Marais watano kumjadili
Mugabe leo
*Ni JK, Mwanawasa, Mbeki, Santos na Mswati
Na Mwandishi Wetu
Na Mwandishi Wetu
MARAIS watano wa nchi za Kusini mwa Afrika, wanakutana leo kujadili hali ya Zimbabwe chini ya Rais Jose Eduardo dos Santos wa Angola.
Wengine watakaoshiriki mkutano huo, ni Rais Jakaya Kikwete ambaye ni Mwenyekiti wa Umoja wa Afrika (AU) na Mwenyekiti wa Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika (SADC), Rais wa Zambia, Bw. Levi Mwanawasa.
Marais wengine ni Msuluhishi wa Nchi za SADC katika Zimbabwe, Rais wa Afrika Kusini, Bw. Thabo Mbeki na Mfalme Mswati III wa Swazilandi.
Mkutano huo ni wa Asasi ya Ushirikiano ya SADC ambayo Mwenyekiti wake ni Rais Dos Santos.
Taarifa iliyotolewa jana Dar es Salaam na Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais, ilisema Rais Kikwete aliondoka jana mchana kwenda Mbabane, Swazilandi kwa ajili ya mkutano huo.
Mkutano huo kwa mujibu wa taarifa hiyo, ni wa siku moja na utajadili jinsi SADC na asasi hiyo vinavyoweza kuisaidia Zimbabwe kuondokana na hali yake ya sasa ya machafuko.
Zimbabwe inajiandaa kufanya uchaguzi mkuu wa marudio wa urais ambao umepangwa kufanyika keshokutwa, huku mgombea wa Movement for Democratic Change (MDC), Bw. Morgan Tsvangirai akiwa ametangaza kujitoa.
Bw. Tsvangirai ambaye katika uchaguzi wa awali alipata ushindi mwembamba hivyo kutokidhi kuongoza nchi, amekuwa akidai kuwa uchaguzi huo wa marudio hauwezi kuwa huru na wa haki kutokana na machafuko yanayoendelea nchini humo.
Kutoka gazeti la Majira, Jumatano 25 Juni 2008
No comments:
Post a Comment