Monday, April 19, 2010

Watatu wajeruhiwa kwa mlipuko wa
bomu Dar es Salaam


Watu watatu wamejeruhiwa wawili kati yao hali zao ni mbaya baada ya kutokea mlipuko unaodhaniwa kuwa ni bomu maeneo ya Tabata Dampo, jijini Dar es Salaam.

Kamanda wa Polisi wa Mkoa wa Ilala, Faustine Shilogile, alisema jana kuwa mlipuko huo ulitokea juzi jioni muda mfupi baada ya watu wawili kufika eneo hilo wakiwa na chuma kinachofanana na chupa ya ndani ya chupa ya chai kwa lengo la kuikata.

Kamanda Shilogile alisema watu hao wakiwa na chuma hicho walifika kwenye karakana inayomilikiwa na Nestory John maarufu kama Magogo kwa lengo la kutoa shaba iliyokuwa kwenye mzunguko wa chini wa chuma hicho wakidhani kuwa ni madini.

“Hawa watu walikuwa wawili mmoja ametambuliwa kwa jina la Peter Kiangele (34) na mwenzake bado tunamtafuta, walipofika eneo hilo walimkuta fundi John akiwa na mfanyakazi wake Geofrey Mkono, na kuwaomba waikate shaba hiyo,” alisema.

Kamanda Shilogile alisema fundi John kwa kushirikiana na Mkono walianza kuikata shaba hiyo kwa kutumia kifaa cha kukatia chuma kijulikanacho kama grenda.

Alisema wakati wakiendelea kuikata ghafla mlipuko mkubwa kama wa bomu ulitokea eneo hilo na kuwajeruhi maeneo mbalimbali mwilini.

Alisema John alijeruhiwa kwenye mguu wa kushoto, usoni na kifuani na hali yake ni mbaya wakati Mkono alijeruhiwa miguu yote na shingoni.

Alisema majeruhi hao hali zao ni mbaya na kwa sasa wamelazwa hospitali ya Taifa ya Muhimbili.

Alisema Kiangele alijeruhiwa kwenye kiganja cha mkono wa kushoto na alitibiwa hospitalini hapo na kuruhusiwa.

Kamanda Shilogile alisema kutokana na tukio hilo Kiangele wanamshikilia wakati juhudi za kumsaka mtuhumiwa mwenzake zikiendelea.

Alisema mabaki ya chuma hicho kwa sasa wanayafanyia uchunguzi kwa kushirikiana na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) ili kujua kama chuma hicho kilikuwa ni bomu au la.


No comments: