JAMHURI
YA MUUNGANO WA TANZANIA
TUME
YA MABADILIKO YA KATIBA
_____________________
MWONGOZO KUHUSU UTARATIBU WA WATANZANIA WANAOISHI UGHAIBUNI KUSHIRIKI
KUTOA MAONI YAO KUHUSU UPATIKANAJI WA KATIBA MPYA
_________________________
Kwa kuwa mchakato wa kupata Katiba
Mpya ni utaratibu unaosimamiwa na Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83;
tunashauri kuwa Watanzania wote wanaotaka kushiriki katika mchakato huo ni
vizuri kuzifahamu Katiba ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania ya mwaka 1977 na
Sheria ya Mabadiliko ya Katiba, Sura ya 83 ambazo zote zinapatikana katika
tovuti ya Tume ambayo ni http://www.katiba.go.tz
Kusoma Sheria hizo kutasaidia
kuielewa Katiba ya sasa ubora na upungufu wake na kuelewa utaratibu na masharti
yanayoainishwa kisheria kuhusiana na mchakato wa upatikanaji wa Katiba Mpya.
1. 1. MAMBO YA
KUZINGATIA
Kwa kuwa uratibu na ukusanyaji wa
maoni unatawaliwa na kusimamiwa na Sheria, Tume inaelekeza mambo yafuatayo
yazingatiwe:
(a)Nani
Mwenye Haki ya Kushiriki:
Mtu yeyote
ambaye ni Mtanzania kwa uraia wake anayo haki ya kushiriki katika mchakato huu.
Mtu ambaye kwa asili yake ni Mtanzania, lakini amepoteza uraia wa Tanzania
hatoweza kushiriki; na akifanya hivyo atakuwa ametenda kosa chini ya Sheria.
(b)Utaratibu wa Utoaji Maoni:
Njia tatu za ukusanyaji wa maoni
zitatumika. Njia hizo ni kama zifuatazo:
(i) Utoaji wa maoni kupitia mitandao
ya kijamii, tovuti (www.katiba.go.tz) barua pepe ya Tume, (katibu@katiba.go.tz ), nukushi + 255-22-2133442 na
+255-224-2230769
(ii)Utoaji wa maoni kupitia nyaraka
na barua zitakazotumwa kwa Tume kutumia anwani ya Tume, ambao ni: Katibu, Tume
ya Mabadiliko ya Katiba, S.L.P. 1681 DSM au Ofisi ndogo ya Tume, S.L.P. 2775
Zanzibar.
Endapo Mtanzania anayeishi Ughaibuni
atabahatika kuwepo Tanzania wakati wa ukusanyaji wa maoni, anaweza kushiriki
katika mchakato huo kama Watanzania wengine walioko nchini kwa kuhudhuria
mikutano ya kukusanya maoni iliyoandaliwa na Tume.
(c)
Utambulisho wa Mtoa Maoni:
Kila mtu
atakayetoa maoni yake Tume anapaswa kubainisha mambo yafuatayo:-
(i) majina
yake matatu;
(ii) namba
ya pasi yake ya kusafiria na mahali ilipotolewa;
(iii) nchi
na mji anaoishi;
(iv) endapo
atatumia nyaraka au barua, ataambatanisha kivuli cha pasi yake (ukurasa
unaoonyesha maelezo ya mtu mwenye pasi hiyo).
Tume inapenda kuwakumbusha
tena Watanzania kuwa utoaji wa maoni ni jambo la uhuru na hiari ya mtu na
kwamba mchakato wa kupata Katiba Mpya unawahusu raia wa Tanzania pekee.
No comments:
Post a Comment