Wednesday, July 25, 2012



RAMADHANI Ighondu, afisa wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS), ndiye ametajwa kuwa mtekelezaji wa mkakati wa utekaji wa Dk. Steven Ulimboka, MwanaHALISI limegundua.

Afisa huyo, licha ya kutambuliwa na Dk. Ulimboka mwenyewe, ndiye simu yake ilitumika kuandaa kikao ambako daktari alitekwa.

Ni afisa huyohuyo wa usalama ambaye alikutana na Dk. Ulimboka dakika chache kabla ya kutekwa. Uchunguzi umegundua kuwa Ramadhani Ighondu (34), ni mfanyakazi wa ikulu aliyekuwa akifanya mawasiliano ya mara kwa mara na Dr. Ulimboka. Ni mfanyakazi huyuhuyu ambaye Dr. Ulimboka amenukuliwa akisema, ‘alinipigia simu na kuniita kwenye kikao ambako muda mfupi baadaye nilitekwa’

Nyaraka nyeti ambazo mwandishi ameona zinaonyesha kuwa Ramadhani ndiye pia huitwa ‘Rama’-jina ambalo hutumia katika kujitambulisha na katika baadhi ya mawasiliano. Rekodi katika simu ya Dr. Ulimboka: Na. 0713731610 zinaonyesha Rama ndiye alifanya mawasiliano ya mwisho na daktari huyo muda mfupi kabla ya kutekwa.

Aidha, ni Rama ambaye alikutana na kiongozi huyo wa Jumuiya ya Madaktari Tanzania, maeneo ya Leaders Club, jijini Dar es Salaam, muda mfupi kabla ya kutekwa. Dr. Ulimboka alitekwa usiku wa 26 Juni, kusukumizwa kwenye gari, kupigwa, kufungwa mikono na miguu, kunyofolewa kucha na kutolewa meno; na hatimaye kutupwa katika msitu wa Mabwepande.

Rama alifanya mawasiliano ya mwisho na Dk. Ulimboka saa 5:52 kupitia simu Na.0713760473. Dokta alitekwa ‘muda mfupi’ baadaye. Rais Jakaya Kikwete aliliambia taifa kwa njia ya televisheni, mwishoni mwa mwa Juni, kuwa serikali yake haihusiki na kuteka, kutesa na kutupa daktari porini. Naye Waziri Mkuu Mizengo Pinda aliliambia bunge kuwa serikali yake haihusiki na utekaji na utesaji; na kuuliza ‘serikali imteke ili iweje?’

Mawasiliano katika simu ya Dk. Ulimboka yanaonesha mtiririko wa simu za Rama wa ikulu hadi muda wa kutekwa katika eneo la Leaders Club. Vyanzo vya taarifa ndani ya idara ya usalama wa taifa vinasema, kwa sasa Rama ‘amehifadhiwa’ kwenye jingo moja la kificho linalotumiwa na idara hiyo lililopo eneo la Ada Estate, Kinondoni, Dar es Salaam.

MwanaHALISI limeweza kuthibitisha, kupitia vyanzo vya taarifa na nyaraka mbalimbali kuwa, simu Na. 0713760473iliyokuwa ikifanya mawasiliano ya mara kwa mara na Dk. Ulimboka, ni mali ya Rama. Huyo ndiye Ramadhani Ighondu (Rama). Mzaliwa wa Makole, Dodoma. Mfanyakazi wa Idara ya Usalama wa Taifa (TISS). Idara hii iko chini ya Ofisi ya Rais (Utawala Bora) inayoongozwa na Othman Rashid. Gazeti hili limepitia nyaraka mbalimbali, likiwamo daftari la kudumu la wapigakura lililoandaliwa na Tume ya Taifa ya Uchaguzi (NEC) ili kupata fununu zaidi juu ya tuhuma za Dk. Ulimboka kwa Rama. Katika daftari hilo ambalo limetumika kwenye uchaguzi mkuu uliopita, Rama anaonekanaa kujitambulisha kama ifuatavyo:

Ramadhani Ighondu,
Nickname: Rama
Born: 28.08.1978
Place :Makole-Dodoma
Voter Registration Card: 49406879
Mobile Number:0713760473

Dk. Ulimboka ambaye anaendelea na matibabu nchini Afrika Kusini, amethibitisha MwanaHALISI kuwa mtu ambaye alikuwa anawasiliana naye mara kwa mara na kumuita kwenye mkutano maeneo ya Leaders Club, 26 Juni 2012, anatumia simu Na. 0713760473. Akizungumza kwa kujiamini Dr. Ulimboka amesema, ‘Ndio. Hiyo namba naikumbuka vizuri. Ni 0713760473. Mwenye namba hiyo alikuwa akijitambulisha kwangu kwa jina la Abeid. Huyo bwana ndiye niliyekutana naye Leaders Club muda mfupi kabla ya kutekwa’.

