Tuesday, August 17, 2010

Kasheshe ya uraia wa Bashe

Uhamiaji wakiri kutuma barua ya
kumthibitisha CCM, Makamba asema
hawakubaliani na barua hiyo

Hussein Bashe



SAKATA la uraia wa Mjumbe wa Baraza Kuu la Umoja wa Vijana wa Chama Cha Mapinduzi (UVCCM), Hussein Bashe aliyeamriwa arejeshe kadi na kumvua mamlaka yote aliyokuwa nayo ndani ya chama hicho tawala, limeibua maswali mengi, huku kukiwa na maelezo kuwa ni raia na chama chake kung'ang'ania kuwa si raia hata kama nyaraka zipo. Baadhi ya nyaraka ambazo zimetolewa na Idara ya Uhamiaji nchini na kuonwa na Mwananchi zilionyesha kuwa Bashe aliyekuwa mgombea ubunge kwa tiketi ya CCM katika Jimbo la Nzega, ni raia wa Tanzania.


Waraka uliothibitisha uraia wake na kutumwa kwa Katibu Mkuu wa CCM, makao makuu Dodoma ambayo gazeti hili imeuona unaeleza kuwa Bashe alikabidhiwa hati ya uthibitisho wa kuwa raia yenye Na. S/N 312 ya Agosti 10 mwaka 2009 na kivuli cha nakala hiyo kiliambatanishwa kwenye barua hiyo ya uthibitisho.

Maelezo ndani ya waraka huo yalieleza kuwa idara ya Uhamiaji inapenda kujulisha kuwa Hussein Mohamed Bashe Ibrahim alithibitishwa kuwa raia wa Tanzania kwa kuzaliwa chini ya kifungu Na.5(1) au 7(8) cha sheria ya Uraia Na. 6 ya mwaka 1995.

Waraka huo ambao nakala yake ilitumwa kwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi na kwa Katibu Mkuu wa Wizara hiyo imetiwa saini na P. W. Nombo kwa niaba ya Kaimu Kamishna Mkuu wa Uhamiaji.

Ingawa alipozungumzia uthibitisho ulioelezewa kwenye waraka huo Katibu Mkuu wa CCM, Yusufu Makamba alisema kuwa ni kweli ameiupata,lakini akasisitiza kuwa Bashe si raia japokuwa chama kinampenda.

"Nimeipata barua, nimeusoma, lakini nasema Bashe si raia, tunampenda na ana uwezo wa kupigiwa kura na kushinda, lakini si raia,"alisema Makamba.

Alisema kuwa uhamiaji huwa wanaangalia vitu vichache tu kumthibitisha mtu hivyo hakubaliani na uthibitisho wa uhamiaji.

"Uhamiaji wanaangalia kitu kimoja tu kama ni raia labda cheti cha kuzaliwa, mimi nasema si raia, hatuwezi kumpitisha na hatukubali kwa kuwa masuala ya uraia yana mambo mengi,"alisema Makamba.

Gazeti hili lilimtafuta Waziri wa Mambo ya Ndani, Lawrence Masha ili azungumzia waraka huo ambao nakala yake imetumwa kwake, lakini simu yake ilikuwa ikiita tu bila kupokelewa.

Alipotafutwa Naibu waziri wa wizara hiyo, Balozi Khamis Kagasheki alisema kuwa yuko katika ofisi za CCM akiomba wanachama wa chama hicho wamdhamini hivyo hawezi kuzungumza.

"Niko katika ofisi za CCM ninaomba udhamini kwa wanachama hivyo 'please' siwezi kuzungumza,"alisema Kagasheki.

Kwa upande wa Idara ya uhamiaji msemaji wa idara hiyo, Abdi Ijimbo alisema kuwa waraka huo ameuona hivyo atautolea ufafanuzi pamoja na mambo mengine baada ya kuupitia vizuri.

"Nimeuona waraka huo baada ya kuutafuta kwa kuwa nilitaka nijiridhishe kwanza na si kuongea tu, hivyo njoo kesho saa tatu asubuhi (leo) nitakupa taarifa kamili pamoja na mambo mengine,"alisema Ijimbo kwa njia ya simu.

Uamuzi wa kumvua madaraka na tamko la kutokuwa kwake raia lilitolewa na Katibu wa Itikadi na Uenezi wa CCM, John Chiligati baada ya kumalizika kwa kikao hicho cha NEC, Bashe alitakiwa pia kuanza mara moja mchakato wa kutafuta uraia wa Tanzania.

Chiligati alisema kwamba Bashe si raia kwa kuwa wazazi wake walivyomzaa walikuwa ni raia wa Somalia.

Kwa upande wake, Bashe alisema kwamba yeye ni raia wa Tanzania na kwamba alikwisha ukana uraia wa baba yeke, kupitia Mahakama ya Kivukoni jijini Dar es Salaam.


"Kesho (leo) nitaongea na waandishi wa habari na kuweka kila kitu wazi ili wananchi wajue ukweli," alisema Bashe alipotakiwa kuongelea suala hilo.



Alisema kwamba baada ya kuongea na wanahabari atakwenda Nzege kuwashukuru wananchi walioonyesha imani kubwa kwake kwa kupata kura zaidi ya kura 14,000.


Tayari wanasheria wa Bashe wameshachukua hatua ya kufuatilia sakata zima la mteja wao kwenye ofisi za Idara ya Uhamiaji. Bashe aliongoza kura za maoni Jimbo la Nzega kwa kupata kura 14, 466, Lucas Selelii 2,706 na Khamis Kigwangala aliyepata kura 1,566. Kigwangala ndiye aliyepishwa kupeperusha bendera ya CCM.

Chanzo: Gazeti la Mwananchi


1 comment:

Chama Cha Watanzania Oslo - CCW Oslo said...

CCM bwana...mambo yale yale waliyomfanyia Jenerali Ulimwengu miaka ile...