Akamatwa kwa kuhusika na
mauaji ya halaiki nchini Rwanda
akiwa na pasipoti ya Malawi
Charles Bandora, Mnyarwanda anayeshutumiwa kwa kushiriki kwenye mauaji ya halaiki nchini Rwanda mwaka 1994, amekamatwa Jumanne juzi kwenye uwanja wa ndege wa Oslo Gardemoen akitokea Ubelgiji.
Bandora alikamatwa akiwa na pasipoti ya Malawi yenye viza ya Schengen inayomruhusu kuingia Norway. Lengo lake la kuja Norway lilikuwa ni kuomba hifadhi ya kikimbizi.
Nchini Ubelgiji aliomba hifadhi ya kikimbizi, lakini wakamkatalia na wakampandisha ndege na kumwambia aje Norway kuomba hifadhi.
Kufuatilia makubaliano ya Dublin, mtu yeyote anayeomba hifadhi ya kikimbizi, akikataliwa kwenye nchi nyingine, basi anarudishwa kwenye nchi ya kwanza ya Schengen aliyoingilia kutoka huko anakotoka. Hivyo Bandora, ameomba kesi yake ikasikilizwe Ubelgiji ambako kuna familia yake.
Bandora amekuwa akitafutwa na idara ya polisi ya kimataifa, Interpol kwa muda mrefu.
Imeandikwa kwenye tovuti ya africafiles.org kuwa, Bandora alikamatwa Januari mwaka huu nchini Malawi, lakini haijulikani aliwezaje kutoka na kwenda Ubelgiji kwa kutumia pasipoti ya Malawi.
Kesi yake iko chini ya mkoa wa polisi wa Romerike na atapalekwa lupango leo hii, amesema wakili wa polisi, Bi. Anne Siv Åvitsland.
No comments:
Post a Comment