Kunyamaza pia ni dawa...!
Nawashukuru sana shoga zangu kwa kujiunga tena nami kupitia ukurasa huu hapa, ...maana bwana kila siku naisema hii; bila ninyi ukurasa huu unakosa msisimko, kwa sababu makala hizi zitakosa msomaji, hebu fikirieni wenyewe itakuwaje?.
Shukrani za dhati ziwaendee waanoendelea kuniandika, inaonyesha ni jinsi gani ninawagusa, mbarikiwe jamani.
Nimegundua pia kuwa tofauti na adhma halisi ya hii kona kuwa ni ya wanawake tu hata wanaume nao wamo, rukhsa!
Naheshimu sana mawazo yenu shoga zangu na ni kwa sababu hizo napenda kuendelea kupokea maoni yenu, hayo ni chachu ya kunifanya niendelee kuleta mambo pande hizi.
mnaweza kuendelea kuniandikia, tumia anuani hii: asmahmakau@mwananchi.co.tz
Leo niko hapa kwa ishu hii.... kunyamaza pia ni dawa!
Mnapoishi wawili katika kuta mmoja suala la kupishana ni jambo la kawaida kabisa. Na nikweli kwamba tatizo linapojitokeza namna hii basi linahitaji kutatuliwa kwanza kisha mengine yatafuata.
Na mara nyingi mizozo inakuja kama matokeo ya kitu fulani, kwa hiyo ugumvi unaweza kuja kuwa sababu ya wewe kuamka kutoka katika usingizi mzito uliolala.
Wengi wetu tunapoudhiwa hukimbilia kuchukua hatua lakini wakati mwingine kunyamaza pia ni njia sahihi ya kutatua matatizo.
Wataalam wengi wa masuala haya wanashauri kuchukua hatua pale unapotendwa visivyo...
Lakini kwa bahati mbaya sana kutotumia njia sahihi ya kutatua matatizo katika mahusiano kunaweza kupelekea mwisho mbaya wa mahusiano yenu na usishangae mkaja kutafutana na visu hapa mjini.
Kwa mujibu wa uchunguzi uliofanywa ambao si rasmi umebaini kuwa si kila ugomvi unafanikiwa kufikia malengo yanayokusudiwa... na kwa sababu hiyo basi ni vyema ukajua wapi useme na wapi unyamaze.
Mpaka hapa nadhani ushanifaham.
Vile watu mnavyogombana unaweza kujua kule uhusiano unakoelekea kama mtadumu milele ama mtafikia mwisho wa safari na kuonana kama paka na panya.
Kama wewe ni mmoja ya wale watu ambao huchagua kupayuka muda wote kuna wakati ni vizuri ukabadilisha stail ili umeweke pahala fulani mwenzako akae chini ajiulize unategemea nini hasa.
Nyamaza, anategemea umuulize usimuulize na badala yake usilipize na wala usimpatilize, utamtia adabu.
Unapoamua kuongea ni vyema ukajua njia sahihi ya kuwasilisha mambo ili kuweza kufikia muafaka.
Na unapoongea mara moja mara mbili mara tatu sasa ni wakati wa kunyamaza. Unapoa mua kuchua hatua hii ya kunyamaza basi ni vyema ukajua kuwa kwa hatua hii pia hujakosea. Wakati huu huu tafakari hatama ya maisha yako...
Mathalani ushamueleza dukuduku lako mara kadhaa sasa...wakati wa kufunga mdomo wako sasa umefika na kuendelea na mambo mengine muhimu katika maisha yako.
Inapokuja katika kutatua migogoro yenu, njia hii ni nzuri wakati mwingine.
Wengi wetu hutumia migogoro kusema na kuropoka bila kutoa nafasi, hali hii inaweza ikazoeleka na kushindwa kuwaleta mabadiliko yoyote. Unapoamua kumpuuza utashangaa mambo yanavyobadilika.
Kujua na kujaribu kutumia njia sahihi ya kugombana kutasaidia kutatua migogoro yenu.
Kivipi? Kama unavyojua kusema maneno yanayoudhi ni kama kumtupia kijinga cha moto mtu ambaye tayari ameshaoga mafuta ya taa.
Kitu cha muhimu katika ugomvi ni kusema kile ambacho unakitaka kifikishe ujumbe wa uliyonayo moyoni, si kumtusi ama kumsema maneno ya kumuudhi kunakoweza kuwaleta katika muafaka. Na ukishasema sana nyamaza...
Gombana ili ueleweke, usigombane ili kuhamisha maumivu kwa mwenzio.
2. Tatua tatizo...
Ukishaelewa kwa nini mnagombana, na ukajua sababu iliyopelekea kwanini mwenzako akachukua uamuzi uliokuudhi, sasa ni wakati wa kutafuta muafaka wa tatizo. Wazungu wanaita compromise.
Wakati mwingine unaweza kukuta jambo kubwa mliligombania linakuwa dogo kutokana na uelewa wenu kwa kila moja wenu. Na njia uliyotumia kufika muafaka huo.
Wakati mwingine unapogombana na mwenzio ukagundua kuwa ugomvi wenu haukuwa wa maana mnaweza kuchagua kukubali kutokubaliana na mkaendelea kuishi, si ushamjua bwana.
3. Kupeana muda, pia inafaa...
Ukishajua anajua kuwa amekuudhi, unaweza ukatumia njia hii. Mpe muda afikirie kwa makini kwa wakati wake na aamue... inatosha.
Ni hayo tu kwa leo. Usikose wiki ijayo.
- Na Asmah Makau
Email to: asmahamakau@mwananchi.co.tz
No comments:
Post a Comment