Aachwa na mume kwa kuzaa watoto wa ajabu
Sofia Rashid (22) mkazi wa Chanika jijini
Dar es Salaam yupo njia panda kwa kutojua hatma ya watoto wake wawili ambao
wote wamekumbwa na maradhi ya ajabu ya kujaa maji kichwani.
Watoto hao Omar Mohamed (4)
na Maulidi Mohamedi mwenye umri wa miezi minne wamelazwa katika Taasisi ya Tiba
ya Mifupa Muhimbili (MOI) kwa ajili ya kupatiwa tiba.
Akiongea akiwa wodini, Sofia
alisema anakabiliwa na mateso moyoni mwake pale anapowaona watoto wake
wanavyoteseka kwa maradhi hayo.
Alisema watoto wake wote
walizaliwa wakiwa na maradhi hayo ambapo walipofikia miezi miwili walianza na
tatizo la kichwa kukua kwa haraka na kusababisha ashindwe kuwabeba.
Sofia alisema kwamba kutokana
na matatizo ya watoto wake, mume wake aliyemtaja kwa jina moja la Mohamed
alimpa talaka kwa madai hawezi kuishi naye kwa sababu anazaa watoto wa ajabu.
Alieleza toka apewe talaka
baba wa watoto hao hajakwenda kumjulia hali wala kumpatia huduma muhimu kwa
ajili ya watoto hao.
“Inaniuma sana nikiona hali
hii, mimi sikupenda kuzaa watoto hawa ila Mungu amepanga, lakini mwenzangu
ananiona kama mimi ndiye mwenye tatizo na kuamua kuniacha,” alisema.
Endapo ukifika kwa mara ya
kwanza na kuwaona watoto hao wakiwa wamelala kwenye kitanda kimoja wodini hapo,
hautaweza kugundua kwa haraka umri wao kama hautaelekezwa na mama yao ambaye
muda wote anakaa karibu nao kwa ajili ya kuwapatia msaada.
“Hawa hawajazaliwa wakati
mmoja, huyu Omar ana miaka minne na mdogo wake ana miezi minne tu, lakini
kutokana na ugonjwa hauwezi kumtambua nani ni mkubwa kiumri,” alisema mama yao
baada ya kuulizwa umri wao na mwandishi wa gazeti hili.
Hata hivyo, alisema licha ya
kupatiwa huduma mbalimbali za matibabu kwenye hospitali hiyo, bado anapambana
na matatizo mbalimbali ikiwemo kukosa pesa ya kununulia chakula pamoja na
mavazi ya watoto hao pamoja na yeye mwenyewe.
“Hapa nilipo sina nguo wala
chakula kwa ajili ya watoto na mimi mwenyewe, namshukuru dada yangu kwa kunipa
msaada lakini kutokana na kutokuwa na kazi maalum inakuwa vigumu kunitosheleza
mahitaji,” alisema.
Sofia aliwaomba wasamaria
wema watakaoguswa na matatizo yake kumsaidia kwa hali na mali kwa ajili ya
kumsaidia kumpatia pesa za kujikimu akiwa wodini hapo.
Afisa Uhusiano wa MOI, Almas
Jumaa alisema Sofia na wanawe walifikishwa hapo miezi minne iliyopita, ambapo
madaktari wanajitahidi kutoa huduma za kuokoa maisha ya watoto hao ikiwemo
kuwafanyia upasuaji wa kichwa.
Alisema baada ya kuwafanyia
uchunguzi imebainika watoto hao wanasumbuliwa na matatizo ya kichwa kujaa maji
na tiba yake inafanyika hospitalini hapo.
Kwa yeyote anayetaka
kumsaidia Sofia kwa huduma ya chakula, mavazi awasiliane na Afisa Uhusiano wa
Moi Almas au afike ofisi ya gazeti la Nipashe Mikocheni na kuwasiliana na Moshi Lusonzo kwa namba +255 717 336368.
No comments:
Post a Comment