WATANZANIA wametakiwa kutowapa nafasi watu wabaya wanaotaka kuigawa nchi kwa dini, kabila, rangi, Bara na Visiwani au Unguja na Pemba.
Pia wametakiwa kuwanyima nafasi wanaotaka kuleta machafuko nchini. Mwito huo ulitolewa jana na Rais Jakaya Kikwete katika salamu zake za Mwaka Mpya alizozitoa kwa Taifa kupitia vyombo vya habari.
“Kamwe tusikubali kuwa kama wale wenzetu tuliowapa hifadhi hapa kwetu au tunaowaona kwenye luninga na kuwasikia katika redio na kuwasoma katika magazeti wakiuana, kuumizana na kuharibiana mali huko nchini kwao. Nina imani kubwa kwamba hatutaiacha nchi yetu ifike hapo,” alisema Rais Kikwete.
Aliwashukuru na kuwapongeza kwa dhati Watanzania kwa ukomavu wa kisiasa, moyo wao wa uzalendo na busara waliyotumia ya kukataa kuwa wahanga wa njama ovu.
Rais alizungumza mengi kuhusu afya, elimu na kilimo ifuatayo ni hotuba yake kamili kama ilivyotangazwa na TBC1
SALAMU ZA MWAKA MPYA ZA RAIS WA JAMHURI YA MUUNGANO WA TANZANIA, MHESHIMIWA JAKAYA MRISHO KIKWETE, KWA WATANZANIA, TAREHE 31 DESEMBA, 2009
Utangulizi
Ndugu Wananchi;
Kama ilivyo ada naomba nianze kwa kumshukuru Mwenyezi Mungu kwa kutujaalia uhai na kutuwezesha kufika siku ya leo ya kuuaga mwaka 2009 na kuukaribisha mwaka 2010. Wapo wenzetu wengi tulioanza nao mwaka lakini hawakujaaliwa kuwa nasi siku hii ya leo kwa kuwa wametutangulia mbele ya haki. Tunamuomba Mwenyezi Mungu awape mapumziko mema. Kwa wenzetu wanaougua tuwaombee awape nafuu ya haraka ili waendelee kutoa mchango wao katika maendeleo yao, jamii zao na taifa zima kwa jumla. Aidha, tuendelee kuomba rehema za Mola wetu atujaalie afya njema na umri mrefu ili tuweze kuushuhudia mwaka wote wa 2010 na miaka mingine mingi ijayo.
Ndugu Wananchi;
Kama wote mlivyosikia, leo, siku ya mwisho ya mwaka 2009, Taifa letu lilipata msiba mkubwa wa kuondokewa na Mzee wetu, Mzee Rashid Mfaume Kawawa, Makamu wa Rais na Waziri Mkuu Mstaafu.
Kama nilivyoeleza wakati nalitangazia taifa kifo chake, huu ni msiba mkubwa kwa Taifa letu. Tumepoteza mmoja wa viongozi mashuhuri. Marehemu alijitoa muhanga kupigania uhuru na maendeleo ya nchi yetu. Wakati wote wa uhai wake alitumia uwezo wake na vipaji vyake alivyojaaliwa na Mola wake kujenga, kuendeleza na kutetea maslahi ya Taifa lake na Chama chake CCM na TANU kabla yake. Mzee Kawawa alikuwa mhimili mkubwa kwa Taifa letu na Chama cha Mapinduzi hata baada ya kustaafu uongozi. Sote tutaendelea kumkumbuka kwa moyo wake wa ubinadamu na mchango wake usiokuwa na kifani kwa nchi yetu na watu wake. Tuendelee kumuombea kwa Mwenyezi Mungu ailaze roho yake mahali pema peponi. Amin.
Nchi Salama na Tulivu
Ndugu Wananchi,
Ni jambo la faraja na kuonea fahari kwamba tunaumaliza mwaka 2009 taifa letu likiwa salama na kwamba amani na utulivu viliendelea kutawala. Aidha, taifa letu limeendelea kuwa moja na watu wake wameendelea kuwa wamoja, licha ya kuwepo kwa changamoto za hapa na pale zilizotokana na harakati za vyama vya siasa na kauli za baadhi ya wanasiasa na viongozi wa kijamii wakiwemo wale wa dini. Wakati mwingine, matendo na kauli zao zimekuwa na mwelekeo wa kuwagawa Watanzania katika makundi yenye mifarakano na uhasama.
Napenda kutumia nafasi hii kuwapongeza na kuwashukuru kwa dhati Watanzania wenzangu kwa ukomavu wa kisiasa, moyo wao wa uzalendo na busara waliyotumia ya kukataa kuwa wahanga wa njama hizo ovu. Badala yake mmechagua kufuata na kufanya mambo yenye maslahi kwa umoja, maendeleo na usalama wa taifa letu. Hakika ni moyo huo na ufahamu huo ndiyo umeliweka taifa letu kuwa moja na lenye amani na utulivu tulionao tangu uhuru wa Tanganyika, mapinduzi ya Zanzibar na baadae Muungano mpaka leo. Nawaomba ndugu zangu tushikilie msimamo huo hasa katika mwaka ujao wa uchaguzi ambapo haya yaliyofanywa mwaka huu yanaweza kufanywa maradufu.
Tusiwape nafasi wakafanikiwa wale watu wabaya wanaotaka kutugawa kwa dini, kabila, rangi, Bara na Visiwani au Unguja na Pemba. Pia tusiwape nafasi wale wote wanaotaka kuleta machafuko nchini. Kamwe tusikubali kuwa kama wale wenzetu tuliowapa hifadhi hapa kwetu au tunaowaona kwenye luninga na kuwasikia katika redio na kuwasoma katika magazeti wakiuana, kuumizana na kuharibiana mali huko nchini kwao. Nina imani kubwa kwamba hatutaiacha nchi yetu ifike hapo.
Mazungumzo Baina ya CUF na CCM
Ndugu Wananchi;
Wakati nikitahadharisha na kuwataka Watanzania wenzangu tuendelee kudumisha amani na utulivu wa nchi yetu sina budi kutambua matumaini mema yanayojitokeza Zanzibar. Hatua ya Mheshimiwa Amani Abeid Karume, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kukutana na kuzungumza na Maalim Seif Sharif Hamad, Katibu Mkuu wa CUF inazidi kuleta matumaini ya amani na utulivu kuendelea kustawi Zanzibar na kote nchini sasa na katika uchaguzi ujao. Tuendelee kuwaunga mkono na kuwapa moyo viongozi wetu hawa ili wakamilishe kwa salama kazi waliyoianza kwa maslahi ya Wazanzibari na Watanzania kwa ujumla.
Uhalifu Unadhibitiwa
Ndugu Wananchi:
Katika mwaka huu tunaoumaliza leo tumeshuhudia kuimarika kwa juhudi za kupambana na uhalifu na maovu katika jamii. Matokeo ya juhudi hizi yameonekana katika kudhibitiwa kwa uhalifu. Wahalifu wengi wamekamatwa na kufikishwa Mahakamani. Njama kadhaa za uhalifu zimezuiliwa. Watuhumiwa wengi wa makosa ya rushwa wamefikishwa mbele ya vyombo vya sheria. Nawapongeza sana wenzetu wa Jeshi la Polisi na Kikosi cha Kuzuia na Kupambana na Rushwa nchini kwa kazi nzuri walioifanya. Nawaomba mwaka 2010 waongeze juhudi maradufu. Mimi naendelea kuwaahidi msaada na ushirikiano wangu na wa Serikali.
Mauaji ya Albino
Ndugu Wananchi;
Mwaka 2009, matukio ya mauaji ya ndugu zetu wenye ulemavu wa ngozi yaani Albino yamepungua. Kumekuwepo na vifo 7 ikilinganishwa na 27 vya mwaka 2008. Hata hivyo, watu 7 kuuawa bado ni wengi mno. Haitakiwi auawe hata mtu mmoja.
Katika mwaka ujao tutaendeleza juhudi za kupambana na uhalifu huu mpaka tuutokomeze. Bahati nzuri taarifa zilizopatikana wakati wa zoezi la kura ya maoni lililofanyika mapema mwaka huu zinasaidia sana vyombo vyetu vya dola katika kuwafuatilia watu wanaoshukiwa kujihusisha na vitendo hivi viovu vya aibu. Ni jambo la kuleta faraja kwamba tayari kesi tatu zimesikilizwa na kuamuliwa na Mahakama. Wahusika wametiwa hatiani na baadhi kuhukumiwa kifo. Haki imetendeka.
Ndugu Wananchi,
Nasikitika kwamba bado hatujafanikiwa kudhibiti ajali za barabarani licha ya wito wangu wa kila mwaka katika salamu kama hizi na ule wa viongozi wenzangu kila zitokeapo ajali mbaya za magari barabarani.
Mwaka huu, hadi mwezi Septemba jumla ya ajali zilizotokea ni 15,798 ikilinganishwa na 13,405 zilizotokea katika kipindi kama hicho mwaka jana. Ajali hizo zimesababisha vifo 2,685 ikilinganishwa na vifo 2,040 vilivyotokea mwaka 2008. Idadi ya majeruhi imeongezeka kufikia 15,508 ikilinganishwa na majeruhi 12,508 mwaka 2008.
Kwa mara nyingine tena narudia wito wangu kwa watumiaji wa barabara hasa madereva kuzingatia Sheria ya Usalama barabarani waendeshapo magari. Ningependa kuona mwaka 2010 ukiwa mwaka wa mabadiliko mema kwa maana ya kupungua kwa ajali za barabarani.
Narudia wito wangu kwa Askari wa Usalama Barabarani kuwa makini katika kusimamia Sheria ya Usalama Barabarani na kuwawajibisha ipasavyo madereva wazembe. Aidha, naomba wahakikishe kuwa ukaguzi wa ubora wa magari yatembeayo barabarani unafanywa kwa dhati na siyo wa kurashiarashia. Na, kwa magari ya abiria ukaguzi ufanywe mara kwa mara. Pia, nawahimiza Wizara ya Mambo ya Ndani kukamilisha mchakato wa kuongeza adhabu kwa madereva wazembe. Nawaomba SUMATRA watafute namna ya kuwawajibisha wamiliki wa magari wasiojali uimara wa magari yao yatembeayo barabarani.
Hali ya Uchumi wa Taifa
Ndugu Wananchi;
Mwaka uliopita ulikuwa mgumu sana kwa ustawi wa uchumi wa nchi yetu. Matarajio na malengo yetu makuu kuhusu ujenzi na maendeleo ya uchumi wetu hatukuweza kuyafikia. Mauzo yetu ya nje ya bidhaa na mazao ya kilimo, mifugo, viwanda na madini yalipungua kwa kukosa masoko katika nchi za Ulaya, Marekani na Asia. Bei za mazao na bidhaa zetu hizo iliporomoka sana. Watalii walipungua na mapato ya utalii kushuka pia. Wawekezaji wameahirisha uamuzi wa kuwekeza nchini. Biashara ya uchukuzi wa mizigo iendayo na itokayo nchi jirani ilipungua sana. Mapato ya Serikali yakapungua kwa asilimia 9. Jumla ya yote kasi ya kukua kwa uchumi inatarajiwa kushuka kutoka lengo la asilimia 7.8 na kuwa asilimia 5. Hii ni athari kubwa sana kwa taifa letu.
Pamoja na kuwepo kwa sababu nyingine, hali hiyo imechangiwa kwa kiasi kikubwa na matatizo makubwa na ya aina yake yanayoukabili uchumi wa dunia kuanzia mwaka 2007 na kuwa mbaya zaidi tangu mwaka 2008 hadi sasa.
Kama mtakavyokumbuka Juni 10, 2009, mjini Dodoma, nilitangaza Mpango Maalum wa Dharura wa Taifa wa kuhami na kuimarisha uchumi wa nchi yetu. Kama nilivyoeleza mpango huo umekadiriwa kugharimu takriban shilingi bilioni 1,600 (au shilingi trilioni moja na bilioni mia sita).
Ndugu Wananchi;
Kwa hakika hii ni gharama kubwa mno kwa nchi maskini kama yetu kubeba lakini ilikuwa hapana budi kufanya hivyo. Kufanya kinyume chake kungeifanya hali ya uchumi wa nchi yetu kuwa mbaya zaidi. Utulivu tulionao katika uchumi mkuu ungetoweka na mambo mengi yangeparaganyika. Kama tungeiacha hali ifikie hapo huenda hata utulivu wa kisiasa tunaojivunia nao ungetetereka pia. Kutofanya chochote isingekuwa uamuzi wa busara kuchukua pamoja na ukweli kwamba kwa kupeleka kiasi kikubwa cha fedha kama hiki kwa ajili ya kunusuru uchumi kumepunguza fedha ambazo zingetumika kwa ajili ya shughuli nyingine za maendeleo na Serikali.
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
Katika Mpango wetu wa Dharura, miongoni mwa hatua zilizochukuliwa ni ile ya Serikali kubeba mzigo wa madeni ya Benki ya makampuni, na watu waliopata hasara kutokana na kupungua kwa mauzo nje na kuanguka kwa bei za mazao na bidhaa wanazouza katika soko la dunia. Nia yetu ilikuwa kuzuia wasifilisike na mabenki yaliyowakopesha yasiathirike. Pia tulichukua uamuzi wa kufidia bei ya pamba kwa shilingi 80 kwa kilo ili kumpunguzia mkulima mzigo wa hasara na kuwapa moyo waendelee na kilimo cha pamba msimu unaofuata. Tulifidia zao la pamba kwa kuwa ndilo zao lililoathirika zaidi kuliko mazao mengine yote.
Ndugu Wananchi;
Katika mpango wetu huo pia tulianzisha mfuko maalum wa uwekezaji ili kuyapa imani mabenki ambayo yalipata hofu ya kukopesha yaendelee kutoa mikopo kwa wafanyabiashara na wawekezaji. Kwa upande wa Serikali yenyewe mpango huo ulilenga kukabiliana na tatizo la kupungua kwa mapato ya Serikali.
Nafurahi kusema kuwa utekelezaji wa Mpango wetu wa Dharura wa Kuhami na Kuimarisha Uchumi unakwenda vizuri na takriban malengo yote tuliyojiwekea yametekelezwa kama tulivyokusudia. Ni matumaini yangu kuwa utekelezaji wa Mpango huu utafanikiwa ili kuzuia kudidimia zaidi kwa uchumi wa nchi yetu na kusaidia kuuimarisha.
Ndugu zangu, Watanzania Wenzangu;
Mwaka 2010 tunaouanza kesho hautakuwa mwepesi ingawaje tunatarajia kuwe na nafuu kiasi kuliko mwaka huu. Yapo mambo mawili yananifanya niwe na matumaini hayo. Kwanza, kasi ya kuporomoka kwa uchumi katika mataifa makubwa tajiri kulikochimbuka matatizo haya inaelekea kudhibitiwa. Pili, hatua za dharura tulizozichukua zinaelekea kufanikiwa kwa kiasi fulani kuzuia uchumi usididimie na baadhi ya sekta zimeonyesha dalili za kuimarika ikiwemo sekta yetu kuu ya utalii.
Pamoja na hayo, sina budi kukumbusha kuwa safari yetu bado ni ndefu na kuna vikwazo vingi vya kuvuka. Hatuna budi kutambua wajibu wetu wa kufanya kazi kwa makini zaidi, bidii zaidi na maarifa ili tuweze kukabiliana sawasawa na athari za msukosuko wa uchumi wa dunia na kushinda.
Hali ya Mvua na Chakula Nchini
Ndugu Wananchi;
Waswahili wana msemo usemao “kila msiba una mwenzake”. Hali hiyo imekuwa kweli kwetu sisi hapa nchini kwa mwaka huu. Wakati tunakabiliwa na athari za msukosuko mkubwa wa uchumi wa dunia unaotishia kufuta mafanikio yote tuliyopata katika mageuzi na ujenzi wa uchumi wetu, ukame umezua changamoto nyingine inayoongeza ugumu katika juhudi zetu za kujinusuru.
Kwa miaka miwili mfululizo sasa mikoa yote inayopata mvua za vuli na masika na baadhi ya mikoa inayopata mvua moja imekuwa na upungufu mkubwa wa mvua. Mikoa hiyo ni Pwani, Dar es Salaam, Tanga, Kilimanjaro, Arusha, Manyara, Mara, Mwanza, Shinyanga na Dodoma. Matokeo yake ni kuwepo kwa upungufu wa chakula katika mikoa hiyo na nchi nzima kwa jumla.
Ndugu Wananchi;
Katika msimu wa mwaka 2008/09 nchini kulikuwa na upungufu wa tani 860,000 za nafaka na katika msimu wa 2009/10 inatarajiwa kutakuwa na upungufu wa tani 1.3 milioni za nafaka. Kwa sababu hiyo, watu wengi katika wilaya kadhaa hapa nchini wamelazimika kutegemea msaada wa Serikali kwa ajili ya kujipatia usalama wao wa chakula. Kwa mfano, mwaka 2008 Serikali ilitoa tani 11,610 za nafaka kama msaada wa chakula kwa watu 425,313 Katika wilaya 30 nchini. Hadi kufikia tarehe 22 Desemba, 2009 Serikali imeshatoa tani 115,837.1 za nafaka katika wilaya 59 nchini, na matarajio yetu ni kutoa zaidi. Napenda kuwahakikishia Watanzania wenzangu kuwa tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha chakula kinapatikana kwa wanaohitaji. Hatutakubali kuona Mtanzania hata mmoja anakufa kwa njaa, labda tusipate taarifa mapema. Iwapo itatokea hatutapata chakula cha kutosha hapa nchini, tupo tayari kutatafuta popote duniani.
Bahati mbaya sana kwa baadhi ya wilaya za Mikoa ya Arusha na Manyara ukame ulikuwa mkali sana na kusababisha mifugo mingi kufa. Familia nyingi za ndugu zetu wafugaji zimejikuta kwenye umaskini mkubwa kwa sababu ya kupoteza mifugo yao. Nilitembelea wilaya ya Longido na kuona kwa macho yangu athari za ukame. Napenda kuwahakikishia ndugu zetu hao kuwa Serikali imeona na imesikia. Tutatafuta namna ya kuwasaidia waanze maisha mapya. Hatuwezi kufanya makubwa lakini madogo tunayaweza. Aidha, tutaendelea kuwapatia msaada wa chakula.
Kilimo Kwanza
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu wa 2009 umekuwa mwaka wa mafanikio ya kutia moyo katika mchakato wetu wa kuleta mapinduzi ya kilimo nchini au mapinduzi ya kijani kama watu wengine wanavyopenda kuyaita. Mambo mengi tuliyopanga kufanya yametekelezwa na kutoa mwelekeo mzuri katika safari yetu ya kuboresha kilimo chetu. Mara baada ya kuingia madarakani tuliamua kuchukua hatua za dhati za kuanzisha mchakato thabiti wa kuleta mapinduzi ya kijani nchini. Mwaka mmoja baadaye tulizindua Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo au Agriculture Sector Development Programme maarufu kama ASDP kwa kifupi.
Madhumuni ya Programu hii ni kuondoa vikwazo vinavyozuia maendeleo ya haraka ya kilimo chetu na kusababisha tija kuwa ndogo na hivyo uzalishaji kuwa mdogo. Vikwazo hivyo pia vinasababisha ubora na thamani ya mazao yetu ya kilimo kuwa ya kiwango cha chini. Kwa sababu hiyo, hali ya usalama wa chakula kwa watu wengi na nchini kwa ujumla kuwa ya mashaka. Sababu hiyo pia imechangia kuwafanya watu wengi nchini kuwa maskini kwani asilimia 80 ya Watanzania huishi vijijini na wanategemea kilimo hicho hicho kwa maisha yao na maendeleo yao. Katika Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo tunayoendelea kuitekeleza hivi sasa, vikwazo vimetambuliwa na kutengenezewa mipango ya kuvitatua.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumefikisha miaka mitatu ya utekelezaji wa Programu hii na nafurahi kusema kuwa mambo yanakwenda vizuri. Tumeongeza maradufu bajeti ya sketa ya kilimo na kufikia shilingi 721.3 bilioni ambayo ni sawa na asilimia 7.5 ya bajeti ya Serikali kwa mwaka huu wa fedha. Ni kweli kwamba kiasi hicho ni chini ya lengo la asilimia 10 lililowekwa na Umoja wa Afrika na SADC. Hata hivyo, hapa tulipofikia mwaka huu ni pakubwa sana ikilinganishwa na tulipokuwa miaka ya nyuma.
Ndugu Wananchi;
Tumeweza kupata mafanikio ya kutia moyo katika kukabiliana na vikwazo katika kilimo nchini. Kwa mfano, tumepanua kilimo cha umwagiliaji na kazi inaendelea. Tumeongeza uagizaji wa matrekta kwa nia ya kupunguza matumizi ya jembe la mkono. Kila Halmashauri ya Wilaya nchini, kwa kuanzia imeagizwa kununua matrekta yasiyopungua 50.
Kwa upande wa upatikanaji wa mbegu bora, tumechukua hatua za dhati za kuongeza uwezo wetu wa uzalishaji wa mbegu bora nchini. Tumeongeza fedha kwa shughuli za utafiti nchini jambo ambalo litanufaisha utafiti wa mbegu nchini. JKT na Jeshi la Magereza yameanza uzalishaji wa mbegu bora kama wakala wa Wakala wa Taifa wa Mbegu. Wakati huo huo juhudi zinaendelea za kufufua mashamba ya mbegu ya Serikali na kuhusisha kwa upana zaidi sekta binafsi katika shughuli hii muhimu.
Upatikanaji wa Mbolea
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine ambalo tumepata mafanikio ya kutia moyo mwaka huu ni la upatikanaji wa mbolea na pembejeo za kilimo. Tumefanikiwa kuongeza fedha za mfuko wa ruzuku ya mbolea na pembejeo nyingine za kilimo kutoka shilingi billion 7 mwaka 2005 hadi shilingi 118 bilioni mwaka huu. Mwaka wa jana katika ugawaji wa mbolea na pembejeo za kilimo za ruzuku, tulianzisha mpango wa vocha ili kuhakikisha kuwa kweli mbolea inawafikia walengwa.
Matokeo ya hatua hizo ni kuongezeka kwa mbolea na pembejeo za kilimo za ruzuku pamoja kwa wakulima na kuongezeka kwa idadi ya wakulima wanaopatiwa pembejeo hizo. Kwa upande wa mazao ya mahindi na mpunga, mwaka huu, wakulima 1,500,000 watanufaika na ruzuku ya mbegu na mbolea kutoka wakulima 750,000 wa mwaka wa jana.
Tumeanzisha pia utaratibu wa ruzuku ya dawa na mbegu kwa zao la pamba mwaka huu, ambapo wakulima wapatao 500,000 watanufaika. Kwa upande wa zao la korosho, ruzuku inayotolewa ni kufidia asilimia 50 ya bei ya dawa. Kwa upande wa mazao ya kahawa na chai, Serikali inatoa ruzuku na kuyawezesha mashirika ya utafiti ya TACRI na TRITI kuuza miche kwa nusu ya bei waliyokuwa wanawauzia wakulima.
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeanzisha mkakati maarufu kwa jina la Kilimo Kwanza. Natambua kuwa wapo watu hawajaelewa ipasavyo dhana iliyobebwa na mkakati huo. Lakini, wapo wenzetu wengine ambao wamediriki hata kubeza kuwa Kilimo Kwanza si lolote si chochote, hata kabla utekelezaji wake haujaanza kwa ukamilifu.
Ndugu Wananchi;
Naomba nirudie kwa kifupi kusema kuwa mkakati wa Kilimo Kwanza si badala ya ASDP bali upo kwa ajili ya kuongeza nguvu na kutoa msukumo zaidi katika utekelezaji wa malengo ya programu yetu hiyo muhimu. Katika Kilimo Kwanza tunatekeleza malengo ya ASDP ila tunataka kuzitumia rasilimali na maarifa ya wenzetu wa sekta binafsi kuleta ufanisi zaidi. Tunataka ndugu zetu wa sekta binafsi wawekeze katika shughuli za kuendeleza kilimo nchini, yaani walime mashamba makubwa na wawekeze katika biashara na viwanda kwa ajili ya kukipatia kilimo chetu mahitaji yake ya zana na pembejeo. Aidha, tunataka wawekeze katika viwanda vitakavyosindika mazao ya kilimo na kuzalisha bidhaa kwa kutumia malighafi zinazotokana na kilimo. Nafurahi kwamba wenzetu wa sekta binafsi ambao walihusika kwa ukamilifu katika matayarisho ya mkakati huo wapo tayari. Tena wengine wameshaanza kuwekeza katika viwanda hivyo.
Kuendeleza Mifugo
Ndugu Wananchi;
Katika kufuatilia kwa karibu utekelezaji wa Programu ya Kuendeleza Sekta ya Kilimo, nimejifunza kuwa shughuli za ufugaji hazipewi fursa sawa kama zile za ukulima wa mazao. Nimeagiza kuwa ili kuitendea haki shughuli ya mifugo, tutayarishe programu maalum kwa ajili ya kuendeleza ufugaji. Hivyo basi, katika mwaka ujao tutegemee kuona shughuli za mifugo zikipewa fursa zaidi ya ilivyo sasa.
Maendeleo ya Miundombinu
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka 2009, tumeendelea kupata mafanikio katika uendelezaji wa miundombinu hasa ya barabara. Mafanikio hayo yamewezekana kutokana na Serikali kuendelea kutenga fedha nyingi kila mwaka katika bajeti ya sekta hiyo. Mwaka huu kwa mfano, tumetenga shilingi bilioni 1,096 ambazo ni sawa na asilimia 11.5 ya bajeti nzima ya Serikali. Hii ndiyo bajeti ya pili kwa ukubwa baada ya ile ya Elimu.
Kwa sababu hiyo, barabara nyingine zimekamilika na nyingine zimeendelea kujengwa kwa kiwango cha lami na changarawe. Aidha, tumeshuhudia uzinduzi wa ujenzi kwa kiwango cha lami wa barabara nyingine kadhaa hapa nchini. Kwa kuongeza fedha katika Mfuko wa Barabara, barabara nyingi za Mikoa na Wilaya zimeimarishwa na zinaendelea kuimarishwa kwa kujengwa kwa kiwango cha changarawe.
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka ujao tunategemea mambo kuwa mazuri zaidi. Kama kila kitu kitakwenda kama ilivyopangwa zile barabara za Tanga – Horohoro, Tunduma – Sumbawanga na Namtumbo – Songea – Mbinga zitaanza kujengwa. Mchakato wa ujenzi wa barabara hizo zinafadhiliwa na Serikali ya Marekani kupitia mfuko wa Millennium Challenge Account, hivi sasa imefikia hatua ya uteuzi wa makandarasi wa barabara hizo. Kazi hiyo ya uteuzi inatarajiwa kukamilika robo ya kwanza ya 2010 na ujenzi kuanza katikati ya mwaka. Ratiba ni hiyo hiyo kwa miradi mingine inayofadhiliwa na MCC.
Ndugu Wananchi;
Jambo lingine la faraja kuhusu ujenzi wa barabara ambalo napenda kulitaja leo ni kule kukamilika kwa ujenzi wa daraja la Umoja katika mto Ruvuma linalounganisha nchi zetu mbili rafiki za Msumbiji na Tanzania. Hatimaye ndoto ya hayati Rais Julius Nyerere wa Tanzania na hayati Rais Samora Machel wa Msumbiji imetimia. Tena jambo zuri na la heshima kuhusu daraja hili ni kwamba nchi zetu zimetumia fedha zake bila msaada wa wafadhili. Hii inadhihirisha kuwa pamoja na ukweli kwamba tunahitaji misaada kutoka nchi zilizoendelea, yapo mambo tunayoweza kuyafanya wenyewe pale tunapokosa misaada kama ilivyokuwa kwa daraja hili.
Bandari, Usafiri wa Anga na Reli
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa huduma za reli, bandari na usafiri wa anga, mwaka 2009 ulikuwa wa matatizo. Kiini cha matatizo yaliyozikabili sekta hizi tatu muhimu ni udhaifu katika uendeshaji na uwekezaji mdogo katika maendeleo ya miundombinu hii muhimu.
Kwa upande wa bandari, tatizo la mlundikano wa meli zinazosubiri kupakua au kupakia mizigo bandarini limepungua sana. Hii imeletwa na ununuzi wa vifaa vipya vya upakuaji na upakiaji wa makontena bandarini na matengenezo ya vifaa vilivyokuwepo ambavyo vilikuwa vimeharibika. Bado lipo tatizo la kasi ya kuyaondoa bandarini makontena yaliyokwishapakuliwa kutoka kwenye meli. Natambua juhudi zinazoendelea kupata ufumbuzi wa tatizo hili. Nawasihi wahusika wote kuongeza kasi, ari na nguvu ya kupata jawabu la kudumu kwa tatizo hili.
Baada ya Serikali kufanikiwa kuondoa ukiritimba wa kampuni TICTS sasa fursa ipo ya kuleta wabia wengine kuendeleza bandari ya Dar es Salaam. Nawaomba wahusika katika Mamlaka ya Bandari kuchangamka kutafuta wawekezaji kwa ajili ya upanuzi wa Bandari yetu.
Usafiri wa Anga
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa usafiri wa anga mwaka huu Serikali imeendelea na jitihada za kuimarisha utendaji na uendeshaji wa Shirika la Ndege la Tanzania. Pamoja na hayo, pia Serikali imeendelea na mchakato wa kupata mbia wa kushirikiana nae kuendesha shirika hilo. Ni matumanini yangu kuwa mchakato huo utakamilika mapema mwaka 2010 ili shirika letu tulipe matumaini mapya ya uhai na maendeleo.
Serikali imeendeleza juhudi za ujenzi na uimarishaji wa viwanja vya ndege nchini. Shughuli za ukarabati na upanuzi wa Uwanja wa Ndege wa Kimataifa wa Julius Nyerere zimeendelea kufanyika. Mwaka huu tunatarajia kazi hiyo kuendelezwa kwa upana na kina zaidi. Aidha, kazi ya kuimarisha viwanja vya ndege vya Arusha, Mwanza, Mpanda, Bukoba na Mafia imeendelea kama ilivyopangwa. Katika mwaka huu, kwa msaada wa wabia wetu wa maendeleo matengenezo makubwa yatafanywa kwa viwanja vya Tabora, Kigoma, Bukoba na Mafia. Naomba Wizara ya Miundombinu na hasa Mamlaka ya Viwanja vya Ndege wamsimamie kwa karibu mkandarasi anayejenga Uwanja mpya wa ndege wa Kimataifa wa Songwe ili uanze kutumika mwaka 2010.
Reli
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa reli zetu mbili, yaani Reli ya TAZARA na ya Shirika la Reli la Tanzania, mwaka huu umekuwa wa misukosuko iliyohusu matatizo ya uendeshaji na uchakavu wa miundombinu ya reli hizo. Kwa upande wa TAZARA mazungumzo yaliyomalizika hivi karibuni mjini Beijing, China baina ya nchi zetu tatu, yaani Zambia, Tanzania na China yemeleta matumaini mapya kuhusu kupata ufumbuzi wa matatizo ya miundombinu ya reli na vyombo vya uchukuzi. Bado tutaendelea kulitafutia ufumbuzi tatizo la menejimenti.
Kwa upande wa Shirika la Reli Tanzania, fedha za kukabiliana na tatizo la miundombinu chakavu ya reli, mabehewa na vichwa vya treni ipo tayari. Kinachochelewesha kuzipata na kuzitumia ni migogoro inayoelekea kuwa sugu ya menejimenti na uendeshaji. Serikali inaendelea kushughulikia tatizo hilo na ni matumaini yangu kuwa mapema mwaka 2010 tutapata ufumbuzi wa kudumu wa tatizo hili, ufumbuzi ambao utakuwa wa maslahi kwa taifa letu.
Elimu
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa elimu mwaka huu umeendelea kuwa wa mafanikio kwa upanuzi wa elimu ya awali, msingi, sekondari na elimu ya juu. Kwa sababu hiyo, tunao wanafunzi wengi katika ngazi zote na aina zote za elimu kuliko wakati mwingine wowote katika historia ya nchi yetu.
Mafanikio haya yameleta changamoto zake na hasa ile ya kupata fedha za kutosha kukidhi mahitaji ya ajira na huduma kwa walimu, majengo na vifaa vya kufundishia kama vile vitabu na vinginevyo. Kupata ufumbuzi kwa matatizo ya sekta ya elimu nchini imekuwa ni moja ya kipaumbele cha juu tangu tuingie madarakani. Kila mwaka tumeongeza bajeti ya elimu na kuifanya bajeti hiyo kuwa ndiyo kubwa kuliko zote. Kwa mfano, mwaka huu tumetenga shilingi bilioni 1,743.9 ikilinganishwa na bilioni 1,430.4 mwaka wa jana na bilioni 669.5 tulipoingia madarakani mwaka 2005.
Pamoja na nyongeza kubwa kiasi hicho, bado tunayo mahitaji makubwa ambayo bado hayajatoshelezwa. Miongoni mwa hayo ni upungufu wa walimu, vitabu, vifaa vingine vya kufundishia, madarasa, maabara, nyumba za walimu pamoja na mikopo kwa wanafunzi wa vyuo vya elimu ya juu. Ninachowaahidi ni kuwa katika mwaka ujao tutaendelea kuiangalia kwa upendeleo bajeti ya elimu ili tuendelee kupunguza vikwazo vinavyozuia elimu yetu kuendelea kustawi.
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa matokeo ya mtihani wa darasa la saba kwa mwaka huu, sina budi kukiri kuwa hayakunifurahisha na kwa kweli yamenishtusha. Nimesikia maelezo mengi ya kila aina kuhusu sababu zilizochangia ufaulu wa watoto wetu kuwa wa chini kiasi hicho mwaka huu. Pamoja na yote yaliyosemwa nimewataka viongozi wa Wizara ya Elimu na Mafunzo ya Ufundi wakae chini na wenzao wa TAMISEMI, Maafisa Elimu wa Wilaya na Wawakilishi wa Walimu kujadili tatizo hili kwa dhati na kutafuta ufumbuzi wake ili lisijirudie tena.
Huduma ya Afya
Ndugu Wananchi;
Mwaka huu tumeendelea kupiga hatua katika kuimarisha huduma ya afya nchini. Vituo vya huduma ya afya kwa maana ya zahanati, vituo vya afya na hospitali vimeongezeka kutoka 5,800 mwaka 2008 hadi 6,240 mwaka 2009. Hali kadhalika tumeendelea kuboresha upatikanaji wa dawa, vifaa vya tiba na watumishi wa afya. Pamoja na mafanikio hayo, bado zipo changamoto nyingi zikiwemo za baadhi ya dawa kuwa pungufu pamoja na uhaba mkubwa wa vifaa vya tiba na watumishi hasa wauguzi na madaktari.
Tumeendelea na juhudi za kukabiliana na matatizo hayo. Tumeongeza bajeti ya afya kwa kiasi kikubwa ili kujenga uwezo wa kukabiliana na changamoto hizi na nyinginezo. Tumeweka msisitizo maalum katika kupambana na maradhi yanayoua watu wengi kama vile malaria, kifua kikuu na UKIMWI. Kwa upande wa UKIMWI tunaendelea na juhudi za kutoa elimu kwa umma ili watu wajikinge na UKIMWI. Na, tunatoa dawa za kurefusha maisha kwa walioathirika.
Kwa upande wa malaria, pamoja na juhudi tuzifanyazo sasa kukabiliana na maradhi hayo, tumeamua kuchukua hatua za kufuta maradhi hayo hapa nchini. Tumefanikiwa Zanzibar, hivyo naamini hata Bara tutafanikiwa. Tunataka kukata mzizi wa fitina kwa kutumia vyandarua vilivyotiwa dawa na kupulizia dawa majumbani na mazalia ya mbu. Tayari tumepata vyandarua vya kumuwezesha kila mtoto mwenye umri wa chini ya miaka 5 kupata chandarua chake. Kazi ya kugawa inaendelea kote nchini. Hivi sasa matayarisho yanaendelea ya kuiwezesha kila kaya kupata vyandarua viwili. Matayarisho yatakapokamilika tutaarifiana.
Jambo lingine kubwa tunaloendelea nalo ni jitihada za kupunguza vifo vya kina mama waja wazito kutokana na matatizo ya uzazi. Tumetengeneza mkakati kabambe ambao tunaendelea kuutekeleza. Nina imani kuwa tutafanikiwa katika dhamira yetu hii njema. Si haki hata kidogo kwa mama kupoteza maisha wakati wa uzazi.
Umeme
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa umeme, mwaka huu tumeongeza kasi ya kutekeleza maelekezo ya Ilani ya Uchaguzi katika kufikisha umeme kwenye miji mikuu ya wilaya. Umeme tayari umefika Mbinga, Simanjiro, Ludewa, Mkinga na Kilolo. Wakati wowote mwezi Januari mwaka 2010 umeme utawaka Kilindi, Uyui na Bahi. Mchakato wa kununua genereta mpya 17 ili kuzipatia umeme Wilaya za Ngorongoro, Kasulu, Kibondo, Kigoma na Sumbawanga unaendelea vizuri. Fedha zimekwishatengwa na mkandarasi amekwishapatikana.
Wilaya ya Bukombe itapata umeme kwa msaada wa Benki ya Maendeleo ya Afrika na mchakato unaendelea juu ya kupata fedha za utekelezaji wa mradi huu muhimu. Mji wa Longido utapata umeme kutoka Namanga na matayarisho ya ujenzi wa njia yanaendelea. Kwa wenzetu wa Kigoma mjini, nafarijika sana kwamba mitambo miwili ya umeme tuliyonunua mwaka huu imeanza kufanya kazi na tatizo la umeme limepungua. Ufumbuzi wa kudumu utapatikana tutakapofunga mashine nyingine mpya 5 ambazo zimeshaagizwa. Kwa mji wa Songea, Serikali imekwishatenga fedha kwa ajili ya ununuzi wa mtambo mpya ili kuimarisha upatikanaji wa umeme mjini hapo wakati tunasubiri umeme wa gridi.
Ndugu Wananchi;
Mwanzoni mwa Oktoba, mwaka huu, mikoa, wilaya, miji na vijiji vinavyopata umeme wa gridi vilikabiliwa na tatizo la mgao wa umeme. Tatizo hili lilitokana na kuharibika kwa mitambo ya Songas na ya Kituo cha Umeme cha Kihansi. Matengenezo ya mtambo wa Songas ulikamilika na Kihansi bado mpaka Januari 2010. Tatizo hilo limesisitiza haja ya kuongeza uzalishaji wa umeme na kuwa na akiba ya kutosha. Kwa sasa hatuna uwezo huo ndiyo maana hitilafu ndogo ikitokea inakuwa ni tatizo kubwa. Kuongeza uzalishaji wa umeme ndilo lengo letu mwaka ujao na mingine ijayo.
Huduma ya Maji
Ndugu Wananchi;
Kuhusu huduma ya maji, katika mwaka wa 2009 tulijitahidi kwa kiasi kikubwa kuboresha huduma ya maji nchini. Mnamo mwezi wa Mei mwaka huu nilizindua mradi mkubwa wa maji kutoka Ziwa Victoria ambao umewapatia maji watu zaidi ya milioni 1 katika miji ya Shinyanga na Kahama na vijiji 54 vya wilaya za Misungwi, Geita, Shinyanga na Kahama. Mradi huu ulitugharimu shilingi 252 bilioni ambazo ni fedha zetu wenyewe. Katika mwaka ujao wa 2010, tutaendelea na jitihada hizi za kuboresha huduma ya maji kote nchini. Kwa ajili hiyo, katika bajeti ya mwaka 2009/2010, tumetenga jumla ya shilingi billion 65 kwa utekelezaji wa miradi mingine ya maji.
Ushirikiano wa Kimataifa
Ndugu Wananchi;
Katika mwaka huu unaoishia leo, nchi yetu imefanikiwa kuimarisha uhusiano na mataifa mengine duniani na mashirika ya kimataifa. Tanzania imeendelea kuheshimiwa katika medani za kimataifa. Kwa ajili hiyo, tumeshirikishwa katika masuala mengi makubwa ya kimataifa. Tumetembelewa na viongozi mashuhuri wengi waikiwa Wakuu wa Nchi kadhaa. Viongozi wakuu wa nchi yetu nao wamealikwa na kutembelea nchi nyingine duniani. Mahusiano hayo yamekuwa na manufaa ya kusaidia maendeleo na ustawi wa nchi yetu. Tumeendelea kupata masoko ya bidhaa na mazao yetu pamoja na misaada ya maendeleo na mitaji ya uwekezaji.
Ndugu Wananchi;
Pengine katika heshima kubwa na muhimu tuliyoipata mwaka huu ni ile ya kuchaguliwa kuwa mwenyeji wa mkutano mkubwa wa kimataifa wa masuala ya kiuchumi Barani Afrika uitwao World Economic Forum on Afrika. Hii itakuwa mara ya kwanza kwa mikutano hyo kufanyika nje ya Cape Town, Afrika Kusini. Ni heshima kubwa kwa Tanzania, hivyo nawaomba Watanzania wenzangu na hasa wananchi wa Dar es Salaam kuwapokea vizuri wageni wetu wazito kwa utajiri na maarifa. Tuoneshe ukarimu wetu wa kawaida kwa wageni wetu ili wapende kurudi tena Dar es Salaam na Tanzania kwa mikutano mingine au matembezi na shughuli nyingine.
Uchaguzi Mkuu wa 2010
Ndugu Wananchi;
Kwa upande wa kukuza na kuendeleza demokrasia, mwaka 2009 kulifanyika uchaguzi wa Serikali za Mitaa kwa mafanikio makubwa. Napenda kuitumia nafasi hii kuwapongeza viongozi na wananchi wote kwa jumla kwa mafanikio haya ya kutia moyo. Inathibitisha, kwa mara nyingine tena, kuwa demokrasia inazidi kuota mizizi Tanzania. Kwa niaba ya CCM naomba niwashukuru Watanzania wenzetu kwa kuendelea kukiamini Chama chetu. Imani huzaa Imani. Hatutawaangusha.
Mwaka 2010 ni mwaka wa Uchaguzi Mkuu kuchagua Rais, Wabunge na Madiwani. Ni matumaini yangu kuwa tutaidumisha sifa ya nchi yetu ya nchi ya demokrasia ya kweli iliyojengeka juu ya msingi wa uhuru na haki. Hiyo ndiyo siri ya kudumishwa kwa amani na utulivu Tanzania. Sisi, Serikalini tumejipanga vizuri kuhakikisha kuwa mahitaji yote ya rasilimali yanayotakiwa na Tume ya Uchaguzi yanapatikana kwa ukamilifu na kwa wakati. Tumetenga fedha za kutosha katika bajeti ya mwaka huu na tutamalizia katika bajeti ijayo. Aidha, tutafanya kila tuwezalo kuhakikisha kuwa uchaguzi unakuwa huru na wa haki na unafanyika katika mazingira ya utulivu na amani.
Ndugu Wananchi;
Wito wangu kwenu wananchi wenzangu ni kuwa mjitokeze kwa wingi kushiriki katika mchakato wa uchaguzi katika hatua zake zote. Kwa wale ambao hawajajiandikisha kwenye daftari la wapiga kura wajiandikishe wakati ukifika. Wakati wa uchaguzi ukifika wajitokeze kupiga kura kuchagua viongozi wanaowapenda.
Kwa viongozi, wanachama na wafuasi wa vyama vya siasa nawaomba tushiriki katika mchakato wa uchaguzi tukizingatia taratibu na sheria za nchi. Nataka uchaguzi ujao uwe ni fursa ya kuimarisha zaidi demokrasia yetu na kupata viongozi walio bora. Kamwe tusiruhusu uchaguzi uwe chanzo cha migogoro, chuki, mivutano na uvunjifu wa amani ndani ya vyama, baina ya vyama na kwenye jamii kwa ujumla. Kila mmoja wetu anayo nafasi yake katika kuhakikisha kwamba haiwi hivyo.
Hitimisho
Ndugu Wananchi; Watanzania Wenzangu;
Napenda kumalizia salamu zangu za mwaka mpya kwa kumshukuru tena Mwenyezi Mungu kwa rehema zake alizotujalia mwaka 2009. Tumuombe atuzidishie maradufu yale yaliyo mema na kutunyooshea yasiyokuwa na maslahi mema kwetu katika mwaka ujao 2010. Nawashukuru tena Watanzania wenzangu wote kwa imani yenu kwangu na kwa ushirikiano wenu kwangu na kwa Serikali yetu. Umoja na juhudi za kila mmoja wetu kwa nafasi yake ndivyo vilivyotuwezesha kumaliza mwaka, taifa letu likiwi tulivu, lenye umoja na mshikamano. Ndiyo siri ya mafanikio tuliyoyapata. Tunajali na kuthamini michango yenu na ushirikiano mnaotupatia katika utekelezaji wa majukumu mliyotukabidhi.
Kesho, tunapouanza mwaka mpya, napenda kuwahakikishia kuwa mimi na wenzangu wote serikalini tutaendelea kuwatumikia kwa moyo wetu wote na nguvu zetu zote katika kuyatafutia majawabu matatizo yanayolikabili taifa letu. Naamini kwa umoja wetu, juhudi na maarifa tutafanikiwa.
Nawatakieni nyote heri na fanaka tele katika mwaka mpya 2010.
Mungu Ibariki Afrika!
Mungu Ibariki Tanzania!
Asanteni kwa kunisikiliza!
No comments:
Post a Comment