Rais
Kikwete, CCM hawataki Katiba Mpya
VIONGOZI wa Chama Cha Mapinduzi (CCM) na serikali yake, hawataki
katiba mpya. Wanataka kubakiza katiba iliyopo na kuiita “Katiba Mpya.”
Hili lilianza kuonekana tangu Rais Jakaya Kikwete aliposema,
“…serikali yangu itaanzisha mchakato wa kuitazama upya katiba ya nchi yetu kwa
lengo la kuihuisha ili hatimaye tuwe na katiba inayoendana na taifa lenye umri
wa nusu karne.” Hawakumuelewa.
Lakini limejidhihirisha baada ya Kikwete kuendesha mkutano wa
Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) ya chama chake mjini Dodoma na kuazimia kipi
kiingizwe katika katiba mpya na kipi kiachwe.
Nyaraka kadhaa zinaonyesha Kikwete, ambaye ndiye aliunda kamati
ya kukusanya maoni, ndiye aliyesimamia kikao kilichoweka masharti hayo. Je, uko
wapi hapa moyo wa kuleta katiba mpya?
Kwa mfano, Jakaya Kikwete na chama chake wameweka “pendekezo”
kuwa rais apatikane kwa wingi wa kura (simple majority).
Wanasema, “Siyo kweli kuwa mshindi anayepata kura chache anakuwa
amekataliwa na wananchi…fursa iliyotolewa kwa wagombea wengine kupigiwa kura ni
kielelezo cha kuwapo demokrsia.”
Hili ni moja ya mapendekezo yalilosukuma wananchi kuchukia
katiba iliyopo na kudai katiba mpya. Kikwete anajua hili. CCM
wanajua hili, viongozi wanajua hili na wanachama wanalijua pia.
Lakini
ndani ya chama cha Kikwete, mshindi hupatikana kwa zaidi ya asilimia 50 ya kura
halali. Je, kama utaratibu wa yule mwenye kura nyingi ndiye mshindi, hata kama
aliyeshinda amezidi kura tano, kwa nini CCM wasiutumie utaratibu huo kwenye
chaguzi zao? Au Kikwete anataka kusema CCM ni bora kuliko taifa?
Kisingizio
kinachotolewa na chama hiki, ni kwamba Tanzania ni nchi maskini; hivyo ikiwa
kutakuwa na duru mbili za uchaguzi, baada ya kushindwa kupatikana mshindi
katika duru la kwanza, nchi haitaweza kumudu gharama zake. Huu ni mchoko wa
kufikiri.
Kwanza,
lini uchaguzi wa Tanzania umeendeshwa kwa fedha za ndani peke yake? Hata kabla
ya kuanza kwa mfumo wa vyama vingi, sehemu kubwa ya gharama za uchaguzi imetoka
kwa wafadhili.
Pili,
kama kigezo cha kutaka uchaguzi ufanyike mara moja ni ukosefu wa fedha
unaotokana na umasikini wa taifa, mbona CCM ambayo ndiyo masikini zaidi
inaendesha chaguzi mbili pale mshindi anapokosekana kwenye duru la kwanza?
Ndivyo
ilivyotokea kwenye uchaguzi wa kutafuta mgombea ubunge wa jimbo la Arumeru
Mashariki, Februari mwaka huu. Siyoi Sumary ambaye alishinda kura za maoni
kwenye duru la kwanza, hakutangazwa mshindi hadi duru la pili la uchaguzi
lilipofanyika na kushinda. Hivi CCM na Tanzania nani masikini?
Tatu, ni
aibu kwa mtu mwenye akili timamu kusema Tanzania ni masikini. Utajiri upo
lakini umasikini wa taifa hili unaletwa na watawala. Angalia magari wanayotumia
viongozi wa serikali – wingi na gharama yake.
Angalia
anasa za watawala? Angalia utajiri walionao baadhi ya watumishi wa umma na
familia zao – watumishi wa nyumbani, watoto, wazazi na nyumba ndogo – kila
mmoja na kigari chake.
Tanzania
imejitwisha zigo la mawaziri na naibu mawaziri 55 kutoka 50 waliokuwapo awali.
Kwa viwango vya India vya waziri mmoja kuhudumia watu 35 milioni, Tanzania
ingeweza kuwa na mawaziri wawili tu au mmoja na nusu.
Haki na
utashi wa raia haviwezi kuwekwa rehani kwa madai kuwa hakuna fedha. Kitendo cha
kumtangaza aliyeshinda kwa kura chache kuwa ndiyo rais – bila kurudiwa uchaguzi
– chaweza kuingiza nchi kwenye machafuko.
Jingine
ambalo linaonyesha CCM hawataki katiba mpya – wanataka kuweka viraka katiba ya
sasa na kuita mpya – ni kule kung’ang’ania muundo wa sasa wa Muungano wa
Tanganyika na Zanzibar.
Chama
hiki kinajua vema kuwa kwa muundo wa sasa wa Muungano, hicho wanachokiita
Muungano wa Tanganyika na Zanzibar, kimeshakufa siku nyingi. Kilichobaki sasa
ni jina tu – Serikali ya Muungano.
Viongozi
wa serikali ya Zanzibar wamenyofoa kila kitu kwenye Muungano na kukifanya chao
binafsi.
Serikali
ya Muungano imeshindwa kuchukua hatua yeyote kuidhibiti Zanzibar. Imeishia
kuunda kamati ya kutatua inachoita, “Kero za Muungano,” badala ya suluhisho la
matatizo.
Nayo
kamati iliyoundwa kutatua kero za Muungano imegeuka kero nyingine. Viongozi
wake wakuu, wote wawili – Dk. Mohammed Gharib Billal, makamu wa rais wa Jamhuri
na Balozi Seif Iddi, makamu wa pili wa rais wa Zanzibar – ni “raia wa kutoka
Zanzibar.”
Wasaidizi
wao wengine wawili wakubwa, Samia Suluhu, waziri wa nchi ofisi ya makamu wa
rais (Muungano) na Mohammed Aboud, waziri ofisi ya mkamu wa pili wa rais
Visiwani, pia ni “raia wa kutoka Zanzibar.”
Wazanzibari
hawa wanne wamejifungia kwenye kivuli cha Muungano na kuondoa kile ambacho
Zanzibar na Wazanzibari wanataka kiondoke.
Ndivyo
ilivyofanyika kwenye suala la mafuta na gesi ya Zanzibar. Limetolewa kwenye
Muungano. Kilichosalia sasa ni serikali kuwasilisha muswada bungeni
utakaoruhusu Zanzibar kuchimba mafuta yake.
Wakati
Zanzibar wakiondoa gesi yao, ile inayochimbwa kutoka bara imebaki kuwa mali ya
pamoja. Madini na vito vilivyoko bara ni mali ya Muungano. Mafuta yaliyopo
bara, nayo ni mali ya Muungano.
Ndani ya
Muungano kuna marais wawili – rais wa Jamhuri na rais wa Zanzibar. Ndivyo
katiba ya Zanzibar inavyoeleza. Lakini katiba ya Muungano inasema, “Zanzibar ni
nchi ndani ya Muungano.”
Je, hapa kuna Muungano au usanii? Hicho kinachoitwa na CCM,
“Muungano ulianzishwa kwa hiari na umetazama faida za kiuchumi, kibiashara na
kijamii,” kinatoka wapi?
Au ni kule upande mmoja kufaidi mapato ya upande mwingine,
wakati upande mwingine ukikumbatia kila kilichochake?
Vilevile, CCM wamependekeza na watahubiri kwa wananchi kwamba
mawaziri watokane na wabunge kwa madai kuwa utaratibu huo umekuwa “chachu kati
ya mihimili ya Bunge na serikali.”
Kazi ya Bunge ni kusimamia serikali. Sasa mbunge ambaye amekula
kiapo cha kusimamia serikali atawezaje kutimiza wajibu wake huo wa kikatiba
wakati yeye ni waziri?
Haya ni miongoni mwa mengi ambayo wamependekeza yabaki kama
yalivyo.
Muhimu hapa ni wananchi kukataa baadhi ya mapendekezo ya CCM,
chama ambacho kimetawala kwa miaka mingi kwa kutegemea mitaji mikuu: ujinga na
umasikini.
Wananchi wasimame kidete kutaka Katiba Mpya na siyo viraka.
Chanzo: Gazeti la Raia Mwema
No comments:
Post a Comment