Sunday, June 28, 2009

Sheikh Suleiman Gorogosi

afariki dunia katika

ajali ya gari




Na Said Hauni, Lindi, 27.6.2009


KAIMU Mufti wa Tanzania, Sheikh Suleiman Gorogosi amefariki dunia katika ajali ya gari iliyotokea kwenye Kijiji cha Mnolela Wilaya ya Lindi Vijijini baada ya tairi ya mbele ya gari alilokuwa akisafiria kutoka Mtwara kupasuka na kupinduka.

Habari zilizopatikana na kuthibitishwa na Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Lindi, Sifuel Shirima zinaeleza kuwa tukio hilo lilitokea jana saa 8:09 katika barabara ya Mtwara-Lindi wakati akitokea Uwanja wa Ndege Mtwara baada ya kushuka kwenye ndege akitoa jijini Dar es Salaam.

Kamanda Shirima alisema katika gari hilo kulikuwa na watu watatu, akiwamo Bakari Maguo, mfanyabiashara wa Lindi ambaye ni mmiliki wa gari hilo na aliyewahi kuwa Mwenyekiti wa CCM Lindi mjini, Bakari Fundi ambao wamejeruhiwa na kulazwa katika Hospitali ya Ligula mkoani Mtwara.

Gorogosi alikuwa amekwenda Lindi kufungisha ndoa ya mtoto wa Maguo ambaye ni mfanyakazi mstaafu wa Shirika la Taifa la Mfuko wa Hifadhi ya Jamii (NSSF), ambayo ilikuwa ifungwe leo.

Ndugu wa marehemu Abilahi Mohammed aliiambia Mwananchi Jumapili jana kuwa mazishi wa Gorogosi ambaye alikuwa Sheikh Mkuu wa Mkoa wa Lindi yatafanyika saa 10:00 jioni leo jioni mjini humo.

Pia Baraza la Waislam Tanzania (Bakwata), lilitoa taarifa jana jioni likieleza kuwa Gorogosi lilithibitisha kifo cha Gologosi na kueleza kuwa atazikwa leo.

Marehemu ameacha wake wawili. Kabla ya kifo chake alikuwa pia mjumbe wa baraza la Ulamaa la Bakwata.

Siku za hivi karibuni, Sheikh Gorogosi alikuwa akisumbuliwa na ugonjwa wa kisukari ambao ulimfanya kulazwa katika hospitali binafsi ya Fire jijini Dar es Salaam kwa wiki mbili, na juzi aliruhusiwa kurudi nyumbani kabla ya kwenda Lindi.

Mufti Sheikh Issa Bin Shaaban Simba alivunja baraza la maulamaa na kamati ya hija ya baraza hilo na kuviunda tena vyombo hivyo, huku akimkabidhi kukaimu nafasi yake Sheikh Gorogosi.

Mufti Simba, ambaye awali alikuwa Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Shinyanga, alichaguliwa na Mkutano Mkuu wa Bakwata kushika wadhifa wa Umufti Oktoba 13, mwaka 2002, mkoani Dodoma katika uchaguzi ambao, masheikh tisa walijitokeza kuwania wadhifa huo. 



Masheikh hao, ni pamoja na marehemu Sheikh Gorogosi, Sheikh Suleiman Kilemile, Mbunge wa zamani wa Kibiti, Profesa Juma Mikidadi, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Ma`amur, jijini Dar es Salaam, Sheikh Ahmed Twalib, Imamu Mkuu wa Msikiti wa Manyema, Kariakoo, Hamid Jongo.

Wengine, ni aliyekuwa Naibu Mufti, Sheikh Abubakar Zubeir, aliyekuwa Mjumbe wa Baraza la Ulamaa la Bakwata, Sheikh Ahmed Zubeir, Sheikh wa Bakwata Mkoa wa Kigoma, Tawfiq Malilo na aliyekuwa Msaidizi wa Mkurugenzi wa Idara ya Dini (Kitengo cha Usuluhishi) ya Bakwata, Sheikh Twaha Majaliwa.

Kutoka Mwananchi

No comments: