Revocatus Makaranga, Dodoma
HabariLeo; Thursday,June 14, 2007 @00:04
SUALA la kama Jeshi la Kujenga Taifa ni chombo cha Mwungano au la, lilisababisha mjadala mkali bungeni jana. Hali hiyo ilijitokeza baada ya Naibu Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Omar Yussuf Mzee na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Johnson Mwanyika kusema kuwa JKT si sehemu ya Mwungano. Naibu Waziri na Mwanasheria Mkuu wa Serikali waliyasema hayo walipokuwa wakijibu na kutoa ufafanuzi wa maswali ya nyongeza ya baadhi ya wabunge yaliyotokana na swali la msingi la Mbunge wa Viti Maalum, Mwajuma Hassan Khamis. Mjadala ulianza baada ya Mbunge wa Ziwani, Ali Said Salum –CUF kusema kuwa hakuwa na sababu na kuwa na vyombo viwili vinavyofanya kazi moja yaani Jeshi la Kujenga Uchumi Zanzibar na Jeshi la Kujenga Taifa Tanzania Bara. Mbunge huyo ambaye alikuwa akiuliza swali la nyongeza alipendekeza JKU ifutwe ili ibakie JKT tu ambacho alisema ni chombo cha Mwungano.. Akimjibu, Naibu Waziri, Omar alisema kwa kuwa JKU iliundwa kwa mujiubu wa sheria iliyotungwa na Baraza la Wawakilishi na JKT iliundwa kwa mujibu wa sheria iliyotungwa na Bunge la Muungano, chombo chenye mamlaka ya kuifuta JKU ni Baraza la Wawakilishi. Naibu Waziri alimweleza Mbunge huyo kuwa JKT si chombo cha Mwungano kama aanavyofikiri Mbunge huyo, ingawa ina sura ya kitaifa. Alisema Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ndicho chombo cha Mwungano. Kutokana na majibu hayo, Kiongozi wa Upinzani bungeni, Hamad Rashid Mohamed alisimama na kusema kwamba inakuwaje JKT isiwe sehemu ya Mwungano wakati ni sehemu ya JWTZ ambacho ni chombo cha Mwungano. Hata hivyo, Naibu Waziri alizidi kusisitiza kuwa JKT si chombo cha Mwungano ingawa Wazanzibari nao wana haki ya kujiunga na JKT kwa vile ni Watanzania. Lakini wakati Naibu Spika, Anna Makinda alipokuwa akitoa matangazo kwa ajili ya kuahirisha kikao cha Bunge baada ya muda wa maswali kumalizika, Mbunge wa Bariadi Mashariki, John Cheyo –UDP aliamka na kuomba ufafanuzi kuhusu matamshi ya Naibu Waziri kuwa JKT si chombo cha Mwungano. Cheyo alisema matamshi hayo ya Naibu waziri yanaleta wasiwasi kwa Watanzania wengi kwa vile hata yeye alikuwa anafahamu kuwa ni chombo cha Mwungano kwa sababu ni sehemu ya JWTZ. “…Wengine imetupa wasiwasi kwa Wazanzibari wanaweza wasiitambue JKT…tunaomba kpata ufafanuzi,” alisema. Alisema tafsiri ya Ibara ya 147 ya Katiba ya Jamhuri ya Mwungano inaonyesha kuwa JKT ni sehemu ya JWTZ ambacho ni chombo cha Mwungano hivyo JKT ni sehemu ya Mwungano. Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Mnyika akitoa ufafanuzi alisisitiza kuwa JKT si chombo cha Mwungano. Alisema Ibara ya 147 ya Katiba inahusu vyombo ambavyo si vya Mwungano na kwamba Wazanzibari wanaingia katika JKT kwa vile ni Watanzania na JKT ni chombo cha Watanzania. Majibu hayo ya Mwanyika yalisababisha Wabunge wengi kuguna na wengine kuamka wakitaka kuendeleza mjadala lakini Naibu Spika alisema suala hilo halikuhitaji mjadala zaidi na akaahirisha kikao cha Bunge hadi leo asubuhi. Awali, Naibu Waziri alisema kuwa tangu JKT irejeshwe mwaka 2001 imekwisha kupkea vijana 370 ktuoka Zanzibar na kuwa mwaka 2006/07 ilichukua vijana 260 kutoka Zanzibar katika operesheni Maisha Bora. Naibu Waziri alikuwa akimjibu Mbunge wa Viti Maalum, Mwajuma Hassan Khamis aliyetaka kujua vijana kutoka Zanzibar walioingia JKT tangu irejeshwe. Soma kuhusu hili kutoka Tanzania Daima: http://www.freemedia.co.tz/daima/2007/6/14/habari2.php | |
No comments:
Post a Comment