Alipoulizwa anawezaje kukumbuka namba iliyokuwa inafanya mawasiliano nay eye wakati kipigo alichokipata kutoka kwa watekaji kilikuwa kikubwa hadi kupoteza fahamu, Dr. Ulimboka alisema: ‘Ninafahamu ninachokisema. Huyo bwana ilikuwa ninawasiliana naye mara nyingi na niliwahi kukuta naye katika mgogoro ule wa kwanza wa madaktari’ Kauli hii ya Dk. Ulimboka inafanana na ile aliyoitoa kabla ya kupelekwa Afrika Kusini kwa matibabu, 30 Juni 2012. Katika mahojiano yake yanayopatikana kwenye mtandao wa kijamii wa You Tube, Dr. Ulimboka anasema, ‘Huyu bwana kwa muda wa siku tatu mfululizo alikuwa anajaribu kuwasiliana na mimi lakini kwa bahati mbaya ratiba yangu ilikuwa haiwezekani kumuona.

‘Nilishawahi kukutana naye kwenye mgogoro ule mwingine, lakini this time of course (mara hii) alikuwa serious (makini) akinitafuta… Huyu bwana anafanyakazi ikulu’. Katika mahojiano hayo, Dk. Ulimboka anasisitiza kuwa wakati anatekwa alikuwa na akili timamu na hivyo anamfahamu aliyemteka kkuwa ni mtu kutoka ikulu. Dr. Ulimboka anasimulia ‘mtu wa ikulu’ alivyoingia kwa gari pale walikomwambia wameketi na kumuuliza iwapo alikuwa na Deo (Dk. Deogratias Michael) na kwamba walianza majadiliano yaliyohusu hali ya mgomo na jinsi wao walivyokuwa wakiona unaweza kutatuliwa.

‘Sisi tukasema mambo yote yanafahamika. Tukaongea naye kwa muda mfupi tu; akawa anaandika… kwa hiyo pia alikuwa very busy communicating, (akionekana kujishughulisha zaidi na mawasiliano ya simu). Unaona ?’

MwanaHALISI limegundua kabla ya Dk. Ulimboka kutekwa, Rama alianza kufanya mawasiliano naye saa 12:25 jioni. Mawasiliano hayo yaliendelea 3:29 usiku, saa 4:52, saa 5:27, saa 5:40 na mwisho ilikuwa saa 5:52 usiku. Haya mawasiliano ambayo Dk. Ulimboka aliishasimulia kuwa yalielekea katika kukutana kwake na mwenye simu Na. 0713760473. Ni mwenye simu hii aliyeandaa mkutano, anakumbuka Dk. Ulimboka. Kabla simu ya Rama kumwita Dk. Ulimboka kwa mara ya kwanza siku hiyo, saa 12:25, ilifanya mawasiliano na Buruani Ntilongwa, mmiliki wa simu Na. 0712359533.

Mawasiliano hayo yalifanyika kati ya saa 2:08 na 2:24 usiku. Aidha, nyaraka zinaonesha kila pale Rama alipowasiliana na Dr. Ulimboka, alifanya mawasiliano pia na Moshi Marungu Shabani anayemiliki simu Na. 0761132663 na 0655162663. ‘Nakwambia ndugu yangu, kila pale ambapo Rama alifanya mawasiliano na Dk. Ulimboka, utaona hapohapo alifanya mawasiliano na Abdallah Kunja na Ntilongwa. Hawa ni watu muhimu sana kwenye sakata hili.’ Taarifa zimeeleza.

MwanaHALISI limegundua kuwa siku mbili kabla ya Dk. Ulimboka kufanyiwa unyama huo (24 June 2012), simu ya Rama iliingizwa salio la Sh. 252,849. Hili ni salio kubwa pekee kuingizwa kwenye simu hiyo tangu mwanzo ya mwaka huu. Nyaraka zinaonyesha tarehe 4 Mei 2012 simu ya Rama iliwahi kuishiwa salio kabisa hadi kufikia kiwango cha Sh.1. Kwa mujibu wa nyaraka hizo zilizosambazwa na kituo cha sheria na haki za binadamu sehemu mbalimbali duniani, Rama kila alipomaliza kumuita Dk. Ulimboka, haraka alipiga simu kwa Kunja, Ntilongwa na Marungu.

Wengine ambao walikuwa na mawasiliano ya mara kwa mara na Rama kabla ya kutekwa kwa Dk. Ulimboka ni

Mohammed Hassan Na. 0655524444,
Shomari Kondo Na. 0714666304,
Optat Jacob Marandu Na. 0716611625,
Mbega Hisbert Na. 0715222778


Kwa mujibu wa kumbukumbu zilizopo kwenye daftari la wapigakura la NEC, Mohammed Hassan, ni mkazi wa Ilala, Dar es Salaam. Alizaliwa 12 Agosti 1980. Mbali na kumiliki namba hiyo, anatumia pia namba nyingine: 0717242789. Naye Shomari Kondo amezaliwa 1 Januari 1976. Ni mkazi wa Dar es Salaam. Anamiliki simu nyingine Na. 0713671640. Marandu ametambuliwa kwenye daftari hilo kuwa amezaliwa 1979 mkoani Dodoma; huku Mbega akionyeshwa kuzaliwa 16 Mei 1978 na mkazi wa Tabata, jijini Dar es Salaam.

Taarifa nyingine kutoka ndani ya idara ya usalama wa taifa zinasema, tangu 26 Juni 2012, pale jaribio la kumteka Dk. Ulimboka lilipofanikiwa , Rama aliacha kutumia simu yake hiyo. Alianza kutumia tena simu yake, tarehe 1 Julai kwa kutuma ujumbe mfupi (sms). Namba alizokuwa anatumia sana kuwasiliana kuanzia 1 Julai 2012 ni:

0714293425
0717030405
0713510585 na
0715466995.

Toleo lililopita la gazeti hili lilimnukuu mtoa taarifa akisema, ‘Wakati wakimtesa Ulimboka, ni Rama aliyekuwa akisisitiza kuelezwa kama Ulimboka ametumwa na CHADEMA na kwamba ni nani hasa katika CHADEMA anayemtumia’ Mmoja wa watoa taarifa wa ndani ya idara ya usalama anasema, ‘Wazzo lililopo Usalama wa Taifa ni kuwa Ulimboka anatumiwa na Mnyika pamoja na Dk. Slaa’ Wengine ambao ni maswahiba wa Rama aliowasiliana nao mara nyingi katika kipindi hicho ni; Abdi Abdi Na. 0713229919, Najma Damian Na. 0712704908, Spa Wilson I. Sima Na. 0712540502 na Zulfa Swalehe Na. 0719496505.

Katika daftari la wapigakura, Abdi Abdi anaonyesha amezaliwa 1977; Spa Wilson I. Sima amezaliwa mwaka 1960 na Zulfa Swalehe amezaliwa mwaka 1950. Rama ni mfanyakazi wa idara ya usalama wa taifa sliyepo chini ya naibu mkurugenzi wa idara ya usalama anayeshughulikia siasa, Jack Zoka. Anadaiwa kushiriki kikamilifu kumtesa Dk. Ulimboka katika moja ya majumba ya kificho na hatimaye kumtelekeza msituni Mabwepande, nje ya jiji la Dar es Salaam.

Uchunguzi huu unakuja baada ya gazeti hili kuripoti kuwa Zoka, ndiye mtuhumiwa Na. 1 kwenye sakata la utekaji na utesaji wa Dk. Ulimboka. Zoka anatajwa pia katika kilichoitwa ‘njama za kutaka kuangamiza maisha ya katibu mkuu wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), Dk. Willibrod Slaa, mbunge wa Ubungo, John Mnyika na wengine waliopachikwa jina la ‘wakosoaji wakuu wa serikali’

Taarifa mpya za uchunguzi juu ya maandalizi na kutekwa kwa Dk. Ulimboka, zinakuja wiki moja tangu Kamanda wa Kanda Maalum ya Polisi mkoani Dar es Salaam, Suleiman Kova atangaze kufikisha mahakamani mtu mmoja aliyedai amekiri kuhusika na utekaji wa Dk. Ulimboka. Kova aliwaambia wandishi wa habari kuwa polisi wamekamata mtu aitwaye Joshua Malundi kutoka Kenya ambaye amekiri kuteka na kutesa Dk. Ulimboka. Amedai kuwa mtuhumiwa alikwenda kutubu katika Kanisa la Ufufuo na Uzima, Kawe Dar es Salaam. Lakini tayari mchungaji wa kanisa hilo, Josephat Gwajima amekana kauli ya Kova juu mtuhumiwa wake na kusema ‘Serikali lazima ieleze vizuri’

Mchungaji Gwajima amewaambia waamini wake,’Kwanza huyo mtu hajaja kwetu kutubu…. Kama kutubu, basi mtu huyo angetubu huko kwao Kenya na kuhoji, ‘kwani kwao Kenya hakuna Mungu?.

No comments: