Wednesday, September 23, 2009

Zamadamu zagunduliwa

Engaro Sero, ziwa Natron



Wizara ya Maliasili na Utalii, inapenda kuujulisha umma kuwa nyayo zingine za Binadamu wa Kale (Zamadamu) zimeonekana katika mwamba ulioko katika Kempu ya Engare Sero iliyoko karibu na Ziwa Natron Mkoani Arusha.

Nyayo hizo ambazo zinakadiriwa kuwa na umri wa miaka 120,000 ziligunduliwa mwaka 2006 na mfanyakazi wa Kempu ya Engare Sero, Gerald, na mpwa wa mmiliki wa Kempu hiyo, Juliana Von Mutirs, waliokuwa katika matembezi ya jioni katika kempu hiyo.

Wawili hao, mara baada ya kuziona nyayo hizo walimtaarifu mmiliki wa kempu hiyo Bw. Tim Leach ambaye aliwasiliana na mtaalamu wa akiologia kutoka Chuo Kikuu cha Pennsylvania Marekani, Dkt. Godwin Mollel na mshauri wake kutoka Chuo Kikuu cha Rutger cha Marekani, Dkt. Carl Swisher, kuja nchini kuchunguza nyayo hizo.

Mwaka 2008, wataalam hao wakiongozwa na Bw. Jim Brett wa Taasisi ya Elimu ya Uhifadhi iliyoko Pennsylvania, walipata kibali cha kufanya utafiti katika eneo zililopo nyayo hizo. Walichukua sampuli ya majivu na sehemu ya nyayo kutoka kwenye nyayo nyingi zilizopo eneo hilo kwa ajili ya kuzifanyia uchunguzi kwenye maabara ya Malikale nchini Marekani.

Jopo hilo la wataalam 7 wakiwemo watanzania wawili, Dkt. Godwin Mollel na Godfrey Ollemoita wanaendelea na utafiti kuhusu nyayo hizo za Engare Sero ambazo zinaonyesha dhahiri unyayo na alama za vidole vyake. Hadi sasa jumla ya nyayo 57 zimeshafukuliwa katika eneo hilo.

Kwa kuwa nyayo hizo zina umri wa miaka 120,000, huu ni uthibitisho kuwa hizo ndizo nyayo kongwe kuliko zote zilizowahi kugunduliwa za binadamu anayefanana na kizazi hiki ajulikanaye kama Homo Sapiens.

Nyayo hizi ziko kwenye mwamba imara zaidi ukilinganisha na ule ambao Nyayo za Laetoli zipo.

Mwezi Agosti 2009, Katibu Mkuu wa Wizara ya Maliasili na Utalii, Dkt. Ladislaus Komba na Mkurugenzi wa Mambo ya Kale, Bw. Donatius Kamamba, walitembelea eneo la Ziwa Natron kujionea nyayo hizo, na sasa Wizara inaandaa utaratibu wa kuzihifadhi nyayo hizo za Binadamu wa Kale.

Dkt. Ladislaus Komba

KATIBU MKUU

No comments: