Sunday, October 07, 2007



Picha kutoka: City of Bergen



*Alikwenda kwa shughuli za sanaa, hakurudi akaolewa huko huko

*Bado anaenzi nyumbani, amejenga shule ya msingi kwao Singida

Na Rashid Kejo

MARA baada ya Richa Adhia kutangazwa kuwa Mrembo wa Tanzania mwaka huu, mengi yalisemwa kumhusu na zaidi yalijielekeza katika misingi ya asili yake. Wapo waliopinga kwa kuwa tu ana asili ya Kihindi!

Licha ya maelezo ya mrembo huyo kwamba ni mzawa kwa maana ya kuzaliwa na kukulia Tanzania, mjadala mkubwa ulitawala na kubeba hisia za kibaguzi.

Lakini kwa baadhi ya mataifa, suala la asili au rangi halina nafasi tena. Mengi hivi sasa yanajikita katika kuvuna rasilimali watu kwa maslahi ya taifa.

Zipo habari za wataalam wengi wa nchi maskini hasa za Afrika kuchukuliwa kwenda kufanya kazi nje ya bara hili hususan Ulaya na Marekani na baadhi au wengi wao huishia kuyakana mataifa yao hasa yale ambayo bado yanakumbatia mfumo wa uraia wa nchi moja kama Tanzania.

Chiku Mkalu Ali, ni mmoja wao. Huyu ni Diwani katika Jimbo la Bergen nchini Norway. Kwa kauli yake, yeye ni Mwafrika, bila shaka kutoka Tanzania, wa kwanza kuingia katika Baraza la Manispaa ya Bergen na pengine Norway nzima.

"Nimekuwa Diwani wa Bergen tangu mwaka 1995 na hivi majuzi tu Septemba 10, mwaka huu nimechaguliwa tena," anasema na akaongeza kwamba amepata nafasi hiyo kupitia Chama cha Red ambacho ni moja ya vyama vidogo nchini humo lakini chenye mwelekeo wa kutetea masilahi ya wanyonge," anasema katika mahojiano yaliyofanyika hivi karibuni Dar es Salaam.

"Chama chetu ni cha watu wa chini, ni chama cha watu, kinatetea masilahi ya wanyonge kama walemavu, wazee na watu wengine wasiojiweza ingawa kule hakuna masikini.

Mambo ya msingi tunayosimamia ni kama kuhakikisha kwamba watoto wote wanapata haki ya kwenda chekechea. Kulea ni ghali hasa kwa wakimbizi kuweza kumudu gharama. Sasa hii ndiyo nguzo ya elimu kwa mtoto akiikosa anaweza kupoteza mwelekeo wa maisha yake.

Pia ninatetea masilahi ya wazee. Kule wazee wanaishi katika nyumba zao maalum sasa utakuta wanasauhaulika, hawapati fursa ya kujumuika katika shughuli mbalimbali. Jambo jingine ninaloshughulikia ni programu kwa watu walioathirika kwa matumizi ya dawa za kulevya," anafafanua mama huyo.

Tofauti na mfumo wa madiwani nchini, Chiku anasema kwamba Baraza lao lina wajumbe 67 wanaochaguliwa katika jimbo tofauti na mfumo wa kata.

Mchango wa vyombo vya habari

Aliwezaje kufika ngazi hiyo ilhali ni mtu mweusi katika taifa la weupe? "Sikupata matatizo ya ubaguzi. Nilibebwa na media (vyombo vya habari)," anaeleza.

Umaarufu wa Chiku unatokana na kazi zake za sanaa na ndizo hizo hizo zilizomlazimisha kuchukua uraia wa Norway mwaka 1995 kama anavyosimulia kwa majonzi: "Nilichaguliwa kwenda China katika Mkutano wa Wanawake Duniani wa Beijing. Kule nilitakiwa kwenda kucheza mchezo wangu ambao niliuita My 10th calabash (Kibuyu changu cha 10). Ulikuwa mchezo wa kutetea mambo ya ukeketaji ambayo ndiyo ninayojishughulisha zaidi nayo, anaeleza.

Sasa nilipoomba viza ya kuingia China kwa hati ya Tanzania niliambiwa nisubiri kwa miezi mitatu jambo ambalo lingeninyima fursa ya kwenda huko. Hivyo nililazimika kuomba uraia wa Norway ambao nilipewa katika muda wa wiki moja tu na kupata viza ya kwenda China.

Lakini mimi najihesabu pia kama Mtanzania na ndiyo maana ninasaidia mambo mengi katika nchi yangu. Na mimi na mume wangu siku moja tutarudi kuishi Tanzania," anasisitiza.

Hivi karibuni Chiku alikuwa kijijini alikozaliwa Samumba Ikungi, Singida ambako anajenga shule ya msingi na kwa mujibu wa maelezo yake, inakaribia kumalizika: "Madarasa manne tayari pamoja na vyoo viwili na nyumba mbili za walimu. Hadi sasa imeshanigharimu Sh 25 milioni, anasema.

Kilichonisukuma kujenga shule ni kuwaokoa watoto na hatari mbalimbali. Hivi sasa wanalazimika kutembea saa mbili kufika shuleni, huko njiani kuna hatari nyingi za wanyama na kubakwa.

Lakini pia ninajenga kisima. Kule kuna shida kubwa ya maji lengo langu ni kuwaokoa watoto dhidi ya ukeketaji. Unajua kutokana na uhaba wa maji watoto wengi hawasafishwi vema na ndiyo maana wanapata maambukizo na wazee hudhani kwamba ni sababu ya kutokeketwa.

Si kwetu Singida tu. Mimi ni mtetezi wa haki za wanawake na kule Norway tuna chama kinachoitwa Wanawake Mbele (Kvinnefronten) ambacho kinasaidia Kikundi cha Kupambana dhidi ya Ukimwi Kilimanjaro (Kiwakuki) na tunakisaidia kikundi cha Wanawake Chole Mafia ambacho tumekijengea chekechea, kituo cha afya na wadi ya wazazi. Pia tumewapeleka watoto wao katika mafunzi ya majahazi na kuwasomesha watoto wa kike."

Alivyokwenda Norway

Mbali ya kumsababishia kuutema uraia wa Tanzania, sanaa hiyo hiyo ndiyo chanzo cha maisha yake huko Norway.

Mwaka 1984, akiwa mtumishi wa Serikali wakati huo, Chiku akishirikiana na wenzake watatu, Freddy Macha, George Chioko na Patrick (sasa Nasibu) Mwanukuzi "Ras Nas" walianzisha kikundi cha mtaani ambacho kilikuwa kinatoa burudani ya muziki wa asili lakini kitaalam zaidi.

Kikundi hicho kilikuwa kikifanya maonyesho yake bure katika mwembe uliopo nje ya Kijiji cha Makumbusho Kijitonyama, Dar es Salaam na katika Pwani ya Msasani.

"Kila mtu alikuwa na kazi yake. Kwa hiyo kikundi kile kilikuwa kwa ajili ya kutoa ujumbe na kuendeleza utamaduni wetu. Nakumbuka tulikuwa na nyimbo zilizozungumzia vifo vya wanafunzi wa kike wanaotoa mimba, wanawake kukaa majumbani na kunyanyaswa, anaeleza.

Baadaye taasisi ya Ujerumani ya Goethe Institute ilituona na kutuomba tufanye mazoezi katika ofisi zao. Hapo tukaanza kuandikwa na kutangazwa sana katika vyombo vya habari.

Lakini kama kawaida tulikuwa tunakwenda Makumbusho kuburudisha. Nakumbuka Jumamosi moja tulipokuwa tukifanya kazi zetu pale, kundi la wazungu ambao baadaye tulikuja kujua kwamba ni la kampuni ya NORAD ya Norway, lilipita na walisimama kutuangalia muda wote wa onyesho letu la saa tatu.

Baada ya kumaliza wakatutaka tuwape anuani zetu. Fred akawapa kwa niaba yetu. Hiyo ilikuwa Machi 1984, miezi mitatu baadaye nakumbuka Juni 13, 1984 tukaletewa barua ya mwaliko kushiriki katika tamasha la miezi mitatu Norway.

Nilisindikizwa na viongozi wangu wa Wizara ya Utamaduni na Vijana hadi Uwanja wa Ndege. Nikiwa huko tulitembelea katika Mji wa Bergen ambako nikutana na Steinar Eide na tukapendana."

Baada ya kumalizika kwa ziara hiyo Chiku hakurejea na wenzake, badala yake alikwenda kwa mume wake... "Lakini sikuishi naye hivi hivi tu. Tulifunga ndoa kwa idhini ya ubalozi wetu kwa kuwa mimi nilikuwa Mtanzania na mtumishi wa Serikali. Hata hivyo, mwaka 1993 tuliachana naye," anafafanua.

Hivi sasa Chiku ameolewa na Dk Bjorn Blomberg ambaye anasema ni mwenyeji wa Tanzania kwani ameshawahi kufanya kazi katika Hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Ushiriki katika sanaa

Chiku ambaye alizaliwa Machi 18, 1958 aliingia katika ulimwengu wa sanaa kama masihara

Alikuwa akipenda kucheza ngoma na maigizo mambo ambayo alikuwa akiyafanya sambamba na masomo yake. Baada ya kumaliza elimu yake ya sekondari katika Shule ya Tumaini mwaka 1976, anakumbuka Mkuu wa Mkoa wa Singida wakati huo, marehemu Moses Nnauye alikuwa akisaka vijana wenye vipaji katika sanaa.

"Katika Mkoa wa Singida nilichanguliwa mimi peke yangu. Baada ya kutangazwa nikaondoka Singida kuja Dar es Salaam ambako tuliungana na wengine waliochaguliwa katika mikoa mingine katika Chuo cha Sanaa cha Taifa Chang'ombe wakati huo, anaeleza.

Baada ya kufika tuliingia mkataba wa miaka mitano na Serikali. Katika kipindi hicho hatukuruhusiwa kuolewa wala kuzaa. Tulikuwa tunatakiwa kupata mafunzo ya kina ya kuelezea utamaduni wa Kitanzania. Sasa wakati huo baba yangu alikwishanitafutia mchumba nikiwa kidato cha pili na mahari alishakula.

Ilibidi kumshawishi kweli kweli kwamba nitakaa kwa mwaka mmoja tu akakubali. Sasa kazi ikaja pale tulipotakiwa kusaini fomu za kukubali masharti. Baba anajua kwamba mimi nakaa mwaka mmoja, nikajiuliza itakuwaje?

Nikaamua kwenda kwa mjomba wangu, Mujengi Gwao ambaye alikuwa anaishi hapa Dar nilipomweleza akanielewa na akaamua kubeba jukumu la kunisimamia kama mzazi

Sasa wakati nipo chuoni, mchumba wangu akapata habari. Alikuwa anasoma Chuo Kikuu Dar es Salaam. Nikaambiwa kwamba atakuja kuniona jioni. Siku hiyo nikapanga na mwenzangu akae chini hosteli kwa kuwa wageni walikuwa hawaruhusiwi kuingia ndani ili akija aniite.

Sasa alipokuja matron akamwambia mwenzangu 'mwite Chiku ana mgeni wake' naye akasimama pale pale akaniita kwa nguvu nami nikaitika huko huko abeee.... akasema 'kuna mgeni wako' nikamjibu nanii... akamtaja jina. Kwa kuwa tulishapanga nikamjibu nikiwa huko huko. Mwambie hayupo.

Basi tangu siku hiyo ukawa ndio mwisho wake. Akaandika barua kali nyumbani ikamfikia mama. Baada ya kuisoma hakutaka kumwonyesha baba kwani ingekuwa balaa. Alimweleza tu kwamba mchumba wangu amesema hawezi kusubiri hivyo arudishiwe mali zake. Baba hakusita akarejesha."

Akiwa mtaalam wa sanaa, Chiku aliiwakilisha Tanzania katika matamasha mbalimbali ya kimataifa kama Libya, Nigeria na anakumbuka pia kwamba alikuwa mmoja wa wasanii waliokwenda Sweden kwa mwaka mmoja mwaka 1981.

Lakini anasema baada ya kumaliza shule, wenzake karibu wote walipelekwa Bagamoyo kufundisha na kuanzisha Chuo cha Sanaa lakini yeye akahamishiwa makao makuu ya Wizara ya Utamaduni na Vijana akiwa Ofisa Mwandamizi wa Utamaduni mwenye jukumu la kuhamasisha sanaa shuleni.

"Hili halikunipendeza. Kwanza niliona nimepewa jukumu zito nikiwa bado mdogo na damu yangu ilikuwa bado inahitaji kufanya kazi kwa vitendo ndiyo maana niliamua kujiunga na akina Fred Maro na kuanzisha kikundi kile ambacho tulikiita Sayari Cultural Group, anasema Chiku.

Hata huko Bergen anakoishi, bado Chiku anaendelea na kazi hiyo ya kufundisha sanaa kwani mara baada ya kufika alijiunga na Chuo Kikuu cha Bergen kusomea shahada ya Anthropolojia ambayo anasema imempa mwanga wa kuelewa tamaduni mbalimbali. Mbali ya elimu hiyo amesomea kozi mbalimbali za utamaduni wa Norway na lugha na haishangazi anaposema kwamba anazungumza Ki-Norway kama anavyozungumza Kinyaturu ambacho ndio lugha yake ya asili na Kiswahili.

"Tena mimi nazungumza kile cha ndani cha Bergen. Bila ya hivyo watu hawawezi kukuelewa na mimi nikiwa pia mwanasiasa nisingeweza kuomba na kupewa kura."

Maisha na familia

Chiku hakujaliwa kupata mtoto lakini anasema anayo majukumu makubwa ya kuwasomesha watoto wa ndugu zake. "Hivi sasa tunasomesha watoto wanne wa ndugu zangu, mmoja yuko Aga Khan, mwingine Msigani na Green Acres, anaeleza.

Lakini pia nimewajengea nyumba wazazi wangu na nimewasomesha ndani na nje ya nchi wadogo zangu. Sasa nikimaliza kujenga shule nitaanza kujenga nyumba ambayo nikirejea nyumbani nitaishi na mume wangu."

Courtsey of

Viunganishi na http://watanzaniaoslo.blogspot.com


1 comment:

Unknown said...

Hongera sana Chiku Ali. Wee ni kati ya wachapakazi wakubwa wa mfano toka Bongo na fahari yetu. Ni vizuri hizi blogu zikiandika habari za wanawake kama hawa kuwapa moyo wasichana wanaopambana na maisha magumu nyumbani Afrika.
Lakini niwaulize wanablogu wa CCW. Nukuu ya Mwalimu pale juu KABISA ktk Bango...la samawati haijakosewa kiduchu kweli? Je alisema : "Binadamu wazima na wafahamu zao..." au "Binadamu wazima na fahamu zao..."?