*Awaita watatu tu wapya
*Kaseja, Athuman Iddi, Mgosi nje
Na Phillip Nkini
KOCHA Marcio Maximo juzi alitangaza kikosi cha wachezaji 23 kwa ajili ya ziara ya mazoezi nchini Dernmark na Uswisi, akiwa ameita sura mpya tatu na kuwaacha kipa Juma Kaseja, kiungo Athuman Iddi na mshambuliaji Mussa Hassan Mgosi.
Kikosi hicho kitakachoondoka mwishoni mwa wiki hii, kimeitwa kwa ajili ya ziara hiyo ya wiki mbili ya Denmark na Uswisi, mechi ya mwisho ya Mataifa ya Afrika dhidi ya Msumbiji utakaofanyika Septemba 8, mechi za Kombe la Chalenji na michuano ya awali ya Kombe la Dunia, alisema Maximo.
''Tanzania ilishawahi kuweka rekodi huko nyuma, lakini nina imani kwamba kwa kikosi hiki tunaweza kuweka historia nyingine," alisema kocha huyo Mbrazili.
"Wachezaji wengi ni vijana lakini nina imani nao wanaweza kufanya kile tunachotaka.
"Mechi ya Msumbiji si ya mwisho. Bado tuna mashindano mengi mbele yetu kwa hiyo tukimaliza mechi ya Msumbiji, tutakuwa na Kombe la Chalenji na Kombe la Dunia."
Maximo, ambaye alimtema Kaseja tangu mwezi Machi baada ya timu kurejea kutoka Dakar, ameendelea kumuamini kipa nambari moja, Ivo Mapunda, kipa wa pili kwa Kaseja, Ally Mustapha 'Barthez' na kumwita kipa mpya toka JKT Ruvu, Shaaban Dihule.
Hata hivyo, Maximo alisema kipa huyo mrefu wa JKT hatakwenda Ulaya, kama itakavyokuwa kwa beki Victor Costa, kwa kuwa anamuachia mtu wa kumpa mazoezi ya kupunguza uzito. Costa bado anauguza mguu.
Mabeki ni Shadrack Nsajigwa, Nadir Haroub 'Cannavaro', Amir Maftah (Yanga), Victor Costa (Simba), Salum Sued, Mecky Maxime, Meshack Abel (wote Mtibwa), Erasto Nyoni (Vital'O).
Mbrazil aliwataja viungo kuwa ni Shaaban Nditi, Nizar Khalfan (Mtibwa), Abdulkarim Amour (Ashanti), Henry Joseph (Simba).
Washambuliaji ni Haruna Moshi, Joseph Kaniki, Danny Mrwanda (Simba), Said Maulid, Abdi Kassim (wote Yanga), Maregesi Mwangwa (Kagera), Jerry Tegete, Kigi Makasi (wote Makongo).
Maximo hakutaka kuzungumzia wachezaji walioachwa, lakini akazungumza kwa ujumla kuwa tatizo kubwa lililosababisha wengi kuachwa ni utovu wa nidhamu.
''Natumia vitu vingi kuteua kikosi changu," alisema. "Kwanza nataka wachezaji wenye umri mdogo, pia naangalia uwajibikaji wake sio uwanjani tu bali hata nje ya uwanja, halafu nidhamu na pia naangalia mchezaji alipopata nafasi kwenye kikosi alifanya nini.
"Kwa hiyo kama mtu anajua mchezaji ni mzuri lakini hayupo kwenye kikosi hiki aangalie mambo hayo hapo.''
Alisema ziara ya Dernmark ni kwa ajili ya kupunguza ugumu wa mchezo dhidi ya Msumbiji kwani anajua kwamba ni timu ngumu na yenye wachezaji wengi nje ya nchi.
Kuhusu kumwita beki wa Yanga, Shadrack Nsajigwa, ambaye alionyeshwa kadi nyekundu katika mechi dhidi ya Burkina Faso, Maximo alisema amemuita ili ajifunze mambo mbali mbali kwa ajili ya soka la Tanzania la baadaye.
Stars inatakiwa ishinde mechi hiyo ya Msumbiji ili kuongeza uwezekano wa kufuzu kwenda Ghana kwenye fainali za Mataifa ya Afrika.
Chanzo cha habari gazeti la Mwananchi.
No comments:
Post a Comment