Monday, November 12, 2007

Rais Jakaya Kikwete.

Kikwete ajitoa suala la Mahakama ya Kadhi.

Asema iliandaliwa na Mkapa, Mangula, Kingunge.

na Agnes Yamo.

RAIS Jakaya Kikwete, jana kwa mara ya kwanza alilizungumzia hadharani suala linalozidi kushamiri katika mijadala ya kijamii, la uanzishwaji wa Mahakama ya Kadhi, na kueleza kuwa hakuhusika kuliweka katika Ilani ya Uchaguzi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM).

“Ndugu zangu napenda mtambue kuwa, mgombea urais ahusiki na uandaaji wa Ilani, wala ahusishwi… nawasihi tu tuwe watulivu na tuiache kamati ifanye kazi yake, ni watu wenye busara, naamini hawatafanya maamuzi mabaya,” alisema.

Rais Kikwete aliyasema hayo jana wakati alipokuwa akizungumza katika Ibada ya kumsimika Askofu Mkuu wa Kanisa la Kiinjili la Kilutheri Tanzania (KKKT), Alex Malasusa, katika Kanisa Kuu la Azania Front, Dar es Salaam.

Katika hotuba yake, Rais Kikwete alisema ameamua kulizungumza suala hilo kwa sababu ameziona dalili zinazoashiria kuwa “tusipokuwa waangalifu, upendo na mshikamano baina ya Waislamu na Wakristo hapa nchini utaharibika” kutokana na mjadala kuhusu Mahakama ya Kadhi.

Lakini aliwasihi Watanzania kuwa na subira kwa sababu suala hilo, ambalo mjadala wake unashika kasi, hatma yake itajulikana Februari mwakani, Tume ya Kurekebisha Sheria, itakapotoa ripoti yake.

Hata hivyo, Rais Kikwete alionekana kuwatupia lawama wanasiasa kuwa ndio wanaochochea suala hilo kutokana na manufaa yao binafsi.

Alisema kuwa kiini cha mjadala kuhusu Mahakama ya Kadhi ni wanasiasa.

“Chimbuko la kinachosemwa sasa kuhusu Mahakama ya Kadhi ni bungeni, na muasisi wa hoja hii ni Mheshimiwa Augustino Lyatonga Mrema alipokuwa Mbunge wa Temeke.

“Bwana Mrema alikuja na hoja ya binafsi bungeni ya kutaka kuundwa kwa Mahakama ya Kadhi nchini,” alisema Rais Kikwete na kubainisha kuwa hoja hiyo iliungwa mkono na aliyekuwa Mbunge wa Bagamoyo wakati huo, marehemu Baruti Rajabu.

Alisema kuwa baadaye ikafuatiwa kwa nguvu na hoja binafsi ya aliyekuwa Mbunge wa Moshi Vijijini kupitia TLP, Thomas Ngawaiya.

Alisema kwa busara za Spika wa kipindi hicho, Pius Msekwa, akisaidiwa na kiongozi wa shughuli za serikali bungeni, Frederick Sumaye, ambaye alikuwa Waziri Mkuu, alikataa hoja hiyo kujadiliwa bungeni moja kwa moja kutokana na kile alichokitaja kuwa ni unyeti wake, na kuamua kuipeleka katika Kamati ya Bunge ya Katiba na Sheria, ambako kamati hiyo iliongozwa na wenyeviti wawili tofauti, Arcado Ntagazwa ambaye alipoteuliwa kuwa waziri, nafasi hiyo ilishikwa na Athumani Janguo.

Alisema baada ya kamati hiyo kukamilisha utafiti na kukabidhi ripoti kwa Spika, aliikabidhi serikalini ambako inafanyiwa kazi ili kutoa ushauri upasao.

“Serikali imekabidhi Tume ya Kurekebisha Sheria kulifanyia kazi jambo hilo na kushauri ipasavyo. Tume inaendelea na kazi yake ya utafiti wa kina na kwa taarifa nilizonazo, huenda mwezi Februari mwakani watamaliza kazi yao ya utafiti na kuwa na lolote la kushauri,” alisema Kikwete.

Aliwahakikishia Watanzania kuwa serikali haitafanya uamuzi ambao hauna maslahi kwa nchi na wala jambo hilo halitaamuliwa kinyemela.

Alisema suala la Mahakama ya Kadhi si lake binafsi, na kuwa lilikuwepo kabla yake na mchakato wake ameukuta.

Aidha, alisema mchakato wa suala hilo haukuanza na Ilani ya Uchaguzi ya CCM ya mwaka 2005, kama wengi wanavyodai na kuwa Ilani hiyo ya uchaguzi imeutambua mchakato huo kujipa dhima ya kuuendeleza ili kujaribu kutafuta ufumbuzi.

Akikanusha kuhusika kwake kuliweka suala hilo katika Ilani, alisema kuwa mchakato wa kuandika Ilani huanza kabla ya uteuzi wa mgombea urais.

“Ilani ilitayarishwa chini ya uongozi wa Mwenyekiti, Mheshimiwa Benjamin Mkapa (ambaye naye alikuwepo kwenye ibada hiyo), Katibu Mkuu, Philip Mangula na Mwenyekiti wa Kamati, Mheshimiwa Kingunge Ngombale Mwiru. Ilani iko hivi ili kumbana mgombea asijipendelee kuweka mambo mepesi ambayo ataweza kuyatekeleza,” alisema.

Kwa upande wake, katika salamu zake, Askofu mteule Alex Malasusa, alikemea tabia ya baadhi ya viongozi kuzungumzia masuala ya imani kwa lengo la kujitafutia umaarufu.

“Mambo yahusuyo imani yasizungumzwe kisiasa, na viongozi wanaopenda kupata umaarufu kupitia imani waache mara moja,” alisema Askofu Malasusa.

Akizungumzia suala la migogoro inayolikumba kanisa, Askofu Malasusa alisema kila mara anamuomba Mungu kuwezesha katika uongozi wake kuwe na mshikamano na amani miongoni mwa waumini na viongozi wa kanisa hilo.

“Naomba msamaha kwa wale wote waliokwazwa au kuumizwa katika migogoro iliyotokea katika kanisa letu, na nawaomba waliofungua kesi kuzifuta mara moja, ninatubu kwa ajili ya wote… watusamehe na tuanze upya,” alisema kwa masikitiko.

Awali, kanisa lilitoa zawadi ya gari, ng’ombe wa maziwa pamoja na fedha taslimu sh milioni 2.5, ikiwa ni shukrani kwa uongozi mzuri kwa Mkuu wa Kanisa mstaafu, Askofu Dk. Samson Mushemba, ambaye aliongoza kanisa hilo kwa miaka 15.

Akizungumza baada ya kupokea zawadi hizo, Dk. Mushemba alisema kanisa linapaswa kuwafundisha wananchi mbinu bora za kuinua maisha yao.

Aliitumia nafasi hiyo pia kuwakemea wafanyabiashara wanaopandisha bezi za bidhaa maradufu kwa lengo la kujipatia faida kubwa na kusababisha kukithiri kwa umaskini miongoni mwa jamii.


Kutoka: Tanzania Daima


No comments: