Na Paulina David, Mwanza. Alhamisi 11. Oktoba 2007
MAHAKAMA ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Mwanza, imemuamuru Mmisionari wa Kanisa Katoliki, Raia wa Italia, Angelo au Yunus Santy (67), kuondoka nchini baada ya kupatikana na hatia ya kupiga picha chafu za wasichana wawili na kukutwa na sehemu za siri za bandia za kiume.
Amri hiyo ya mahakama imetolewa juzi na Hakimu Auginea Lujwahuka, baada ya raia huyo kupatikana na hatia ya makosa hayo.
Kabla ya Hakimu Lujwahuka kuamuru raia huyo kuondoka nchini, alihukumiwa kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini ya Sh300,000 baada ya kukiri makosa hayo.
Hakimu Lujwahuka alisema kuwa mshtakiwa huyo, amepatikana na hatia ya kutenda kosa la jinai kinyume cha Sheria ya Kujamiana ya mwaka 1998, hivyo atatumikia kifungo cha miaka mitano jela au kulipa faini hiyo.
Hakimu huyo alisema mbali na mahakama kutoa adhabu hiyo, raia huyo anatakiwa kuondoka nchini kwa makosa aliyofanya ambayo ni kukiuka sheria hiyo kwa mujibu wa katiba ya nchi.
Angelo alilipa faini ya Sh300,000 na Polisi kumkabidhi Idara ya Uhamiaji, Mkoa wa Mwanza kwa hatua za kumuondoa nchini.
Awali Mwendesha Mashtaka wa Polisi,Inspekta Msaidizi, Inongu Kimasa aliiambia mahakama kuwa Septemba 20, mwaka huu katika eneo la Unguja, mshtakiwa huyo alikutwa akipiga picha za ngono na wasichana wawili.
Inspekta Kimasa alisema raia huyo alikutwa chumba namba 2 cha Hoteli ya Paradise na wasichana hao akipiga nao picha hizo.
Alisema baada ya kufanyiwa upekuzi alikutwa na sehemu mbili za kiume za bandia.
Kwa mara ya kwanza, Mmisonari huyo alifikishwa mahakamani hapo Septemba 21, mwaka huu na kusomewa shtaka la kupiga picha hizo.
Hata hivyo, hakimu huyo aliamuru arudishwe polisi baada ya kubainika hakuwa ametoa maelezo ya kutosha kutokana na kutokujua lugha ya Kiingereza wala Kiswahili.
Kutokana na hali hiyo, polisi ililazimika kutafuta raia wa Italia kwa ajili ya kumhoji Angelo na kufafanua zaidi, kisha kumfikisha tena mahakamani ambako amehukumiwa na kulipa Sh300,000 na kisha kuamriwa kuondoka nchini.
No comments:
Post a Comment