TAARIFA KWA UMMA KUHUSU KUWEPO KWA MGONJWA WA
EBOLA, WILAYA YA KARAGWE MKOA WA KAGERA, TANZANIA
Utangulizi
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii inapenda kutoa
taarifa kwa umma, kuhusu tetesi zilizokuwa zimeenea hapa nchini kutoka kwenye
vyombo mbali mbali vya habari kuhusu kuwepo kwa mgonjwa wa Ebola,wilayani
Karagwe mkoa wa Kagera.
Mnamo tarehe 3 Agosti 2012, Wizara ya Afya na
Ustawi Wa Jamii ilipokea taarifa kutoka kwa mganga mkuu wa wilaya ya Karagwe ya
kuwepo kwa mgonjwa aliyekuwa anahisiwa kuwa na dalili za ugonjwa wa Ebola,
katika hospitali ya Wilaya ya Nyakahanga.
Aidha,taarifa hiyo ilibainisha kuwa mgonjwa huyo
alikuwa ni mtoto wa kiume mwenye umri wa miaka (6) kutoka katika kijiji
cha Nyakatundu wilayani Karagwe. Mgonjwa huyu alikuwa na dalili za homa kali,
kulegea, kutokwa damu puani, kutapika damu, na kukojoa damu.
Maelezo kutoka kwa mama mzazi zilieleza kuwa mtoto
huyu alianza kuugua kuanzia tarehe 30 Agosti 2012, ambapo alipatiwa dawa ya
Septrin baada ya hospitali binafsi kuonyesha kuwa ana ugonjwa
wa“Typhoid”.
Uchunguzi wa awali katika hospitali ya Nyakahanga
ulionyesha kuwa mtoto huyu alikuwa anasumbuliwa na uambukizo kwenye haja
ndogo (Urinary Tract Infection).Vile vile alifanyiwa uchunguzi wa kimaabara na
Vipimo vya malaria, Hepatitis na Typhoid havikuonyesha kuwepo kwa
magonjwa haya. Hospitali inaendelea kumpatia matibabu mtoto huyu na imewaweka
mgonjwa na mama yake anayemtunza kwenye chumba maalum (Isolatiom room) kwa
ajili ya uangalizi zaidi.
Aidha mnamo tarehe 4 Agosti 2012, timu za
wataalamu kutoka Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii kwa kushirikiana na timu ya
mkoa wa Kagera imeweza kufika na kumfanyia uchunguzi wa kina pamoja na kuchukua
sampuli za damu kwa ajili ya uchunguzi zaidi katika maabara ya Taifa ya
uchunguzi wa magonjwa na Maabara za nje ya nchi, ili kubaini kama ameathirika
na ugonjwa wa Ebola.
Timu hiyo ya wataalamu imetoa taarifa kuwa hali ya
mgonjwa huyu kwa sasa imeimarika ikiwa pamoja na kutokuwa na homa, kutapika na
kukojoa damu kumekoma pia, uchunguzi uliofanywa kwa mama wa mtoto umeonyesha
kuwa hana dalili zozote za ugonjwa wa Ebola.Vile vile hakuna taarifa ya mtu
mwingine yeyote kwenye familia hiyo au kwenye maeneo ya kijiji hicho au cha
jirani kuwa na dalili za ugonjwa huo.
Kufuatia taarifa hii, Wizara ya Afya na Ustawi wa
Jamii kwa kushirikiana na Mkoa wa Kagera imechukua hatua zifuatazo;
• Imepeleka timu ya wataalamu mbali mbali kutoka
Wizarani na mkoa kwa lengo la kwenda kufuatilia na kutoa taarifa kuhusu
kuwepo kwa ugonjwa huo.
• Imetoa elimu ya Afya kuhusu njia za kuzuia kuenea
ugonjwa wa Ebola pamoja na dalili za ugonjwa huu, kwa wananchi na watumishi
wa afya katika hospitali ya Nyakahanga
• Kupeleka vifaa kinga katika hospitali ya
Nyakahanga pamoja na maeneo ya mipakani
• Kutoa matangazo kwa jamii kwa kutumia vipaaza
sauti na kupitia radioni (Radio Karagwe) kuhusu ugonjwa huu. Aidha,
vipeperushi pia vimetolewa.
Hitimisho
Wizara inapenda kuufahamisha umma kuwa mpaka sasa
hakuna mgonjwa yeyote aliyethibitishwa kuwa na ugonjwa wa Ebola hapa
nchini.Aidha, Wizara ya Afya imejiaanda kikamilifu kukabiliana na ugonjwa huu
iwapo utatokea hapa nchini.
Kwa sasa timu za wataalum zipo katika mikoa
ya Mara, Mwanza, Kagera, Kigoma, Kilimanjaro na Arusha, kutoa elimu juu ya
ugonjwa huu kwa wataalamu na kwa wananchi na vilevile kufuatilia ugonjwa huu
sehemu za mipakani.
Wizara inaendelea kutoa wito kwa wananchi kutoa
taarifa haraka kwenye kituo chochote cha kutolea huduma za afya, mara wanapoona
dalili za ugonjwa huu.
Imetolewa na:
kitengo cha Mawasiliano
Wizara ya Afya na Ustawi wa Jamii
Tarehe 6 Agosti, 2012.
No comments:
Post a Comment