Mwakyembe siri yafichuka
Siku tatu baada ya kutiwa mbaroni, Daniel Mwakalinga, anayeshukiwa kuandaa njama za kumdhuru Mbunge wa Kyela, Dk Harrison Mwakyembe, ujumbe uliokutwa kwenye simu yake unadaiwa kuwahusisha vigogo wa Mkoa wa Mbeya katika maandalizi ya kummaliza kisiasa.
Hatua ya ujumbe mfupi uliokutwa kwenye simu ya mtuhumiwa, unadaiwa kuweka hadharani majina ya vigogo hao wanaohusika na njama hizo ambao kwa muda mrefu wamekuwa wakituhumiwa kumhujumu kisiasa.
Taarifa za polisi zinadai kuwa ujumbe mbalimbali uliokutwa kwenye simu za mtuhumiwa zilizochukuliwa kwa uchunguzi, zinawahusisha moja kwa moja vigogo kadhaa wa CCM na serikali ya Mkoa wa Mbeya kuhusika na njama hizo.
“Sms (ujumbe) hizi zinathibitisha taarifa ambazo tumekuwa nazo kwa siku nyingi...anahusika na vurugu zote za kisiasa zinazotokea Kyela kwa lengo la kumdhoofisha Dk Mwakyembe,” kilidai chanzo chetu kutoka polisi.
Licha ya chanzo hicho kushindwa kutoa undani wa sms hizo, mmoja wa wasaidizi wa Dk Mwakyembe (jina linahifadhiwa), alidai kuwa aliweza kuona baadhi ya ujumbe huo baada ya kumfikisha mtuhumiwa polisi.
Pia zinaonyesha mtiririko wa fedha kutoka nje ya nchi kupitia moja ya mikoa ya Kaskazini kabla ya kuwafikia walengwa mkoani Mbeya.
Mmoja wa wanaotishiwa ni mwandishi wa habari Richard Kilumbu ambaye anadaiwa kumuunga mkono Dk Mwakyembe.
Ujumbe mwingi unatoa taarifa kutoka kwa mtu wanayemwita 'mzee' na nyingine zinamtaja kigogo mmoja wa mkoa moja kwa moja.
Taarifa za mtandao huo zinadai, mmoja wa wapambe wa kigogo huyo na wapigadebe wa mwanamtandao anayeishi nje ya nchi, tayari anafanya kampeni kuwania ubunge mwenyewe.
“Hawa na kundi lao wanaendesha kampeni kali vijijini za kujinadi sambamba na kundi la ... kwa Kyela hakuna cha muda rasmi kuanza kampeni maana wote hawa wana baraka zote za kigogo wa Serikali mkoa na CCM,” alidai mjumbe wa Halmashauri Kuu ya CCM Mkoa wa Mbeya. Majina na sms hizo kwa sasa tunayahifadhi.
Baadhi ya wananchi waliohojiwa walidai kuwa, hali tete ya kisiasa imesababishwa na uamuzi wa makosa au makusudi kuteua mtu ambaye ana uhasama na mbunge.
Hoja hiyo inaungwa mkono na wazee na vijana na kwamba, lawama zote za kudhurika kwa mbunge wao zitabebwa na serikali.
“Mbona haijafanya hivyo kwa majimbo mengine? Kyela tu! Mbunge wetu kakosea nini?” alihoji Mzee Kandambili Malundi, mkazi wa Ikolo.
Taarifa zilizotufikia jana jioni zilidai kuwa mwandishi wa habari, Richard Kilumbo, tayari amefungua jalada la malalamiko polisi kuhusiana na sms anazopata kutoka wanamtandao hao.
Akizungumzia matukio hayo, Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Mbeya, Advocate Nyombi alisema jana jioni kuwa vielelezo vya Mwakalinga vimechukuliwa kwa uchunguzi zaidi.
Nipashe ilitaka kujua iwapo simu ya Mwakalinga nayo inashikiliwa, hivyo RPC Nyombi alikuwa na haya ya kujibu: "Nimekueleza kwamba vielelezo vyote ya mtuhumiwa vinashikiliwa nadhani unaelewa maana ya kusema hivyo."
Kutoka Nipashe
No comments:
Post a Comment