Tuesday, April 27, 2010

Ray C mabalaa hayamwishi!


Kama ulikuwa na imani kwamba staa wa Bongo Fleva, Rehema Chalamila ‘Ray C’ anaishi raha mustarehe kwenye makazi mapya, anza kudai kiingilio, kwani siri zilizomo ndani ya mjengo huo wa ghorofa kwa sasa zipo nje.

Kabla ya Ray C kuhamia kwenye mjengo huo wa ghorofa, uliopo Sinza, Dar, mwanamuziki huyo alikumbwa na mikasa kadhaa, kama vile kuishi gesti, kutupiwa vitu nje na wifi yake na kutuama kwenye nyumba isiyo na kiwango chake.

Ijumaa Wikienda a.k.a The Biggest IQ Paper halina cha kupoteza kwa kuiweka hadharani kesi inayomkabili Ray C ya kupata mali kwa njia ya udanganyifu ambayo amefunguliwa na ‘mdada’ aliyempangisha hapo.

Gazeti hili limebaini kuwa Ray C amefunguliwa madai hayo kwenye Kituo cha Polisi Urafiki, Dar es Salaam chini ya kesi iliyohifadhiwa kwenye kitabu cha kumbukumbu za jeshi (Riport Book au RB) kwa namba URP/RB’3665/10 KUPATA MALI KWA NJIA YA UDANGANYIFU.

Katika kesi hiyo, inaelezwa kuwa mdai ambaye ni Agnes Edward Kasango alimkopesha Ray C mapazia yenye thamani ya shilingi 320,000 lakini mpaka leo hajalipwa pesa zake.
Inaelezwa kuwa Agnes alikuwa akiishi kwenye mjengo huo wa ghorofa ambao Ray C anaminya kwa sasa na alimuachia kwa makubaliano maalum.

Kutokana na madai hayo, gazeti hili lilimtafuta Agnes ambaye alipopatikana alikiri kumfungulia mashtaka Ray C na kuongeza kwamba amelazimika kufanya hivyo baada ya kuhangaika kwa muda mrefu kupata pesa zake bila mafanikio.

“Unajua mimi ndiye nilimpangisha Ray C nyumba anayokaa, kwahiyo wakati anaingia akaniomba nimuachie mapazia lakini mpaka leo pesa zangu hajanipa,” alisema Agnes na kuongeza:

“Ray C namdai pesa nyingine za kodi ya nyumba shilingi 400,000 lakini nazo ananizungusha kunipa.”

Akijibu maswali ya mwandishi wetu, Agnes alisema kuwa yeye alipanga kwenye nyumba hiyo kwa mkataba wa mwaka mzima na aliingia makubaliano na Kampuni ya Agumba Computers ambayo ndiyo yenye mamlaka.

“Niliishi miezi minne nikapata safari ya kwenda Afrika Kusini. Akaja Ray C, mimi nilikuwa simjui ila rafiki yangu anamjua. Akaniomba nimuamini. Sehemu niliyopanga ni ghorofani, kuna chumba kimoja cha kulala, choo, bafu na jiko.

“Basi nikazungumza na mwenye nyumba akaniruhusu nikubaliane na Ray C. Kutokana na mahesabu ya miezi saba na siku 10, akatakiwa kunilipa shilingi 2,500,000.

“Akaniomba nimpunguzie mpaka tukakubaliana shilingi 2,300,000. Akalipa 1,900,000 ‘keshi’ akaahidi kunimalizia 400,000 baada ya wiki mbili. Tulipokubaliana, nikampa na mkataba ambao niliingia moja kwa moja na mwenye nyumba.

“Hakunilipa kwa muda, nikasafiri kwenda Afrika Kusini, nikarudi, kila nikimuomba fedha zangu hanilipi kwa sababu jumla sasa ni shilingi 720,000, yaani 400,000 iliyobaki kwenye kodi ya nyumba na 320,000 ya mapazia,” alisema Agnes na kuongeza:

“Baada ya kuona ananisumbua ndiyo nimekwenda kumfungulia mashtaka, namdai mapazia yangu, halafu baadaye nitamfungulia mashtaka kuhusu 400,000 ya nyumba.”

Gazeti hili lilifanikiwa kuona hati ya makubaliano kati ya Ray C na Agnes ambapo mashahidi wawili wameanguka sahihi.

Mashahidi hao ni Fanny Ng’ambi kwa upande wa Agnes na Isaac Waziri Maputo ‘Lord Eyez’ kwa Ray C.

Aidha, katika hati hiyo ambayo inaonesha iliandikwa Oktoba 28, 2009, pia Ray C na Agnes kila mmoja ameanguka sahihi yake.

Jitihada za gazeti hili kumpata Ray C hazikuzaa matunda ila uchunguzi wa The Biggest IQ Paper, umeweza kupata uthibitisho ndani ya Kituo cha Polisi Urafiki kwamba mwanamuziki huyo anasakwa kwa tuhuma hizo. 

Global Publishers Ltd (TZ)

2 comments:

Anonymous said...

Si tulisema, Ray C

ana matatizo flani hivi. Wanaomjua jamani msaidieni.

Anonymous said...

MPAKA HAPO WATU WATAAMINI KUWA HUYU BINTI NI TAPELI NA PESA YA MAPROMOTER WA ULAYA KAILA BILA MAELEZO KAMILI.KWELI ZA MIZI FOTE.