Serikali yabadili muundo wa
vyeti vya kuzaliwa Tanzania
Na Felix Mwagara
WAKALA wa Serikali wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), katika kupambana na udanganyifu wa vyeti vya kuzaliwa nchini umeanza kutoa vyeti vipya vya kuzaliwa vyenye alama maalum za usalama.
Vyeti hivyo vinavyotengenezwa kwa kutumia kompyuta, vimeanza kutolewa wiki iliyopita katika maadhimisho ya wiki ya Utumishi wa Umma jijini Dar es Salaam.
Akizungumza a mwandishi wa habari hii jana, Afisa Usajili Msaidizi wa Rita, Joseph Mwakatobe alisema kumekuwa na udanganyifu mkubwa sana wakati wanakuwa wanavihakiki vyeti vingi katika ofisi zao ndio maana wameamua kuvifanyia mabadiliko katika utaalum maalum ili mtu yoyote asiweze kufanya udanganyifu wa vyeti hivyo.
“Tumeanza kufanya mabadiliko kwenye vyeti vya kuzaliwa na kwa kuanzia tuliona vema kuanza kutoa wakati wa maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma na sambamba na ofisi ya Makao Makuu ambayo nayo imeanza kutoa”, alisema Mwakatobe.
Alisema vyeti vipya vina mvuto wa pekee kutokana na karatasi iliyotumika kuwa nzuri na tofauti kabisa na ile ya zamani na kwamba pia vina alama za kiusalama ambayo inawasaidia kutambua kama cheti ni sahihi ama siyo na kwamba vinatengenezwa kwa kompyuta tofauti na vile vya zamani ambavyo vilikuwa vinatengenezwa kwa kuchapa kwenye mashine.
Mwakatobe alisema pamoja na kuanza kuvitoa katika wilaya za Mkoa wa Dar es Salaam ofisi yake bado haijaanza katika mikoa mingine, ingawa inatarajia kuendelkea katika mikoa ya Pwani na Tanga.
Alipoulizwa kuhusu wenye vyeti vya zamani kutambulika kwao, Mwakatobe alisema vyeti vya zamani vitaendelea kutumika na itakapohitajika kila mtu awe na cheti kipya basi serikali itatangaza.
“Kwasasa vile vyeti vya zamani vitaendelea kutumika kama kawaida, itakapofikia muda wa kila Mwananchi awe na cheti kipya na kile cha zamani kisitumike , wananchi watajulishwa” alisema Mwakatobe.
Aidha, Yusufu Bakari mkazi wa Gongolamboto aliyekuwa anatembelea mabanda mbalimbali uwanjani hapo alipohojiwa kuhusu hatua ya Rita kubadilisha vyeti alisema serikali imefanya jambo la msingi kwa kufanya mabadiliko hayo kwani hapo mwanzo hata yeye mwenyewe alipewa cheti feki mtaani kwao.
“Kwa hatua hiyo napenda kuipongeza serikali kwani hata mimi nilishapewa cheti feki lakini kwasasa inabidi nikitafuta hicho kipya, hii tabia ya cheti feki imezagaa mtaani hasa hapa Dar es Salaam” alisema Bakari.
No comments:
Post a Comment