Monday, August 29, 2016


UKUTA WA CHADEMA NA MSIMAMO WA MAGUFULI;

WATUMISHI WA MUNGU MAJARIBUNI!

Imeandikwa na Mchungaji,
Overcomer Daniel-EAGT
MLIMA WA MAKIMBILIO, Dar Es Salaam

Ni somo zuri kama unataka kuwa mpatanishi.


Kwa mara ya kwanza nalazimika baada ya kujizuia sana kuandika au kusema chochote kuhusu kile ambacho kiko masikioni na kwenye akili za Watanzania wengi hivi sasa. Nazungumzia kitu kitu kilichobuniwa na kuratibiwa na Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) yaani UKUTA.

Kwao (CHADEMA) UKUTA ni kifupi cha maneno UMOJA WA KUPINGA UDIKTETA TANZANIA. Wanatuhumu kwamba kuna kila dalili kwamba nchi yetu sasa inanyemelewa na chembechembe za UDIKTETA, kwa hiyo wanachokifanya ni kujenga ukuta ili kuzuia hali hiyo, wanasisitiza kwamba nchi hii ibaki ikiongozwa au kuendeshwa kwa mujibu wa sheria huku Katiba ambayo ndio sheria mama ikiheshimiwa!

Tayari tumeona, mitaani na kwenye mitandao ya kijamii wapo wanaounga mkono kwa hoja au kishabiki wazo hilo la CHADEMA, lakini tena wapo wanaopinga hilo kwa hoja au kishabiki. Na ninapozungumzia hoja hapo juu sio lazima ziwe za maana au za hovyo, lakini ni ngumu kuzuia mtu kufikiri au kusema au kuandika katika dunia hii ambayo inaenda kasi ikichajizwa na maendeleo ya kutisha na kushangaza ya teknolojia habari mawasiliano.

Wa upande mwingine tumesikia na kuona serikali ikitunisha misuli, Rais wetu ameshatangaza kuwabana anayetaka kuanadamana aandamane akione cha moto, na akapigilia msumari kuwa yeye huwa hajaribiwi. Kando tu tumeshudia serikali yetu ikipiga jaramba kupitia jeshi lake la polisi kama salamu kwa wale wote ambao wanakusudia kuandamana na "kujenga ukuta' SEPTEMBA MOSI!! Serikali haijasema wazi kwamba mazoezi ya wazi ya jeshi lake la polisi katika baadhi ya mikoa nchini ni kwa ajili ya kuwatisha hao wa UKUTA, lakini kuna msemo mitaani wanasema

"Hujui kusoma, basi hata picha huoni?" 

Katika ujumla wa hayo yote, baadhi ya wananchi wameingiwa hofu kuu, mimi ni mmoja wa wengi hao ambao wana hofu kubwa. Kwa upande wangu hofu inasababishwa na ukweli kwamba kama kila upande unatunisha misuli, na wanaondamana ni raia, na tayari jeshi la polisi limejipanga, sioni amani siku hiyo. Na niwe mkweli, kama zile silaha ambazo tumeziona kwenye picha za mazoezi ya jeshi la polisi ndilo zitakazotumika (sitaki kuamini hivyo) kuwadhibiti waandamanaji siku hiyo, moyo wangu unaugua kwa maumivu yanayosababishwa na hofu!

Na hapa kuna mtego, kwa hisia zangu napata wakati mgumu sana, sijui kwa upande wa Watanzania wengine. Nawaza hivi, kama zitatindima risasi, zikavunja viuno na miguu ya waandamanaji au hata kuua, je ili kuzuia hayo tufanyeje? Tufanye nini? Majibu yanayonijia kichwani yananiongezea ugumu wa kufikiri na hata pengine kuishi katika Tanzania hii ndani ya mwezi huu wa August!

Je, ili watu wasijeruhiwa au kuuawa siku hiyo tumshauri Rais Magufuli na serikali kwa jumla iwaachie CHADEMA watimize haki yao ya kikatiba? Au tuwaambie CHADEMA waachane na mpango wao wa 'kujenga ukuta' ili kutii amri ya Rais Magufuli?

Nani yuko tayari kati ya 'miamba' hii miwili hapa kumuacha mwenzake apate akitakacho? Au kila mmoja hataki kuonekana ameshindwa? Lakini kushindwa huku ni kwa manufaa ya nani? Kama kushindwa kwa mmoja wapo kutalinda maslahi mapana ya Taifa na raia wake, kuna ubaya gani?

Hata hivyo nisijikite sana huko, sio mjadala wa leo hapa. Kitu ninachotaka kueleza na pengine kutoa ushauri ikiwezekana ni juu yangu kwa Watumishi wa Mungu hapa nchini. Na kila mmoja anaweza kuwa Mtumishi wa Mungu kwa nafasi yake, kama vile madaktari, Polisi, idara ya Usalama wa Taifa, madereva nk, ili mradi wanajihusha na kuwahudumia wananchi kwa namna moja au nyingine.

Nikiwa nchini India mwaka 2013 nilibahatika kukutana na Mtu mmoja anayeheshimika sana nchini humo, hasa jamii ya masikini au tabaka la chini, BINDESHWAR PATHAK, alisema hivi "namna nzuri zaidi ya kumtumikia Mungu ni kuwatumikia watu wake", ndio maana naamini hata Rais kwa nafasi yake ni Mtumishi wa Mungu.

Lakini Watumishi ninawajadili hapa ni wale ambao wako kwenye nafasi za uongozi wa kidini, labda makanisani au misikitini. Taja Wachungaji, Maaskofu, Masheikh nk! Hawa nawaona kama wako katika kipindi kizito cha majaribu, kujaribiwa imani zao kupitia sakata hili linaloendelea. Nadhani wako kwenye majaribu bila hata wao wenyewe kujua kuwa wako majaribuni! 

Kinachowaweka majaribuni zaidi ni masimamo wa CHADEMA na msimamo wa serikali kupitia Rais, Jeshi la polisi, wakuu wa mikoa na wakuu wa Wilaya katika maeneo ambako 'utajengwa ukuta'.

KWA NINI? Nimeona kwenye mitandao Watumishi wa Mungu hasa Wachungaji na Wainjilisti wakitoa maoni ya na kujadili sakata hili. Hapa ninapozungumzia 'sakata' nalenga kusema msimamo wa Rais na msimamo wa serikali kuhusu UKUTA!

Ninadiriki kusema kwamba wako majaribuni kwa sababu wengi wamefeli kabisa kuacha kuwa na upande katika hilo. Wanatoa maoni na ushauri huku wakionekana kabisa kuwa na upande kati ya serikali na CHADEMA. Lakini mbaya zaidi ni pale ambapo tunajikuta tunaitumikia hofu ya Rais tukidhani tunadumisha amani katika nchi huku tukiacha makovu katika mioyo ya wale ambao tunawaongoza, na wakati mwingine tunaunga mkono CHADEMA tukidhani tumesimamia haki kumbe tunajiingiza matatizoni kwa kuwa hatuna hoja za maana tukipimwa!

NATAKA KUSEMA NINI: Kama Watumishi wa Mungu wanajipa jukumu la kuleta utatuzi katika nchi hii au kusuluhisha migogoro ya kisiasa hapa nchini wahakikishe kwamba dhamiri zao zinawashuhudia kwamba hawana upande katika pande mbili zinazopingana. Wahakikishe mioyoni mwao wanamuogopa MUNGU PEKE YAKE na sio Rais, viongozi wa vyama siasa au wananchi.

Kama katika sakata hili Rais ana makosa aambiwe, ashauriwe, arekebishwe, kwa sababu ni mwanadamu, anaweza kughafilika. Kumpigia makofi hata anapoteleza na kuteleza kwake kukatishia amani ya nchi, hatumtendei haki Rais, hatulitendei haki taifa wala hatuzitendei haki huduma na dhamana alizotupa Mungu!

Katika kusuluhisha au kupendekeza njia za utatuzi tusifanye hivyo kwa kujipendekeza kwa Rais au idara zingine za ulinzi na usalama wa nchi yetu. Tusijipendekeze kwao, hata wao wanapenda watu watakaowashauri ukweli kwa upendo na unyenyekevu, wanapenda kupata njia bora za kulitunza taifa ili lidumu katika amani. Wao sio Miungu kwamba hawakosei na kughafilika, ndio maana wanahitaji kushauriwa lakini sio kubezwa au kutukanwa

Viongozi wa dini kwa ujumla tunapoishauri serikali tusiishauri kwa kutaka sifa, tunapomshauri Rais au Waziri Mkuu tusifanye hivyo kwa hila, tufanye hivyo kwa maslahi ya nchi. Wanapoteleza na kughafilika kama wanadamu wasaidiwe, na ukweli peke yake ndio utakaowasaidia viongozi wetu kudumu katika njia salama ya kutupeleka kule tunakotaka. Tusiwaharibu viongozi wetu kwa kuwapamba hata wanapokosea, tujitofautishe!

Kwa mfano, Mkuu wangu mkoa wa Dar es salaam amewaambia polisi wakikutana na wahalifu huko porini wawapige risasi. Kwa kauli hii hatupaswi kumpigia makofi Mkuu wetu (MAKONDA), tumwambie mheshimiwa ulighafilika, na sababu zipo. Moja wapo ni hii, je, kila aliye porini ni mhalifu?, mtu akikutwa porini saa ngapi anakuwa amethibitika kuwa ni mhalifu? Wawakute tu watu porini wawapige risasi? Hapana, tumshauri na kumkumbusha yale ya vijana wafanyabiashara waliuwawa Sinza wakidhaniwa kuwa ni majambazi!

Katika hili la UKUTA, nimemsikia Mtumishi mmona wa Mungu, rafiki yangu kwenye mitandao amesema UKUTA ni mpango wa shetani. Ameandika hadharani, sijui hakusema ni mpango wa Mungu au ni mpango wa wanadamu. Hakujenga hoja yoyote kuthibitisha madai yake zaidi ya kutoa wito kwa watu kuwa waombee amani. 

Katika kizazi hiki cha watu wadadisi, wachokonozi na wanaohoji huwezi kueleta madai mazito kama haya na kuishia hewani kiasi hicho. Na ieleweke kwamba sitetei UKUTA hapa, nasisitiza kwamba tunapoamua kutoa ushauri kwa minajili ya kuleta amani tusifanye kwa kufurahisha upande fulani, haitatusaidia, tunapaswa kusimama kwenye ukweli!

Na zaidi ya yote tunapaswa kutafakari na kuzipima kauli zetu, iwe tunapingana na msimamo wa serikali au msimamo wa UKUTA, tuseme ukweli, tusiingie kwenye mkumbo wa ushabiki badala ya kutengeneza. Ngoja nitoe mfano juu ya hoja hii ya madai kuwa UKUTA ni ushetani!

Hawa jamaa wanataka kuandamana, Rais amewakataza, tujadili. Rais ndiye kiongozi mkuu wa nchi yetu, amewekwa kwa mujibu wa Katiba, aliapa kuilinda Katiba. Katiba hii inaweka mwanzo na mwisho wa mipaka ya Rais wetu, alipoamba kulinda maana yake aliapa kuishi na kutenda ndani ya mipaka aliyopewa na Katiba. 

CHADEMA wanadai kuwa ni katiba hiiminayowapa wananchi haki ya kuandamana, vyama vya siasa vina haki pia ya kikatiba ya kufanya mikutano na bila shaka hata maandamano. Rais amewakataza, CHADEMA wanasema kukataza huku ni kinyume cha matakwa ya KATIBA. 

Kama ndivyo ilivyo, na kama katiba inaruhusu maandamano, watumishi wasiite maandamano kuwa ni ushetani mpaka itakapothibitishwa kuwa amri ya Rais haijaathiri wala kwenda kinyume na katiba ya nchi yetu. Na ikithibitika kuwa aliteleza ashauriwe kwa upendo wa dhati kabisa kwamba "MHESHIMIWA RAIS, PALE ULIGHAFILIKA" Sio kumuunga mkono ili kujipendekeza kwake, nadhani hata Rais Magufuli mwenyewe asingependa aina hii ya VIONGOZI WA DINI kulingana na dhamira njema aliyonayo kwa nchi hii!

Badala yake tungeweza kumshauri Rais kwamba ili kusiwepo mikutano ya kisiasa nchini mpaka wakati wa uchaguzi, angeweza kuandaa muswada na kuupeleka Bungeni utakaopendekeza jambo hili na litungiwe sheria. Kuna ubaya gani kumshauri Rais namna hii kuliko kumuunga mkono kwa uongo ili ionekane kuwa mko upande wake, narudia tena, nadhani hata Rais asingefurahi aina hii ya washauri, vinginevyo tunyamaze, tumsaidie kwa kumuombea tu!

Kwa upande wa pili kama tunataka kushauri na kuleta suluhu, badala ya kubeza kauli za Rais, hata kama kweli amekosea, kwa nini kama tunashindwa kumkabili Rais tusiende kuzungumza na viongozi wa UKUTA ikiwezekana waahirishe kwa muda au watafute namna nyingine ya kufikisha wao kwa serikali na dunia kwa ujumla?

Twende tuwaambie ukweli kwamba wanakosea kufanya maandamano, lakini ikithibitika kuwa wana haki ya kikatiba tuwashauri kama ninavyopendekeza hapo juu. Kuwabeza, kuwatukana na kuwakejeli ili kufurahisha upande mwingine hakuwezi kuleta matokeo tarajiwa ambayo ni amani na utulivu, wao wanasema wana haki, ni sawa, lakini waangalie, kwa ajili usalama wa Watanzania watiifu kwao walitazame hili mara mbili na kuona kuwa pengine kuahirisha mpango wao ni salama zaidi kuliko kuendelea nao.

Yeyote atakayetusikiliza kati ya hao, au atakayetupuuza kazi yetu inakuwa imeishia hapo, mengine kulingana na nafasi zetu tunamwachia Mungu, wananchi na wao kuamua. Lakini sio kukubali kuingia kwenye jaribu la kutumika na upande mmoja wapo bila kujijua. Makanisani mwetu na kwenye misikiti tuna watu wa serikali, chama tawala na vyama vya upinzani, tuna wanaharakati mbalimbali, raia wa kawaida nk. Wote tunapaswa kuwalea bila kujeruhi nafsi zao kwa kauli zetu na misimamo yetu, Tutoe maoni, tushauri, tupendekeze, tukosoe na kupongeza, lakini tusitumikie yeyote kisiasa.

SIASA NI JARIBU KUBWA WA VIONGOZI WA DINI, TULISHINDE! 

MCH. OVERCOMER DANIEL
KANISA LA EAGT
DAR ES SALAAM
Simu ya kiganja: +255 672 663 482


No comments: