Mawaziri wa
Jakaya Kikwete wapingana Bungeni, ni kuhusu wageni wanaofanya kazi kinyume
nchini
na Danson Kaijage,
Dodoma
KATIKA kile kinachoonekana kama
hatua ya serikali kuwakingia kifua wawekezaji wa kigeni wanaoishi na kufanya
kazi nchini kinyume na sheria, mawaziri wawili wa Rais Jakaya Kikwete wametoa
kauli za kukinzana Bungeni kuhusu uhalali wa wafanyakazi hao katika hoteli ya
kitalii ya Holes and Lodges Tanzania Ltd ya jijini Arusha.
Mawaziri hao, Dk. Emmanuel Nchimbi
wa Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi na Dk. Makongoro Mahanga, ambaye ni Naibu
Waziri wa Kazi na Ajira, walitofautiana wakati wakijibu hoja ya Mbunge wa Arumeru
Mashariki, Joshua Nassari (CHADEMA).
Mbunge huyo alimuuliza Waziri
Nchimbi mwishoni mwa wiki iliyopita wakati wabunge wakipitisha bajeti ya Wizara
ya Mambo ya Ndani, akitaka kujua kama serikali inatambua uwepo wa raia wa
kigeni ambao wanafanya kazi zinazoweza kufanywa na Watanzania.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kuhusiana na
wageni wanaoishi nchini na kufanya kazi kinyume na sheria, sasa nimemwandikia
waziri majina ya watu watatu raia wa India ambao wamekuwa wakiishi na kufanya
kazi kwenye kampuni inayomiliki hoteli za Holes and Lodges Tanzania Ltd ya
jijini Arusha, ambazo zamani zilikuwa zikimilikiwa na serikali.
“…Na watu hawa wanafanya kazi za
kawaida za ufundi na uhasibu, ambazo zinaweza kufanywa na Watanzania, kwa hiyo
naomba waziri atuambie wageni hao wanaishi nchini kwa kufuata vibali gani kwa
muda huo wa miaka mitano,” alisema Nassari.
Hata hivyo katika ufafanuzi wake,
Dk. Nchimbi licha ya kumshukuru Nassari kufanya kazi nzuri ya kuisadia Idara ya
Uhamiaji katika mkoa wake, alisema kuwa taarifa alizozitoa na watu aliowataja,
ilithibitika kuwa walikuwa na vibali halali vya kuishi nchini na mmoja wao
kibali chake kilikuwa kimeisha muda wake.
“Kwa maana hiyo katika kumsaidia
mheshimiwa Nassari ili awe anapata data kamili na za kusaidia, namwelekeza kwa
Afisa Uhamiaji Mkoa wa Arusha atoe ushirikiano kwa kumuelimisha azijue taratibu
za uhamiaji,” alijibu Waziri Nchimbi, jambo ambalo halikumridhisha muuliza
swali.
Mbunge huyo aliamua kulielekeza
swali hilo kwa Wizara ya Kazi na Ajira, wakati wa kupitisha bajeti yao Jumanne
wiki hii, ambapo katika majibu yake, Dk. Mahanga alitofautiana na Dk. Nchimbi
kuhusu wageni hao.
Katika majibu yake, Dk. Mahanga
alikiri kupokea taarifa za kuwepo kwa wageni hao na kuliezea Bunge kuwa,
amewahi kufika hotelini hapo mwaka jana na kuamuru wafukuzwe nchini, na hivyo
akashangaa kusikia bado wanaendelea kufanya kazi.
“Mheshimiwa Mwenyekiti, kimsingi
nakubaliana na mheshimiwa Nassari, na nikiri kwamba natambua kuwepo kwa watu
ambao waliingia nchini bila kuwa na kibali chochote, nimefika kwenye hiyo
hoteli na nikaagiza waondoke nchini haraka...naagiza tena kuwa tukimaliza
kupitisha bajeti yetu hii wawe wameondoka,” alisema Mahanga.
Majibu hayo ya mawaziri yalionekana
kuwakoroga wabunge, huku baadhi yao wakihoji inakuwaje waziri mwenye dhamana ya
mambo ya ndani hana taarifa za wageni waliowahi kufukuzwa nchini, lakini
wakakaidi.
Akizungumza na Tanzania Daima, muda
mfupi baada ya Bunge kuahirishwa juzi jioni, Nassari, alisema kuwa pamoja na
serikali kudai ilimfukuza mfanyakazi huyo si kweli kuwa aliondoka nchini.
Alisema kuwa kilichofanyika ni
kwamba alikimbilia Zanzibar katika hoteli ya kampuni hiyo na kujificha, lakini
akasisitiza kuwa kimsingi bado yupo nchini bila kuwa na vibali halili.
Mbunge huyo, alishangazwa na hatua
ya viongozi wa serikali kuwa na ujasiri wa kusema uongo bungeni wakati wakijua
wazi kuwa mtu kuingia nchini kinyume na taratibu za nchi ni jambo la hatari
ambalo linaweza kusababisha maafa makubwa kiusalama.
Chanzo: Tanzania Daima
No comments:
Post a Comment