Thursday, November 22, 2007


Nani anayeuzima mshumaa wa Serikali?

Maggid Mjengwa.

KUTOKANA na mambo yanavyoenenda katika jamii yetu sasa, mmoja wa wasomaji wangu ameniandikia kuniomba niwakumbushe wasomaji juu ya kisa kifuatacho nilichopata kuhadithia zamani kidogo.

Naam, miongoni mwa viongozi waliopata kuongoza dola ya Kiislam, baada ya Mtume Muhammad (SAW) na baada ya masahaba ni Amir Muuminina Khalifa Umar bin Abdulaziz.

Wanazuoni wa Kiislam wanatuambia, kuwa utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ulijaa uadilifu. Si kwa viongozi tu, hadi kwa raia wake. Inasemwa, kuwa moja ya mafanikio makubwa ya utawala wa Khalifa Umar bin Abdulaziz ni kukusanya zaka. Katika Uislam, zaka ni ibada ya lazima kwa mwenye nacho kuwapa masikini, yatima, wajane,wasafiri, raia na wengineo wenye kuhitaji.

Watu walijengewa imani kubwa, kiasi hakuna aliyethubutu kukwepa kutoa zakka. Hata wale waliopokea zaka walikuwa waadilifu, hawakupokea zaka mara mbili kama walikwisha kupokea kabla. Wote waliostahili kupata zaka walipata zaka. Hakika, zaka zilitolewa zikajaa mabohari.

Siku moja raia mmoja alikwenda kwenye ofisi ya Khalifa Umar bin Abdulaziz, katika maongezi, Khalifa Umar alikuwa akihangaika kupuliza na kuzima mshumaa mmoja na kuwasha mwingine.

Alikuwa na mishumaa miwili mezani. Kadri mazungumzo yalivyoendelea, Umar aliendelea kufanya hivyo. Alipuliza mshumaa mmoja ukazimika, kisha akawasha mwingine. Jambo hilo lilimstaajabisha sana mgeni wake.

Akauliza; "je, ni kwa nini unazima mshumaa huu na kuwasha mwingine, kisha huo nao unauzima na kuwasha ule wa kwanza?

Khalifa Umar bin Abdulaziz akamjibu; "mshumaa huu ni wa serikali, wewe unaponiuliza habari za serikali nauwasha. Lakini naona mara unauliza habari za familia yangu, ndiyo maana nauzima wa serikali na nauwasha mshumaa wangu mwingine nilioununua kwa pesa za mfukoni mwangu. Nachelea nisije fanya dhuluma kwa mali ya nchi.

"Ewe msomaji, nasisitiza, hiki si kisa cha kutunga au chenye dhamira ya kukuburudisha, ni kisa cha kweli chenye kutuachia mafundisho makubwa katika suala zima la maadili.


RAIS Jakaya Kikwete

Julai mwaka 2005 akiwa Chuo Kikuu cha Dar es Salaam, Rais Jakaya Kikwete alizungumza na wasomi juu ya masuala ya uongozi Afrika Mashariki. Wakati huo Kikwete alikuwa mgombea urais kwa tiketi ya CCM.

Katika hotuba yake hiyo Kikwete alikemea tabia ya ufisadi na ubinafsi wa viongozi wa bara hili. Kupitia safu hii niliandika, kuwa kama Jakaya Kikwete alimaanisha alichosema, basi, akibahatika kuupata urais huko twendako, historia itamhukumu kwa kauli na matendo yake.

Naam. Jakaya Kikwete ndiye Rais wa sasa wa nchi.

Amekwisha kuanza na anaendelea kuhukumiwa kwa kauli na matendo yake. Lakini hiyo ndiyo maana pia ya uongozi. Kiongozi husifiwa, hulaumiwa pia. Wakati mwingine lawama huzidi hata sifa za kiongozi. Busara si kuzuia njia zinazofanya kiongozi kusikia lawama kutoka kwa anaowaongoza.

Wasiomtakia mema kiongozi, ni wale wenye kufanya kila njia, na hata hila, ili kumficha kiongozi asisikie lawama za anaowaongoza. Wanajipendekeza na hata kusahau, kuwa hata lawama humsaidia kiongozi.

Kitokacho kwa waongwazwao, iwe sifa au lawama, ni sawa na kioo cha kujitazama usoni. Kiongozi naye awe kioo cha anaowaongoza. Kwa kuonyesha mfano wa yaliyo mema.

Pale Chuo Kikuu, wakati ule Kikwete alikemea ufisadi miongoni mwa viongozi. Leo tunasikia, kuwa baadhi ya viongozi mafisadi wamo hata ndani ya Serikali ya Kikwete. Kwa ubadhirifu na wizi, wanatafuna mabilioni ya shilingi kila mwaka. Fedha za walipa kodi. Tunaambiwa kuna walio na vitabu viwili vya stakabadhi za mapato, kimoja cha Serikali na kingine cha kwao wenyewe!

Rais mwenyewe ameonyesha kushtushwa, lakini huenda ameshtushwa na kuona kichuguu cha ufisadi, kuna milima ya ufisadi iliyojificha. Taifa linatafunwa. Kuna baadhi ya viongozi wanaoshindwa hata kuficha ulafi wao. Ubinafsi na ulafi yote ni misamiati yenye kuzungumzia uchoyo.

Kiongozi mbinafsi ni mchoyo pia, hapendi kuona hata kilicho kidogo kinagawiwa sawa kwa misingi ya haki. Kiongozi mbinafsi ana hulka za kujipendelea, kujali maslahi yake kwanza. Hili ni tatizo la viongozi wetu wengi barani Afrika.

Kiongozi mchoyo na mbinafsi pia ni mwenye hulka ya kujiweka mbele zaidi ya wenzake. Anapenda sana kusifiwa na hata kuimbiwa nyimbo za kutukuzwa. Anapenda utukufu. Lugha yake mara nyingi ni ya kujisifu, huwa hasubiri kusifiwa na wengine kwanza. Hudiriki kujisifu mwenyewe.

Na hata ukimsifia kiongozi wa namna hiyo, mathalan kwa matokeo mazuri ya kazi aliyofanya au hata mavazi aliyovaa, usishangae ukajibiwa; " Ah! Ndio, mimi ni mchapa kazi kweli kweli! Au " Kuonekana nadhifu namna hii ni kawaida yangu!"

Mara nyingi mafanikio kwake yeye ni matunda ya juhudi yake binafsi, si mwepesi wa kutambua mchango wa wengine katika mafanikio yake. Husahau hata mchango wa mkewe au mumewe. Yeye ni yeye. Katika ubinafsi wa viongozi wetu, mara nyingi kiongozi wa Kiafrika hapendi kukosolewa.

Hana busara ya kutambua, kuwa hakuna mwerevu wa kila jambo, kwamba sote hatujakamilika, tuna mapungufu yetu. Kwa kiongozi wa staili hii, akitamka jambo, basi hakuna wa kufikiri jingine. Fikra zake siku zote ni sahihi.

Kumkosoa kiongozi katika nchi zetu hizi, inaweza ikawa ni sawa na kumwambia hafai. Unatishia nafasi yake ya madaraka aliyopewa na Mwenyezi Mungu! Ni kufuru, ni dhambi. Kiongozi wa namna hii, kila anaposikia akishutumiwa, akikosolewa, na baya zaidi hadharani na wengine wanasikia, basi, huwa mkali kama mbogo.

Dhana ya kwamba anayekukosoa anakutakia mema, anataka ujirekebishe. Kwamba anayekosoa anaitakia mema na kuipenda nchi yake, dhana hii haikubaliki kwenye mitazamo ya viongozi wa kada hii. Anayekukosoa ni adui, ni mpinzani, na huenda kuna aliyemtuma.

Plato, mwanafalsafa wa Uyunani ya kale anasema; katika nchi, kiongozi wa namna hii, hufikia kukoma kuwa kama wanadamu wengine, hugeuka mbweha. Atawaandama "wapinzani" wake. Wengine atawaua kwa kuwapachikia mashitaka batili, na wengine atawalazimisha kwenda kuishi uhamishoni.

Wasomi , ambao mara nyingi huwa wadadisi, wenye kuhoji mamlaka, ni waathirika wa mwanzo wa kiongozi wa namna hii. Ikumbukwe, viongozi wengi Afrika hupata madaraka ya ghafla na utajiri wa ghafla.

Tofauti na mfanyabiashara wa kawaida, mara nyingi kiongozi Afrika huwa hana historia yenye kueleweka ya jinsi alivyoupata utajiri wake. Wengi wao, bila hata kujiandaa sana kiuongozi , hujikuta ghafla wamepata madaraka makubwa, na ghafla hulewa madaraka hayo, huwa ni walevi wa madaraka. Mlevi wa madaraka hupungukiwa haraka maadili ya uongozi.

Basi, ghafla huwa mla rushwa mkubwa kwa kutumia ofisi aliyokabidhiwa. Na hatimaye, ghafla huwa tajiri mkubwa, bilionea! Vyote hivi huweza kumtokea kiongozi wa Kiafrika kwa kasi ya kutisha sana.

Leo unapishana na Mwafrika mwenzako akiendesha baiskeli, kesho anaukwaa uongozi. Baada ya miaka 10 tu, anajenga Ikulu yake mwenyewe ya kifahari, anaweza kuwa nazo mbili au tatu za namna hiyo na magari kadhaa ya kifahari.

Kuna baadhi ya nyumba za waheshimiwa utadhani ni yadi za kuuzia magari. Je, yote haya ni kwa kipato halali?

Naam. Mtu wa namna hii kamwe hawezi kukupa historia yenye kueleweka juu ya utajiri wake wa ghafla.

Huyo si mhalifu kama walivyo wezi wa kuku au wenye kuvunja madirisha usiku. Huyo ni jambazi, ni mhalifu mkubwa anayetishia uhai wa raia na usalama wa taifa husika.

Neno langu la mwisho; ni heri kufa na kuacha fikra zinazoishi, kuliko kuishi bila kufikiri. Fikiri kwa bidii.

Kiselule: 0754 678 252,
Baruapepe: mjengwamaggid@hotmail.com
Blogu: http://mjengwa.blogspot.com



No comments: