Vigogo
uhamiaji wauza vibali, pasipoti; wamekuwa matajiri wa kutisha
KASHFA nyingine imeibuliwa katika Idara
ya Uhamiaji.Taarifa mpya yenye kurasa tano, imewataja vigogo hao saba wakidaiwa
kuwa na utajiri wa kutisha. Taarifa hiyo ambayo tunayo nakala yake, imedai kuwa
vigogo hao wanamiliki mali na mamilioni ya shilingi katika akaunti zao binafsi.
Maofisa saba wametajwa kwa majina na
vituo vyao vya kazi ambavyo ni Lindi, Dar es Salaam, Uwanja wa Ndege wa
Kimataifa wa Kilimanjaro (Kia) na Moshi.
Tuhuma hizo zimekuja wakati Tume
Maalumu iliyoundwa kuchunguza tuhuma za ufisadi na utoaji wa vibali bandia kwa
wageni, ikitajwa kuanza kazi juzi. Hata hivyo, habari kutoka wizarani zinaeleza
kuwa timu hiyo itaanza rasmi kazi zake leo.
Habari za uhakika kutoka ndani ya
Uhamiaji, zimedai kuwa baadhi ya wajumbe wa tume hiyo wamemhoji meneja wa benki
moja kubwa ya Moshi ili kupata ukweli wa madai kuwa kigogo mmoja wa Uhamiaji
mwenye cheo cha Naibu Kamishna (DCI), anamiliki akaunti ya fedha za kigeni.
Kigogo huyo anahusishwa pia na mtandao
wa utoaji vibali bandia kwa raia wa kigeni wanaofanya kazi mkoani Kilimanjaro
au kufanya kazi za kujitolea.
Ripoti hiyo imetaja taasisi 13,
zikiwamo zisizo za kiserikali (NGO), hospitali na hoteli za kitalii zinazodaiwa
wageni wake walipewa vibali bandia.
Mbali na kumhoji meneja huyo, inadaiwa
pia walifanya mahojiano na uongozi wa kiwanda kimoja kinachodaiwa kukutwa na
vibali bandia vya wageni 84.
Taarifa hizo zilidai kuwa maofisa
wengine waandamizi wa Uhamiaji kutoka Makao Makuu, Dar es Salaam walitarajiwa
kuwasili Moshi juzi kuungana na wenzao.
Baadhi ya maofisa waliotajwa katika
ripoti hiyo kwamba wana utajiri ni wale waliokumbwa na uhamisho katika idara
hiyo, Kia miezi mitatu iliyopita.
Katika ripoti hiyo, kigogo mmoja mwenye
cheo cha DCI anadaiwa kukutwa na Sh700 milioni katika akaunti yake, achilia
mbali kumiliki mali za mamilioni.
Mbali na maofisa hao kumiliki mamilioni
ya fedha taslimu, pia wanadaiwa ‘kufanya kufuru’ ya kununua magari ya kifahari,
nyumba na viwanja.
Ripoti hiyo inayodaiwa kuandikwa na
Maofisa Uhamiaji wazalendo, imepinga hatua ya kuhamishwa kutoka kituo kimoja
kwenda kingine, maofisa wanaotuhumiwa kukutwa na utajiri ambao haulingani na
vipato vyao.
“Tunataka ufanyike ukaguzi wa kina wa
vibali vyote vilivyotolewa kati ya 2009/2010, 2010/2011 hadi 2012 na taasisi
zote zionyeshe nakala za vibali,” imedai.
Pia taarifa hiyo imependekeza wenzao
wote wanaotuhumiwa kuwa na utajiri wa kutisha wachunguzwe na Taasisi ya Kuzuia
na Kupambana na Rushwa (Takukuru).
“Haikuwa sahihi kuwahamisha na kuishia
hapo, walipaswa wapelekwe Takukuru wachunguzwe chanzo cha utajiri wao.”
Pia wametaka kigogo anayemiliki akaunti
ya Dola, achunguzwe ili kujua alikuwa akifanya biashara gani nje ya utumishi wa
umma na kama alilipa kodi kiasi gani.
Baadhi ya maofisa Uhamiaji
wamependekeza kusimamishwa kazi kwa kigogo huyo katika kipindi hiki kwa hofu ya
kuingilia na kuvuruga uchunguzi.
Wiki iliyopita, Kamishna Mkuu wa
Uhamiaji, Magnus Ulungi aliwaambia waandishi wa habari kuwa imeundwa kwa tume
ya kumchunguza kigogo huyo.
Hata hivyo, taarifa zilizopatikana jana
zilisema tume hiyo imepanua wigo wa uchunguzi juu ya kuwapo kwa vibali bandia
katika taasisi mbalimbali.
Kabla ya kuhamishiwa Wizara ya Ulinzi
na Jeshi la Kujenga Taifa, aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani, Shamsi Vuai
Naodha alikaririwa akisema Kilimanjaro ni moja kati ya mikoa minane inayomtia
kichefuchefu nchini.
Waziri huyo alisema baadhi ya watumishi
wamekuwa wakijihusisha na mtandao wa uingiaji wahamiaji haramu nchini pia kutoa
vibali bandia kwa wageni.
Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi, Dk
Emmanuel Nchimbi alipoulizwa juzi kuhusu sakata hilo alisema ni vyema Uhamiaji
ikapewa nafasi ya kuchunguza suala hilo kwa kuwa tayari imeshateua tume ya
uchunguzi.
“Kamishna Mkuu wa Uhamiaji tayari
amelifanyia kazi jambo hilo kwa uzito unaostahili. Tuwape nafasi walichunguze
si vyema kuanza kuingilia katika hatua hii ya mwanzo,” alisema.
Serikali, bila mafanikio, imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukomesha tatizo
la wahamiaji haramu linalotajwa kuwa chanzo cha utajiri wa baadhi ya vigogo wa
Idara ya Uhamiaji.
Miongoni mwa mikakati iliyowahi
kutangazwa na Wizara ya Mambo ya Ndani ni pamoja na idara hiyo kufanya utafiti
kwa kushirikiana na Chuo Kikuu cha Mzumbe kubaini chanzo cha ongezeko la
wahamiaji haramu nchini.
Akiwasilisha Bajeti ya Wizara yake
bungeni mwaka 2007/2008 , aliyekuwa Waziri wa Mambo ya Ndani ya Nchi wakati
huo, Joseph Mungai alisema matokeo ya utafiti huo ni kuisaidia Serikali kujua
chanzo cha tatizo hilo na jinsi ya kupambana nalo kwa ufanisi zaidi.
Hatua nyingine zinazochukuliwa ni
pamoja na maofisa Uhamiaji kushiriki katika vikao mbalimbali kuanzia ngazi ya
vijiji, ili kuwapa wananchi elimu juu ya masuala yanayohusu uraia na jinsi ya
kukabiliana na wahamiaji haramu; Kutoa elimu kwa umma kupitia vyombo vya
habari; Kuweka mtandao wa kompyuta katika vituo vyote vya Uhamiaji ili
kuviunganisha na makao makuu.
Pamoja na Serikali kutangaza mkakati
huo miaka mitano iliyopita, wahamiaji haramu limeendelea kuwa tatizo sugu
linalotia doa utendaji wa idara hiyo.
Kutoka Mwananchi
No comments:
Post a Comment