Friday, August 05, 2011

Tamko la Wabunge wa Jiji la DSM Kuhusu Kashfa ya Shirika la UDA

Wabunge wa Jiji la Dar es salaam tumesikitishwa na tuhuma za ufisadi, ukiukwaji wa sheria, kanuni na maslahi ya wananchi katika mchakato wa ubinafsishaji wa Shirika la Usafiri Dar es salaam (UDA).

Wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam tunamshukuru Waziri Mkuu Mizengo Pinda kwa taarifa na ufafanuzi alioutoa bungeni tarehe 4 Agosti 2011 wakati wa kipindi cha maswali kwa mujibu wa Kanuni za Bunge kifungu cha 38 (4) ya kuelekeza vyombo vya dola hususan Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) , Mkaguzi wa Hesabu za Serikali (CAG) na Ofisi ya Upepelezi wa Makosa ya Jinai (DCI) kufanya uchunguzi kuhusu tuhuma husika.

Wabunge wa Jiji la Dar es salaam tuko tayari kutoa ushahidi kwa vyombo hivyo pamoja na kushirikiana na serikali kwa ujumla wake ili kuwezesha hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa haraka kuhusu tuhuma hizo kwa lengo la kulinda mali za umma na pia kutetea maslahi ya wakazi wa jiji letu wanaohangaika na adha ya usafiri.

Pamoja na kuagiza vyombo vya dola kufanya uchunguzi, wabunge wa Jiji la Dar es salaam tunatoa mwito kwa Serikali kuagiza kusitishwa mara moja kwa mkataba batili na maamuzi haramu yaliyofanyika ya kukabidhi hisa, mali na uendeshaji wa kampuni ya UDA kwa Kampuni ya Simon Group Limited ili katika kipindi hiki cha uchunguzi masuala yote ya kampuni hiyo yaratibiwe na bodi huru itayoundwa na kusimamiwa na Shirika la Hodhi ya Mali za Mashirika ya Umma (CHC) kwa mujibu wa sheria zinazohusika.

Wabunge wa Jiji la Dar es Salaam kwa nafasi yetu kama wajumbe wa Baraza la Halmashauri ya Jiji la Dar es salaam tunasisitiza kuufahamisha umma wa wakazi wa mkoa wetu na watanzania kwa ujumla kwamba maamuzi yote yaliyofanywa na Mstahiki Meya Didas Massaburi yanayotajwa kuridhiwa na vikao vya jiji ni batili kwa kuwa yamefanyika kwenye vikao visivyokuwa halali bila kuzingatia sheria, kanuni na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam.

Izingatiwe kuwa tarehe 10 Juni 2011 Meya Massaburi kwa kushirikiana na kaimu Mkurugenzi wa Jiji walishiriki kikao batili kilichoitwa mkutano maalum wa wanahisa wa UDA na kufanya maamuzi haramu ya kukabidhi Shirika na mali zake kwa kampuni ya Simon Group. Wabunge wa Jiji la Dar es salaam tunaunga mkono kuvunjwa kwa bodi iliyokuwepo ya UDA na hatua za haraka za kunusuru hisa na mali za UDA hata hivyo, hatua za kuvunja kwa bodi hiyo hazikupaswa kuambatana na na kukiuka sheria na kanuni kwa kuhamisha umiliki huo.

Maamuzi hayo yalifanyika bila kuheshimu maelekezo ya barua ya Ofisi ya Waziri Mkuu ya tarehe 28 Februari 2011 yenye kumbu. Na CAB. 185/295/01/27 ambayo iliagiza kusitisha mara moja mchakato wa kuuza hisa ambazo hazijagawiwa barua ambayo nakala yake iliwasilishwa kwa mkurugenzi wa Jiji na Meneja Mkuu wa UDA pamoja na Wizara zingine zinazohusika.

Izingatiwe kwamba mkutano alioufanya Meya Massaburi ulitanguliwa na kikao batili cha bodi ya wakurugenzi wa UDA chini ya uenyekiti wa Iddi Simba cha tarehe 28 January 2011 kilichofanya maamuzi haramu ya kuuza hisa zisizogawiwa (unallotted shares) kwa kampuni ya Simon Group Limited bila kuzingatia sheria, kanuni, taratibu na maslahi ya wananchi wa Dar es salaam.

Vikao hivyo vya kamati ya uongozi pamoja na baraza la madiwani vimeitishwa kinyemela wakati wabunge wakiwa kwenye bunge la bajeti Dodoma bila kuwashirikisha wabunge kwa ukamilifu wetu ambao ni wawakilishi wa wananchi wote wa mkoa wa Dar es Salaam.

Mikutano maalum iliyoitishwa kuhalalisha maamuzi haramu yaliyofanywa na Meya Massaburi kuhusu UDA yaani kikao cha kamati ya fedha na uongozi ya tarehe 29 Juni 2011 na Baraza la Madiwani wa Halmashauri ya Jiji tarehe 20 Julai 2011 ilikuwa batili kwa notisi kutolewa bila kuzingatia kanuni na maamuzi kufanyika bila mikutano kuwa na akidi.

Kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Mikutano na Shughuli za Halmashauri ya Jiji la Dar es Salaam (Zilizotungwa chini ya Kifungu cha 42 cha Sheria ya Serikali za Mitaa-Mamlaka za Miji ) na. 8 ya mwaka 1982) kifungu 8(2) na 52 akidi katika mikutano maalum ni theluthi mbili ya wajumbe hivyo vikao vyote vilivyofanyika ni batili na maamuzi yote yaliyofikiwa ni haramu.

Hivyo, wabunge wa Mkoa wa Dar es salaam tunataka Meya Massaburi, Mkurugenzi wa Jiji Bakari Kingobi na watendaji wote wa jiji la Dar es salaam waliohusika wasimamishwe mara moja katika kipindi chote cha uchunguzi na kuchukuliwa hatua stahili baada ya uchunguzi huo kwa mujibu wa sheria, kanuni na maslahi ya umma. Aidha, hatua kali zaidi za kisheria zichukuliwe kwa mwenyekiti wa bodi ya UDA, wajumbe wote wa bodi na watendaji wote wa UDA waliohusika na kashfa hiyo.

Aidha, pamoja na Waziri Mkuu kueleza kwamba taarifa ya vyombo vitakavyochunguzwa itatolewa kwa Kamati ya Miundombinu , wabunge wa Dar es salaam tunataka taarifa na ufafanuzi zaidi kutolewa na serikali bungeni kwa kutokana na mgogoro wa kimaslahi ulioelezwa kuhusu kamati ndogo iliyoundwa na kamati ya miundombinu na pia kutozingatiwa kwa ukamilifu kwa kanuni za bunge katika kutoa majukumu kwa kamati kuhusu kashfa hii ya UDA.

Serikali izingatie kwamba uhalali wa kimaadili wa kamati ndogo iliyoundwa uko mashakani kutokana na mwenyekiti wa kamati hiyo, Mheshimiwa Athuman Juma Kapuya (Mb) kuelezwa kwamba ana uhusiano na kampuni ya Simon Group Limited kutokana na kutajwa kwenye nyaraka za wanahisa wa kampuni hiyo ambayo mkataba na matendo yake yanapaswa kuchunguzwa na kuchukuliwa hatua na vyombo vya dola.

Serikali izingatie kwamba Kamati inayopaswa kuhusishwa kwa karibu katika hatua za haraka zinazopaswa kuchukuliwa ni Kamati ya Hesabu za Mashirika ya Umma kwa kwa mujibu wa Kanuni za kudumu za Bunge kifungu ya 115 na Nyongeza ya Nane kipengele cha 13 (d) (e) ndiyo inayohusika na majukumu ya kutathmini ufanisi wa mashirika ya umma ikiwemo UDA na kufuatilia utekelezaji wa Sera ya ubinafsishaji wa Mashirika ya Umma likiwemo UDA ambalo mpaka sasa halijaondolewa katika orodha ya mashirika yaliyowekwa kwenye mchakato huo kwa mujibu wa kanuni na sheria.

Wabunge wa Dar es salaam wanataka Serikali izingatie kwamba pamoja na udhaifu kwenye uongozi wa Jiji la Dar es salaam matatizo ya UDA yamechangiwa pia na Ofisi ya Msajili wa Hazina kutokuwa makini katika hatua zote kwa kushirikiana na CHC katika masuala ya ubinafsisaji wa UDA. Hivyo, tunataka Waziri wa Fedha atoe kauli na Serikali ichukue hatua kwa watendaji wote wa Wizara ya Fedha waliosababisha taifa kuingia katika hasara, mali za umma za UDA kupotea na wananchi wa Dar es salaam kuendelea kupata matatizo ya usafiri.

Wabunge wa Dar es salaam tunataka mali zilizobaki za kampuni ya UDA hususani magari, majengo na viwanja kufanyiwa tathmini upya na ya haraka ili kuunganisha mchakato wa Mradi wa Mabasi yaendayo Haraka (DART) ambao uko chini ya ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwa na mfumo thabiti zaidi na mamlaka itakayosimamia vizuri zaidi mfumo wa usafiri wa umma (mass transit) katika mkoa wa Dar es salaam ili kuongeza ufanisi, kupunguza adha ya usafiri kwa wananchi na kuchangia katika kupunguza msongamano wa magari katika jiji la Dar es salaam.

Wabunge wa mkoa wa Dar es salaam tunawaomba wakazi wa mkoa wetu na wananchi kwa ujumla kuendelea kutuunga mkono katika hatua zote tunazochukuwa kuhusu suala la UDA na mali nyingine za jiji la Dar es salaam kama sehemu ya wajibu tuliotumwa wa kuwawakilisha na kuisamamia serikali.

Tamko hili limetolewa tarehe 4 Agosti 2011 na wabunge wafuatao wa mkoa wa Dar es salaam:

  • Abas Mtemvu-Mwenyekiti,
  • John Mnyika-Katibu,
  • Mussa Zungu,
  • Dr Faustine Ndugulile,
  • Philippa Mturano,
  • Mariam Kisangi,
  • Zarina Madabida,
  • Iddi Azzan,
  • Halima Mdee,
  • Eugine Mwaiposa,
  • Angellah Kairuki
  • Prof. Fennella Mukangara

No comments: