Mgomo wa daladala jijini Dar es Salaam wiki ijayo
Na Harrieth
Mandari, Dar es Salaam
CHAMA cha Wamiliki wa Daladala Dar es Salaam
(DARCOBOA), kimetangaza kuanza mgomo Jumatatu ya wiki ijayo, hadi Serikali
kupitia Mamlaka ya Udhibiti wa Usafiri wa Nchi Kavu na Majini (SUMATRA)
itakapobadilisha mfumo wa ukamataji madereva wanaokiuka sheria za barabarani.
Akizungumza na MTANZANIA Dar es Salaam jana,
Mwenyekiti wa DARCOBOA, Sabri Mabrouk, alisema wamiliki wa mabasi madogo ya
kusafirishia abiria (daladala) wamechoshwa na matatizo na malalamiko
wanayoyapata kutoka kwa waajiriwa wao ambapo magari hukamatwa bila mpangilio.
“Kwa kifupi sisi hatukatai kutii sheria na
tunasisitiza kuwa iwapo dereva au kondakta atakamatwa akivunja sheria
achukuliwe hatua, lakini siyo kupitia askari ‘maruhani’ ambao huwakamata na
kuwabambikiza makosa madereva wanayodai ya zamani,” alisema Mabrouk.
Alisema askari hao wanajulikana kama
‘maruhani’, jina ambalo limetokana na kitendo cha kuendesha mpango wa
kuwakamata kwa kujificha vituoni na kuwakamata madereva na kuwabambikizia
makosa mengi bila mpangilio.
“Hatukatai kuwa makosa yapo, lakini kwa nini
hao ‘maruhani’ wasitambulike rasmi na kukamata pale pale dereva anapokosa,
badala ya kukamata kwa makosa wanayodai wamewakuta nayo ambayo mengi kwa mujibu
wa madereva wetu ni ya uongo,” alisema Mabrouk.
Alisema askari hao ambao wengi wao walikuwa
madereva zamani, wamekuwa wakiomba rushwa kwa lazima mara wanapowakamata na
inapotokea wananyimwa wanawabambika makosa ya ziada.
Alisema ni vyema SUMATRA itamke rasmi kuwa
imewaajiri na wadau wa usafiri jijini wawatambue ili kuepusha migogoro
isiyokuwa na lazima.
“Tunaishauri SUMATRA isimamie mpango huo wao
wenyewe kwa kushirikiana na Jeshi la Polisi kwa ajili ya kudhibiti uombaji
rushwa kupita kiasi na kukamata magari bila mpangilio, ambapo hadi sasa zaidi
ya magari 100 yameshakamatwa,” alisema Mabrouk.
Naye, Katibu Mkuu wa Chama cha Madereva na
Makondakta jijini Dar es Salaam (UWAMADA), Shukuru Mlawa, alisema usumbufu
wanaoupata kutoka kwa askari wa ulinzi shirikishi wanaotumiwa na SUMATRA ni
batili, kwa kuwa wao kama wadau hawawatambui.
Aliishauri SUMATRA kutumia kitengo cha
ukaguzi badala ya askari hao ambao wamekuwa wakiendesha mpango huo bila
mpangilio.
SUMATRA hivi karibuni walianza mpango wa
kukamata madereva na makondakta wa daladala wanaokiuka sheria za barabarani.
Chanzo: Mtanzania
No comments:
Post a Comment