lafungwa na serikali
Serikali ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
imelifungia kutochapishwa gazeti la MwanaHalisi kuanzia 30 Julai, 2012 kwa muda
usiojulikana kutokana na mwenendo wake wa kuandika habari na makala za
uchochezi, uhasama na uzushi likiwa na nia ya kusababisha wananchi kukosa imani
na vyombo vya dola hali inayoweza kuhatarisha amani na mshikamano uliopo
nchini.
Katika matoleo yake hivi karibuni, gazeti la
MwanaHalisi toleo Na. 302 la Jumatano Julai, 11 – 18, 2012 na toleo Na. 303 la
Jumatano Julai 18 – 24, 2012 na toleo Na. 304 la Jumatano Julai 25 hadi 01
Agosti, 2012 na mengine yaliyotangulia yamekuwa yakichapisha habari na makala
zenye kueneza na kujenga hofu kwa jamii.
Mhariri wa gazeti la MwanaHalisi, ameitwa na
kuonywa mara nyingi, lakini hataki kukiri kuwa maudhui ya makala zake hazina
tija kwa jamii, pia hazifuati weledi na maadili ya taaluma ya uandishi wa
habari.
Mhariri, mara zote katika utetezi wake amekuwa
akinukuu kifungu cha 18 cha Katiba ya nchi yetu ambacho kinatoa uhuru wa kutoa
maoni na kwa makusudi kutonukuu kifungu cha 30 cha Katiba hiyo kinachoweka
ukomo wa uhuru.
Uamuzi wa Serikali
Serikali imeamua kulifungia kutochapishwa kwa muda
usiojulikana gazeti la MwanaHalisi, kwa mujibu wa Sheria ya Magazeti ya mwaka
1976, kifungu Na. (25) (i), adhabu hiyo itaanza tarehe 30 Julai, 2012 kwa
mujibu wa Tangazo la Serikali (Government Notice) Na. 258 lililochapishwa
katika Gazeti la Serikali na kutolewa jijini Dar Es Salaam tarehe 27 Julai,
2012.
Serikali inawataka wamiliki, wahariri na
wanahabari kuzingatia sheria, uzalendo, weledi na maadili ya taaluma ya
uandishi wa habari katika kutekeleza wajibu wa kuhabarisha, kuelimisha na kutoa
burudani kwa wananchi.
Kama ilivyoelezwa Bungeni wakati wa kuwasilisha
Bajeti ya Wizara ya Habari, Vijana, Utamaduni na Michezo hivi karibuni
waandishi na watangazaji wa habari wanatakiwa kuhakikisha kuwa habari wanazoziandika
na vipindi wanavyoandaa vinazingatia taaluma na kuweka mbele maslahi ya Taifa
letu na uzalendo. Uhuru na haki ya vyombo vya habari uendane na wajibu.
Kuanzia sasa Serikali haitasita kuchukua hatua
dhidi ya vyombo vya habari ambavyo kwa maksudi vitatoa taarifa za uchochezi
ambazo zitahatarisha hali ya amani na utulivu uliopo nchini mwetu.
Imetolewa na
OFISI YA MSAJILI WA MAGAZETI
WIZARA YA HABARI, VIJANA, UTAMADUNI NA
MICHEZO
30 Julai, 2012
No comments:
Post a Comment