Midladjy Maez
HabariLeo; Friday,November 23, 2007 @00:07
NIMEPATA fadhaa na kukerwa na maoni ya baadhi ya Watanzania, hasa wasomi, ambao hukipaka mafuta Kiswahili kwa mgongo wa chupa na kukibeza na kuonyesha jinsi wanavyoabudu lugha ya Kiingereza.
Nitaeleza sababu kadhaa ambazo wasomi hao wanazijua, lakini hawataki kuzikubali. Kila tunapofanya hatua za zima moto kukuza kiwango cha elimu, kwa mfano kwa kuwapeleka watoto wetu katika shule zinazosomesha ‘Kiingereza’ kwa kutumia walimu wasiojua Kiingereza, ndio ukweli tunadidimiza elimu yetu kwa jumla kitaifa!
Kuna watu wanajichanganya na kuonea wivu ‘wakubwa’ wanaopeleka watoto wao ama hapa nchini katika shule nilizotaja hapo awali au katika nchi jirani au hata Ulaya, Marekani na Australia.
Utafiti mdogo uliofanywa unaonyesha kuwa karibu theluthi mbili ya watoto wa wakubwa, wana uwezo duni kimasomo na mara nyingi huko Ulaya wamepelekwa kuficha aibu ya kifamilia.
Mara nyingi watoto hao si mfano mzuri wa tabia na wamebobea katika ugoigoi kimasomo. Ni kweli wanaweza wakawa mahiri katika kuzungumza ‘Kiingereza’ cha mitaani, lakini hawana tofauti sana na matapeli wa vijiweni, wajulikanao mijini kama ‘ misheni tauni’
Tumepoteza miaka 45 kitaaluma tukichapa mguu, wakati mataifa mengine yamejitahidi kufanya mabadiliko kadhaa ili kuboresha elimu yao.
Kwa mfano, katika Karne ya 18 Urusi kupitia wasomi wake ilibadili mfumo wa kukiabudu Kifaransa na katika Karne ya 20 wakawa wa kwanza kupeleka mtu angani. Wangekuwa bado wanakiabudu Kifaransa wangekuwa bado wanakamua maziwa na kulima kwa ngwamba.
Ukisema Warusi wana rasilimali za kutosha na sisi vivyo hivyo tumejaaliwa tunazo. Zipo nchi nyingi tu zilizopata maendeleo ya haraka ambazo zilikuwa na kiwango duni cha maendeleo na mfano ni Korea zote mbili.
Mwaka 1960 nchi hizo za Korea Kaskazini na Korea Kusini, zilikuwa kitaaluma na kiuchumi sawa na sisi, lakini wametumia Kikorea kusonga mbele na sasa ziko katika Dunia ya Kwanza!
Sisemi na sisi tungekuwa kama Korea, lakini kama tungechanga karata zetu vizuri, ikiwamo kukitumia vizuri Kiswahili, basi tungekuwa katika hatua bora zaidi ya maendeleo kuliko sasa.
Zamani Kilatini kilitawala dunia na Kiingereza kinachopigiwa debe sasa, kilikuwa lugha ya wawindaji na ya jikoni na hakikutumika hata kwa kutungia mashairi.
Dola ya Kirusi haikuanza kupiga hatua katika tafiti za sayansi na teknolojia, hadi pale ilipoanza kutumia rasmi Kirusi. Urusi ilianza kusonga mbele katika karne ya 18 baada ya Kirusi kuchukua nafasi ya Kifaransa, kilichokuwa lugha ya watawala na mabwanyenye.
Tuna bahati Kiswahili kilipewa kipaumbele hata na Wakoloni. Wazungu walikitumia Kiswahili kutufikishia amri zao. Lakini, pia wakati wa kupigania uhuru wanasiasa wetu nao walikitumia Kiswahili kama silaha ya ukombozi. Walikitumia kuunganisha makabila zaidi ya 120 yaliyopo Tanzania na kujenga Taifa moja linalozungumza Kiswahili.
Hivi sasa tunapiga kelele mikataba ya madini na mingine ya miradi mikubwa imekuwa ni mizigo. Tuna malalamiko na hofu nyingi, lakini hakuna anayethubutu kusema hiyo mikataba imeandikwa Kiingereza na wanaofahamu ni wachache! Nina uhakika kama mikataba ingeandikwa kwa Kiswahili, mambo yangekuwa afueni.
Utafiti wa wataalamu wa Chuo Kikuu unaonyesha kuwa ufahamu wa Kiingereza katika jamii unashuka siku hadi siku . Utafiti katika shule mojawapo ya sekondari ulionyesha kuwa katika walimu 55 wa mchepuo wa Sayansi, ni watano tu katika hao, ndio waliokuwa wanajimudu kusomesha kwa Kiingereza.
Waliobakia yaani 50 walikuwa ‘wanajikongoja’. Sasa hii elimu gani kwani kuna hatari ya kuzalisha wataalamu waliobobea kinadharia tu lakini kivitendo hawajimudu!
Watu wameng’ang’ania Kiingereza wakati ukweli hawakiwezi. Kukifanya Kiingereza kama somo mojawapo ni vema zaidi kuliko zoezi la sasa la kutaka kufanya iwe lugha ya kufundishia. Kwa maoni zoezi hilo ni njama za kuua kabisa elimu.
Tutumie mbinu waliyotumia Warusi, Wajapani na Wakorea ya kupeleka vijana wao kusomea taaluma za sayansi na teknolojia katika nchi kadhaa na halafu kuteka chembechembe za taaluma hizo na kuzirejesha nyumbani kwao ambako zilizalishwa kulingana na mahitaji na vipaumbele vyao na matokeo yake ni maendeleo makubwa tunayoyasifia sasa.
Hali hiyo haikuja kwa kubahatisha kwa kutumia lugha za watu. Chembechembe za taaluma zilitafsiriwa katika lugha zao za kitaifa na kurudufiwa kitaaluma ndani ya jamii yote, hivyo kuifanya sehemu ya utamaduni wa jamii.
Elimu inayofunzwa kwa lugha ya kigeni, siku zote haitokuwa sehemu ya jamii husika, hivyo haitochangia kuinua maendeleo yoyote katika jamii husika.
Lugha ya Kiswahili inaweza kuwa mkombozi. Inaweza kutumika kutaifisha teknolojia yoyote ya kigeni na kuileta nchini na kuitumia kwa maendeleo yetu.
Mimi naamini kabisa kama miaka 20 iliyopita Kiswahili kingepewa dhima ya kuwa lugha ya kutolea taaluma katika vyuo vyetu vikuu, basi hivi sasa wataalamu wetu katika fani nyingi, wangekuwa wanaongoza kwa idadi kama mabingwa.Tungeweza kuwa na hata na maprofesa 100 wa Kiswahili!
Kiswahili kina uwezo na silaha. Kama vile kilivyotumika kama silaha ya kumfukuza mkoloni, kinaweza kutumika kutimiza dhima yoyote, mfano kutoa elimu ya juu. Elimu ya sasa kwa kutumia Kiingereza kibovu, iwe katika shule za ‘academy’ au za Serikali, inafanya kiwango chetu cha elimu kuwa duni.
Katika miaka ya 1980 kulikuwa na vuguvugu la kukifanya Kiswahili lugha ya kufundishia vyuo vikuu, badala ya Kiingereza !
Ilikuwa patashika nguo kuchanika, kwani Uingereza ilikuja na mradi wa kuboresha ufundishaji wa Kiingereza. Nadhani mradi ule ndio uliozaa hizo shule za ‘academy’ .
Uingereza ilitoa maelfu ya paundi kukwamisha hatua hiyo ya ukombozi wa lugha yetu ya Kiswahili.
Ukichunguza ni nani aliyefaidika na mradi huo, jibu ni watu binafsi kwa kupata fursa ya kwenda majuu na kujipatia fursa ya kununua bidhaa adimu, ikiwamo magari. Mradi huo haukuzaa matunda, kwa vile kiwango cha uelewa wa Kiingereza kimezidi kuporomoka.
Nikiwa mtaalamu wa Uandishi wa Habari mwenye Stashahada, ilichukua mwaka mmoja kufahamu Kirusi cha kusomea taaluma ya juu ya Uandishi wa Habari.
Hivyo hivyo kwa Watanzania wengine tuliokwenda Urusi miaka hiyo ya 1986-1992, wako walioenda kusomea udaktari, uhandisi wa umeme, mitambo na ujenzi. Wote hao walisomea kwa Kirusi. Hivi sasa wapo hapa nchini wanajenga Taifa katika sekta mbalimbali na wengine wako katika ngazi za Kitaifa.
Niliwahi kupata fursa ya kutembelea Sweden. Kule katika kila watu wawili, mmoja anajua Kiingereza. Lakini hakuna hata mara moja, utasikia Waswidish wanataka Kiingereza kuwa lugha ya kufundishia!
Fikiria katika Tanzania ambako katika watu milioni 36, sio ajabu labda milioni moja ‘wanajua’ Kiingereza na labda 20,000 kati ya hao, ndio wanaweza kukizungumza bila matatatizo yoyote katika’warsha’ na semina.
Lakini ukweli unabakia wengi wanaozungumza siku hizi, wanataka kusifiwa kuwa wanajua Kiingereza kama ishara ya kuwa wamesoma, lakini hali halisi inabakia kuwa ni mambumbumbu kitaaluma. Kung’ang’ania kukitumia Kiingereza ni kufanya upeo wetu wa kitaaluma kuwa duni kwa ujumla.
Hatuna rasilimali za kutosha za kuifanya nchi yetu iwe kama Sweden, ambapo nusu ya wananchi wake wanazungumza Kiingereza. Hata hivyo wanatumia Kiswidish kama lugha yao ya Taifa, ambayo inazalisha magari ya ‘Volvo’ na Scania’ si mnazifahamu!
Kukifanya Kiswahili kuwa lugha ya Taifa ni hatua ngumu, lakini ni ya ukombozi ambayo ilitakiwa ichukuliwe mapema. Kwa sababu kama Urusi waliweza katika Karne ya 18, kwa nini sisi tusiweze wakati huu wa Karne ya 21 ? Kiswahili kitaendelea kutukomboa na kutufanya tupae haraka.
No comments:
Post a Comment