Monday, October 15, 2007
Ukoo wa Mwalimu Nyerere sasa taabani
*Yatima, vitegemezi wake wakosa msaada
*Dada yake afariki kwa kukosa nauli ya Dar
*Kikwete,Museveni wafichwa ukweli wa mambo
Waandishi wetu Dar na Butiama.
AKIZUNGUMZA kwa hisia huku wakati fulani akionekana dhahiri kulazimika kusita na kuvuta pumzi nzito, mpwa wa Mwalimu, Bw. Anhthony Nyerere, amelithibitishia Majira Jumapili na Watanzania kwa ujumla kuwa pamoja na wanasiasa wengi kujisifu hadharani kuwa wanamuenzi Mwalimu Nyerere, halisi halisi ya ukoo wake ni taabani na inasikitisha.
Akizungumza katika mahojiano maalum na gazeti hili nyumbani kwake, Dar es Salaam juzi, Bw. Anthony ambaye pia kwa mujibu wa mila za Kizanaki ndiye mrithi wa mali za mjomba wake (Mwalimu Nyerere), anasema miaka nane sasa ndugu wa Mwalimu walioko Butiama, yatima aliokuwa amewachukua na kuwalea, jamaa wengine na watu wengi waliokuwa wakimtegemea Mwalimu wana hali mbaya kuliko ambavyo jamii inaweza kuamini.
"Nimeamua kuvunja ukimya na kuyaeleza haya kwa Watanzania si kwa nia mbaya bali kuielewesha jamii kuwa tofauti na hisia zao, tangu Mwalimu alipofariki ukiondoa wanafamilia chini ya Mama Maria, wana ukoo wengine ambao walikuwa wakilelewa na Mwalimu na ambao hakuwaachia mali zozote, wako taabani, hali zao kimaisha zinatisha," alisema Anthony ambaye ni mtoto wa Nyakigi Nyerere, mdogo wa Mwalimu.
Akifafanua hali ilivyo sasa Bw. Anthony alisema kwa ujumla ukoo wa Mwalimu hata mwenyewe alipokuwa hai haukuwa na maisha ya kifahari kwa sababu Mwalimu alikuwa si tajiri, lakini alikuwa akijitahidi kuwasaidia shida ndogondogo huku akilea yatima kadhaa.
"Mwalimu aliweza kutoa vjifedha kila alipopata kuhakikisha kuwa anawatunza watoto wengi yatima aliowachukua sehemu mbalimbali, kuwasaidia ndugu zake wengine ambao wana umasikini mkubwa kwa kusaidia gharama kama vile za maji, umeme na chakula.
"Kwa mfano Mwalimu alikuwa akilipa ankara za maji na umeme kwenye nyumba ya Mama Nyakigi lakini tangu alipofariki,huduma hizo zimesitishwa katika nyumba hiyo na hakuna aliyeweza kujitolea kusaidia," alisema.
Akasisitiza: "Huyu Nyakigi ambaye ndiye mama yangu yeye ni wa tano wakati Mwalimu ni wa nne kuzaliwa. Ni mmoja wa ndugu waliokuwa wakipendana sana na Mwalimu kiasi kwamba Mwalimu alikuwa siku zote akimwita dada yake huyu kwa jina la shangazi.
"Lakini tazama Mama Nyakigi aliyekuwa akilipiwa gharama hizo na kupewa fedha za kujikimu na Mwalimu mwenyewe, aliishi kizani kuanzia Mwalimu alipofariki akiwa hana maji pia hadi mwaka 2002 alipofariki."
Akizungumzia kifo cha Nyakigi, Bw. Anthony kwa masikitiko alisema mama huyo alikosa japo nauli ya kusafirishwa kwenda hospitali ya Muhimbili kwa matibabu.
"Tulikosa fedha za kumsafirisha kwenda Muhimbili na akafariki mwaka 2002. Hata kwenye maziko yake, hatukupata hata senti ya mtu," alisisitiza.
Kuhusu yatima waliokuwa wakilelewa na Mwalimu, Anthony alisema kwa sasa wengi wamesambaratika, huku waliopo wakiendelea kuishi katika nyumba ya mama yake Mwalimu ambayo hata hivyo ni chakavu na haina umeme.
"Sina pesa kwa sasa, mimi kama mkuu wa ukoo inanilazimu kuikarabati lakini siwezi, hata nyumba ya mama Nyakigi imebaki ina nyufa na jiko lake la nyuma limebomoka. Aliishi maisha ya shida sana,"alisema.
Bw. Anthony alisema kuna watoto wa mjomba wa Mwalimu aitwae Salim Nyakomge, mtu ambaye ndiye Mwalimu alitumia ngo'mbe wake kupata fedha za kwenda Chuo Kikuu Makerere, hao nao maisha yao ni taabani na sasa wanaishi kwenye vibanda vya tope vilivyoezekwa kwa nyasi.
Alimtaja mtu mwingine ambaye anataabika kuwa ni mpishi wa Mwalimu, Mzee Mohammed Sheikh ambaye amekuwa na Mwalimu tangu alipokuwa Waziri Mkuu mwaka 1960 hadi na kuendelea na kazi hiyo hadi alipostaafu mwaka 1983.
"Huyu Mzee ana matatizo makubwa. Ameunguliwa na nyumba yake huko Tanga na yuko hapa Dar es Salaam kwa wajukuu zake nako anapata shida tu. Hana pa kuishi, hana pa kwenda, hana pa kujishikiza," aliongeza.
Kielelezo kingine cha matatizo yanayoukabili ukoo wa Mwalimu kwa sasa ni hali ya sasa ya Kiboko Nyerere, mdogo wa mwisho na mmoja wa vipenzi wake.
Kiboko kwa mujibu wa Bw. Anthony hivi sasa yuko kitandani akiwa mgonjwa, msaada pekee alionao ni kijana wake mmoja wa kiume anayemsaidia na pia kipato chake cha sh. 15,000 anachokipata kwa mwezi kutokana na wapangaji wa nyumba yake.
"Tumejitahidi kuchanga fedha wakati fulani tukampeleka Mwanza kupata matibabu, lakini hivi sasa amerudishwa nyumbani hatuna fedha. Bahati nzuri ana nyumba aliyojengewa na marehemu Sokoine, ina vyumba vinne. Kwa sasa amepangisha vyumba vitatu kila kimoja sh. 5,000 kwa mwezi hivyo anashukuru Mungu kuwa na sh. 15,000 kwa mwezi lakini hali ya afya yake ni mbaya,"alisema.
Bw. Anthony alisema kitu kinachomuuma zaidi kuliko umasikini huo ambao yeye anasema "tumeuzoea na Mwalimu alishatuandaa kuishi hivyo," ni kubaini kuwa kuna viongozi ambao hufika na kuahidi kuwasaidia wanaukoo hao lakini wanakwazwa na watu aliowataja kuwa ni warasimu.
"Mama Nyakigi aliwahi kuomba msaada kwa Rais (mstaafu) Benjamin Mkapa ambaye alikuwa tayari kusaidia lakini akaambiwa 'Mzee fedha za kuwatunza hawa mbona zipo.' lakini hazikuonekana,'," alisena na kuongeza:
"Kuna wakati alikuja Rais (Joseph) Kabila wa DRC, akakutana na Mama Nyakigi akaliliwa shida naye akaahidi kuleta fedha. Najua alileta fedha nyingi sana, lakini zilikokwenda hazikuwafikia wanaukoo wa Mwalimu."
Bw. Anthony pia alisema alikasirishwa na kitendo cha hivi karibuni, Rais Yoweri Museven wa Uganda na Jakaya Kikwete walipokuwa Butiama, ambapo watu aliowaita 'vimbelembe' hawakudirika hata kuwafahamisha viongozi hao kuwa mmoja wa vipenzi vya Mwalimu; Kiboko, alikuwa mahututi kitandani.
"Hili jambo mimi lilinikera sana na kila ninapolitafakari naona ulikuwa ni unyama mkubwa sana. Kama Museveni na Kikwete wangefahamishwa kuwa kuna kipenzi cha Mwalimu alikuwa kitandani mahututi sijui ingewapunguzia nini hao waliokuwa na viongozi hao," alionesha kukerwa.
Kutokana na shida hizo, baadhi ya vijana, waliokuwa wakiishi na Mwalimu kwa muda mrefu na kusaidiana naye kazi za shamba kule Butiama, sasa wamekimbia kutokana na hali hiyo, kama anavyothibitisha mmoja wao, Bw. Hamis James Kiberiti, alipofanya mahojiano na Mwandishi Gladness Mboma, jijini Dar es Salaam wiki hii.
"Najua watanzania wengi hawataamini, lakini naomba waamini kuwa toka alipofariki Mwalimu Nyerere ukoo wake kwa sasa uko taabani ukiishi katika mazingira magumu kimaisha," alisema Bw. Kiberiti.
Alisema ukoo wa Mwalimu Nyerere umekumbwa na hali ngumu ya maisha na hata kufarakana kutokana na kumtegemea Mwalimu Nyerere enzi za uhai wake kwa kila jambo.
"Sikufichi Mwalimu alikuwa akilima na kisha mazao anayopata anayagawa kwa ndugu zake yaani kaka, dada zake na wengineo pamoja na kuwasaidia pia kwa mahitaji mengine ya muhimu.
"Lakini baada ya kifo chake, vitu hivyo vyote vilikosekana,hivyo baadhi ya vijana walikimbilia mijini na maisha yao bado yanatisha kama unavyoniona mimi, huwa naona aibu kumweleza mtu kuwa mimi niliishi karibu na Nyerere," alisema kijana huyo ambaye anafanya kazi za 'deiwaka' na pia kulinda kiwanja cha mtu eneo la Kimara, Dar es Salaam huku akiishi kwenye kibanda kilichojengwa kwa mabati chakavu.
"Kama mnataka kuamini hilo ninaomba Watanzania wenye uchungu na ukoo wa Mwalimu siku moja waende kutembelea Butiama wajionee wenyewe.
"Mkifika ombeni kuonana na ndugu zake Mwalimu Nyerere aliozaliwa nao tumbo moja mjionee maisha wanayoishi, nyumba zimechoka wao wenyewe wamechoka wako hoi taabani, mimi ni kijana nina nguvu lakini nina waonea huruma wazee wangu hao," alisema.
Alitoa mfano wa mdogo wa Mwalimu, Bw. Kiboko kuwa sasa yupo hoi kitandani, anaumwa ni wa kugeuzwa na hana msaada wowote anaoupata.
Kijana huyo anakiri kuwa aliamua kukimbilia mjini kutafuta maisha kutokana na ugumu ulioibuka kijijini.
Majira Jumapili pia lilizungumza na wakazi wa Butiama ambako mwandishi wetu, Joyce Mabiti, anathibitisha kuwa wazee waliokuwa marafiki wa Mwalimu, nao 'wanalia njaa.'
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hilo kijijini hapo wiki hii umeonesha kuwa pamoja na hali inayowakabili wanaukoo wengi wa Mwalimu kuwa tata, wazee waliokuwa marafiki wakubwa wa Mwalimu, walisema shida zimeongezeka.
Akiongea kwa niaba ya wazee wenzake, Bw Marwa Ihunyo (82) alidai kuwa enzi za uhai wa Mwalimu, walikuwa wakipata misaada mbalimbali ikiwemo pesa kwa ajili ya kujikimu jambo ambalo amedai kuwa hivi sasa halipo kabisa.
Mzee Ihunyo ambaye alisoma na Mwalimu mwaka 1933 katika Shule ya Msingi Mwisenge iliyoko mjini Musoma pamoja na misaada hiyo waliokuwa wakipata kutoka kwake alikiri pia kuwa Mwalimu alikuwa akiwaelimisha mambo mbalimbali ya kisiasa, kilimo na maendeleo kwa ujumla.
Alisema kuwa inasikitisha kuona viongozi wa Serikali wamewasahau wazee hao na badala yake wamekuwa wakiwakumbuka katika kipindi cha maadhimisho ya kumbukumbu ya kifo cha Nyerere pekee.
Aliwashauri viongozi wa Serikali kuwa na tabia ya kuwatembelea wazee hao mara kwa mara ili kujua matatizo yao na kuweza kuwasaidia.
"Unajua Mwalimu alipenda sana mshikamano kati ya viongozi na wananchi hivyo nawashauri viongozi wa serikali kuendeleza tabia hiyo ili kuweza kuondoa matatizo yanayowakabili wananchi hasa sisi wazee," alisisitiza.
Akihitimisha kuhusu hali iliyoukumba ukoo wa Mwalimu miaka nane baada ya kifo chake, Bw. Anthony amewataka Watanzania kujua kuwa wanaukoo hao hawalilii kuwa na maisha ya gharama, wanajua Mwalimu aliwafundisha uvumilivu lakini wameamua kuweka bayana ili jamii na hasa wahisani wanaotoa fedha zao nyingi pia wajue haziwafikii walengwa.
Subscribe to:
Post Comments (Atom)
No comments:
Post a Comment