Rais Banda amfukuza kazi mkuu wa polisi
Rais Joyce Banda wa Malawi.
Rais mpya
wa Malawi Joyce Banda amemfuta kazi mkuu wa polisi Peter Mukhito, kwa mujibu wa
taarifa zilizotangazwa na vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali.
Bibi Banda aliapishwa kuwa Rais Jumamosi
baada ya kifo cha Rais Bingu wa Mutharika wiki iliyopita. Amekuwa makamu wa
Rais tangu mwaka 2009, lakini alikorofishana na Bw Mutharika na kujiondoa
kutoka chama chake kinachotawala.
Hakuna sababu iliyotolewa ya
kuondolewa kwa Bw Mukhito, lakini mwandishi wa BBC nchini humo anasema
ameshtumiwa kwa uongozi mbaya wakati wa ghasia za kuipinga serikali zilizotokea
mwaka jana.
Bw Mutharika, mwenye umri wa miaka
78, alipatwa na mshtuko wa moyo siku ya Alkhamisi iliyopita ingawa kifo chake
hakikuthibitishwa mpaka siku ya Jumamosi.
Alitawala Malawi kwa kipindi cha
miaka minane lakini hivi karibuni alishtumiwa kwa kufisidi uchumi na kutawala
kwa mabavu.
Malawi imekumbwa na ukosefu wa
mafuta na fedha za kigeni tangu Uingereza na wahisani wengine kufuta misaada
yao.
Mwandishi wa BBC Raphael Tenthani
akiwa mjini Blantyre anasema aliyekuwa mkuu wa polisi alianza kupata sifa mbaya
mwaka uliopita baada ya kumhoji mhadhiri mmoja kwa kulinganisha vuguvugu la
upinzani katika nchi za Tunisia na Misri kuwa sawasawa na mgogoro wa mafuta
nchini Malawi.
Tukio hilo hatimaye lilisababisha
kufungwa kwa tawi moja la chuo kikuu cha Malawi.
Mnamo mwezi wa Julai mwaka jana
,takriban watu 19 waliuawa kwa kupigwa risasi na polisi wakati wa maandamano ya
kuipinga serikali kuhusu uchumi unaozidi kuzorota nchini humo.
Wakati huo huo maafisa wa serikali
wanasema matayarisho yanafanywa kurudisha maiti ya Rais Muthariika kutoka
Afrika ya Kusini ambako alisafirishwa baada ya kupatwa na mshtuko wa moyo.
Kutoka BBC Kiswahili
No comments:
Post a Comment