Saturday, July 18, 2009

Ubabe wa polisi:

Nilimuonya askari

asitembee na mke wangu,

lakini akanishtaki'




Keneth Goliama na Farida Abdul

MSHTAKIWA Yasin Adam (39), mkazi wa jijini Dar es Salaama ameieleza Mahakama ya Kimara kuwa alibadilishiwa kesi baada ya kwenda kituo cha polisi cha Kibo na kumtaka askari CPL Yahya D.8602 aache kutembea na mke wake.

Mshitakiwa jana alidai baada ya kubadilishiwa kesi hivi sasa amefunguliwa kesi ya kufanya fujo na kutishia kumuua koplo Yahya pamoja na kuambulia kipigo.

Mbele ya Hakimu Tabu Lwambali wa Mahakama hiyo, Adam alidai kuwa kabla ya kwenda katika kituo hicho na kupigwa, Koplo Yahya alimwambia kuwa anatembea na mke wake kwa sababu mke wake hamtaki.

"Mimi nilikwenda kituoni siyo kuleta fujo, bali nilikwenda kumwambia Koplo Yahya aachane na mke wangu kwani mara nyingi nimewahi kumkuta na mke wangu maeneo mbalimbali, ikiwemo buchani akimnunulia nyama na baa ya Kibo," Adam aliiambia Mahakama alipopewa nafasi ya kujitetea.

Awali mbele ya Hakimu Tabu Lwambali ilidaiwa kuwa Mei, mwaka huu mshtakiwa alimtishia kwa maneno CPL Yahya D.8602 kuwa angemuua.

Awali katika shtaka la kwanza mbele ya Hakimu Joyce Moshi ilidaiwa kuwa Julai 11, mwaka huu katika Kituo cha Polisi cha Kibo Ubungo, saa 9.00 mchana, mshtakiwa alimfanyia fujo CPL Jumanne E.1568 kwa kukataa kuingia mahabusu.

Hata hivyo mtuhumiwa alikana mashtaka yote na kesi hizo mbili zinazomkabili mtuhumiwa huyo, zimehairishwa mpaka Julai 29 mwaka huu.

Akizungumza na Mwananchi nje ya mahakama Adam alisema kuwa alitoa taarifa polisi kumuonya askari huyo, ili aachane na mke wake na askari huyo, alikubali kuvunja uhusianp na mke wake, lakini hakufanya hivyo.

Alisema ana hofu kuwa mahusiano kati ya mkewe na askari huyo yalianza baada ya mke wake kushikiliwa katika kituo cha Kibo mwaka 2007 kutokana na kosa la , kumjeruhi kwa chupa tumboni mshtakiwa huyo.

"Pamoja na mke wangu kunipiga na kunichana na chupa, lakini tulisharudiana kwa kuombana msamaha na mambo yakaisha, nampenda sana hivyo ninachokitaka ni haki itendeke," alisema Adam.

Kutoka Mwananchi

No comments: