Kuraani Tukufu inasema : Baada ya kuyakinisha jua limetua, waliofunga ni lazima juu yao kufuturu (tafsiri ya Sheikh Said Mussa kwenye kitabu chake cha Kiswahili: Saumu na shuruti zake, uk.16). Hii ina maana tunatakiwa kufunga mpaka tutapoona jua limezama! Kipindi hiki huku, kwa hapa Oslo nilipo jua linazama kwenye saa 3 na nusu hadi nne za usiku saa za ulaya ya kati (Saa 4 na nusu hadi tano za usiku za Afrika Mashariki).
Kwa wale wanaoishi kaskazini ya Norway, ndio usiseme. Jua linazama kwenye saa 5 hadi 6 za usiku za ulaya ya kati (CET = Central European Time) au saa 6 hadi 7 za usiku za Afrika Mashariki (EAT = East African Time). Mwisho wa kula daku huku, ni kwenye saa 9 na dakika 25 za alfajiri au saa 10 na dakika 25 za alfajiri za Afrika Mashariki. Huku Kaskazi ya dunia tumeanza kufunga kwa masaa 18 badala ya masaa 13 ya Makka (kuchwa na kucha kwa jua): Ni masaa mengi.
Kadri siku zinavyoenda, jua taratibu linawahi kuzama na linachelewa kutoka. Lakini mpaka mwezi wa Ramadhani ukiisha, bado mchana utakuwa mrefu ukilinganisha na usiku.
Waislamu tunaofunga huku tumekuwa tunajiuliza maswali kadhaa wa kadhaa juu ya nyakati za majira ya Kiangazi yalivyo huku kwenye mwezi huu mtukufu wa Ramadhani, ukilinganisha na nchi Afrika, Asia, Mashariki ya Kati, Marekani ya Kusini na Kaskazini. Wanatheolojia na wanazuoni wa Kiislam huku wameshindwa kutoa majibu ya ufasaha juu ya majira ya Kiangazi huku (mchana mrefu usiku mfupi) na muda wa kufunga na kula daku. Wanahitilafiana sana.
Imam Senaid Kobilica, Sheikh Mkuu wa Baraza la Waislam Norway (IRN = Islam Råd Norge) amesema juzi kuwa; wataitisha kikao cha Mashehe na Maimam baada ya Ramadhani kwisha ili kujadili utata uliojitokeza wa suala hili. Imam Kobilica anakubaliana na Imam Basim Ghozlan wa msikiti wa Rabita hapa Oslo kuwa watu wanaweza kufuata masaaa 13,5 ya kufunga ya Makka. Wakati Imam Syed Nehmat Shah wa msikiti wa Central Jamaat-e Ahl-e Sunnat na Imam Hafiz Mehboob ur Rehman wa Islamic Cultural Centre hapa Oslo wanasema kuwa lazima waumini wa Kiislam wafuate masaa yaliyoandikwa kwenye Kuraani Tukufu; Kucha na kuchwa kwa jua!
Mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwakani utaangukia Julai. Na huku hizi nchi za Kaskazini Julai ni katikati ya Kiangazi! Jua linapotea kama saa moja sana sana masaa mawili.
Je, itakuwaje kwa wale watakaojaliwa kuufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani?
Je, itakuwaje kwa wale watakaojaliwa kuufunga Mwezi Mtukufu wa Ramadhani?
Manaake itabidi wafunge kama masaa 23 hivi. Kwa wale waishio kuvuka nyuzi za Actic wao itabidi wasifunge, kwani jua huwa halizami kabisa!!!
Watu mpaka tumefikia kusema kuwa: Wakati dini ya Kislamu inaanza watu waliokuwa wanaishi enzi hizo hawakujua kama kuna nchi huku kaskazini zilizo na majira ambayo ni tofauti na yale yaliyoko huko kulikoanzia Uislam na matokeo yake ndo utata huu tulionao kama kwenye mwezi Mtukufu wa Ramadhani mwaka huu. Wangejua kuwa huku wakati wa majira ya theluji kukoje na wakati wa majira kiangazi kukoje, labda utata huu usingekuwepo.
Mwamedi Semboja,
Oslo,
Norway.
3 comments:
Duh! Hiyo kali!!!! Poleni nyote mnaoishi kaskazini ya dunia
Mie nakubaliana na Imam Senaid. Mwakani fungeni masaa ya Makka yaani masaa 13,5.
Ni kweli kama alivyomalizia Semboja kuwa kama Uislam wakati unaanza watu enzi hizo huko Mashariki ya kati wangejua kuwa kaskazini ya dunia nako kuna watu wanaishi na majira ni tofauti na mashariki ya kati, basi leo huko kaskazini msingekuwa mnajiuliza maswali hayo. Haya ni maoni yangu...
Post a Comment