karibu asilimia 40 ya mapato yake kutokana na bidhaa bandia za sigara.

“ICR vile vile inakadiria kuwa nchi wanachama wa Afrika Mashariki zinapoteza karibu dola za Marekani milioni 20 kila mwaka kama mapato ya kodi kwa bidhaa bandia,” alisema Mponela.

Naye Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Ushindani, Godfrey Mkocha, aliwaomba watumiaji wa bidhaa zinazoingia nchini wahakikishe ni zile zinazokubalika kwa mujibu wa sheria na kwamba kila mwananchi anayo haki ya kuisaidia tume hiyo kulinda mazingira ya uchumi kupunguza gharama na kuongeza ubora wa huduma nchini.

Aliwatahadharisha wananchi kutonunua bidhaa bandia kwenye maeneo yao akisema kuwa zina athari kwa afya zao na zitawaathiri katika uchumi.


Friday, November 23, 2007

‘Tukitumia vizuri Kiswahili kitatukomboa na kufanya tupae’


Midladjy Maez

HabariLeo; Friday,November 23, 2007 @00:07

NIMEPATA fadhaa na kukerwa na maoni ya baadhi ya Watanzania, hasa wasomi, ambao hukipaka mafuta Kiswahili kwa mgongo wa chupa na kukibeza na kuonyesha jinsi wanavyoabudu lugha ya Kiingereza.

Nitaeleza sababu kadhaa ambazo wasomi hao wanazijua, lakini hawataki kuzikubali. Kila tunapofanya hatua za zima moto kukuza kiwango cha elimu, kwa mfano kwa kuwapeleka watoto wetu katika shule zinazosomesha ‘Kiingereza’ kwa kutumia walimu wasiojua Kiingereza, ndio ukweli tunadidimiza elimu yetu kwa jumla kitaifa!

Kuna watu wanajichanganya na kuonea wivu ‘wakubwa’ wanaopeleka watoto wao ama hapa nchini katika shule nilizotaja hapo awali au katika nchi jirani au hata Ulaya, Marekani na Australia.

Utafiti mdogo uliofanywa unaonyesha kuwa karibu theluthi mbili ya watoto wa wakubwa, wana uwezo duni kimasomo na mara nyingi huko Ulaya wamepelekwa kuficha aibu ya kifamilia.

Mara nyingi watoto hao si mfano mzuri wa tabia na wamebobea katika ugoigoi kimasomo. Ni kweli wanaweza wakawa mahiri katika kuzungumza ‘Kiingereza’ cha mitaani, lakini hawana tofauti sana na matapeli wa vijiweni, wajulikanao mijini kama ‘ misheni tauni’

Tumepoteza miaka 45 kitaaluma tukichapa mguu, wakati mataifa mengine yamejitahidi kufanya mabadiliko kadhaa ili kuboresha elimu yao.

Kwa mfano, katika Karne ya 18 Urusi kupitia wasomi wake ilibadili mfumo wa kukiabudu Kifaransa na katika Karne ya 20 wakawa wa kwanza kupeleka mtu angani. Wangekuwa bado wanakiabudu Kifaransa wangekuwa bado wanakamua maziwa na kulima kwa ngwamba.

Ukisema Warusi wana rasilimali za kutosha na sisi vivyo hivyo tumejaaliwa tunazo. Zipo nchi nyingi tu zilizopata maendeleo ya haraka ambazo zilikuwa na kiwango duni cha maendeleo na mfano ni Korea zote mbili.

Mwaka 1960 nchi hizo za Korea Kaskazini na Korea Kusini, zilikuwa kitaaluma na kiuchumi sawa na sisi, lakini wametumia Kikorea kusonga mbele na sasa ziko katika Dunia ya Kwanza!

Sisemi na sisi tungekuwa kama Korea, lakini kama tungechanga karata zetu vizuri, ikiwamo kukitumia vizuri Kiswahili, basi tungekuwa katika hatua bora zaidi ya maendeleo kuliko sasa.

Zamani Kilatini kilitawala dunia na Kiingereza kinachopigiwa debe sasa, kilikuwa lugha ya wawindaji na ya jikoni na hakikutumika hata kwa kutungia mashairi.

Dola ya Kirusi haikuanza kupiga hatua katika tafiti za sayansi na teknolojia, hadi pale ilipoanza kutumia rasmi Kirusi. Urusi ilianza kusonga mbele katika karne ya 18 baada ya Kirusi kuchukua nafasi ya Kifaransa, kilichokuwa lugha ya watawala na mabwanyenye.

Tuna bahati Kiswahili kilipewa kipaumbele hata na Wakoloni. Wazungu walikitumia Kiswahili kutufikishia amri zao. Lakini, pia wakati wa kupigania uhuru wanasiasa wetu nao walikitumia Kiswahili kama silaha ya ukombozi. Walikitumia kuunganisha makabila zaidi ya 120 yaliyopo Tanzania na kujenga Taifa moja linalozungumza Kiswahili.

Hivi sasa tunapiga kelele mikataba ya madini na mingine ya miradi mikubwa imekuwa ni mizigo. Tuna malalamiko na hofu nyingi, lakini hakuna anayethubutu kusema hiyo mikataba imeandikwa Kiingereza na wanaofahamu ni wachache! Nina uhakika kama mikataba ingeandikwa kwa Kiswahili, mambo yangekuwa afueni.

Utafiti wa wataalamu wa Chuo Kikuu unaonyesha kuwa ufahamu wa Kiingereza katika jamii unashuka siku hadi siku . Utafiti katika shule mojawapo ya sekondari ulionyesha kuwa katika walimu 55 wa mchepuo wa Sayansi, ni watano tu katika hao, ndio waliokuwa wanajimudu kusomesha kwa Kiingereza.

Waliobakia yaani 50 walikuwa ‘wanajikongoja’. Sasa hii elimu gani kwani kuna hatari ya kuzalisha wataalamu waliobobea kinadharia tu lakini kivitendo hawajimudu!

Watu wameng’ang’ania Kiingereza wakati ukweli hawakiwezi. Kukifanya Kiingereza kama somo mojawapo ni vema zaidi kuliko zoezi la sasa la kutaka kufanya iwe lugha ya kufundishia. Kwa maoni zoezi hilo ni njama za kuua kabisa elimu.

Tutumie mbinu waliyotumia Warusi, Wajapani na Wakorea ya kupeleka vijana wao kusomea taaluma za sayansi na teknolojia katika nchi kadhaa na halafu kuteka chembechembe za taaluma hizo na kuzirejesha nyumbani kwao ambako zilizalishwa kulingana na mahitaji na vipaumbele vyao na matokeo yake ni maendeleo makubwa tunayoyasifia sasa.

Hali hiyo haikuja kwa kubahatisha kwa kutumia lugha za watu. Chembechembe za taaluma zilitafsiriwa katika lugha zao za kitaifa na kurudufiwa kitaaluma ndani ya jamii yote, hivyo kuifanya sehemu ya utamaduni wa jamii.

Elimu inayofunzwa kwa lugha ya kigeni, siku zote haitokuwa sehemu ya jamii husika, hivyo haitochangia kuinua maendeleo yoyote katika jamii husika.

Lugha ya Kiswahili inaweza kuwa mkombozi. Inaweza kutumika kutaifisha teknolojia yoyote ya kigeni na kuileta nchini na kuitumia kwa maendeleo yetu.

Mimi naamini kabisa kama miaka 20 iliyopita Kiswahili kingepewa dhima ya kuwa lugha ya kutolea taaluma katika vyuo vyetu vikuu, basi hivi sasa wataalamu wetu katika fani nyingi, wangekuwa wanaongoza kwa idadi kama mabingwa.Tungeweza kuwa na hata na maprofesa 100 wa Kiswahili!

Kiswahili kina uwezo na silaha. Kama vile kilivyotumika kama silaha ya kumfukuza mkoloni, kinaweza kutumika kutimiza dhima yoyote, mfano kutoa elimu ya juu. Elimu ya sasa kwa kutumia Kiingereza kibovu, iwe katika shule za ‘academy’ au za Serikali, inafanya kiwango chetu cha elimu kuwa duni.

Katika miaka ya 1980 kulikuwa na vuguvugu la kukifanya Kiswahili lugha ya kufundishia vyuo vikuu, badala ya Kiingereza !

Ilikuwa patashika nguo kuchanika, kwani Uingereza ilikuja na mradi wa kuboresha ufundishaji wa Kiingereza. Nadhani mradi ule ndio uliozaa hizo shule za ‘academy’ .

Uingereza ilitoa maelfu ya paundi kukwamisha hatua hiyo ya ukombozi wa lugha yetu ya Kiswahili.

Ukichunguza ni nani aliyefaidika na mradi huo, jibu ni watu binafsi kwa kupata fursa ya kwenda majuu na kujipatia fursa ya kununua bidhaa adimu, ikiwamo magari. Mradi huo haukuzaa matunda, kwa vile kiwango cha uelewa wa Kiingereza kimezidi kuporomoka.

Nikiwa mtaalamu wa Uandishi wa Habari mwenye Stashahada, ilichukua mwaka mmoja kufahamu Kirusi cha kusomea taaluma ya juu ya Uandishi wa Habari.

Hivyo hivyo kwa Watanzania wengine tuliokwenda Urusi miaka hiyo ya 1986-1992, wako walioenda kusomea udaktari, uhandisi wa umeme, mitambo na ujenzi. Wote hao walisomea kwa Kirusi. Hivi sasa wapo hapa nchini wanajenga Taifa katika sekta mbalimbali na wengine wako katika ngazi za Kitaifa.

Niliwahi kupata fursa ya kutembelea Sweden. Kule katika kila watu wawili, mmoja anajua Kiingereza. Lakini hakuna hata mara moja, utasikia Waswidish wanataka Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia!

Fikiria katika Tanzania ambako katika watu milioni 36, sio ajabu labda milioni moja ‘wanajua’ Kiingereza na labda 20,000 kati ya hao, ndio wanaweza kukizungumza bila matatatizo yoyote katika’warsha’ na semina.

Lakini ukweli unabakia wengi wanaozungumza siku hizi, wanataka kusifiwa kuwa wanajua Kiingereza kama ishara ya kuwa wamesoma, lakini hali halisi inabakia kuwa ni mambumbumbu kitaaluma. Kung’ang’ania kukitumia Kiingereza ni kufanya upeo wetu wa kitaaluma kuwa duni kwa ujumla.

Hatuna rasilimali za kutosha za kuifanya nchi yetu iwe kama Sweden, ambapo nusu ya wananchi wake wanazungumza Kiingereza. Hata hivyo wanatumia Kiswidish kama lugha yao ya Taifa, ambayo inazalisha magari ya ‘Volvo’ na Scania’ si mnazifahamu!

Kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa ni hatua ngumu, lakini ni ya ukombozi ambayo ilitakiwa ichukuliwe mapema. Kwa sababu kama Urusi waliweza katika Karne ya 18, kwa nini sisi tusiweze wakati huu wa Karne ya 21 ? Kiswahili kitaendelea kutukomboa na kutufanya tupae haraka.
Mwanafunzi afanyiwa umafia!

Mwanafunzi wa kidato cha tatu (jina lake na shule anayosoma kapuni) hivi karibuni amejikuta akifanyiwa umafia na wanaume wanne anaodaiwa kuwagonganisha kimapenzi.

Habari kutoka wilayani humu mkoani Shinyanga zilisema kuwa, binti huyo ambaye pia amedaiwa kuwa muimba kwaya mzuri alijikuta akifanyiwa vitendo vichafu kwa zamu na vijana wasiojulikana.

Ilidaiwa kuwa, kabla ya kufanyiwa umafia huo mwanafunzi huyo alikuwa na uhusiano wa kimapenzi na miongoni mwa vijana hao kwa nyakati tofauti....

“Tamaa ya chipsi kuku ndiyo iliyomponza, vijana hao wote alikuwa anafanya nao mapenzi, huenda siku hiyo waliamua kumkomesha kwa tabia hiyo ya kuwagonganisha,” kilisema chanzo chetu ambacho kilidai kufahamu nyendo za mwanafunzi huyo.

Ilidaiwa kuwa siku ya tukio msichana huyo na mmoja kati ya wapenzi wake walipanga ahadi ya kukutana kwenye gesti bubu (isiyo rasmi), ilioyoko eneo la Nyihogo ambako vijana wengine watatu walikwenda pia.

Habari zilisema wakati msichana huyo akiwa chumbani na mvulana aliyepanga kukutana naye, vijana hao waliingia na kuanza kubadilishana kwa staili ya mtu kutoka na mwingine kuingia kiaina.

Hata hivyo, licha ya binti huyo kukutwa na wahudumu akiwa hoi alisita kuripoti tukio hilo kituo cha polisi kwa madai kuwa atajiaibisha.

Uchunguzi uliofanywa na Amani ulibaini kuwa, wasichana wengi katika maeneo ya miji wamekuwa wakirubuniwa kwa vitu vidogo na kujikuta wakifanyiwa vitendo hivyo viovu.

Gazeti hili linawaomba mabinti kuwa makini na mfumo wao wa maisha na kuhakikisha wanaangalia masomo kwanza na kuweka mapenzi pembeni.

Mpaka leo hii bado hajatimiza ndoto yake ya kuwa Raisi wa pili wa Tanganyika.Lakini jambo moja ambalo ameshatimiza ni kuandikwa kwenye vitabu vya historia ya Tanzania kama mwanasiasa machachari na ambaye hachoki.Jina lake ni Christopher Mtikila.Ila kwa heshima ya nafasi aliyonayo katika masuala ya imani ukimuita Mchungaji Christopher Mtikila ndio unakuwa umepatia zaidi.

Ukitaka kuelewa kidogo kuhusu alipotokea Mchungaji Mtikila,basi soma mahojiano aliyowahi kufanya na jamaa wa pbs.org siku za nyuma kwa kubonyeza hapa.

Photo credit:Mrocky

Kutoka Bongo Celebrity.
Mabadiliko ya kimaumbile na msongo wa mawazo

Lucy Ngowi.

Karibu mpenzi msomaji wa safu hii. Leo tutakaangalia jinsi ya kumsaidia mtoto, mambo yanayokupata, hali za kimaumbile na kihisia unazokabiliana nazo uwapo na msongo wa mawazo. Endelea nami pale ulipoishia wiki iliyopita.

UNAWEZA kumsaidia mtoto wako aweze kukabiliana na msongo wa mawazo kwa kuongea naye juu ya mambo yanayoweza kusababisha hali hiyo, ili aweze kuelewa. Ninaamini kuwa kwa pamoja, mnaweza mkapata baadhi ya njia zitakazoleta ufumbuzi kwake.

Baadhi ya majukumu anayokabiliana nayo mtoto, yanaweza kupunguzwa baada ya kutoka shuleni, pia ni vizuri kama atatumia muda wake mwingi kuzungumza na wazazi au walimu wake. Pia awe anafanya mazoezi ya viungo kama kwa kucheza michezo mbalimbali, au unaweza kupanga safari na kwenda.

Pia unaweza kumsaidia mtoto wako kwa kumwandalia kwenda kwenye warsha au mafunzo ambayo yatamwezesha kukabiliana na hali hiyo. Pia umpe uhuru aweze kujua muda atakaoweza kumwona daktari kwa ajili ya kuzungumza naye juu ya hali hiyo.

Kumbuka baadhi ya misongo ni hali ya kawaida, hivyo mwache mtoto wako aelewe kuwa si jambo la ajabu kuwa na hasira, kushtuka, upweke, au hali ya wasiwasi. Mwache ajue kuwa watu wengine nao wanapatwa hali kama hiyo siyo yeye peke yake.

Jinsi ya kushughulika na mtoto aliyepatwa na msongo wa mawazo Wakati watoto wanapatwa na shida katika kuzungumzia hali hiyo, itasaidia utakapozungumza na mtoto wako kuhusu mambo yako mwenyewe yanayokushughulisha. Hii itamsaidia kuona kuwa uko tayari kuzungumza naye kuhusu mambo yako unayokabiliana nayo, hali hiyo itamwezesha naye kujihisi utayari wa kuzungumza nawe jambo lolote linalomtatiza.

Kama mtoto wako ataendelea kuwa na hofu na kushindwa kuzungumza nawe kama mzazi wake, njia nyingine ya kumsaidia ni kumtafutia mshauri mwingine au daktari aliyebobea katika masuala hayo na kuzungumza naye.

Wazazi wengi wana uwezo wa kujua mawazo yanayowapata watoto wao, ikiwamo wakati wanaposoma na kukosa muda wa kupumzika. Mzazi kama utashindwa kukabiliana na hali inayomsumbua mtoto wako baada ya kufanya jitihada mbalimbali, mwone daktari wa mtoto wako, zungumza na washauri pamoja na walimu pale mtoto wako anaposoma. Baada ya kuzungumza nao, watakuwezesha kujua ukutane na mtaalamu gani ili aweze kumsaidia mtoto wako.

Tukiachana na jinsi ya kumsaidia mtoto wako ili aweze kukabiliana na msongo anaokuwa nao, pia kuna mabadiliko mbalimbali ya kimaumbile kwa mtu mwingine yeyote anapokuwa na msongo wa mawazo.

Mwitikio wa kimaumbile katika hisia kali uliumbwa ili kuweza kutuokoa katika siku zile ambazo watu waliishi katika mapango. Kwa mtu wa Zama za mawe, mwitikio wa kimaumbile uliojulikana kama ‘ruka au pigana’ ulimwandaa kwa ajili ya jambo lolote.

Mwitikio huo ulikuwa ni muhimu sana kwa matukio yaliyokuwa yakitokea mara chache pale alipokuwa akikimbizwa na wanyama wakali kama vile chui au alipokuwa akifanya mawindo kwa ajili ya chakula. Kwa sasa baada ya mamilioni ya miaka kuwa yamepita, bado mwitikio huo una visababisho sawa na vile vya wakati ule, lakini ni matokeo ya mibinyo tunayokumbana nayo katika maisha ya kila siku.

Ni kitu gani kinachotokea katika miili yetu tunapokuwa na msongo wa mawazo? Tunajikuta tunapatwa na shinikizo la damu, tunapumua kwa nguvu, masikio, macho na pua zetu zinakuwa na tahadhari mara zote. Mabadiliko haya ni matokeo ya kemikali zinazokwenda kwenye damu na kusababisha msongo kutokea.

Wakati unapoendelea kuwa na mawazo kwa muda mrefu, au yanapotokea mara kwa mara na kwa wakati mbaya inachangia kuwepo kwa hisia mbaya. Mwanadamu anapata onyo la kutoka kwenye ubongo ambalo linamwambia acha na upumzike.

Wakati tunapokataa kuchukua ushauri kutoka kwenye ubongo, inatuletea matatizo katika miili yetu. Hali hii inatofautiana kati ya mtu na mtu.

Ni jinsi gani mwonekano wako unavyoathirika?Baadhi ya watu wanaonekana kuishi katika maisha yenye mambo mengi ya kimitindo. Wengine wanaonekana kuwa na misongo kwa kiwango kidogo. Wote tuko kipekee kutokana na jinsi tunavyoshughulikia msongo. Kwa hakika msongo hautokani tu na yale yanayotusibu, lakini pia hutegemeana na jinsi tunavyofikiri.

Wanasaikolojia wanasema kuwa haiba tofauti hutenda tofauti na kukabiliana na msongo kwa njia tofauti. Kundi A la haiba ni wale ambao huwa na haraka katika mambo fulani, washindani na walio makini na hao ni wepesi wa kukumbwa na msongo. Kundi B la haiba ni wale ambao hawaonekani kujali sana, huchukulia kila jambo kama la kawaida tu hata kama ni kubwa kiasi gani. Hawa ni rahisi kukabiliana na msongo.

Kwa upande mwingine tuangalie tabia za kimaumbile katika msongo wa mawazo. Tabia hizo husababisha mtu kuogopa sana hadi kusababisha maumivu ya tumbo, kukosa hamu ya kula, kupatwa na maumivu ya kifua, kuharisha, kukondesha watoto, kukauka midomo, kutoka mkojo mara kwa mara, kuumwa kichwa, chakula kutokusagika vizuri tumboni, kukaza kwa misuli, kuwa na tahadhari ya mara kwa mara, mapigo ya moyo kupiga kwa nguvu bila kutegemea, kutopata usingizi, kutoka jasho jingi na kupatwa na maumivu yasiyoelezeka.

Tabia za kihisia unapokuwa na msongo wa mawazo. Mtu hujikuta kuwa na mabadiliko makubwa ambayo huchangia kuongezeka kwa wasiwasi, kero na kuwa na hali ya kutoeleweka. Hujikuta mambo madogo madogo yamkasirisha mara kwa mara na kumfanya ashindwe kuwa mstahamilivu.

Kwa mfano, ukweli ni kwamba watoto wanataka kucheza mchezo kwenye luninga, na wakati huo ndiyo kwanza umerudi nyumbani kutoka kazini, na unachotaka kukifanya ni kukaa na kunywa kinywaji chako huku ukiangalia luninga, kutokana na hali uliyonayo inakukusukuma kuwaondoa watoto wako na kukaa mwenyewe.

Pia kunakuwa na mabadiliko ya kutokuwa na hamu ya kula na wakati mwingine uzito kupungua. Baadhi ya watu wanakosa hamu ya kula, wengine wanakula kawaida. Uwezo wako wa kuendana na mazingira ya kazini na nyumbani unaweza kuwa tofauti, na unaweza kujikuta kuwa huwezi kulipa Ankara zinazokukabili lakini mambo huwa mabaya zaidi pale ambapo unakuta simu yako imekatwa kutokana na deni, ubongo wako unakuwa unawaza mambo tofauti na kukuongezea msongo. Unaanza kuvuta sigara au kunywa pombe au vyote kwa pamoja, hali ambayo unafikiri inakupunguzia mawazo, unapokuwa unakosa usingizi usiku.

Hali ya kihisia inayokupata unapokuwa na msongo wa mawazo. Unakuwa na hali ya kuhangaika au sononeko, unajikuta huwezi kufanya maamuzi, siku zote anakuwa na hofu au hali ya kutishika, hofu ya kutokea kuzimia au kuanguka, kusikia hali ya kupatwa na shinikizo la damu, kuhisi ubongo umekauka, kuhisi wasiwasi na kushindwa kupumzika, kuhisi kutoelewana na watu, kupatwa na msukumo wa kutaka kukimbia au kujificha, kuongeza majonzi pamoja na kuwa katika hali ya kutokutulia, na kutokuwa na uwezo wa kuwa makini na jambo.

Tukutane wiki ijayo.

lcyngowi@yahoo.com
0713 331455/0733 331455


Thursday, November 22, 2007


Nani anayeuzima mshumaa wa Serikali?

Maggid Mjengwa.

KUTOKANA na mambo yanavyoenenda katika jamii yetu sasa, mmoja wa wasomaji wangu ameniandikia kuniomba niwakumbushe wasomaji juu ya kisa kifuatacho nilichopata kuhadithia zamani kidogo.

Naam, miongoni mwa viongozi waliopata kuongoza dola ya Kiislam, baada ya Mtume Muhammad (SAW) na baada ya masahaba ni Amir Muuminina Khalifa Umar bin Abdulaziz.

Wanazuoni wa Kiislam wanatuambia, kuwa utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ulijaa uadilifu. Si kwa viongozi tu, hadi kwa raia wake. Inasemwa, kuwa moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ni kukusanya zaka. Katika Uislam, zaka ni ibada ya lazima kwa mwenye nacho kuwapa masikini, yatima, wajane,wasafiri, raia na wengineo wenye kuhitaji.

Watu walijengewa imani kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa zakka. Hata wale waliopokea zaka walikuwa waadilifu, hawakupokea zaka mara mbili kama walikwisha kupokea kabla. Wote waliostahili kupata zaka walipata zaka. Hakika, zaka zilitolewa zikajaa mabohari.

Siku moja raia mmoja alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin Abdulaziz, katika maongezi, Khalifa Umar alikuwa akihangaika kupuliza na kuzima mshumaa mmoja na kuwasha mwingine.

Alikuwa na mishumaa miwili mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar aliendelea kufanya hivyo. Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha akawasha mwingine. Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wake.

Akauliza; "je, ni kwa nini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?

Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu; "mshumaa huu ni wa serikali, wewe unaponiuliza habari za serikali nauwasha. Lakini naona mara unauliza habari za familia yangu, ndiyo maana nauzima wa serikali na nauwasha mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu. Nachelea nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi.

"Ewe msomaji, nasisitiza, hiki si kisa cha kutunga au chenye dhamira ya kukuburudisha, ni kisa cha kweli chenye kutuachia mafundisho makubwa katika suala zima la maadili.


RAIS Jakaya Kikwete

Julai mwaka 2005 akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alizungumza na wasomi juu ya masuala ya uongozi Afrika Mashariki. Wakati huo Kikwete alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM.

Katika hotuba yake hiyo Kikwete alikemea tabia ya ufisadi na ubinafsi wa viongozi wa bara hili. Kupitia safu hii niliandika, kuwa kama Jakaya Kikwete alimaanisha alichosema, basi, akibahatika kuupata urais huko twendako, historia itamhukumu kwa kauli na matendo yake.

Naam. Jakaya Kikwete ndiye Rais wa sasa wa nchi.

Amekwisha kuanza na anaendelea kuhukumiwa kwa kauli na matendo yake. Lakini hiyo ndiyo maana pia ya uongozi. Kiongozi husifiwa, hulaumiwa pia. Wakati mwingine lawama huzidi hata sifa za kiongozi. Busara si kuzuia njia zinazofanya kiongozi kusikia lawama kutoka kwa anaowaongoza.

Wasiomtakia mema kiongozi, ni wale wenye kufanya kila njia, na hata hila, ili kumficha kiongozi asisikie lawama za anaowaongoza. Wanajipendekeza na hata kusahau, kuwa hata lawama humsaidia kiongozi.

Kitokacho kwa waongwazwao, iwe sifa au lawama, ni sawa na kioo cha kujitazama usoni. Kiongozi naye awe kioo cha anaowaongoza. Kwa kuonyesha mfano wa yaliyo mema.

Pale Chuo Kikuu, wakati ule Kikwete alikemea ufisadi miongoni mwa viongozi. Leo tunasikia, kuwa baadhi ya viongozi mafisadi wamo hata ndani ya Serikali ya Kikwete. Kwa ubadhirifu na wizi, wanatafuna mabilioni ya shilingi kila mwaka. Fedha za walipa kodi. Tunaambiwa kuna walio na vitabu viwili vya stakabadhi za mapato, kimoja cha Serikali na kingine cha kwao wenyewe!

Rais mwenyewe ameonyesha kushtushwa, lakini huenda ameshtushwa na kuona kichuguu cha ufisadi, kuna milima ya ufisadi iliyojificha. Taifa linatafunwa. Kuna baadhi ya viongozi wanaoshindwa hata kuficha ulafi wao. Ubinafsi na ulafi yote ni misamiati yenye kuzungumzia uchoyo.

Kiongozi mbinafsi ni mchoyo pia, hapendi kuona hata kilicho kidogo kinagawiwa sawa kwa misingi ya haki. Kiongozi mbinafsi ana hulka za kujipendelea, kujali maslahi yake kwanza. Hili ni tatizo la viongozi wetu wengi barani Afrika.

Kiongozi mchoyo na mbinafsi pia ni mwenye hulka ya kujiweka mbele zaidi ya wenzake. Anapenda sana kusifiwa na hata kuimbiwa nyimbo za kutukuzwa. Anapenda utukufu. Lugha yake mara nyingi ni ya kujisifu, huwa hasubiri kusifiwa na wengine kwanza. Hudiriki kujisifu mwenyewe.

Na hata ukimsifia kiongozi wa namna hiyo, mathalan kwa matokeo mazuri ya kazi aliyofanya au hata mavazi aliyovaa, usishangae ukajibiwa; " Ah! Ndio, mimi ni mchapa kazi kweli kweli! Au " Kuonekana nadhifu namna hii ni kawaida yangu!"

Mara nyingi mafanikio kwake yeye ni matunda ya juhudi yake binafsi, si mwepesi wa kutambua mchango wa wengine katika mafanikio yake. Husahau hata mchango wa mkewe au mumewe. Yeye ni yeye. Katika ubinafsi wa viongozi wetu, mara nyingi kiongozi wa Kiafrika hapendi kukosolewa.

Hana busara ya kutambua, kuwa hakuna mwerevu wa kila jambo, kwamba sote hatujakamilika, tuna mapungufu yetu. Kwa kiongozi wa staili hii, akitamka jambo, basi hakuna wa kufikiri jingine. Fikra zake siku zote ni sahihi.

Kumkosoa kiongozi katika nchi zetu hizi, inaweza ikawa ni sawa na kumwambia hafai. Unatishia nafasi yake ya madaraka aliyopewa na Mwenyezi Mungu! Ni kufuru, ni dhambi. Kiongozi wa namna hii, kila anaposikia akishutumiwa, akikosolewa, na baya zaidi hadharani na wengine wanasikia, basi, huwa mkali kama mbogo.

Dhana ya kwamba anayekukosoa anakutakia mema, anataka ujirekebishe. Kwamba anayekosoa anaitakia mema na kuipenda nchi yake, dhana hii haikubaliki kwenye mitazamo ya viongozi wa kada hii. Anayekukosoa ni adui, ni mpinzani, na huenda kuna aliyemtuma.

Plato, mwanafalsafa wa Uyunani ya kale anasema; katika nchi, kiongozi wa namna hii, hufikia kukoma kuwa kama wanadamu wengine, hugeuka mbweha. Atawaandama "wapinzani" wake. Wengine atawaua kwa kuwapachikia mashitaka batili, na wengine atawalazimisha kwenda kuishi uhamishoni.

Wasomi , ambao mara nyingi huwa wadadisi, wenye kuhoji mamlaka, ni waathirika wa mwanzo wa kiongozi wa namna hii. Ikumbukwe, viongozi wengi Afrika hupata madaraka ya ghafla na utajiri wa ghafla.

Tofauti na mfanyabiashara wa kawaida, mara nyingi kiongozi Afrika huwa hana historia yenye kueleweka ya jinsi alivyoupata utajiri wake. Wengi wao, bila hata kujiandaa sana kiuongozi , hujikuta ghafla wamepata madaraka makubwa, na ghafla hulewa madaraka hayo, huwa ni walevi wa madaraka. Mlevi wa madaraka hupungukiwa haraka maadili ya uongozi.

Basi, ghafla huwa mla rushwa mkubwa kwa kutumia ofisi aliyokabidhiwa. Na hatimaye, ghafla huwa tajiri mkubwa, bilionea! Vyote hivi huweza kumtokea kiongozi wa Kiafrika kwa kasi ya kutisha sana.

Leo unapishana na Mwafrika mwenzako akiendesha baiskeli, kesho anaukwaa uongozi. Baada ya miaka 10 tu, anajenga Ikulu yake mwenyewe ya kifahari, anaweza kuwa nazo mbili au tatu za namna hiyo na magari kadhaa ya kifahari.

Kuna baadhi ya nyumba za waheshimiwa utadhani ni yadi za kuuzia magari. Je, yote haya ni kwa kipato halali?

Naam. Mtu wa namna hii kamwe hawezi kukupa historia yenye kueleweka juu ya utajiri wake wa ghafla.

Huyo si mhalifu kama walivyo wezi wa kuku au wenye kuvunja madirisha usiku. Huyo ni jambazi, ni mhalifu mkubwa anayetishia uhai wa raia na usalama wa taifa husika.

Neno langu la mwisho; ni heri kufa na kuacha fikra zinazoishi, kuliko kuishi bila kufikiri. Fikiri kwa bidii.

Kiselule: 0754 678 252,
Baruapepe: mjengwamaggid@hotmail.com
Blogu: http://mjengwa.blogspot.com