TAARIFA kwamba Serikali ipo kwenye mchakato wa kuzitafsiri baadhi ya sheria kutoka kwenye lugha ya Kiingereza kwenda Kiswahili, imetolewa katika wakati unaofaa.
Habari hizo zilitolewa na Waziri wa Sheria na Katiba, Dk Mary Nagu ambaye alisema Wizara yake imeanza kuzishughulikia sheria zinazoonekana ngumu zaidi na kadri uwezo utakaporuhusu zitaendelea kutafsiriwa nyingine.
Tunasema tamko hilo limetolewa katika muda unaofaa kwa kuzingatia kwamba licha ya miaka zaidi ya 45 ya uhuru, sheria nyingi nchini na ambazo ni muhimu, bado ziko katika Kiingereza.
Na hali hiyo iko hivyo, ingawa taifa linajivuna kuwa na Kiswahili kinachozungumzwa na wananchi wote na ambayo ni lugha ya taifa!
Tunaipongeza Wizara husika kwa kuona umuhimu wa kuziweka sheria hizo katika lugha ya taifa ambayo kama tulivyosema, ndiyo inazungumzwa na wananchi wengi.
Kutafsiriwa kwa sheria zetu siyo tu kutawasaidia wananchi wa kawaida, bali hata wasomi na wanataaluma kuweza kuzielewa na kuzifuata barabara sheria hizo.
Isitoshe ni hatua muhimu katika kuikuza lugha yetu ya Kiswahili ambayo (inashangaza) imekuwa ‘ikipigwa vita’ isitumike shuleni na vyuoni kama lugha ya kufundishia kwa kisingizio kuwa baadhi ya vitabu na nyaraka mbalimbali ni vigumu kutafsiriwa katika Kiswahili.
Sheria hizo zikitafsiriwa katika Kiswahili bila shaka zitaongeza mwamko na ari ya wananchi kuzisoma na kuzielewa na kwa hiyo kuondoa visingizio vya baadhi ya watu kutenda makosa wakidai kutokujua sheria inasemaje.
Ingawa sheria haitambui kama mtendaji kosa anaijua au haijui sheria, lakini itakuwa ni kuwatendea haki wananchi kwa kuwawekea sheria katika lugha rahisi na wanayoielewa.
Kwa maana hiyo tunapenda kuzishauri Wizara na taasisi mbalimbali, za umma na binafsi ziige mfano wa Wizara ya Sheria na Katiba kwa kushirikiana hata na Baraza la Kiswahili Tanzania (Bakita) kutafsiri nyaraka zao.
Matarajio ni kwamba yakiwapo mafanikio katika kutafsiri nyaraka mbalimbali kutoka Kiingereza kwenda Kiswahili – hasa sheria- taifa litakuwa limepiga hatua kubwa katika maendeleo na kuienzi na kuikuza lugha ya taifa ya Kiswahili.
No comments:
Post a Comment