Na Salma Said, Zanzibar
___________________
POLISI Mkoa wa Kusini Unguja wamemsimamisha kazi askari polisi Pandu Ndame baada ya kutuhumiwa kumbaka mwanafunzi katika kituo cha Polisi Chwaka. Mwanafunzi huyo alifikishwa na mwenzake katika kituo hicho baada ya kubakwa na watu wasiojulikana wakati wakitafuta kuni katika Msitu wa Pongwe, mbali kidogo na wanapoishi.
Kaimu Kamanda wa Polisi Mkoa Kusini Unguja, Khamis Ramadhan, alithibitisha kutokea kwa tukio hilo na tayari polisi wanaendelea na uchunguzi kabla ya kufikisha katika vyombo vya sheria. Akielezea tukio hilo, Kamanda huyo alisema wasichana hao wawili wiki iliyopita waliondoka nyumbani kwao majira ya saa 11.00 jioni kwenda kutafuta kuni, lakini hawakurejea hadi saa moja usiku.
Alisema kitendo hicho kiliwatia wasiwasi wazazi wao na kuamua kuwatafuta na baada ya kuwapata, wasichana hao walisema wamekumbana na mkasa mkubwa wakati wakitafuta kuni msituni. Ramadhan alisema waliamua kuwapeleka katika kituo cha Chwaka ili uchunguzi uweze kufanyika na kuwatafuta watu waliowabaka katika msitu wa Pongwe.
Alisema askari waliokuwepo kituoni walichukua maelezo na baadaye kuongozana na wazazi na askari kwenda kuwasaka wahalifu msituni, lakini hawakufanikiwa kuwapata. Hata hivyo alisema wakati wasichana hao wamebaki kituoni, askari Ndame aliwageukia na kufanikiwa kumbaka mmoja wao ndani ya kituo cha polisi na ndio maana wameamua kumsimamisha kazi ili kutoa nafasi ya uchunguzi zaidi. Tulipopokea taarifa hizi tuliamua kuzifanyia uchunguzi haraka kwa kuzingatia uzito wake na sehemu lililofanyika tendo hilo,? alisema Kamanda huyo. Alisema kwamba hivi sasa polisi wanasubiri ripoti ya daktari kabla ya kuchukua hatua nyingine za kisheria.
Habari kutoka katika eneo la tukio zinasema kwamba tukio hilo limezusha mjadala mkubwa katika Kijiji cha Chwaka na Pongwe kwa vile ni tukio la kwanza kutokea kwa msichana kubakwa ndani ya kituo cha Polisi. Taarifa zaidi zinasema kuwa baada ya wazazi kurejea kutoka msituni wakiwa na askari, msichana huyo aliwashangaza wazazi wake pale alipowahoji kwa nini wanahangaika kuwatafuta watu waliofanya mchezo mbaya wakati hapo walipo kituoni tayari wamefanyiwa mchezo kama huo.
Baada ya kauli ya msichana huyo, hali ilichafuka kituoni hapo kati ya askari na wazazi wa wasichana hao na kusababisha baadhi ya wananchi kutoka katika Kijiji cha Pongwe kufika katika kituo hicho kushuhudia kilichotokea. Hata hivyo hali ilikuwa ya utulivu baada ya Mkuu wa Wilaya, Ali Hassan Khamis, kuingilia kati suala hilo na kujaribu kuwatuliza wazazi wa watoto hao.
Hivi karibuni Waziri wa Kazi, Maendeleo ya Vijana, Wanawake na Watoto, Asha Abdallah Juma akiwasilisha Bajeti ya wizara yake ya mwaka wa fedha 2007/2008 katika Baraza la Wawalikilishi aliwaeleza wajumbe kwamba vitendo vya ubakaji vimekuwa vikiongezeka visiwani Zanzibar ambapo mwaka uliopita jumla ya kesi 39 za ubakaji ziliripotiwa katika vituo mbali mbali vya polisi.
Hivi karibuni Askari Magereza Hijja Mchwao alifunguliwa mashitaka katika kituo cha Polisi Madema baada ya kutuhumiwa kumtorosha mwanafunzi wa kidato cha tatu katika
shule ya Moshi na kumuweka kinyumba katika Mtaa wa Miembeni. Askari huyo tayari amefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kumtorosha mwanfunzi bila ya ridhaa ya wazazi wake na baadaye ya kumbadilisha dini kutoka kwenye Ukiristo na kuwa muislamu.
shule ya Moshi na kumuweka kinyumba katika Mtaa wa Miembeni. Askari huyo tayari amefikishwa mahakamani na kusomewa mashitaka ya kumtorosha mwanfunzi bila ya ridhaa ya wazazi wake na baadaye ya kumbadilisha dini kutoka kwenye Ukiristo na kuwa muislamu.
Mwanafunzi huyo hivi sasa amerejeshwa Dar es Salaam baada ya mahakama kuamuru mwanafunzi huyo arejeshwe kwa wazazi wake kwa vile alisilimishwa na kuozeshwa bila ridhaa yao
Chanzo: Gazeti la Mwananchi, Jumatano, Agosti 15, 2007.
No comments:
Post a Comment