JANA tarehe 18 Julai, 2012, majira ya
alasiri kumetokea ajali ya kuzama kwa meli ya MV SKAGIT katika eneo la Chumbe,
Zanzibar. Meli hiyo iliyokuwa ikitokea Dar es Salaam kueleka Zanzibar
ilikuwa imebeba watu 290.
Kati yao watu wazima 250,
watoto 31 na wafanyakazi wa meli 9.
Amiri Jeshi Mkuu, Mheshimiwa Jakaya Mrisho
Kikwete aliagiza vyombo vya ulinzi na usalama vya Serikali ya Muungano yaani
JWTZ na Polisi waanze kazi ya uokoaji mara moja.
Kazi hiyo imefanywa kwa kushirikiana na
vyombo vya usalama vya Serikali ya Mapinduzi Zanzibar na meli za makampuni
binafsi. Mpaka giza lilipokuwa limeingia na hivyo kazi ya uokoaji
kusitishwa mpaka kutakapokucha tarehe 19 Julai, 2012, watu 136 walikuwa wameokolewa na maiti 31 zilikuwa zimepatikana. Aidha, mali
zilizokuwa kwenye meli hiyo hazikuweza kuokolewa.
Kufuatia ajali hiyo, Rais wa Jamhuri ya
Muungano alizungumza na Dkt. Ali Mohamed Shein, Rais wa Serikali ya Mapinduzi
Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi. Alimpa pole kwa ajali iliyotokea
hasa kwa vifo na majeraha waliyopata Watanzania wenzetu na watu wasiokuwa raia
wa Tanzania.
Alimuomba afikishe salamu za rambirambi
kwa ndugu zetu waliopotelewa na jamaa zao na kuwapa pole waliopata majeraha na
maumivu maungoni mwao. Rais wa Jamhuri ya Muungano alisema kuwa huu ni msiba
wetu sote na kwamba majonzi yao ni majonzi yake na ya Watanzania wote.
Kwa ndugu zetu waliojeruhiwa tunawaombea kwa Mwenyezi Mungu awape ahueni na
wapone haraka ili waweze kuendelea na shughuli zao za kujiletea maendeleo na
kulijenga taifa letu.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
amempongeza Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi, Dkt. Ali
Mohamed Shein na viongozi wote wa ngazi mbalimbali kwa uongozi wao thabiti
tangu taarifa ya kutokea kwa ajali mpaka sasa. Aidha, amewapongeza
maafisa na askari wa vyombo vya ulinzi na usalama na wafanyakazi wa meli
binafsi, kwa juhudi kubwa walizozifanya za uokoaji wa ndugu zetu waliopatwa na
maafa haya makubwa na ya aina yake. Amewataka waendeleze juhudi hizo leo
na siku zijazo.
Rais amewataka wananchi wawe na moyo wa
subira na uvumilivu wakati kazi ya uokoaji inaendelea. Kama ilivyofanyika
katika ajali ya MV Spice Islander miezi 10 iliyopita, uchunguzi wa kina
utafanyika kubaini chanzo cha ajali.
Kutokana na ajali hiyo na msiba huu
mkubwa, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mheshimiwa Rais Jakaya Mrisho
Kikwete, ametangaza maombolezo ya taifa ya siku tatu ambapo bendera zitapepea
nusu mlingoti kuanzia leo, tarehe 19 Julai, 2012.
Asanteni sana.
Imetolewa na:
Kurugenzi ya Mawasiliano ya Rais,
Ikulu.
Dar es Salaam.
19 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment