Friday, April 23, 2010

Wanaume wa Kinorwejiani
wanadanganywa kama watoto.

Wanaume wengi wa Kinorwejiani wamekuwa wakidanganywa na ”wanawake” wanaokutana nao kwenye mtandao kwa minajili ya kujenga urafiki wa muda mrefu, kufikia kuoana.

Kitengo cha polisi kinachoshughulikia ufisadi na uharibifu wa mazingira, Økokrim kimesema kuwa kina kesi kama 15 hivi ambazo wanaume wa Kinorwejiani wameingia mtego uliowekwa na ”wanawake” kutoka Afrika Magharibi. Mchezo ni rahisi, jamaa huko Afrika Magharibi wanakaa kwenye Mikahawa ya kompyuta na kufungua ”profile” kama wanawake na kuweka picha za wanawake wazuri kuwa wanatafuta wanaume wa kuwaoa.

Wanaume wa Kinorwejiani waliokosa masoko hapa kwao, wananaswa kwenye mtego, kwa kuanza kudanganywa kuwa, mama anaumwa na anahitaji msaada wa hela za hospitali na dawa. Baadaye uhusiano wa mtandaoni unapozidi kushamiri, mwanamke anaomba aletewa hela ya tiketi kuja huku.
Wanaume hawa, wanatoa hela, baada ya hapo mchezo unakuwa umekwisha, washatapeliwa.

Kesi zingine ni za wanaume walioweka rehani nyumba zao kwa ajili ya kuwaridhisha ”wanawake wao wa Kiafrika Magharibi”

Mpaka sasa hivi, wanaume wa Kinorwejiani wameshatapeliwa jumla za kroner milioni thelathini na saba.

Mtaalamu wa utapeli wa Økokrim; Bi. Anne Dybo amesema kuwa; wanaume wa Kinorwejiani wanaonywa kila siku, lakini hawasikii.


No comments: