Rais Kikwete ana kwa
ana na Rais Barack Obama
Awa kiongozi wa kwanza wa Afrika kukutana na Rais huyo wa Marekani
Rais Obama asema kuwa inatokana na uongozi ulitukuka wa kiongozi wa Tanzania
· Rais Obama ahaahidi kuendelea kusaidia jitihada za Serikali ya Rais Kikwete kuleta maisha bora kwa Watanzania
Ataka kuja kutembelea Tanzania wakati wowote Rais Kiketwe akiwa tayari kumwalika
Rais Barack Obama wa Marekani amemhakikishia Rais Jakaya Mrisho Kikwete kuwa ataendelea kuunga juhudi za Serikali yake katika kupambana na umasikini na kuwaletea Watanzania maisha bora.
Ili kuhakikisha kuwa ahadi hiyo inatekelezwa ipasavyo, Rais Obama amemwelekeza Waziri wa Mambo ya Nje wake, Mama Hillary Clinton na wasaidizi wake katika Ikulu yake ya Washington kufutilia kwa karibu na kwa makini ahadi hiyo.
Rais Obama ametoa ahadi hiyo leo, Alhamisi, Mei 21, 2009, wakati alipomkaribisha Rais Kikwete katika Ikulu ya Marekani kwa mazungumzo, akiwa kiongozi wa kwanza wa Afrika kukutana na Rais Obama tokea achukue madaraka ya kuongoza Marekani Januari 20, mwaka huu.
Mama Clinton alikuwa mmoja wa maofisa sita waandamizi wa Serikali ya Obama waliohudhuria mazungumzo hayo katika Ofisi ya Rais wa Marekani ya Oval Office. Wengine waliokuwapo ni pamoja na Mshauri wa Rais Obama wa uchumi, Larry Summers ambaye amepata kuwa Waziri wa Fedha wa Marekani, Mshauri wa Masuala ya Usalama Jenerali James Jones, Msaidizi wa Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani anayeshughulikia Afrika, Balozi A.S. Carson, ambaye alipata kuwa mwalimu wa kujitolea katika shule ya Malangali ya Iringa wakati wa ujana wake.
Rais Obama amemwambia Rais Kikwete kuwa uamuzi wake wa kumkaribisha na kumfanya kiongozi wa kwanza wa Afrika kukutana naye tokea kuapishwa kuwa Rais wa Marekani, kunatokana na sera za mafanikio na uongozi ulitukuka wa Rais Kikwete.
“Napenda kukupongeza kwa uongozi wako mzuri wa Tanzania na pia kwa uongozi wa Umoja wa Afrika (AU), hata kama umemaliza muda wa uongozi wako wa umoja huo,” Rais Obama amemwambia Rais Kikwete na kuongeza:
“ Nataka ufanikiwe katika uongozi wako. Niambie unataka tukuunge mkono vipi ili uendeleza mafanikio ambayo Serikali yako imeyapata…Unakuwa kiongozi wa kwanza kukutana nami tokea niingie madarakani. Hii ni ishara ya imani yangu na ya Serikali yangu katika uongozi wako. Ninafurahishwa na uongozi wako.”
Bila kusita Rais Obama amemwambia Rais Kikwete: “Nataka kuja kutembelea Tanzania. Mara ya mwisho niliiona Tanzania kutokea upande wa pili wa Hifadhi ya Taifa ya Serengeti.”
Ameongeza Rais Kikwete katika mkutano huo: “ Serikali yangu nzima inavutiwa na uongozi wako. Tunapenda kuunga mkono uongozi wako na kufanya kila linalowezekana kufanikisha hilo ili uendelee kuwatumikia wananchi wa Tanzania.”
Rais Obama pia amemsifu Rais Kikwete kwa uongozi wake katika kuboresha elimu nchini, na kumhakikishia kuwa misaada yote ya ujenzi wa miundombinu itakayotolewa chini ya akaunti ya Millennium Challenge Account (MCC) itaharakishwa, ili ujenzi wa miradi hiyo uanze.
“Msimamo wako wa kuweka mkazo katika elimu ni mfano usiokuwa na kifani wa uongozi. Hii miradi ya MCC… tutaangalia nini kifanyike ili ianze kutelekezwa haraka iwezekanavyo, na kama lazima tuiongeze.”
Utawala wa Serikali ya Rais George W Bush uliondoka madarakani baada ya kuwa umeidhinisha msaada wa kiasi cha dola milioni 700 kwa ujenzi wa miundombinu katika Tanzania chini ya MCC.
Obama hakusema kuwa ataongeza kiasi gani katika raundi ijayo ya misaada ya MCC kwa Tanzania ama kama anakusudia kukipiku kiasi hicho kilichotolewa na Rais Bush.
Rais Kikwete amempongeza Rais Obama kwa kuendelea kuiunga mkono Tanzania na Afrika, lakini akataka Marekani kuunga zaidi juhudi za Tanzania katika jitihada za kufuta umasikini, kuhakikisha kuwa kuna chakula cha kutosha katika Afrika kwa kuunga mkono jitihada za kuboresha kilimo, kuendelea kuunga mkono jitihada za kuboresha elimu na hasa ile ya sayansi, na kuendeleza mapambano dhidi ya magonjwa ya malaria, ukimwi na kifua kikuu.
Rais Kikwete pia ameutaka uongozi wa Rais Obama kuendeleza na juhudi za kupunguza vifo vya akinamama wakati wa uzazi na kuisadia Tanzania na Bara la Afrika kukabiliana na athari za kuvurugika kwa uchumi duniani.
Viongozi hao pia wamejadili baadhi ya migogoro mikubwa katika Afrika ukiwemo ule wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC), Darfur katika Sudan, Somalia na hali ya kisiasa ilivyo katika Kenya.
Rais Kikwete pia amemweleza Rais Obama kuhusu jitihada zinazofanywa na Serikali yake kuleta suluhu ya kisiasa katika Zanzibar.
Rais Obama amemwomba Rais Kikwete kuendelea kuwasilisha na Serikali ya Marekani kwa namna ya kushauri kuhusu jinsi gani Serikali hiyo inavyoweza kuchangia katika kutafuta utatuzi wa migogoro inayolikabili Bara la Afrika hasa ile ya DRC na Darfur.
Mapema kabla ya kukutana na Rais Obama, Rais Kikwete leo amekutana na kufanya mazungumzo na Waziri wa Mambo ya Nje wa Marekani, Mama Hillary Clinton kwenye Wizara ya Mmbo ya Nje ya Marekani mjini Washington.
Mama Clinton alitaka kujua jinsi gani Marekani inaweza kulisaidia Bara la Afrika kuondokana na matatizo yake, na Rais Kikwete ametoa maelezo ya kina kuhusu jinsi gani jambo hilo linaweza kufanikishwa.
Viongozi hao pia wamejadili Kenya na hali ya kisiasa katika Zanzibar na kuhusu migogoro mingine inayolibaliki Bara la Afrika.
Rais Kikwete leo anaendelea na ziara yake katika Marekani kwa kukutana na viongozi wa vyombo vya kimataifa vya fedha duniani.
Kutoka: Ikulu Mawasiliano
1 comment:
Hawa ni maraisi wawili duniani wanaopendwa sana na wananchi wao, na mabao unaweza kusema wamechaguliwa si wananchi tu bali na ulimwengu mzima.
Post a Comment