Tuesday, November 20, 2007

Maisha ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini,

Zitto Kabwe

yamezungukwa na utata.

Na Luqman Maloto.

Maisha ya Mbunge wa Kigoma Kaskazini (CHADEMA), Zitto Kabwe (pichani) yamezungukwa na utata, huku kukiwa na matukio matano ambayo yanatajwa kuweza kumsababishia kifo mheshimiwa huyo kijana, Ijumaa Wikienda linakupa ripoti ya kutisha.


Kwa mujibu wa ripoti hiyo ya uchunguzi, matukio hayo matano ambayo yangeweza kumsababishia kifo mbunge huyo ni ajali za gari alizonusurika, kunywa sumu, pamoja na kuugua.

Ripoti hiyo iliyoshirikisha vyanzo mbalimbali, inamhusisha pia aliyekuwa Mbunge wa Viti Maalumu kwa tiketi ya Umoja wa Vijana CCM (UVCCM), Marehemu Amina Chifupa kama mtu aliyewahi kumuokoa Zitto kwenye jaribio la kifo.

“Ilikuwa ni Aprili, mwaka huu, tarehe siikumbuki vizuri, Zitto alikunywa kahawa yenye sumu, Marehemu Amina ndiye aliyemuokoa, alimwambia ile kahawa ina sumu,” alisema kada mmoja maarufu wa CHADEMA ambaye aliomba hifadhi ya jina lake gazetini.

Kada huyo aliongeza, Zitto alikunywa kahawa hiyo kwenye hoteli moja ya kitalii (jina kapuni) iliyopo katikati ya Jiji la Mwanza: “Baada ya kuambiwa kwamba amekunywa kahawa yenye sumu, alikimbizwa kwenye hospitali iliyo karibu na hoteli hiyo kwa matibabu.

“Wakati anakimbizwa hospitali, hali yake ilikuwa mbaya, wakati huo alishaanza kupoteza fahamu, alipofikishwa hospitali na kupimwa, ilionekana kweli alikunywa sumu. Mpaka leo haijulikani Amina alijuaje kama ile kahawa ilikuwa na sumu, iliwekwa na nani na kwa sababu gani?”

Tukio la pili ni ajali ya gari ambayo Zitto aliipata Agosti, 2004 wakati alipokuwa akisafiri kutoka Dar es Salaam kuelekea Kigoma kwa ajili ya mikutano ya hadhara ya chama chake.
Ilielezwa kwamba katika ajali hiyo Zitto alinusurika, ingawa aliumia kiasi.

Ripoti hiyo inalitaja tukio la tatu kuwa ni la mbunge huyo kuugua ghafla alipokuwa safarini nchini Ujerumani, Novemba 2006, ambako alifanyiwa upasuaji wa mgongo.

“Ilikuwa ni ugonjwa wa ajabu, wenyeji wake walidhani angeaga dunia kutokana na jinsi hali yake ilivyokuwa mbaya,” alisema kada huyo wa CHADEMA ambaye mara nyingi huambatana na Zitto katika ziara za chama kitaifa.

Tukio la nne ambalo lilikaribia kuondoa uhai wa mbunge huyo ni lile la kuugua tumbo wakati wa kampeni za Uchaguzi wa mwaka 2005, ambapo baadhi ya watu walifikia hatua ya kutumiana ujumbe kwamba Zitto ameaga dunia.

“Hatujui ni kwanini, lakini kuna watu walitumiana ujumbe kwamba ndugu yetu amefariki dunia. Nakumbuka wakati huo alikuwa Dar es Salaam akiwa kwenye maandalizi ya kwenda Norway katika safari ya kazi za chama,” alisema kiongozi mmoja wa CHADEMA wa ngazi za juu (jina kapuni) wa Wilaya ya Kigoma Vijijini.

Aidha ripoti hiyo inafunga na tukio la tano kwamba Zitto alinusurika kimiujiza katika ajali ya gari iliyokatisha maisha ya aliyekuwa Naibu Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia na Watoto, Salome Mbatia, iliyotokea Oktoba 29, mwaka huu kwenye Kijiji cha Kibena, Njombe, mkoani Iringa.

Habari zinasema kwamba gari la Zitto ndilo lililokuwa mbele ya lile la Salome lililogongwa na fuso, lakini ilipobaki hatua chache kutoka eneo la ajali, mbunge huyo alimuamuru dereva wake apaki pembeni na waingie kwenye ‘grocery’ iliyokuwepo kijijini hapo kwa ajili ya kununua kinywaji aina ya redbull.

Chanzo chetu kimoja kilitupasha kwamba: “Kitendo cha kuingia grocery, ndiyo kilitoa mwanya kwa gari la Mheshimiwa Salome, kulipita lile alilokuwamo Zitto. Baada ya kumaliza kununua vinywaji, walianza safari na dakika tano baadaye ndipo walipofika eneo la ajali.

“Kinachooneka hapa ni kuwa kama Zitto asingemuamuru dereva wake kupaki pembeni kwa ajili ya kununua redbull, pengine yeye ndiye angeanza kukutana na fuso na kumgonga kwa sababu lilikuwa linatembea ‘saiti’ siyo yake, tena likiwa katika mwendo wa kasi.”

Ijumaa Wikienda, lilipomtaka Zitto azungumzie matukio hayo, alishindwa kukubali wala kukataa, ingawa alisema: “Nakumbana na matukio mengi ya kutisha, lakini nayachukulia kama changamoto, kwahiyo siogopi kwa sababu naamini Mungu yupo na mimi.”

No comments: