Wednesday, August 18, 2010

Sakata la Bashe lafichua siri nzito
Mzozo na Ridhiwani Kikwete wahusishwa




UKWELI kuhusu sakata la uraia wa kada wa Chama Cha Mapinduzi (CCM), Hussein Bashe, aliyetimuliwa uanachama na kupokwa nyadhifa zake zote ndani ya chama hicho tawala umejulikana, Tanzania Daima Jumatano limebaini.

Sakata hilo limeelezwa na wachambuzi wa duru za siasa nchini kwamba ni mwendelezo wa siasa za chuki na mizengwe inayoibuka nyakati za uchaguzi na hali hiyo inatosha kuonyesha jinsi mfumo wa siasa za ndani ya CCM na maingiliano yake yanavyoweza kutumika pasipo kuangalia haki na uadilifu wa kuendesha shughuli za siasa kwa manufaa ya mfumo murua wa kisiasa.

Uchunguzi wa kina uliofanywa na gazeti hili na yaliyojiri ndani ya kikao cha Halmashauri Kuu ya CCM, (NEC), mwishoni mwa wiki iliyopita mjini Dodoma, umebaini kuwa Bashe ambaye alishinda kura za maoni za ubunge katika Jimbo la Nzega, mkoani Tabora kwa kumbwaga, Lucas Selelii, amepata ajali hiyo ya kisiasa kutokana na mambo makubwa matatu.

Mosi, uchunguzi umebaini kuwa ndani ya UVCCM kada huyu kijana alikuwa na upande unaomuunga mkono miongoni mwa vigogo wa CCM, akiwamo Mbunge wa Igunga, Rostam Aziz, ambao ndio wanaosadikiwa kumsaidia kufikia hapo alipofika kisiasa.

Wanaomjenga Bashe wanaelezwa kuwa na dhamira ya kumtumia kijana huyo kwenye harakati za kutengeneza mazingira ya kupata nafasi ya uongozi wa juu baada ya Awamu ya Nne (yaani mwaka 2015), kwa kuweka ushawishi ndani ya jumuiya hiyo muhimu kwenye siasa za CCM.

Pamoja na hayo, zipo habari zinazosadifu kuwepo kwa ‘vita ya kisiasa’ baina ya makundi yanayojijenga kisiasa ndani ya siasa za CCM kwa kuitumia UVCCM.
Tatu, ni uhusiano wake mbaya wa kisiasa kati yake na Kaimu Mwenyekiti wa Umoja wa Vijana (UVCCM), Beno Malisa na swahiba wake, Ridhiwani Kikwete, ambaye ni mtoto wa Rais Kikwete.

Vyanzo vya habari kutoka ndani ya UVCCM, vimeliambia Tanzania Daima Jumatano kuwa uhusiano wa Bashe na mahasimu wake hao kisiasa ulianza wakati wa harakati za kusaka nafasi ya mwenyekiti wa jumuiya hiyo taifa.

“Wakati wa kampeni za kusaka nafasi hiyo, kulikuwa na rafu sana, kwa sababu Beno alikuwa akisaidiwa na kuungwa mkono na Ridhiwani, wakati Bashe alikuwa akiungwa mkono na Rostam Aziz na vigogo wengine wenye fedha. Rafu hizo zilimfanya Rais Kikwete atumie busara kuamua nafasi hiyo iende Zanzibar.

“Hata nafasi hiyo ilipokwenda Zanzibar kama alivyoagiza Rais Kikwete, Bashe aliamua kumuunga mkono Yusuf Masauni (mwenyekiti aliyejiuzulu), Beno akaambulia nafasi ya umakamu na tangu wakati huo Masauni alikuwa na Bashe, Beno na Ridhiwani na makundi yao yalikuwa yakiwindana na kusababisha mpasuko mkubwa ndani ya umoja huo,” kilisema chanzo chetu cha habari.

Kwa mujibu wa habari hizo, Beno na Ridhiwani wanadaiwa kutoridhishwa na hatua ya Masauni kumteua Bashe kuingia kwenye Baraza Kuu la UVCCM, kwani katika mikutano ya baraza hilo, kada huyo alikuwa mwiba mkali kwa Beno na Ridhiwani.

Uhasama wa makundi hayo unadaiwa kuongezeka katika mkutano wa baraza hilo mjini Iringa, ilipoibuka ghafla ajenda ya kumng’oa Masauni, kwa madai kuwa amedanganya umri wake kupata nafasi hiyo.

“Kilichotokea ni nini? Beno na swahiba wake wanadaiwa kusuka mkakati huo wakati Bashe alitumia fedha nyingi kuwashawishi wajumbe wa baraza kuikataa hoja hiyo, hasa wale wa kutoka Visiwani Zanzibar. Kibaya zaidi baadhi ya wajumbe waliandika mabango kumkashifu Rais Kikwete,” kilisema chanzo hicho cha habari.

Hata hivyo Ridhiwani amepata kuripotiwa mara kadhaa kupitia vyombo vya habari, likiwemo gazeti hili kwamba hakuhusika kwa namna yoyote katika sakata hilo zima.

Kilichotokea Dodoma
Sakata la Bashe kwamba si raia wa Tanzania, lilianza kujadiliwa kwenye Kamati Kuu (CC), mjini Dodoma. Hoja hiyo ililetwa CC ikitokea kwenye Kamati ya Maadili.
Kulikuwa na mjadala mkali kuhusu hoja hiyo na hatimaye wajumbe walipitisha mapendekezo ya kukata jina lake kuwania ubunge licha ya kuibuka na ushindi wa kura 14,000, huku mbunge mtetezi akiambulia kura 2,000.

Wakati wa kupitia majina ya wagombea walioshinda kwenye kura za maoni za ubunge na Baraza la Wawakilishi, Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Rais Kikwete alipotaja Jimbo la Nzega, wajumbe wengi walipaza sauti kwamba apitishwe aliyeshinda.

“Unajua sehemu nyingi ambazo hazikuwa na matatizo, mwenyekiti alikuwa akitaja jina la jimbo na wajumbe tulikuwa tukiitikia apite huyo huyo. Ilipofika Nzega wajumbe walisema apite huyu huyo, lakini rais alisema hapana, kwa sababu kuna maneno hapa na Kamati Kuu imependekeza kuchukua mshindi wa tatu.”

Baada ya kusema hivyo, mjumbe mmoja wa NEC kutoka Zanzibar aliyejulikana kwa jina moja la Mtanda, alisimama na kuuliza swali moja, lenye vipengele vitatu. Mosi alitaka kujua sababu za kumwacha Bashe, pili alitaka kujua sababu ya kumuacha mshindi wa pili Lucas Selelii, aliyepata kura 2,000 na sababu ya kumchukua mshindi wa tatu, Hamis Andrea Kigwangala.

Akijibu swali hilo kwa utulivu na umakini mkubwa, Rais Kikwete alisema Bashe si raia wa Tanzania, hivyo kuwataka wajumbe kutopitisha jina lake.
Akifafanua suala hilo, Rais Kikwete alisema kada huyo alipotakiwa kuwasilisha vielelezo kuthibitisha uraia wake, aliwasilisha cheti cha kuzaliwa cha mama mzazi, kilichosainiwa mjini Tabora na cheti cha kuzaliwa cha bibi yake, kilichosainiwa mjini Moshi.

“Ukiangalia vyeti hivi viwili, utaona kuwa vimesainiwa sehemu tofauti, lakini zimewekwa saini na mtu mmoja na ‘serial’ namba zake zinafuatana, moja ni namba 75 na kingine 76, hiyo inaonyesha kabisa Bashe amefoji kupata vyeti hivyo,” mtoa habari wetu alimkariri Rais Kikwete.

Kikwete pia amekaririwa akisisitiza kwamba kuna kughushi katika baadhi ya vielelezo vya Bashe, kwani hata kwenye umri wake wa kuzaliwa, vipo vinavyoonyesha amezaliwa mwaka 1975, vingine mwaka 1976 na vingine mwaka 1978.

Kikwete alikwenda mbali zaidi kwa kuwaambia wajumbe hao kwamba licha ya barua kutoka Uhamiaji kusema kwamba hakuna utata wa uraia wake kama ilivyokuwa kwa Waziri wa Fedha na Uchumi, Mustafa Mkulo, alisema taarifa za kiusalama zinaonyesha nyaraka zote zilizowasilishwa na Bashe kuthibitisha uraia wake ambazo zimesainiwa na Kaimu Kamishna Mkuu wa Uhamiaji ni batili na hazitambuliki.

“Nasikia maneno mengi kuhusu Hussein Bashe kwamba ni mkorofi, alisumbua sana kwenye mkutano wa Baraza Kuu la Vijana kule Iringa, namshauri arekebishe haya mazongozongo yake, atulie, maana wakati mwingine utulivu unalipa,” alikaririwa akisema Kikwete.

Kuhusu Selelii, mwenyekiti huyo aliwaambia wajumbe hao kuwa Kamati Kuu imependekeza jina la mshindi wa tatu kwa sababu katika hali ya kawaida, mbunge huyo wa zamani anaonyesha hakubaliki.

“Kama Bashe amepata kura 14,000, Selelii amepata kura 2,000, maana yake hakubaliki sana, hebu tumpe huyo wa tatu, hili tatizo la jina la bandia na nini tutaliangalia mbele ya safari, ila hatuwezi pia kumhukumu kwa makosa ya nyuma,” alihitimisha hoja hiyo Rais Kikwete.

Sakata la Bashe kukatwa jina na kuvuliwa uongozi, limewashtua wengi kutokana na ukweli kwamba ameshawahi kuwania na kushika nyadhifa mbalimbali ndani ya UVCCM, lakini hakupata kuhojiwa juu ya uraia wake.

Hadi anavuliwa nyadhifa zake, Bashe alikuwa ni mjumbe wa Baraza Kuu la UVCCM, mjumbe wa Halmashauri Kuu (NEC) na amewahi kuwania nafasi mbalimbali za uongozi, ikiwamo ubunge wa Nzega mwaka 2005 na uenyekiti wa taifa wa UVCCM.

Sakata la Bashe linafananishwa na lile lililowahi kumkumba Mwenyekiti wa Bodi ya Wahariri ya Raia Mwema, Jenerali Ulimwengu, ambaye alivuliwa uraia na Serikali ya Rais Benjamin Mkapa.

Ulimwengu alipata kuwa mbunge, mkuu wa wilaya na mwakilishi wa vijana katika Umoja wa Vijana wa Afrika (Algeria).

Swali la kujiuliza ni serikali/chama kilikuwa wapi kwa miaka yote ya utumishi wa watu hawa hata kuwaacha washike nyadhifa nyeti ndani na nje ya ulingo wa utendaji wa serikali na chama tawala?

Chanzo : Gazeti la TanzaniaDaima

No comments: