Sunday, September 06, 2009

Brazil yaiabisha Argentina

mjini Rosario

(Argentina – Brazil 1-3)





Brazil tayari imeshapata tiketi ya kucheza Afrika Kusini. Argentina iko kwenye hatari ya kukosa fainali za kombe la dunia la soka, baada ya kunyukwa nyumbani magoli 3-1 na Brazil. Argentina iko kwenye nafasi ya nne kwenye kundi la Amerika ya kusini. Kama wakifungwa na Paraguay Jumatano ya keshokutwa, halafu Colombia wakiifunga Uruguay, Argentina itakuwa na hali ngumu.

Dakika ya 24, Elano alipiga frikiki na Luisao hakufanya ajizi, akafunga goli la kwanza la Brazil kwa kichwa. Kabla Argentina, hawatulia na mshtuko wa goli la kwanza, Kaka alifanya kazi nzuri na kumpa pasi Maicon akapiga shuti na kipa wa Argentina Mariano Andujar akautema mpira, bila kufanya mzaha Luis Fabiano akafunga goli la pili.

Kwenye dakika ya 65 baada ya kipindi cha pili, Jesus Datolo, alipiga kwenye toka mita 30 na kuipatia Argentina kifutia chozi. Bila Argentina kujua nini kinatendeka, Brazil walifanya shambulizi kama la nyuki, Kaka alianza tena na akatoa pasi murua kwa Luis Fabiano aliyemtoka Nicolas Otamendi na kumvisha kanzu golikipa wa Argentina na kuandika goli la tatu kwa Brazil. Kama Brazil watacheza kama walivyocheza usiku wa kumkia leo na Argentina, nchi zingine zilie tu zitakapocheza na Brazil kwenye fainali nchini Afrika Kusini, kwani Brazil wameonyesha soka safi sana ambalo ni vigumu kwa timu ingine yoyote kulihimili.


No comments: