Umasikini unaleta uroho
Adam Lusekelo
Neno ‘fisadi’ limekua linatumika sana siku mbili tatu hizi. Mimi mafisadi nawaita kwa neno tulilolizoea. Haya ni majizi na miroho tu. Kwa nini tunamwita anayeiba kuku au simu ya mkononi, ‘mwizi’ na anayeiba mabilioni fisadi? Ni kumpa heshima mwizi wa mabilioni?
Labda tuseme ukweli – Afrika yetu haikuwa tayari kujitawala. Maana yake wengine tunajikuta kuwa tumefikia kiwango cha kukata tamaa. Mimi nilifikiria kuwa tukijitawala, waAfrika tutakuwa na uchungu na nchi zetu. Lakini haijatokea hivyo.
Ghafla tumejikuta tumemwondoa mkoloni ili kuweka kundi la majizi, tena majizi yasiyokuwa na uchungu na wananchi wao. Hatuwezi kuendelea namna hii. Hatuwezi kukaa na hali hii ambayo sasa kwa kweli inatia kinyaa.
Wanasaikologia wanasema kwamba watu walio toka kwenye umasikini mkali wakipata madaraka mara nyingi wanabadilika sana. Mtu anajaribu kuukimbia umasikini ule aliouacha na kuuweka mbali sana nayo. Kwa hiyo wengi wao wanakuwa hawana kiasi. Kila wakiona fedha wanataka kuziiba ziwe zao (EPA).
Wengine wanaweza kuuza hata wake zao, mradi tu wapate fedha. Na nchi hii imeuzwa sana. Yaani sasa karibu kila mahali pananuka katika nchi yetu. Na kama kawaida hakuna hatua inayochukuliwa. Porojo nyingi tu.
Ni nini hasa kinachowafanya watu wengine wanaojiita viongozi (mimi nawaita watawala) wasiwe hata na chembe ya uoga wa wizi mkubwa kiasi hicho?
Maana yake sasa wananchi wanajua kwamba watawala walikua wanafanya kampeni,siyo kwenda kuwatumikia wananchi, bali kwenda kuwaibia. Mara nyingi watawala walikua wanajikinga kuwa kama kuna wizi unatokea basi wangependa kupata ushahidi ndiyo wachukue hatua.
Sasa kuna ushahidi wa kutosha. Mwenyezi Mungu ameamua kukaa upande wa wananchi wengi wanaodhulumiwa na kuibiwa na watu wanaojiita viongozi. Lakini hatua yo yote haijachukuliwa. Wakifumwa jamaa wanajiuzuru na kuendela kula mabilioni waliyotuibia. Hii itaendelea mpaka lini? Au tulie tu?
Sasa yamefika kwa wafadhili wetu. Nao sasa kinawakera sana. Huku watawala wanaziomba nchi zilizoendelea zifute madeni yetu na hapo wanawaibia wananchi utafikiria watawala hao hawana akili nzuri! Anakuwa masiala hayo!
Sasa Norway nayo imeanza kuwanyooshea kidole watawala wa Tanzania. Jumanne iliyopita waziri wa wa Mazingira na Maedeleo ya Kimataifa wa Norway, Bwana Erik Solheim amesema kuwa WaTanzania wahakikishe kuwa fedha za misaada zinatumiwa kwenye kazi inayouhusika.
Amesema walipa kodi wa Norway wanaanza kudhani kuwa wanafanywa mabwege, kutoa fedha za misaada ambazo zinaishia kukwapuliwa na watawala.
Lakini tutahakikishaje, wakati sirikali ni siri kali na inaendelea kuwa sirikali? Kama Profesa Shivji anavyosema wanasiasa na wabunge wako kwenye kazi hiyo kwa ajili ya kupata fedha na kuiba tu na mimi sioni watumishi waadilifu wa WaTanzania hapa!
1 comment:
Interesting.Lakini ukweli ni kwamba uroho upo hata kwa matajiri;witness the GFC. Ukweli ni kwamba pesa ni chanzo cha maovu mengi duniani!
http://wachumi.blogspot.com/
Post a Comment