Monday, April 26, 2010


Dr. Willbrod Slaa, Mbunge wa Karatu (CHADEMA)


Taifa linawahitaji kina Dk. Slaa wengi



Josephat Isango


NANI anabisha kuwa bila ya Mbunge wa Karatu, Dk. Willbrod Slaa (CHADEMA), nchi yetu pengine ingeshauzwa na mafisadi? Nani anabisha kuwa rais wetu hana wanashauri makini? Je, ni sisi tu ndio tunajua kuwa rais hana washauri makini au hata yeye mwenyewe anajua kuwa hana washauri makini?

Huenda yeye asijue kwa kuwa amewachagua, je, yanayotendeka hajui kuwa yanamshushia hadhi yeye, si tu kama rais ila hata kama ni mwanadamu wa kawaida anayestahili heshima?

Inasikitisha sana, rais wetu alishauriwa mapema, lakini hakushaurika, akaambiwa lakini hakusikia, akatahadharishwa lakini akapuuzia. Sijui magazeti yanapofika pale Ikulu, yenye vichwa vinavyosomeka kuwa Serikali yagaragazwa Bungeni, huwa rais wetu anajisikiaje?

Dk. Willbrod Slaa, ndiye aliyeushtua umma kwa kuweka bayana uchomekeaji mambo uliofanywa na baadhi ya watendaji, ambao wanaonekana kutojua au kujali chochote juu ya matamshi ya kiongozi huyo wa upinzani.

Mbunge huyo alivunja ukimya kwa kuweka wazi kuwa ameshangazwa na kilichotokea Ikulu siku ya kusaini sheria ya kudhibiti gharama za uchaguzi, ambapo amelibaini kuwa kuna mtu au kikundi cha watu kimejivika ujasiri wa kuchomeka kipengele katika sheria hiyo na ikasainiwa na rais pasipo idhini ya Bunge.

Kibaya zaidi, Rais Kikwete alisaini kwa mbwembwe, pasi na kujua kuna watu waliingiza mikono yao na yeye kwa kuwa alikuwa akiwaamini aliamua kusaini pasipo kusoma au kuhoji.

Je, ni kweli kuwa kuna vipengele vilivyoongezwa baada ya kupitishwa kwa muswada wa sheria hiyo na Bunge? Je, kuna kanuni inayoruhusu vipengele kuongezwa pindi Bunge likimaliza majadiliano?

Kama si ruhusa kufanya hivyo, kina nani wameshiriki kuongeza vipengele hivyo na kwa sababu zipi? 

Wamepanga kumdhalilisha rais ili aonekane si msomaji wa jambo analolisaini? Na kama walipanga kumdahalilisha ni kweli wamefanikiwa, lakini je, rais mwenyewe katika hili anajisikiaje?

Kama jambo hili limetiwa mikono na watu wengine nje ya Bunge, basi watendaji wanaomzunguka rais wetu hawamtakii mema yeye na nchi kwa ujumla. Na kama imegundulika uchomekeaji huo, nani amechukuliwa hatua.

Najua viongozi wetu si wawajibikaji na msamiati wa kujiuzulu mara inapobainika kuwa makosa yametendeka kwao ni kitendawili kilichokosa mteguaji, lakini si vibaya umma ukaelezwa wale waliohusika kumpotosha rais na umma.

Binafsi hizo naziona njama za kumdhalilisha rais wetu zilizofanywa na watu wenye ujasiri wa hali ya juu kwa dhamira ambayo mpaka sasa sijaielewa lakini najua kama Rais Kikwete akiamua kuwashughulikia umma utafahamishwa walifanya hivyo kwa lengo gani.

Haya ni baadhi ya maswali yanayonifanya nikose majibu. Hata hivyo bado nitaendelea kujiuliza kuwa watu hao waliofikia hatua ya kuongeza kinyemela vipengele hivyo walimlenga nani zaidi na kwa faida ya nani?

Je, kabla ya kusaini sheria hiyo, rais alikaa na kuipitia ili kuona kile kilichokubalika bungeni ndicho kilichokuwa mikononi na machoni mwake? Kama hakufanya vile ni kwanini? Je, hii ni moja ya kazi zake au siyo?

Rais Kikwete ni miongoni mwa watu waliochangia kwa kiasi kikubwa kukamilika kwa sheria hiyo, kwa sababu alionyesha dhamira ya kukomesha matumizi makubwa ya fedha chafu katika uchaguzi, japo katika uhalisia ameonekana kuwa mkiukaji wa kwanza kuhusu sheria hiyo.

Labda tujiulize je, alifuatilia kwa makini mijadala ya wabunge na kile kilichokuwa mbele yake au ndiyo aliwaamini watendaji wake?

Ni mambo mengi sana ambayo bila Dk. Slaa, nchi yetu ingekuwa imeangamia kabisa, tukianzia suala la wizi wa pesa za EPA, suala la Richmond, Kagoda, Meremeta, Kiwira, na mengineyo ambayo mpaka sasa yamekosa majibu ya kina kutoka serikalini.

Ununuzi wa ndege ya rais ambayo mpaka sasa ufanyaji kazi wake na kuiendesha ni gharama kubwa sana ni miongoni mwa mambo yaliyoligharimu taifa fedha nyingi ambazo zingeweza kutumika kuboresha huduma za kijamii ambazo zinazidi kudorora.

Leo hii viongozi wa serikali na chama tawala wamekuwa wakipita vichwa chini kwa aibu kutokana na ufisadi ambao ulifanywa na makada wenzao waliokuwa mstari wa mbele wakipinga jitihada za baadhi ya wabunge wa upinzani kukemea ufisadi.

Taifa limekuwa likipelekwa pabaya kutokana na kulindana kunakofanywa ndani ya serikali ambayo inaongozwa na CCM, tulishaona namna walivyomshughulikia Mbunge wa Kigoma Kaskazini, Zitto Kabwe (CHADEMA) pale alipoibua suala la mgodi wa Buzwagi, Bunge lilimsimamisha kwa madai kuwa amedanganya.

Ni aibu na hatari kwa wabunge, hasa wa CCM ambao ndio wengi, kupitisha mambo bila kujua athari yake au kwa sababu ya maagizo fulani kutoka serikalini au chamani.

Je, bila Zitto Kabwe tungejua kuwa aliyekuwa Waziri wa Nishati na Madini, Nazir Karamagi, amesaini mkataba wa kifisadi tena nje ya nchi, kujipendekeza kwa Wazungu kwa kuuza dhahabu yetu ya mgodi wa Buzwagi?

Ndani ya chama tawala walikuwapo wabunge mahiri kwa kukemea maovu kiasi cha kupachikwa majina ya ‘wazee wa kulipua mabomu’ lakini hivi sasa wamekuwa kimya kabisa, kisa ni kulindana na kutunziana heshima wakati taifa linazidi kuangamia.

Bila Dk. Slaa tungegundua kuwa mambo machafu haya yanayotuangamiza yanavyopitishwa? Sasa serikali ituambie ni kwanini wanatufanyia haya? Wasipokuwapo wabunge wa kariba ya Dk. Slaa si ndiyo tungejikuta hata sisi tunauzwa?

Uzalendo na huruma ya viongozi wetu imekwenda wapi? Ninatarajia Mwanasheria Mkuu, Fredrick Werema, aliyekuwa anatishia wenzake bungeni kuwa yeye ni jaji, atajiuzulu. Huwezi kuwa mwanasheria unayepotosha sheria, tena kwa kulazimisha wenzako wakuunge mkono kwa kuhofia taaluma yako hata kama umekosea.

Hayo yote pengine yalifanyika ili kujijengea heshima ya kumlinda rais aliyemteua yeye, lakini kwa sasa hakuna kitu kilichofanyika zaidi ya kumwaibisha rais, huenda bila ya viongozi makini kama Dk. Slaa leo hii sisi na mali zetu tungekuwa tunamilikiwa na wawekezaji wa nchi Fulani.

Tunahitaji viongozi makini wenye uzalendo wa kweli ambao kila waonapo baya hulikemea kwa nguvu pasipo kuogopa kumuudhi mtu au chama anachotoka, idadi kubwa ya viongozi tulionao sasa ni wenye kuangalia maslahi binafsi badala ya taifa.

Kimya hiki cha serikali katika kueleza ufisadi uliofanyika Meremeta, Kagoda, Deep green, na ufisadi mwingine aliowahi kuusema Dk. Slaa unaonekana ni kweli, kama ingekuwa vinginevyo kwa nini serikali inachukua muda mrefu kutoa majibu na badala yake inasingizia kuwa ni kwa ajili ya masuala ya Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ).

Nchi hii ni yetu sote, wabunge au viongozi wanaojidanganya kuwa wao hawataathirika kwa maamuzi mabovu wanayoyafanya hawajitendei haki, ipo siku watarudiwa na ubaya walioufanya hasa watakapokuwa nje ya madarakani au chama chao kitapoangushwa.

Inawezekana kabisa baadhi ya viongozi wamelewa utamu wa madaraka, wanajisahau kuwa kabla ya wao walikuwapo wengine ambao walifanya juu chini kujenga misingi mizuri ya rasilimali zilizopo ziwanufaishe Watanzania wengi.

Hakuna sababu ya kulindana, ni vema kila aliyehusika na utendaji mbovu akawajibishwa bila kujali wadhifa wake serikalini au kwenye chama tawala. Mwanasheria Mkuu aliahidi kuwa kama itagundulika kuwa kuna maneno yameongezwa, basi angeomba radhi, na afanye hivyo, japo hakutaondoa tuhuma zetu kwake.

Ninaamini kuwa tukianza kujenga utaratibu wa kuwajibishana, mambo mengi yatanyooka, kwa kuwa baadhi ya watendaji wamekuwa wakitekeleza majukumu yao ya kila siku kwa mazoea badala ya kufuata maadili ya kazi yanavyotaka.

Mazoea haya ndiyo wanayowajengea ujasiri wa kupiga hodi hadi ikulu na kufanya wanavyotaka pasi na kujali kuwa wanachokifanya kina hatari kwa taifa au kinamdhalilisha rais ambaye mara kadhaa ameshaweka wazi kuwa urais wake hauna ubia.

Nchi hii ni yetu sote, tusivumilie uozo unaofanywa na watu wanaojiona wao ndio wanaojua kila kitu au wanaotumia mwanya wa Watanzania kutokupenda kusoma kupindisha baadhi ya mambo au kutunga sera, sheria na mipango ambayo kwa kiasi kikubwa itayanufaisha makundi ya mafisadi.

Watanzania ni wajibu wetu kuepukana na aibu kama hii, kwa kusema ukweli kuwa rais wetu pamoja na wasaidizi wake wamekosa umakini mkubwa katika kutuongoza, kulindana kumezidi na sisi tutaishi kwa huruma ya Dk. Slaa hadi lini?

Kutoka Tanzania Daima.


3 comments:

Anonymous said...

Taifa linasikitisha kutokana na viongozi wabovu na mfumo wa uongozi uliopitwa na wakati.Viongozi wengi hawakuwa na hawana sifa za uongozi toka Awamu ya kwanza hadi sasa. Wengi walipata madaraka kutokana na kuwa wanyeyekevu na marafiki kwa Maraisi na wale ambao waliokuwa na uwezo ila tuu hawakukubaliana na sera za Maraisi waliachwa nje.Ni viongozi wachache tuu ambao leo hii waliyoyafanya yananufaisha Taifa.

Anonymous said...

Napenda kumpongeza Bwana W.Slaa kwa kazi nzuri anayoifanya kwa Taifa.Yeye ni muwakilishi na mtetezi wa mali ya Umma amechaguliwa na wananchi,kwahiyo yeye anauwezo wa kuikosoa Serikali,kinyume na Mawaziri/wabunge ambao wana kofia mbili[mguu serikalini mguu bungeni]na Wabunge wengine ni wale walio teuliwa na Rais je unathani watampinga Rais aliyewapa vyeo,ni mfumo uliopitwa na wakati na si democrasia ya kweli,na hakuna branch Tatu ni moja tuu ya Rais.

Anonymous said...

Africa ina viongozi wengi wazuri lakini kutokana na mfumo mbovu wa kuteuliwa na Rais wengi wao wapo nje ya madaraka,kwani nafasi za juu za uongozi kama Province/Regional/state,District commissioner ni marais ndio anae wateua wengi wao ni wabovu hawana uwezo wa kazi.Ni Nigeria hadi sasa walio badilisha mfumo huo ambao umeonyesha matunda mazuri na ukomavu wa kisiasa Africa.Viongozi hao wanachangi kiasi kikubwa kuzorota kwa nchi.