Tuesday, November 27, 2007


Waziri Mkuu Canada atonesha kidonda cha madini Tanzania.

* Asema matatizo ni sheria mbovu ya madini hapa nchini

*Ampongeza Kikwete kwa hatua ya kupitia mikataba ya madini

* Suala la madini Tanzania lazua mjadala Bunge la Canada

* Wabunge upinzani walaumu serikali kwa sheria mbovu

Na Kizitto Noya

SERIKALI ya Canada imetonesha kidonda katika mjadala unaoendelea kwenye sekta ya madini nchini kwa kusema kuwa, sio mpango wa makampuni ya nchi yake kuinyonya Tanzania bali ni mapungufu ya sheria zake katika mikataba ya uwekezaji kwenye sekta hiyo.

Akizungumza jana jijini Dar es Salaam, Waziri Mkuu wa serikali hiyo, Stephen Harper, alisema kuwa uwekezaji katika sekta ya madini nchini unafanywa kwa kutumia sheria za ndani za nchi, hivyo kasoro zinazojitokeza kwenye madini ni matokeo ya ubovu wa sheria hizo.

Harper aliyasema hayo wakati akijibu swali la waandishi wa habari kuhusu mtazamo wa Canada juu ya uamuzi wa Tanzania kupitia upya sheria za mikataba ya madini kwa kuwa iliyopo inawanufaisha zaidi wawekezaji kuliko wazawa. Canada ni mwekezaji namba moja wa makampuni ya madini nchini.

“ Siku zote Canada inaitakia Tanzania mafanikio na ndio maana imekuwa ikiisaidia katika sekta mbalimbali. Kwa hili la kupitia upya sheria za madini, Canada haina tatizo ni afadhali kufanya hivyo ili kuondoa upungufu uliopo,” alisema Harper

Alisema tangu kuanza kwa uhusiano baina ya Tanzania na Canada, nchi hiyo imekuwa mstari wa mbele kuisaidia katika sekta mbalimbali ikiwamo elimu, afya na miundombinu na hata uwekezaji katika madini ulifanywa kama mwendelezo wa jitihada za nchi hiyo, kuikomboa katika umaskini.

Akifafanua kuhusu suala hilo, Rais Kikwete alisema kuwa, uamuzi wa Tanzania kupitia upya sheria zake katika mikataba ya madini, umetokana na ukweli kwamba sheria zilizopo zinatoa fursa kwa wawekezaji kunufaika zaidi na rasilimali hiyo, kuliko Watanzania.

Alisema kinachofanywa ni kupitia na kufanyia marekebisho sheria za ndani za nchi kuhusu madini kwa lengo la kuziboresha ili ziwanufaishe Watanzania na wawekezaji kwa uwiano unaokubalika.

“ Hatuwezi kuwalaumu wawekezaji kwa sababu wanawekeza kwa kutumia sheria zetu wenyewe. Tunachofanya katika zoezi hili ni kupitia sheria hizo na kuweka wazi nani atapata nini na atapataje katika madini,” alisema Kikwete.

Hivi karibuni Rais aliteua Kamati ya kuangalia upya na kupitia mikataba ya uchimbaji wa madini nchini kwa lengo la kuifanyia marekebisho ili iweze kuleta faida baina ya Tanzania na wawekezaji.

Kamati hiyo yenye wajumbe 11 baada ya mmoja kujitoa, inaongozwa na Mwanasheria Mkuu wa Serikali Mstaafu, Jaji Mark Bomani. Wajumbe wake ni pamoja na Mbunge wa Kigoma Kaskazini (Chadema), Zitto Kabwe, Mbunge wa Bariadi Mashariki (UDP), John Cheyo na Mwanasheria wa Wizara ya Nishati na Madini, Salome Makange.

Wengine ni Kamishina wa Sera Wizara ya Fedha, Mugisha Kamugisha, Mkurugenzi Msaidizi Idara ya Makazi Wizara ya Ardhi na Makazi, Edward Kihundwa na Mbunge wa Kyela (CCM), Dk Harrison Mwakyembe.

Wajumbe wengine ni Mbunge wa Msalala (CCM),Ezekiel Maige, Mkaguzi wa Mahesabu kutoka Kampuni ya Kimataifa ya Ukaguzi wa Mahesabu, PriceWater Coopers, David Tarimo ambaye ni mtaalam wa masuala ya kodi, Iddi Simba na Mkurugenzi wa Madai na Sheria za Kimataifa, Wizara ya Katiba na Sheria, Maria Kejo.

Pamoja na mambo mengine, kamati hiyo itakuwa na kazi ya kuchambua mfumo wa kodi unaotumika katika sekta ya madini na kupitia mfumo wa usimamizi wa shughuli za uchimbaji mkubwa unaofanywa na serikali.

Kamati hiyo iliyopewa muda wa miezi wa mitatu kumalizia kazi yake pia inajukumu la kukutana na taasisi zinazosimamia madini na wadau wengine na kutakiwa kutoa taarifa yenye mapendekezo na kupitia mikataba ya madini na nyaraka nyingine zitakazohusu migodi mikubwa nchini.

Katika hatua nyingine, kumeibuka mjadala katika Bunge la Canada wiki iliyopita kuhusu ziara ya waziri mkuu wa nchi hiyo, huku baadhi ya wabunge wakihoji sababu za kutembelea ofisi za Kampuni ya Barrick katika nchi alizotembelea.

Paul Dewar, Mbunge wa Ottawa ya Kati (NDP), aliitaka Serikali nchi hiyo Bungeni kueleza sababu za Waziri Mkuu huyo kufanya hivyo wakati kuna taarifa kuwa, makampuni ya Barrick yamekuwa yakituhumiwa kwa utendaji mbovu katika nchi yanakofanya kazi.

“ Mheshimiwa Spika, Waziri Mkuu amekuwa na tabia ya kutembelea ofisi za Barrick Gold anapokuwa nje ya nchi, amefanya hivyo alipokuwa nchi Chile na sasa yuko Tanzania ambako atazungumzia maslahi ya kampuni hiyo ya Canada ambayo imekuwa ikituhumiwa kwa makosa mengi. Kwa nini Waziri Mkuu aitangaze Barrick ? ” alihoji Dewar

Wakati Waziri Mkuu huyo alipofanya ziara Chile na kutembelea ofisi za Kampuni ya Barrick, alipata upinzani mkubwa ambao ulisababisha walinzi wa nchi hiyo, kumpitishia mlango wa nyuma kwa kuhofia waandamanaji.

Akijibu swali hilo , Katibu wa Bunge katika Wizara ya Mambo ya Nje ya Canada, Deepak Obhrai, alisema Waziri Mkuu huyo, anaitembelea Tanzania kuendeleza uhusiano uliopo baina ya nchi hizo na kutangaza makampuni ya biashara ya Canada yaliyoko huko.

Alisema katika kufanya hivyo, amelazimika pia kutembelea makampuni yote ya biashara ya Canada yanayofanya biashara katika nchi hizo ili kujua namna yanavyofanyakazi.

Kuhusiana na makampuni ya Barrick kutochangia maendeleo katika nchi yaliyowekeza, Obhrai, alisema Canada wana utaratibu wa kuchochea maendeleo, hivyo hata makampuni ya Canada yanapaswa kufanya hivyo kokote duniani wanakowekeza.

No comments: