‘Rais Kikwete hakumtetea Chitalilo’
RAIS Jakaya Kikwete, hakumtetea Mbunge wa Buchosa, Samuel Chitalilo (CCM), anayekabiliwa na tuhuma za kudanganya kuhusu kiwango chake cha elimu, imeelezwa.
Akizungumza na Tanzania Daima kwa simu kutoka Mwanza jana, Mwandishi wa Habari Msaidizi wa Rais, Premmy Kibanga, alisema alichokizungumzia rais wakati akiwa jimboni Buchosa ni hoja za kishindani zilizojitokeza wakati wa Uchaguzi Mkuu wa mwaka juzi.
“Ile haikuwa tafsiri sahihi. Rais aliposema kuhusu kelele za mlango hazimfanyi mwenye nyumba akose usingizi, alikuwa akizungumzia msigano uliokuwapo Buchosa mwaka 2005 wakati wa Uchaguzi Mkuu.
“Rais anafahamu vyema mwenendo wa mambo kisheria na mara kadhaa amekuwa akikataa kuzungumzia masuala yaliyoko mahakamani. Na alichokisema akiwa Buchosa ni kuwahakikishia wananchi wa jimbo hilo kuwa pamoja na mambo yote hayo, CCM na Serikali vitaendelea kuwatumikia kwa uaminifu,” alisema Kibanga.
Ufafanuzi huo umehitimisha utata uliojitokeza baada ya vyombo kadhaa vya habari juzi (si Tanzania Daima), kumkariri Rais Kikwete akimtetea Chitalilo ambaye shauri lake la kudanganya kuhusu elimu yake bado halijapatiwa ufumbuzi wa kimahakama.
Utata kuhusu kauli hiyo ya Rais ambayo sasa inaonekana kuwa ilitafsiriwa vibaya, ulisababisha vyama viwili vya siasa, Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) na Chama cha Wananchi (CUF) kueleza kushangazwa na huo ulioonekana kuwa msimamo wa Rais Kikwete.
Kibanga katika ufafanuzi wake huo alisema, alichofanya Rais kilikuwa ni kuwataka wananchi wa jimbo hilo kuendelea na shughuli zao kama kawaida, huku wakijua kwamba, serikali yake ilikuwa inatambua wajibu wake wa kuwahudumia pamoja na kuwapo kwa matatizo kadhaa.
Habari zaidi kutoka Mwanza aliko Rais zinaeleza kwamba, Rais alitoa kauli hiyo kutokana na kuwapo kwa maneno mengi yaliyokuwa yakidai kuwa Chitalilo alikuwa hakubaliki jimboni mwake na kwamba kulikuwa na uwezekano mkubwa wa kushindwa.
“Mwaka 2005 kulikuwa na upinzani mkali Buchosa na kulikuwa na taarifa zilizokuwa zikidai kwamba, kwa sababu ya kutokubalika kwake Chitalilo angeshindwa. Ndiyo maana Rais aliwashukuru wananchi kwa kumchagua yeye na mbunge wao pamoja na kuwapo kwa wasiwasi huo wa kushindwa,” alisema ofisa mmoja serikalini aliye katika msafara wa Rais ambaye hakutaka jina lake liandikwe gazetini.
Imepostiwa na Tausi A. Makame: tausi@online.no
Chanzo cha habari: Tanzania Daima mtandaoni, Jumatano, 9.5.2007
No comments:
Post a Comment