Sunday, June 06, 2010

Tarime na Rorya (Tanzania)


Polisi wafanya unyama,
wawalazimisha wanafamilia
kufanya mapenzi kwa nguvu!!!


Asha Bani, Tanzania Daima

JESHI la Polisi Kanda Maalum ya Kipolisi Tarime na Rorya, mkoani Mara, limekumbwa na kashfa nzito ya uvunjifu wa haki za binadamu, baada ya kudaiwa kuwalazimisha watu wa familia moja kufanya mapenzi kwa nguvu!

Wakizungumza na waandishi wa habari makao makuu ya Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) jana, kina mama wanaodai kutendewa vitendo hivyo, wamelitupia lawama Jeshi la Polisi nchini kwa kushindwa kuwachukulia hatua askari wake wote waliohusika na tukio hilo.

Mmoja wa kina mama hao, Rhobi Wambura, ambaye alitoa ushuhuda wake mbele ya waandishi wa habari, alielezea manyanyaso ambayo polisi wamekuwa wakiyatenda kwa wananchi wa kijiji cha Kibweye alikozaliwa.

Alisema, usiku wa manane wa Mei 4 kuamkia Mei 5, askari Polisi wa Kanda Maalum walifika nyumbani kwake na kumlazimisha kufungua kwa nguvu mlango wa nyumba yake.

“Nililazimishwa kufungua mlango wa nyumbani na polisi kwa nguvu, nikaogopa sana nikihofia huenda ni majambazi, ghafla polisi walivunja mlango kwa nguvu na kumdondokea mwanangu mwenye umri wa mwaka mmoja aliyekuwa amelala na kumuumiza,” alisema Wambura.

Alisema baada ya askari kuingia ndani, waliwakamata shemeji zake watatu ambao ni Mgaya Chandi, Mwita Chandi na Nyahedi Chandi na kuwafunga kamba bila kuelewa sababu ilikuwa ni nini.

“Polisi wakiwa ndani, walinilazimisha kuvua nguo zote mbele ya shemeji zangu hao huku wakitupiga hovyo hovyo kwa fimbo na kutukata mapanga sehemu mbalimbali za miili yetu; kwa kweli nilipoona kipigo kinazidi niliamua kuvua nguo ili nisife.

“…Baada ya mimi za shemeji zangu kuvua nguo na kuwa watupu kama tulivyozaliwa, askari waliniambia nianze kushika sehemu za siri za shemeji zangu na kuzinyonya, nilikataa huku wakinipiga bila huruma, baada ya kuona nazidiwa niliamua kufanya kama walivyotaka ili nipunguze kipigo kile kikali na cha kikatiri!” alisema Wambura.

Alisema baada ya kumaliza kitendo hicho, polisi walimsukuma hadi ndani ya nyumba na kumwamuru alale kwa vile walikuwa wametimiza masharti yaliyotakiwa.

Wambura, aliendelea kusema kuwa baada ya askari hao kuondoka nyumbani kwake, waliivamia nyumba ya jirani wakiambatana na wale shemeji zake wote wakiwa uchi vilevile kama awali hadi kwa jirani zao hao.

Naye Hellen Mgaya (22), ambaye ameathirika na tukio hilo, akizungumza huku akilia, alisema vitendo vya unyama vimeendelea kutawala, licha ya serikali kuunda kanda maalum ya kipolisi.

“Siku ya Mei 4 kuamkia Mei 5 sitaisahau kabisa maishani mwangu; walikuja polisi nyumbani kwangu nikiwa nimelala na mume wangu walitulazimisha kufungua mlango kwa nguvu,” alisema Mgaya.

Alisema, baada ya kufungua mlango huo, akaamrishwa kwa sauti kali na polisi kuvua nguo zote na mumewe pamoja na shemeji zake ambao polisi walikuwa wakizunguka nao.

“Wakati wanatoa amri hiyo, tulikuwa tunapokea kipigo kikali, baada ya kuona maumivu yanazidi tulivua nguo na mimi kuanza kuwachezea sehemu za siri shemeji zangu hao ambao walikuwa wametoka nyumba ya jirani wakiwa watupu!” alisema Mgaya huku akibubujikwa machozi.

“..Nilipigwa kweli, lakini baadaye nikakubali nikaanza kuwachezea sehemu za siri shemeji zangu huku polisi wakiwa wananitukana matusi ya nguoni, baada ya hapo waliondoka na shemeji zangu kwa ajili ya kwenda nyumba nyingine,” alisema Mgaya.

Mkazi mwingine Sophia Marwa (43), akielezea tukio hilo, alisema siku polisi walipomuamuru kuvua nguo mbele ya watoto wake na kulazimishwa kuwashika sehemu za siri huku mwenyekiti wa kijiji cha Kibweye aliyemtaja kwa jina moja la Ambrose akishuhudia tukio hilo.

“Wanangu nawaambia hii ni aibu ya mwaka, nililazimishwa kuwashika wanangu wa kuwazaa sehemu za siri mbele ya mwenyekiti wa kijiji changu, Ambrose,” alisema Marwa.

“…Baada ya hapo walinipiga kweli, walinivua nguo lakini nilisema nivueni nguo, nipigeni, nidhalilisheni ila sitokubali kufanya mapenzi na watoto wangu na wala sitokubali kuwanyonya sehemu za siri labda mniue,” alisema Marwa.

Alisema baada ya unyama huo, polisi hao waliondoka na wanae ambao mpaka sasa wameswekwa rumande bila kosa lolote.

Wakati huohuo, mwanaharakati ambaye pia ni Mwenyekiti wa Baraza la Wanawake wa CHADEMA (BAWACHA), Letricia Gati, alisema inaaminika chanzo cha unyama huo ni Chama Cha Mapinduzi (CCM) kushindwa katika uchaguzi wa serikali za mitaa katika kijiji hicho hivi karibuni.

Alisema, katika uchaguzi huo, CCM ilishindwa nafasi ya mwenyemkiti wa kijiji, huku diwani wao kupitia CHADEMA, John Kisiri, akiwa anashikiliwa na jeshi hilo baada ya kumbambikizia kesi.

Alipoulizwa kuhusiana na tukio hilo, Kamanda wa Kanda Maalumu ya Kipolisi, Tarime na Rorya, SSP Constantine Massawe, alikiri kuwepo kwa tukio hilo na kwamba wanasubiri maelekezo kutoka ngazi ya juu dhidi ya wahusika.

“Ni kweli tukio hili lilitokea mimi mkuu wa kanda nilimtaarifu mkubwa wangu wa kazi (Mkuu wa Jeshi la Polisi, Inspekta Jenerali Said Mwema) kwa ajili ya hatua zaidi,” alisema Kamanda Massawe.

Alisema baada ya taarifa hiyo, IGP Mwema aliunda tume ya maafisa kutoka makao makuu ambayo ilikwenda Tarime na kufanya uchunguzi wa tukio hilo.

“Siwezi kusema mengi zaidi ya hapo, baada ya tukio afande IGP aliunda tume imefanya uchunguzi wake na imemaliza kazi kwa hiyo tunapaswa kusubiri majibu,” alisema Kamanda Massawe.

Naye Kamishna wa Operesheni na Mafunzo, CP Paul Changoja, alipoulizwa, alisema yuko tayari kuwasikiliza waathirika wa tukio hilo kama watafika ofisini kwake.

“Unajua Tarime ni eneo ambalo lina mambo mengi mno, tukio hili nilikuwa sijalisikia, niko tayari kuwasikiliza kina mama hawa kama watakuja ofisini. Nimesikitika kusikia wamekwenda CHADEMA kuongea wakati vyombo vya dola vipo,” alisema Kamishina Chagonja.

No comments: