Tuesday, August 14, 2007

Kiswahili Sanifu Waandishi wa habari wanabananga Kiswahili


Barnabas Maro
_________________________

LUGHA ya Kiswahili imepewa nafasi ya sita kwa umaarufu duniani. Pamoja na heshima hii kuidondokea Tanzania, tumeshindwa kabisa kuienzi lugha hii azizi inayowaunganisha Watanzania milioni 37 wa makabila 120 na lugha zaidi ya makabila hayo. Leo popote uendapo Tanzania waweza kuwasiliana na mtu wa kabila lolote bila wasiwasi.

Kwa mshangao, vyombo vya habari badala ya kuwa kioo cha jamii vimekuwa sumu inayoiua taratibu lugha hii. Maneno yanayotumiwa na magazeti, redio na televisheni yanabanangwa mno kiasi cha kutia shaka kama kweli Kiswahili ni lugha ya taifa. Maneno yanayotumiwa katika habari, makala na maelezo ya picha ni tofauti mno na unenaji wa lugha.

Maneno yanayochanganywa sana, tena kila siku ni "ushauri nasaha". Nadhani maneno haya mawili hutumiwa kwa maana ya kutia msisitizo katika "ushauri" bila kujua kuwa maneno hayo yana maana ileile.

"Ushauri" maana yake ni nasaha, rai, wazo, pendekezo, aso, elekezo, kauli, neno, bamba au tamko. Tunatambua sasa kuwa ushauri maana yake ni nasaha. Kwa hiyo unaposema "ushauri nasaha" ni sawa kabisa na kusema "ushauri ushauri!" Waweza kumwambia mtu "njoo nikupe ushauri" au "njoo nikushauri" ama "ushauri wangu ni …" pia "nakushauri …"

Nasaha maana yake ni mawaidha, shauri, mwongozo, ibra, maelezo, rai, pendekezo, waadhi, neno, wazo, fikira, gezo, elekezo, mgogoyo, ushauri, kauli au tamko. Ni muhali kutumia neno hili sanjari na "ushauri" kwani yote yana maana ile ile. Kama nilivyoainisha katika aya iliyoitangulia hii, ni kama kusema "nasaha nasaha" au kumwambia mtu njoo nikupe "nasaha nasaha", yaani kurejea neno lile lile kwa mfuatano.

Ni vema basi kusema "kumshauri" mtu, "kumnasihi", "nasihisha" au -pa mtu "nasaha". Ndugu zetu wa TACAIDS wameshauriwa mara nyingi kuhusu matumizi ya maneno hayo lakini bado wanaendelea kuyatumia kwenye maandishi na vipeperushi vinavyotawanywa kwa wananchi. Kama ni kutia msisitizo, isemwe "ushauri muhimu" yaani -enye maana, bora au -enye kutopuuzika. Wakishindwa hivyo waseme "ushauri mahususi" kwa maana ya halisi, maalumu, -a kutambulika, -a kujulikana.

Siku hizi (kama ni kile kisemwacho kukua kwa lugha, mimi sijui) kuna neno litumikalo isivyostahili ingawa linatamkwa kila siku na karibu kila mtu, wakubwa kwa wadogo. Neno hilo ni "hamna." Hebu fikiri unamwuliza mtu iwapo leo alikwenda sehemu fulani kisha akakujibu "hamna", utakuwa na mawazo gani?

"Hamna" ile sehemu au nini? Jibu sahihi hapa ni "hapana", ikimaanisha hukwenda kule ulikoulizwa na mwuliza swali. Lakini inasikitisha kuwa neno hilo sasa limeenea mno kiasi kwamba ni wengi sana wanapoulizwa jambo lolote husema "hamna" kwa maana ya kukataa badala ya neno halisi "hapana". Sasa hata watoto wadogo wameshikilia neno "hamna" badala ya "hapana". Kwa faida ya hao wanaolitumia neno hilo yafaa watambue kuwa "hamna" maana yake ni kutokuwemo kitu ndani ya; bila ya kuwemo kitu; mtupu; mweupe.

Kwa mujibu wa Mwalimu Mohamed Mwinyi wa Baraza la Kiswahili la Taifa (BAKITA), kikanushi "hamna" kimemeza vikanushi vyote. Kuna maswali mengine ya aina tofauti yanayoweza kupima nadharia hii. Kwa mfano: Je, jana ulikwenda shuleni? Baba yako analima shambani? Leo umekula nini? Ng'ombe wote wamerudi? Leo unaumwa?

Kwa maswali yote haya, kwa mujibu wa Mwalimu Mwinyi, angeulizwa mtu wa wilaya ya Iringa Vijijini au Mufindi na kama jibu ni kukanusha, maswali yote hayo angejibu "hamna". Kikanushi "hamna" kimechukua nafasi ya vikanushi vyote katika Kiswahili kwa watu wa wilaya hizo.

Hebu sasa tuangalie matumizi sahihi ya maneno "hapana", "hakuna" na "hamna". Kwanza kabisa maneno haya yanakataa au yanakanusha jambo fulani.

Tuanze na neno "hamna". Maana halisi ya neno hili ni kutokuwamo kitu ndani ya kitu fulani, bila ya kuwamo kitu au sehemu ambayo ni tupu au mtupu. Kikanushi "hamna" hakitumiki kujibu swali linalokanusha kuhusu uwezo wa kitu fulani ndani ya … Kwa mfano: Humo chumbani mna mtu? Ndani ya bakuli mna maji? Chunguni mna mboga?


Kwa maswali hayo hapo juu, kama ni kukanusha, basi jibu la swali la kwanza ama litakuwa "hamna" au "hamna" mtu. Katika swali la pili, jibu litakuwa ama "hamna" au "hamna" maji na swali la tatu jibu litakuwa ama "hamna" au "hamna" mboga.

Utoaji wa majibu ya kukanusha katika maswali hayo hapo juu, yaani swali la kwanza mpaka la tatu, unategemea namna yalivyoulizwa. Kwa mfano kama muulizaji angeweka neno "kuna" katika maswali haya, basi majibu yake yangebadilika.
Hebu sasa tuangalie maswali hayo tena: Je, kuna mtu chumbani? Ndani ya bakuli "kuna" maji? Chunguni kuna mboga?

Katika sehemu ya pili ya maswali unaweza kuona majibu yamebadilika kulingana na jinsi swali lilivyoulizwa. Kwa mfano swali la namba moja kama jibu ni kukanusha, basi linaweza kuwa ama "hakuna" au "hakuna" mtu. Hali kadhalika katika swali la pili na tatu. Hebu tuangalie matumizi halisi ya kikanushi "hapana". Neno hili linahitaji umakini katika kulitumia. Kabla ya kuangalia matumizi yake hebu kwanza tuangalie maana yake halisi. Kikanushi "hapana" ni neno la kukataa, siyo,na hutumika kwa maana ya kutoruhusu, kutoidhini. Tuangalie mifano ya maswali yafuatayo: Jana ulikuja shuleni? Je, leo unaumwa? Juma atakuja leo?

Kama jibu la maswali hayo hapo juu liko katika hali ya kukanusha, basi jibu litakuwa "hapana". Jibu hilo linaweza kuongezewa neno lingine mbele au ukaacha kama lilivyo kutegemeana na mazingira ya mzungumzaji. Kwa mfano katika swali namba moja jibu linaweza kuwa "hapana" au "hapana, sikuja. Katika maswali hayo hapo juu huwezi kutumia kikanushi kingine zaidi ya "hapana". Hata kama kitatumika kikanushi kingine ni vizuri zaidi kutanguliza kikanushi "hapana".

Mwalimu Mwinyi anahitimisha ufafanuzi wake kwa kutunasihi tuchunguze kwa makini jinsi swali lilivyoulizwa ndipo tutajua ni kikanushi gani kinafaa kutumika kujibu swali. Mfano unapotaka kutumia kikanushi "hamna" au "hakuna" lazima uangalie: Je, sentensi/swali hilo lina maneno "kuna" au "mna"? Iwapo swali hilo litakuwa na neno "mna", basi jibu la swali hilo litakuwa "hamna". Iwapo katika swali kuna neno "lipo", basi ujue wazi kwamba jibu la kukanusha litakuwa ama "hakuna" peke yake au "hakuna" pamoja na maneno mengine mbele.

Jamani, kama ni kukienzi Kiswahili, basi tutumie maneno yanayoeleweka badala ya kuyachanganya. Kwa mfano dada , kaka, mama, baba. Mara nyingi husikia watu wakisema "mdada" mmoja, "mkaka" mmoja.Kwa kweli huwa nakereka sana na kuanza kufikiri "mdada" au "mkaka" ni madubwana gani kumbe ni "dada" na "kaka"! Tangu lini dada akawa" mdada" na kaka kuwa" mkaka"? Nachukua nafasi hii kuwafahamisha hao wanaosema "mkaka" kuwa maana ya neno hilo ni mti wa porini wenye kiini cheusi na wenyewe ni mgumu sana. Kama ndivyo, iweje kaka afananishwe na mti?


Kadhalika hakuna wingi wa mama wala baba. Lakini imekuwa kawaida siku hizi kusikia watu (hasa ndugu zangu Wakristo) wakisema "wamama" au "wababa". Kwa kadiri ya welewa wangu mdogo hakuna maneno kama hayo katika msamiati wa Kiswahili. Ni vema basi watu wakatamka "akina mama" au "akina baba." Neno lingine nililolikuta kwenye msamiati wetu wa Kikristo ni "haijalishi". Mara nyingi wainjilishaji wanapohubiri hupenda sana kutumia neno hilo. Utasikia, kwa mfano, "Bwana Mungu anakupenda wewe jinsi ulivyo, haijalishi una dhambi kiasi gani …"

Waonaje kama ingesemwa: "Bwana Mungu anakupenda jinsi ulivyo, bila kujali dhambi ulizo nazo", au "Bwana Mungu anakupenda, haidhuru una dhambi kiasi gani" Wainjilishaji pamoja na watangazaji wa vituo vya redio za Wakristo hutangaza, kwa mfano, "sasa nitakwenda" au "nakwenda kuomba/kuimba." Wanaposema hivyo sio kama wanaondoka pale walipo, bali huwa palepale! Kwanini basi wasiseme "sasa nitaomba au nitaimba?" Kwa sababu kwenda ni kutoka eneo moja hadi jingine. Iweje basi mtu kusema anakwenda ilhali yuko palepale mimbarini?.

Wakatabahu

Marobarnabas@yahoo.com Simu 0756 855 314 au 0784 334 096.

Makala hii ilichapwa kwenye HabariLeo; Ijumaa ,August 10, 2007 @00:02

No comments: