Saturday, June 20, 2009

USANII WA KUHAMIA DODOMA:

Tutakamilisha kuhamia

Dodoma baada ya karne nzima






Bunge la Jamhuri ya Muungano mjini Dodoma.

Marmo:Kuhamia Dodoma si wimbo
Imeandikwa na Basil Msongo, Dodoma;

Ofisi ya Waziri Mkuu imesema, bado kuna dhamira ya dhati ya kuhamisha makao makuu ya Serikali kutoka Dar es Salaam kwenda Dodoma na itatungwa sheria ya kuitambua Dodoma kuwa ni Mji mkuu wa Tanzania.

Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ya mwaka 2005 imeelekeza kutungwa kwa sheria hiyo baada ya mjadala wa kitaifa wa kukusanya maoni ya wananchi na wadau mbalimbali ili kuboresha mkakati wa kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Waziri Mkuu, Sera, Uratibu na Bunge, Philip Marmo amepinga mtazamo kuwa kuhamia Dodoma kutaendelea kuwa wimbo kwa kuwa majengo ya Serikali yanaendelea kujengwa Dar es Salaam.

“Dhamira ya dhati ilikuwepo muda ule na hadi sasa dhamira hiyo ipo” Marmo amesema na kubainisha kwamba, mpango kabambe wa kuhamishia makao makuu Dodoma utaangaliwa upya.

Wakati akiwasilisha bajeti ya Ofisi ya Waziri Mkuu kwa mwaka wa fedha 2008/2009, Waziri Mkuu, Mizengo Pinda alisema, kutakuwa na mjadala wa kitaifa kuhusu kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma.

Waziri Marmo amesema bungeni jana kuwa, kuhamia Dodoma kunahusisha mambo mengi ikiwa ni pamoja na kuimarisha miundo mbinu mingine.

“Tunaposema kuhamishia makao makuu hatuongelei majengo tu” amesema kiongozi huyo wa Serikali kwenye kikao cha tisa, mkutano wa 16 wa Bunge unaoendelea Dodoma.

Alikuwa anajibu swali la Mbunge wa Viti Maalum, Esther Nyawazwa aliyesema kuhamia Dodoma imekuwa wimbo na akahoji mbona majengo ya Serikali yanaendelea kujengwa Dar es Salaam.

Waziri Marmo pia alikuwa akijibu swali la Mbunge wa Iramba Mashariki, Mgana Msindai aliyetaka kufahamu kwa nini Serikali haiharakishi kuhamishia makao makuu ya Serikali Dodoma.

Mbunge huyo pia alitaka kufahamu kwa nini Serikali isitenge fedha katika bajeti ya mwaka ujao kuboresha miundombinu ya Dodoma badala ya kuzisubiri dola za Marekani milioni 28 zilizoahidiwa na Benki ya Dunia.

Awali, Msindai alimuuliza Waziri Mkuu ni kwa nini Serikali isiwasilishe bungeni muswada ili kubadili utaratibu wa kuanzishwa kwa Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu(CDA) na kama haioni kama kuna mgongano wa mkubwa kati ya mamlaka hiyo na Manispaa ya Dodoma.

“Serikali ina mpango na inakusudia kuwasilisha bungeni Muswada wa sheria unaolenga kuitambua Dodoma kuwa Mji Mkuu wa Nchi yetu ambao pia utaanishwa bayana na kutambulisha shughuli za ustawishaji makao makuu” amesema.

Waziri huyo amesema, CDA na Manispaa ya Dodoma hazina mgongano wa kimaslahi kwa vile mamlaka hizo zimeundwa kwa kuzingatia misingi ya sheria ikiwa ni pamoja na kila moja kuanishiwa majukumu yake kwa mujibu wa sheria na kwamba, Waraka wa Baraza la Mawaziri namba saba wa mwaka 1998 umeainisha majukumu ya CDA na manispaa ya Dodoma.

Kwa mujibu wa Waziri Marmo, mpango kabambe uliopo sasa wa mwaka 1974 umepitwa na wakati kwa kuwa ulilenga kuhudumia jumla ya watumishi na wafanyabiashara 120,000 ambao wangehamia Dar es Salaam.

Amesema, idadi ya waliohamia Dodoma ni mara 200 ya watu waliokadiriwa katika mpango huo kabambe na ametoa mfano kuwa, Chuo Kikuu cha Dodoma kinakadiria kuongeza watu 60,000, na vyuo vingine watu 40,000.

Marmo amelieleza Bunge kuwa, Serikali imeanza kuwashirikisha wafadhili kutekeleza programu ya Ustawishaji makao makuu na kwamba, Benki ya Dunia imeahidi kutoa jumla ya milioni 28 za Marekani kwa ajili ya kuendeleza miundombinu.

“Kati ya fedha hizo Mamlaka ya Ustawishaji Makao Makuu imeahidiwa kupewa dola milioni 14 za Marekani kwa ajili ya kutekeleza miradi ya barabara na mfumo wa maji machafu, wakati dola milioni 14 nyingine zitatumiwa na manispaa kukarabati miradi iliyo chini yake” amesema Marmo.

No comments: