Ali Karume ataka Serikali
ya Umoja Zanzibar
ya Umoja Zanzibar
Na Ali Suleiman, Zanzibar
SERIKALI ya Umoja wa Kitaifa ndilo suluhisho pekee la kumaliza mgogoro wa kisiasa visiwani hapa kwa kuwa ushindani wa kisiasa ni mkubwa, imeelezwa.
Akizungumza na waandishi wa habari mwishoni mwa wiki iliyopita, Balozi wa Tanzania nchini Italia, Bw. Ali Abeid Karume, alisema bila Serikali ya aina hiyo matatizo ya kisiasa ya Zanzibar ambayo huibuka kila mara unapomalizika uchaguzi mkuu baada ya miaka mitano, itakuwa ndoto kumalizika.
"Huo ndio ukweli uliopo ambao watu wengi hawapendi kuusema ... hali ya kisiasa iliyopo katika visiwa vya Unguja ni ngumu ambapo kasi na nguvu ya chama cha CUF kubwa zaidi katika kisiwa cha Pemba ... Serikali ya Mseto ndilo suluhushi la matatizo," alisema.
Alisema utulivu wa kisiasa tangu kuanza kwa uchaguzi wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi mwaka 1995 umekuwa katika matatizo makubwa kutokana na matokeo na nguvu zinazokaribiana kati ya CCM na CUF.
Balozi Karume alisema hali hiyo imesababisha kuwepo kwa malumbano makubwa na kusababisha uhasama mkubwa kati ya wananchi wa visiwa hivi, ambao ni ndugu kwa muda mrefu.
"Kupunguza malumbano na kujenga Taifa lenye umoja na mshikamano hatuwezi kuepuka Serikali ya umoja wa kitaifa, ambayo itatoa nafasi kwa wananchi wa vyama vyote," alisema Balozi Karume.
Alivitaka vyama vya siasa vya CCM na CUF kujaribu kupanua zaidi mazungumzo ya Muafaka yanayoendelea sasa, katika maeneo mbali mbali.
"Hakuna matatizo, chama kitatoa Rais kwa kura nyingi na chenye kura chache kitatoa Waziri Kiongozi...utaratibu huo ndilo suluhisho la matatizo ambalo litamaliza chuki na uhasama," alisema.
Hiyo ni kauli ya kwanza kutolewa na kiongozi wa ngazi za juu wa Serikali katika masuala ya Muafaka na kuwapo kwa uwezekano wa Serikali ya umoja wa kitaifa.
Uchunguzi uliofanywa na gazeti hili, umegundua kwamba wananchi wengi wa Unguja na Pemba wanataka kupatikana kwa dawa ya kudumu kumaliza malumbano ya kisiasa Unguja na Pemba.
Mazungumzo ya Muafaka kati ya vyama vya siasa vya CCM na CUF yanaendelea nchini, huku yakielezwa kuwapo mafanikio makubwa kwa mujibu wa taarifa za pande mbili husika.
Wiki iliyopita, mazungumzo ya Muafaka kati ya viongozi wa vyama vya siasa vya CCM na CUF yalifanyika chini ya makatibu wakuu, Maalim Seif Shariff Hamad na Bw. Yussuf Makamba wa CCM.
Malumbano ya kisiasa kati ya vyama vya siasa vya CCM na CUF yaliibuka mara ya kwanza mwaka 1995 mara baada ya kumalizika kwa uchaguzi mkuu wa kwanza katika mfumo wa vyama vingi, ambapo Rais mstaafu, Dkt. Salmin Amour aliibuka na kupata ushindi mwembamba dhidi ya mpinzani wake wa karibu, Maalim Seif.
Kumekuwa na juhudi za kumaliza migogoro ya kisiasa katika visiwa vya Unguja na Pemba ikiwemo Muafaka wa kwanza wa kisiasa, ambao hata hivyo haukufanikiwa licha ya kusimamiwa na Katibu Mkuu mstaafu wa Jumuiya ya Madola Chief Emeka Anyaoku.
No comments:
Post a Comment